Habari za Kitaifa

Tahadhari yatolewa maafa ya ajali barabarani yakiongezeka 2024

Na HILLARY KIMUYU August 31st, 2024 1 min read

WATU 3,056 wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabara kuanzia Januari 1  2024.

Kulingana na takwimu ya Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA), idadi hiyo imeongezeka kwa watu 146 ikilinganishwa na mwaka wa 2023.

Visa 2,910 vya ajali vilitokea kati ya Januari hadi Agosti mwaka jana,

“Tangu mwaka uanze, Wakenya 7,114 walihusika kwenye ajali, ikiwa ni zaidi ya 703 ya mwaka jana ambapo watu 3,674 walipata majeraha mabaya na wengine 585 kupata majeraha madogo,” ilisema ripoti ya NTSA.

Takwimu hizo zilionyesha kuwa ajali ya watu wanaotembea imeongezeka kwa asilimia 15.

Hii ikiwa na idadi ya 1,177 ikilinganishwa na 1,044 waliopoteza maisha yao mwaka wa 2023.

Vile vile, idadi ya abiria waliofariki iliongezeka kwa asilimia 15, abiria wapatao 595 wakipoteza maisha barabarani, ikilinganishwa na 519 mwaka 2023.

Idadi ya madereva walipoteza maisha imepungua kutoka 262 hadi 260.

Vifo vilivyohusishwa na pikipiki vikipungua kutoka 756 hadi 710.

Vifo vya abiria wa baiskeli vikipungua na 7, mwaka jana NTSA ilirekodi visa 60.

Mwaka wa 2023, zaidi ya watu 4,300 waliangamia kwenye ajali za barabarani huku 22,885 wakipata majeraha ya maisha kutokana na ajali. Ongezeko la ajali hizi linadizidi kushuhudiwa nchini.