• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Kalembe Ndile kumpa Wambua ekari mbili za shamba wiki hii

Kalembe Ndile kumpa Wambua ekari mbili za shamba wiki hii

NA WANGU KANURI

Siku kadhaa baada ya Julius Wambua Musyoka kutoka jela ya Kamiti alipotumikia kifungo cha miaka kumi kwa shtaka la kumbaka bintinye, sasa ana sababu ya kufurahia zaidi wakati huu wa sherehe za Krismasi kwa mapochopocho aliyotunukiwa.

Aliyekuwa mbunge wa Kibwezi, Kalembe Ndile, alimuahidi Wambua ekari mbili za shamba eneo la Kibwezi, Kaunti ya Makueni. Bw Ndile atampa ekari hizo mbili wiki hii.

Isitoshe, aliahidi kumjengea Wambua nyumba kwa kipande hicho cha shamba alichomtunuku.

Desemba 20, 2020, Tom Musau, mfadhili kutoka Uingereza alimpa Wambua pikipiki mpya, simu ya mkononi na  Sh10,000 za matumizi yake ya kila siku. Mfadhili huyu aliwaambia wanahabari kuwa ufichuzi wa Wambua wa kuachwa bila makao alipokuwa akitumikia kifungo chake ulimgusa ndiposa akamtunuku.

Bw Wambua, mwenye umri wa miaka 56, alikuwa akifanya kazi kama mlinda lango katika ajenti wa bustani la Kenya Wine mjini Yatta, Kaunti ya Machakos wakati ambapo alitiwa mbaroni usiku wa Aprili 28, 2011 kwa madai yaliyobadilika na kuwa ya kusingizwa baadaye. Alihukumiwa Januari 24,2012 na kufungwa kifungo cha maisha ambako alikaa tu kwa miaka tisa.

Miaka mitatu baada ya kuhukumiwa, Mwende mwenye wingi wa majuto, alimtembelea gerezani na kufichua kuwa alikuwa ameelezwa na mamake Jackline Nzilani atakachosema ili amsingizie babake. Korti ilisikia kuwa bi Nzilani alikuwa anategemea kesi iamuliwe upande wake baada ya kuvurugana na bwana Wambua sababu ya kipande cha shamba.

Ufichuzi huu ukaanza safari ndefu ambayo iliishia kwa bwana Wambua kuachiliwa huru Alhamisi ya wiki iliyopita. Jaji George Odunga wa mahakama ya juu, alitupilia mbali hukumu iliyotolewa na korti  mahakama ya majaji ya Kithimani.

Hata hivyo, hakukuwa na sherehe ya kumkaribisha nyumbani bwana Wambua kwani hakuwa na pahala ambapo angepaita nyumbani kwani aliyekuwa bibi yake aliuza shamba yao ya Kithimani, kaunti ya Machakos.

Bwana Wambua alitakikana kuwasilisha ombi lake katika korti ya Kithimani, Disemba 22, 2020 baada ya jaji Odunga kuamuru kesi hiyo kusikizwa upya.

You can share this post!

Polisi kuimarisha doria sherehe za Krismasi

Huenda aina mpya ya corona ikazimisha uchumi wa dunia