Wapigakura eneo la Kibra waanza kutekeleza haki yao kidemokrasia

Na COLLINS OMULO na SAMMY WAWERU

WAKAZI wa Kibra, Kaunti ya Nairobi na ambao ni wapigakura wameanza kutekeleza haki yao ya kidemokrasia leo Alhamisi asubuhi na mapema kuchagua mbunge katika uchaguzi mdogo hii ikiwa ni baada ya kifo cha Ken Okoth kilichotokea Julai baada ya kuugua saratani kwa muda.

Vituo vimefunguliwa saa kumi na mbili asubuhi ambapo foleni ndefu zinashuhudiwa katika wadi tano za eneobunge hilo ambazo ni Sarang’ombe, Woodley/Kenyatta Golf Course, Makina, Laini Saba, na Lindi.

Kuna jumla ya wagombea 24 wanaowania kiti hicho. Idadi ya wapigakura ni 118,658.

Chama cha ODM alichotumia Okoth wakati wa uhai wake sasa kimemdhamini nduguye ambaye ni Bernard Imran Okoth, nacho chama tawala cha Jubilee kimemdhamini McDonald Mariga.

Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna amesema kila kitu kilikuwa kikiendelea vizuri huku akielezea matumaini kwa mgombea wao.

“Kufikia sasa hakuna tukio lolote la kuhujumu mchakato huu,” amesema Sifuna.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga amekuwa mstari wa mbele kipindi chote cha kampeni kumpigia debe Imran Okoth huku Naibu Rais William Ruto akimpigia debe mwanasoka Mariga.

Wagombea wengine ni Eliud Owalo wa Amani National Congress (ANC) na Khamisi Butichi wa Ford-Kenya.

Kabla ya Jumapili, muda rasmi rasmi uliowekwa na tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka (IEBC) harakati za kampeni kufikia kikomo, viongozi wa vyama shirika walijitokeza na kupigia debe wawaniaji wao.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga, alivutia na anaendelea kuvutia ngoma upande wa Imran, akidai Kibra ni ngome ya ODM. Mariga, akionekana kuleta ushindani mkali, Naibu wa Rais Dkt William Ruto amefanya ziara kadhaa eneo hilo, kumfanyia kampeni mwanasoka huyo.

Sawa na viongozi hao, Musalia Mudavadi wa ANC na Seneta Moses Wetangula wa Ford – Kenya, wamekuwa katika mstari wa mbele kutetea wawaniaji wao.

Ni kinyang’anyiro ambacho kimeonekana kuleta mgawanyiko katika chama tawala cha Jubilee, baadhi ya viongozi wake wakiongozwa na mbunge maalum Maina Kamanda na gavana wa Kirinyaga Anne Mumbi Kamotho, wakijitokeza hadharani kuunga mkono mgombea wa ODM.

Ingawa hatua hiyo inakosolewa na baadhi ya wandani wa Dkt Ruto, inaonekana kama kuimarika kwa demokrasia. Wajuzi wa masuala ya kisiasa wanasema mkondo wa aina hiyo ukiigwa katika siku za usoni, hususan wakati wa uchaguzi mkuu, utaonesha ukomavu wa demokrasia Kenya.

“Si jambo la kawaida chama pinzani kuungwa mkono na kile tawala. Viongozi wanapaswa kuchaguliwa kulingana na rekodi ya utendakazi. Hilo linaonesha ukomavu wa demokrasia,” asema Dan Machuki.

Hatua ya Imran kupigwa jeki na baadhi ya viongozi wa Jubilee kuibuka mshindi, Naibu Rais anaitafsiri ‘Odinga kuomba msaada’ kwa kuwa ‘kitanda chake’ eneobunge la Kibra alipohudumu kama mbunge kwa muda mrefu linataka kukombolewa.

Mjadala huo pia umezua mdahalo mkali mitandaoni, wanablogu na wachangiaji wakieleza hisia na mtazamo wao.

Uchaguzi huo unachukuliwa kama njia ya Dkt Ruto kupimana nguvu na Bw Raila, katika kurithi siasa za kaunti ya Nairobi.

Shughuli ya uchaguzi huo mdogo zikiendelea, idadi ya watu waliojitokeza kushiriki inasemekana kuwa ya chini mno.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga tayari amepiga kura yake, akihimiza wakazi wa Kibra kujitokeza kwa wingi.

“Watu waruhusiwe kuonesha haki yao kidemokrasia kwa kushiriki uchaguzi huu mdogo bila kushawishiwa na yeyote. Tuko katika kitanda chetu, na ninasihi watu wajitokeze kwa wingi,” Waziri huyo Mkuu wa zamani akasema, akionekana kulenga madai kuwa kuna uhongaji wa wapigakura.

“Watu wanaotoa pesa na wengine kupokea, uhongaji, huo ni ufisadi na haionyeshi demokrasia,” akaeleza Bw Odinga.

Kwa mujibu wa sajili ya IEBC, eneobunge la Kibra lina jumla ya wapigakura 118,658. Lina jumla ya vituo 183 vya kupiga kura.

Vituo vitafungwa saa kumi na moja za jioni, kisha shughuli za kuhesabu kura zing’oe nanga na kutumwa katika kituo maalum cha shughuli hiyo.

Kulingana na IEBC, matokeo hayatapeperushwa kieletroniki kama ilivyoshuhudiwa 2013 na 2017.

Mariga ataka bangi ihalalishwe

LEONARD ONYANGO na ANITA CHEPKOECH

MGOMBEAJI ubunge katika uchaguzi mdogo wa Kibra kwa tiketi ya Chama cha Jubilee, Bw McDonald Mariga amesema atashinikiza uhalalishaji wa bangi kama atashinda kwenye kinyang’anyiro hicho cha Alhamisi.

Alisema hayo jana wakati kivumbi kilishuhudiwa kwenye kampeni za lala salama zilizoongozwa na Dkt William Ruto aliyeongoza kikosi cha Jubillee, na Bw Raila Odinga aliyeongoza kampeni za mgombeaji wa chama chake, Bw Benard Okoth.

Kikosi cha Jubilee kilikuwa katika Uwanja wa DC huku kile cha ODM kikikusanyika katika uwanja wa Joseph Kangethe, eneo la Woodley.

Pande zote mbili zilionyeshana ubabe kwa njia tofauti, ambapo mkutano wa Jubilee ulipambwa kwa burudani ya muziki kutoka kwa msanii wa regae kutoka Jamaica Kenyatta Hill akiwatumbuiza mamia ya watu waliofika uwanjani hapo.

Msanii huyo ndiye alimwongoza Bw Mariga kutoa wito wa kuhalalisha bangi.

“Tunajua shada (bangi) inatibu kansa kwa hivyo ni lazima tuisukume ihalalishwe. Hatutaki bangi ya kwenda kupiga watu ati umevuta shada. Shada ni dawa. Nataka mniingize bunge tuanze kutetea mambo ya shada,” akasema.

Wito wa kuhalalisha bangi kwa minajili ya matibabu ulikuwa ukivumishwa na aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, marehemu Ken Okoth ambaye alifariki kwa kuugua saratani.

Katika mkutano wa ODM, Bw Odinga aliandamana na viongozi wengi wa vyama tofauti, wengi wakiwa ni wanaounga mkono handisheki kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.

Miongoni mwao ni magavana Alfred Mutua (Machakos), Charity Ngilu (Kitui), Kivutha Kibwana (Makueni), James Ongwae (Kisii) na Anne Waiguru (Kirinyaga) pamoja na wabunge kadhaa akiwemo Maina Kamanda (Maalumu).

Katika eneo la Woodley, Bw Odinga alisema uchaguzi wa Kibra utakuwa mashindano kati ya handisheki na mrengo wa Tangatanga.

Jubilee yataka IEBC imfungie nje mgombea wa ODM Kibra

Na COLLINS OMULO

KAMPENI za uchaguzi mdogo katika eneobunge la Kibra zinazidi kuchukua mkondo wa kutisha, kwani wanasiasa wanaonekana kutumia propaganda zinazotishia kuchochea umma.

Pande mbili kuu pinzani katika uchaguzi huo – ambazo ni chama cha ODM na Jubilee – ndizo zinazozozana zaidi kwa maneno na vitendo ambavyo baadhi ya viongozi wanasema vinastahili kuzimwa mara moja.

Mnamo Jumamosi, gari lililokuwa kwenye msafara wa Bw McDonald Mariga anayepeperusha bendera ya Jubilee lilirushiwa mawe na kuvunjwa vioo na watu wasiojulikana.

Viongozi wa Jubilee mnamo Jumapili waliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imzuie mgombeaji wa ODM, Bw Bernard ‘Imran’ Okoth kuwania wadhifa huo kwani wanaamini shambulio hilo lilitendwa na wafuasi wa ODM.

Lakini kwa upande mwingine, wanasiasa wa ODM wanadai kisa hicho kilikuwa ni njama ya wapinzani wao kutaka Imran aondolewe kwenye kinyang’anyiro.

“Tunataka kushindana kwenye ulingo ulio na amani kwa hivyo hebu wagombeaji wote na vyama vyote vya kisiasa wakumbatie amani na kuwapa watu wa Kibra nafasi ya kujichagulia kiongozi wanayemtaka,” Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa alisema Jumapili, akidai ODM inajaribu kuwahangaisha wasifanye kampeni huko.

Viongozi wa ODM walijitetea na kusema kuwa wanaodai kuwa Mbunge wa Dagoretti Kaskazini, Bw Simba Arati ndiye alihusika, watoe ushahidi.

“Huwezi kusema ni Arati kama huna ushahidi. ODM haikuhusika na tunaomba wafuasi wetu wafanye kampeni kwa amani,” akasema Mbunge wa Makadara, Bw George Aladwa ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa ODM katika Kaunti ya Nairobi.

Madai yaliyozagaa katika eneobunge hilo wakati wa kampeni kama vile ya wanasiasa kuhonga wapigakura, vitambulisho vya wapigakura kununuliwa, na pia wapigakura kuingizwa kwenye sajili kutoka maeneobunge mengine, yamezidisha taharuki ya kisiasa eneo hilo.

Zaidi ya madai hayo, hatua ya Mbunge Maalumu wa Jubilee, Bw Maina Kamanda ambaye anapigia debe ODM, kuingiza masuala ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 katika kampeni hizo pia imeibua wasiwasi kuhusu mkondo unaochukuliwa na kampeni hizo.

Wakosoaji wa Bw Kamanda wanasema ni hatari kufufua suala hilo katika kampeni za kisiasa ilhali inafahamika wazi kuwa ukatili ulioshuhudiwa katika ghasia hizo, ulisababisha zaidi ya watu 1,100 kuuawa na maelfu wengine kuachwa bila makao hadi leo.

Uhuru akosa njia Kibra

Na BENSON MATHEKA

MGAWANYIKO katika chama cha Jubilee kuhusu uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra pamoja na handisheki zimemuacha Rais Uhuru Kenyatta ‘amechanganyikiwa’.

Ingawa Rais Kenyatta alikutana na mgombeaji wa chama hicho kwenye uchaguzi huo Macdonald Mariga katika Ikulu na kumvisha kofia ya Jubilee, matamshi ya wanasiasa walio karibu naye yanaonyesha amechanganyikiwa kuhusu anayefaa kuunga mkono kwenye uchaguzi huo.

Kinyume na sheria ya vyama vya kisiasa, baadhi ya wabunge wa Jubilee wametangaza wazi kuwa hawatamuunga mkono Bw Mariga mkono wakidai wana baraka za Rais Kenyatta kumuunga mgombeaji wa cha ODM, Imran Okoth

Mnamo Jumapili, mbunge wa kuteuliwa Maina Kamanda na aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini, Dennis Waweru waliongoza kampeni za Imran.

“Chama chetu cha Jubilee kimemsimamisha mgombeaji lakini roho ya Rais Kenyatta haiko huko. Roho ya Rais Kenyatta iko kwa Imran Okoth,” akasema Bw Kamanda.

Wanachama wa Jubilee wanaompiga debe Bw Mariga wanadai kuwa wanaomuunga mkono wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto walitumia njia za mkato ili kuhakikisha Rais amemuidhinisha kama mgombeaji wa chama tawala kinyume na mapenzi yake.

Kulingana na Waziri Msaidizi Rachel Shebesh, ambaye amejiunga na wanaomuunga mkono Bw Imran, Rais Kenyatta hakuwa na nia ya kumuidhinisha Bw Mariga.

“Mimi nilikuwa Ikulu wakati huo na ninajua presha aliyowekewa Rais ili kupigwa picha akimuidhinisha Bw Mariga,” Bi Shebesh alidai alipokutana na makundi ya wanawake mtaani Kibra kuwataka wampigie kura Bw Imran.

Japo kanda yake akitoa kauli hiyo ilisambazwa mitandaoni na kuibua hisia kali, Ikulu ya Rais Kenyatta haikukanusha madai yake.

Huku hayo yakijiri, Dkt Ruto amekuwa msitari wa mbele kumpigia debe Bw Mariga na kusisitiza kuwa ana baraka za kiongozi wa chama ambaye ni Rais Kenyatta.

“Si mlimuona kiongozi wa chama akimvisha kofia mgombeaji wa chama? Sasa hawa watu wanataka waambiwe nini kingine,” aliuliza Dkt Ruto akiwasuta wanaodai kuwa Bw Mariga ni mradi wa mrengo wa ‘Tangatanga’ katika Jubilee.

Kujitolea

Kulingana na wadadisi, Rais Kenyatta hakutaka Jubilee kusimamisha mgombeaji Kibra ili kuonyesha kujitolea kwake katika handisheki yake na Bw Raila Odinga, lakini baada ya chama kumkabidhi tiketi alijipata katika hali ya kuchanganyikiwa na ikabidi akubali.

Kiti hicho kilibaki wazi kufuatia kifo cha Ken Okoth aliyekuwa mbunge wa ODM, na kakake Imran.

Alipomuidhinisha Bw Mariga, viongozi wa ODM walitilia shaka kujitolea kwa Rais Kenyatta katika handisheki na baadhi wakamtaka Bw Odinga kuwa mwangalifu.

Hata hivyo mambo yalitulia Bw Kamanda alipokutana na Bw Odinga na kutangaza kuunga mkono Bw Imran “kama mgombeaji wa handisheki.”

Wanaompinga Bw Mariga wanalaumu wanaomuunga mkono kwa kutaka kuvunja handisheki.

Katibu mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju mnamo Jumanne alisema hawana mipango ya kuwaadhibu wanaofanyia kampeni mgombezi wa chama pinzani.

Fujo nyumbani kwa Ruto

Na CECIL ODONGO na CHARLES WASONGA

VIJANA wenye hasira kutoka eneobunge la Kibra, walizua rabsha Jumanne wakitaka kuingia nyumbani kwa Naibu Rais William Ruto katika mtaa wa Karen, Nairobi.

Vijana hao walilalamikia kufungiwa nje ya mkutano ulioandaliwa katika makao hayo rasmi ya Naibu Rais kupanga mikakati ya jamii ya Abagusii kumuunga mkono Bw McDonald Mariga wa chama cha Jubilee kwenye uchaguzi mdogo wa Kibra utakaofanyika Novemba 2019.

Viongozi wa jamii ya Abagusii wakiongozwa na Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi na wabunge wanane, walihudhuria mkutano huo uliofanyika Jumanne asubuhi.

Mbunge wa Mugirango Kusini, Sylvanus Osoro alidai fujo hizo zilisababishwa na watu ambao si wa jamii ya Abagusii.

“Kila aliyefaa kuhudhuria mkutano huo alitumiwa ujumbe kwa sababu tulipanga ziara hiyo kupitia makundi ya jamii yetu Wakisii. Walioalikwa walikuwa wameketi kwenye hema kufikia saa moja asubuhi na walikuwa watu 5,000 wa kabila letu wanaoishi Kibra,” akasema Bw Osoro.

Mbunge huyo wa Chama cha Kenya National Congress (KNC) alisema waliokuwa nje walitarajia kwamba wangehutubiwa na Naibu Rais baada ya kikao hicho, lakini hilo halikufanyika ndiposa wakazua rabsha nje ya makazi hayo.

“Matukio hayo ni kawaida Kibra na sisi Wakisii hatujawahi kushiriki vituko hivyo. Wale ambao huwa na tabia hiyo wanajulikana wazi,” akasema Bw Osoro.

Bw Maangi naye alisema waliozua fujo hawakuwa wamealikwa.

“Mimi ninafahamu kwamba tuliwaalika watu na waliokuwa nje hawangeruhusiwa kwa kuwa mkutano ulikuwa ukiendelea na viongozi walikuwa wameanza kuhutubu. Tunashauri jamii yetu inayoishi Kibra kumuunga mkono Bw Mariga hapo Novemba 7,” akasema Bw Maangi.

Dkt Ruto amekuwa akiandaa vikao vya kisiasa katika makao hayo ya Karen kwa kualika wajumbe kutoka jamii mbalimbali zinazoishi Kibra.

Jamii ya Waluo

Leo Jumatano inatarajiwa wajumbe kutoka jamii ya Waluo wanaoishi Kibra watakutana naye kumdhihirishia kwamba wanamuunga mkono Bw Mariga.

Huku hayo yakijiri, wabunge wa chama cha ODM wameibua madai kwamba kuna njama ya kuvuruga sajili ya wapigakura ya Kibra.

Kwenye kikao cha Jumanne na wanahabari katika majengo ya bunge, wabunge hao walisema leo wataenda katika afisi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuitisha sajili ya wapigakura itakayotumika katika uchaguzi huo mdogo.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi na Mkurugenzi wa uchaguzi Junet Mohamed, walisema ni wajibu wa IEBC kutoa sajili kwa wadau wote katika uchaguzi huo.

Anayepeperusha bendera ya ODM katika uchaguzi huo mdogo ni kakake aliyekuwa Mbunge wa eneo bunge hilo marehemu Ken Okoth, Imran Okoth. Atakapambana na Bw Mariga (Jubilee), Eliud Owalo (ANC), Khamisi Butichi (Ford Kenya) miongoni mwa wengine.

Mwishoni mwa wiki, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi aliitaka serikali kuchunguza madai kuwa kuna watu wanaonunua vitambulisho vya kitaifa katika eneo bunge hilo la Kibra kwa lengo ya kuwanyima wapigakura haki ya kushiriki uchaguzi huo.

Elachi ajitenga na Mariga

Na CHARLES WASONGA

IDADI ya viongozi wa Jubilee wanaojitenga na mgombea wa chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Kibra McDonald Mariga inaendelea kuongezeka kila siku.

Wa hivi punde kumwambaa mwanasoka huyo wa zamani ni Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi.

Akiongea kwenye kipindi cha ‘Day Break’ katika runinga ya Citizen, mwanasiasa huyo wa Jubilee ametangaza kuwa atamuunga mkono mgombea wa ODM Benard Imran Okoth kwa sababu ndiye anaweza kuendeleza kazi iliyoanzishwa na marehemu Ken Okoth.

“Anayejitokeza kugombea kiti cha ubunge cha Kibra sharti awe mtu ambaye anaweza kuendeleza rekodi nzuri ya utendakazi wa marehemu aliyekuwa mbunge wa eneo hilo. Mariga hawezi kwa sababu ni mtu ambaye ‘hajawahi kupiga kura maishani mwake’,” Bi Elachi akasema.

Kulingana na Spika huyo aliyesimamishwa kazi mwaka 2018, Mariga hana tajriba ya kisiasa na kiuongozi kuongoza Kibra.

“Isitoshe, Mariga amevamia eneobunge la Kibra kutaka achaguliwe ilhali hana ufahamu kuhusu mahitaji ya wakazi,” Bi Elachi akasema.

Bi Elachi ambaye alihudumu kama Seneta Maalum katika Bunge la 10 amemshauri Bw Mariga kujizatiti kuelewa mahitaji ya wakazi wa Kibra kwanza kabla ya kutafuta nafasi ya kuwaongoza kama Mbunge.

Miradi

Amemtaka Bw Mariga kutaja miradi ya maendeleo ambayo amewahi kuanzisha katika eneobunge hilo kuwasaidia wakazi kujinasua kutoka kwa umaskini.

“Licha ya kupata nafasi ya kucheza soka ya kulipwa ng’ambo, ambapo alikuwa akilipwa mamilioni ya fedha, hajafikiria kuanzisha miradi ya kukuza talanta katika eneobunge la Kibra. Kwa hivyo, huyu sio mtu anayefaa kuchukua nafasi ya marehemu Okoth,” Bi Elachi akasema.

Viongozi wengine wa Jubilee ambao wametangaza kumuunga Bw Imran ni Mbunge Maalum Maina Kamanda, Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu, Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Wazee wa Mulembe wamruka Mariga

JOHN ASHIHUNDU na VALENTINE OBARA

MGOMBEAJI ubunge kwenye uchaguzi mdogo wa Kibra kwa tikiti ya Chama cha Jubilee, Bw McDonald Mariga amepata pigo baada ya kikundi cha wazee wa jamii ya Waluhya, kuamua kutomuunga mkono.

Baadhi ya wadadisi wa kisiasa wamekuwa wakisema kuwa Bw Mariga, anayeaminika kupendekezwa na Naibu Rais William Ruto, alitarajia kuvutia idadi kubwa ya wanajamii hiyo wanaoishi Kibra ili kupata ushindi.

Katika uchaguzi huo mdogo uliotokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge Ken Okoth, wagombeaji wengine wanaotoka katika jamii ya Waluhya (Mulembe) ni Bw Khamisi Butichi wa chama cha Ford Kenya na Martin Andati wa chama cha Modern Alliance Party.

Hata hivyo, chama cha Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Bw Musalia Mudavadi, aliye mmoja wa vigogo wa kisiasa wa jamii hiyo ya Magharibi, kinamdhamini Bw Eliud Owalo ambaye si wa kutoka katika jamii hiyo.

Kama ilivyo desturi ya siasa za Kenya, wakati mwingi kura hupigwa kwa misingi ya kikabila. Ni kwa msingi huu ambapo huenda msimamo wa wazee hao ukashawishi kwa kiwango fulani msimamo utakaochukuliwa na jamii ya Waluhya ambao watapiga kura Kibra.

Wazee hao wanaosemekana kuwa na ushawishi kwa masuala ya jamii ya Waluhya ambao walizungumza jana katika Kaunti ya Nairobi, walisema walitumia mbinu maalumu kuchagua kati ya ‘wana wao’ watatu.

Bw Butichi aliibuka mshindi kwa kupata alama 470 chini ya 700 na kuwashinda Bw Andati na Bw Mariga walipata alama 430 na 385 mtawalia.

Akitangaza matokeo hayo jana katika ukumbi wa Railway Cub, mwenykiti wa baraza hilo linalojitambua kama Obulala Unity of Purpose, Bw Richard Ekhalie alisema jamii ya Waluhya ndio ina idadi kubwa eneo la Kibra.

“Miongoni mwa mbinu tulizotumia kupata mshindi ni pamoja na uwezo wa kifedha, ujuzi wa uongozi, umaarufu, ajenda zake kwa watu wa Kibra, kabila pamoja na mahojiano ya moja kwa moja na wakazi wa Kibra,” akasema Bw Ekhalie.

Bw Ekhalie alisema kundi lao ambalo lilibuniwa 2014 sio la kisasa, mbali la kuangalia maslahi ya Waluhya kwa jumla.

“Tulipewa jukumu na watu wa jamii ya Mulembe kuwapa mgombeaji mmoja. Tulifanya mahojiano ya moja kwa moja na wagomeaji wote kutoka jamii ya Mluhya ambapo Butichi aliibuka mshindi,” akasema Bw Ekhalie.

Wengine waliokuwa kwenye kamati hiyo ni pamoja na Vincent Shimoli, Jeremiah Imbali, Suma Musine na Moses Wanani.

Hata hivyo, Bw Mariga anatarajiwa kupata ushindani mkali zaidi kutoka kwa Benard ‘Imran’ Okoth wa ODM kinachoongozwa na Bw Raila Odinga.

Wiki iliyopita, baadhi ya viongozi wa eneo la Magharibi waliwalaumu Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula kwa kusimamisha wagombeaji Kibra ilhali wao hudai wanatetea umoja wa Waluhya.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imepanga uchaguzi huo kufanyika Novemba 7.

Mariga atikisa handisheki

Na LEONARD ONYANGO

MUAFAKA wa maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga, maarufu kama handisheki umekumbwa na dhoruba kufuatia hatua ya kiongozi wa nchi kumuidhisha mwaniaji wa ubunge wa Jubilee katika eneobunge la Kibra, McDonald Mariga.

Baadhi ya viongozi na wafuasi wa ODM wameelezea hofu yao kuwa uhusiano kati ya viongozi hao wawili huenda ukazorota zaidi endapo Rais Kenyatta atajitosa katika kampeni za Bw Mariga.

Jana, katika hali ambayo wadadisi wanaona imelenga kumhakikishia Bw Odinga na wafuasi wake kwamba handisheki ingali imara, Mbunge Maalumu wa Jubilee Maina Kamanda alimtembelea waziri huyo mkuu wa zamani afisini mwake Nairobi na kutangaza ataunga mkono Benard Okoth almaarufu Imran, anayepeperusha bendera ya ODM kwenye uchaguzi huo.

Bw Kamanda huchukuliwa kama kiongozi wa kikundi cha Kieleweke kinachojumuisha wanasiasa wa Jubilee ambao wanashabikia handsheki wakimpinga Naibu Rais William Ruto.

“Chama cha Jubilee kimesimamisha mwaniaji wake, lakini mimi nitaunga mkono Bw Okoth wa ODM. Huyu ndiye mwaniaji wa handisheki. Hii ni kwa sababu handisheki imeleta amani nchini na watu wanafanya biashara bila wasiwasi,” akasema Bw Kamanda katika afisi ya Bw Odinga iliyoko jumba la Capitol Hill, Nairobi.

Akizungumza baada ya mkutano wao, Bw Odinga aliepuka kusema wazi kama mwafaka wake na Rais uko mashakani bali akasema Bw Kamanda alimtembelea ili kumfahamisha kuhusu hatua ambazo zimepigwa katika kupigia debe handisheki na BBI jijini Nairobi na katika maeneo mengine nchini ikiwemo Mlima Kenya.

“Tumekuwa tukishirikiana naye (Bw Kamanda) katika kupigia debe BBI ili kuhakikisha kuwa inakubalika katika pembe zote za nchi,” akasema Bw Odinga.

Lakini wachanganuzi wa masuala ya siasa wanasema, hatua ya Bw Kamanda sasa imeonyesha wazi kampeni za Kibra zitakuwa mashindano baina ya wanaounga handisheki na wanaopinga, na hivyo basi kushusha pumzi kwa Wana-ODM wanaohofia kuhusu hatima ya maelewano kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta.

Viongozi wengine wa Jubilee ambao awali walikuwa tayari wameonyesha kuchukizwa kwao na hatua ya kusimamisha mgombeaji Kibra ni Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja.

Mbunge wa Rarieda Otiende Amolo anakiri kuwa handisheki itakuwa taabani ikiwa Rais Kenyatta na Bw Odinga watakabiliana kwenye kampeni za kupigia debe wagombeaji wa vyama vyao Kibra.

“Ninaamini Bw Ruto na wanasiasa wa kundi la Tangatanga walimwekea mtego Rais Kenyatta, hivyo kumlazimu kutangaza kumuunga mkono Bw Mariga,” akasema Dkt Amolo.

“Tunachosubiri kuona ni ikiwa Rais Kenyatta ataongoza msururu wa kampeni kumpigia debe Bw Mariga na upande mwingine pia Bw Odinga aendeshe kampeni kwa ajili ya Imran. Hilo litazua wasiwasi,” akaongezea.

Mbunge huyo wa ODM, hata hivyo, anatumai maazimio ya handisheki ikiwemo utekelezaji wa ripoti ya BBI inayosubiriwa, utatimizwa kikamilifu licha ya uchaguzi huo mdogo unaoibua kiwewe.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alieleza wasiwasi wake kwamba, huenda Bw Odinga alihadaiwa kuweka muafaka na Rais kwani kufikia sasa, maazimio aliyolenga hayajapatikana isipokuwa kuwepo utulivu nchini.

“Baba (Bw Odinga) anafaa kujihadhari na hiki kitu kinachoitwa handisheki. Rais Kenyatta anafaa kuwa mkweli na hii handisheki. Hatutaki kudanganyana na kisha wanakuaibisha,” akaonya.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ODM Junet Mohamed, alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa kwanza wa ODM kueleza hisia zao wakati Bw Mariga alifikishwa Ikuluni mnamo Jumatano.

Akimjibu Dkt Ruto wakati aliweka picha ya Rais akimvisha kofia Bw Mariga kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Bw Mohamed alisema: “Nisikusikie tena vijijini ukidai Raila anavunja Jubilee, na kwamba handisheki na BBI zinahusu siasa za 2022.”

Kimsingi, alionekana kumaanisha Naibu Rais ndiye anagawanya chama hicho zaidi kwa kumsimamisha mgombeaji Kibra ambako ni ngome ya ODM kisiasa. Licha ya hayo, Bw Mohamed jana alisema Bw Kamanda na Bw Odinga wana ushawishi mkubwa kwa siasa za Nairobi hivyo basi wako imara.

“Kila mtu ana haki ya kuunga mkono mwaniaji anayetaka lakini ukweli ni kwamba, chama cha ODM kitahifadhi kiti hicho kwa urahisi,” akasema Bw Junet.

Mara baada ya Rais Kenyatta kutangaza kumuunga Bw Mariga, Naibu wa Rais Dkt Ruto aliwataka wanasiasa wa Jubilee kutoka mirengo ya Tangatanga na Kieleweke kujiunga na kikundi cha kampeni za mwanasoka huyo wa zamani.

Lakini wito huo wa Bw Ruto unaonekana kupuuzwa na wanasiasa wa kundi la Kieleweke.

Bw Mariga Jumatano alisindikizwa Ikuluni na Dkt Ruto, Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale na Kiranja wa Jubilee Bungeni Benjamin Washiali kati ya viongozi wengineo.

KIBRA: Uhuru asema ‘Mariga tosha’

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano alikutana na mgombeaji wa chama cha Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra McDonald Mariga katika Ikulu ya Nairobi na kumtakia ushindi.

Rais ambaye alikuwa ameandamana na Naibu wake William Ruto alimhakikisha Mariga kwamba anamuunga mkono katika kinyang’anyiro hicho cha Novemba 7.

“Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Dkt William Ruto leo katika Ikulu ya Nairobi alikutana na mwaniaji wa Jubilee katika uchaguzi mdogo ujao katika eneo bunge la Kibra McDonald Mariga. Alimhakikishia kuwa anamuunga mkono na akamtakia ushindi,” ikasema taarifa kutoka Ikulu ya Rais.

Bw Mariga alikuwa ameandamana na Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale na kiranja wa wengi Benjamin Washiali, miongoni mwa wengine.

Katika mkutano huo Rais Kenya alimvisha Bw Mariga kofia nyekundu ya chama cha Jubilee, ishara ya kumpa baraka zake.

Hatua ya Rais Kenyatta kujitokeza wazi kumuunga mkono Bw Mariga kumeondoa dhana ambayo imekuwa ikienezwa kwamba uwaniaji wa mwanasoka huyo unaungwa mkono na Dkt Ruto na wabunge wanachama wa mrengo wa Tangatanga pekee.

Hii ni kwa sababu wabunge ambao hawaungi mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu wametangaza waziwazi kwamba wataunga mkono mgombeaji wa ODM Imran Okoth, “kwa moyo wa handisheki”.

Wao ni Maina Kamanda, Joshua Kutuny (Cherangany), Moses Kuria (Gatundu Kusini),  Seneta wa Murang’ a Irungu Kang’ata, kati ya wengine.

Sababu ya Mariga kuruhusiwa kujaribu bahati Kibra

NA SAMUEL OWINO

KORTI inayoshughulikia mizozo ya uchaguzi Jumatatu ilimruhusu aliyekuwa kiungo matata wa timu ya taifa ya kandanda McDonald Mariga kuwa debeni katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra.

Awali, uteuzi wake na chama cha Jubilee ulikuwa umetupiliwa mbali na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kuwa taarifa muhimu kumhusu zilikosekana katika orodha ya wapigakura walioshiriki uchaguzi mkuu wa 2017.

Hata hivyo, mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati, ametangaza Jumatatu kuwa Mariga sasa anaweza kuwania kiti hicho kilichosalia wazi baada ya kifo cha Bw Ken Okoth hapo Julai.

Bw Chebukati amesema mkuu wa uchaguzi eneebunge hilo aliyemzuia Mariga kuwa debeni alisahau kuangalia orodha mpya ya mwaka huu katika eneobunge la Starehe.

Kundi la mawakili waliomwakilisha Bw Mariga, likiongozwa na Elisha Ongoya, liliirai IEBC kusahihisha kosa hilo nakumruhusu mwanaspoti huyo kujaribu bahati yake uchaguzini.

“Simlaumu afisa wa uchaguzi kwa kufanya kosa hilo. Lakini lazime lingesahihishwa na kamati ya uchaguzi ili kuwapa wapigakura wa Kibra nafasi murua ya kuchagua wamtakaye,” akasema.

Aliongeza kuwa Mariga ametimiza masharti yote ya kikatiba kuhusu uchaguzi, akieleza kuwa mwaniaji anapaswa kuwa amesajiliwa kuwa mpiga kura, na mchckato huo huendelea hata wakati hakuna uchaguzi.

Kwa sasa, Bw Mariga ana nafasi ya kujiunga na wanasoka wengine duniani ambao waling’aa kwa siasa baada ya kustaafu kucheza gozi.

Miongoni mwao ni aliyekuwa straika wa Inter Milan na Chelsea Andriy Shevchenko, mshindi wa Kombe la Dunia la 1994 Romario na aliyekuwa straika matata wa PSG,  AC Milan na Monaco George Weah, ambaye sasa ni rais wa Liberia.

Mariga amesema sasa yuko tayari kuogelea katika bahari ya siasa akiusifu uamuzi wa Bw Chebukati.

“Namshukuru Maulana kwa mchakato wa leo. IEBC imenitendea haki. Kwa sasa najitosa kwa kampeni ili niwashawishi wapigakura wa Kibra,” akasema.

 

Ruto kimya Mariga akihangaika

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto jana alizidisha kimya chake huku hatima ya mwaniaji wa Chama cha Jubilee kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra, McDonald Mariga, ikizidi kutiliwa shaka.

Tofauti na awali ambapo Dkt Ruto alijitokeza wazi na hata kuelekea Kibra kuahidi angerejea kuongoza kampeni za Bw Mariga, amekuwa kimya tangu wikendi kabla mwaniaji huyo kupigwa breki na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Jumanne.

Bw Mariga alipokezwa cheti chake cha chama na Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju tofauti na wagombeaji wa vyama vingine waliopokezwa vyeti na vinara wa vyama vyao.

Wakati alienda kuwasilisha stakabadhi zake kwa IEBC, aliandamana na wandani wa Dkt Ruto, akiwemo mbunge wa Langata, Nixon Korir, na aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Dkt Boni Khalwale.

IEBC ilisema Bw Mariga hakuwa amesajiliwa kama mpiga kura nchini na hivyo basi, kisheria hawezi kuruhusiwa kuwania ubunge.

Vilevile, kuna tetesi zilizoibuka kuhusu umri halisi wa nyota huyo wa soka ikidaiwa huenda suala kuhusu uhalali wa kitambulisho chake pia likawa kikwazo kwa azimio lake la kujitosa kwenye ulingo wa siasa.

Jana, Bw Mariga alimshtaki Msimamizi wa Uchaguzi wa eneo hilo Bi Beatrice Muli mbele ya kamati ya kutatua mizozo ya IEBC akimlaumu kwa kukataa kumuidhinisha kugombea uchaguzi huo licha ya kuteuliwa na chama cha Jubilee.

Bi Muli alikuwa amesema hangempitisha Bw Mariga kuwania ubunge kwa kuwa jina lake halikupatikana katika sajili ya wapigakura iliyochapishwa 2017.

Hata hivyo, Bw Mariga anasisitiza kuwa amesajiliwa kisheria kama mpigakura na hatua ya Bi Muli ilikiuka haki zake za kikatiba.“Nilisajiliwa kama mpigakura katika kituo cha kupigia kura cha ukumbi wa kijamii wa Kariokor mnamo Agosti 26, 2019 na nikapatiwa kadi ya kuthibitisha nambari yangu ya mpigakura,” alisema Bw Mariga kwenye hati ya kiapo aliyoambatishwa na ombi lake.

Mwanasoka huyo mstaafu anasema kwamba, kabla ya kuteuliwa, Chama cha Jubilee kilithibitisha kwamba alikuwa ametimiza mahitaji yote ikiwa ni pamoja na kusajiliwa rasmi.

“Nimefahamishwa na wakili wangu na ninaamini ni kweli kwamba usajili wa wapigakura ni shughuli inayoendelea na kwamba majina huwekwa katika sajili kila wakati kwa mujibu wa sheria husika,” anasema.Bw Mariga anataka kamati kuamua kuwa hatua ya Bi Muli haikuwa na msingi wa kisheria na kwa hivyo ni batili.

Dkt Ruto alionekana hadharani mara ya mwisho Jumapili alipozuru Kaunti ya Kirinyaga. Kwenye mitandao yake ya kijamii, hajasema lolote kuhusu masaibu ya Bw Mariga isipokuwa mapema Jumanne alipokashifu vyombo vya habari kwa kudai kuna mpasuko chamani mwake kuhusu uwaniaji kiti Kibra.

Jana, wengi walitarajia angeandamana na Rais Uhuru Kenyatta aliyekuwa katika ngome yake ya kisiasa ya Eldoret kusimamia mahafali ya wanajeshi, lakini hakuwepo.

Bw Mariga anataka kamati ya IEBC kutambua na kuamua kwamba aliteuliwa kihalali na chama cha Jubilee na anastahili aruhusiwe kugombea kiti cha eneobunge cha Kibra kwenye uchaguzi mdogo wa Novemba 7.

Pigo kwa Jubilee Mariga kufungiwa nje na IEBC

Na LEONARD ONYANGO

MGAWANYIKO ndani ya Chama cha Jubilee kuhusu ugombeaji wa ubunge Kibra ulizidi kudhihirika Jumanne wakati wakuu wa chama hicho walikosa kujitokeza kumkabidhi rasmi Bw McDonald Mariga vyeti vya uwaniaji, na kuchangia kufungiwa nje kwa mwaniaji huyo na Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Tofauti na vyama vingine vya kisiasa ambako wagombeaji walilakiwa na wakuu wa vyama baada ya kuteuliwa kuwania wadhifa huo, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto, hawakuwepo katika makao makuu ya Jubilee Bw Mariga alipopewa vyeti.

Badala yake, shughuli hiyo ilisimamiwa na Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju akiandamana na wanasiasa wengine wa chama hicho hasa wa mrengo wa Tangatanga unaomuunga mkono Dkt Ruto.

Tangu kuteuliwa kuwa mwaniaji wa Jubilee, Bw Mariga hajawahi kukutana na Rais Kenyatta ambaye ni kiongozi wa chama hicho.

Duru zilisema, uamuzi wa kuwasilisha mwaniaji wa Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra ulifanywa na Dkt Ruto kwa lengo la kumpinga Bw Odinga.

Ripoti zilisema Rais Kenyatta alikataa mwaliko wa naibu wake aliyemtaka aende kumkabidhi Bw Mariga cheti cha uteuzi katika makao makuu ya chama cha Jubilee.

Viongozi wa Jubilee wanaoegemea mrengo wa Kieleweke unaopinga mienendo ya Tangatanga, wakiwemo Mbunge wa Cherangany Joshua Kutuny na Mbunge Maalumu Maina Kamanda wanadai kuna baadhi ya watu ndani ya Jubilee wanalenga kusambaratisha uhusiano mwema uliopo baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kwa kusimamisha mwaniaji Kibra.

“Naibu wa Rais anajua kwamba hatashinda kiti cha Kibra na lengo lake kuu ni kutaka kuzua uhasama kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga,” akasema Bw Kamanda.

Wakati huo huo, Bw Tuju pia amethibitisha kuwa Rais Kenyatta hatashiriki katika kampeni za ubunge Kibra.

Viongozi wa Vyama vya ODM, Ford-Kenya, na Amani National Congress ambavyo vina wagombeaji wanaomezea mate kiti hicho kilichoachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge, Ken Okoth, wamekuwa mstari wa mbele kutafutia umaarufu wagombeaji wao.

Bw Odinga alimtangaza mbunge wa Suna Mashariki ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ODM, kuwa kinara wa kampeni za Bw Okoth katika uchaguzi mdogo wa Kibra.

Bw Odinga alifanya kikao cha faragha na wawaniaji wote waliopoteza katika uchaguzi wa kura za mchujo uliofanyika Jumamosi iliyopita ili kuwapatanisha baada ya malalamishi kuibuka miongoni mwa baadhi yao awali.

Baada ya kikao hicho, wawaniaji hao walitangaza kumuunga mkono Bw Bernard Otieno Okoth, almaarufu Imran, aliyeibuka mshindi.

“Hii ilikuwa mechi ya kirafiki, hivyo hakuna uhasama kati yetu. ODM ni chama kinachozingatia demokrasia na sasa tutaunga mkono Bw Imran Okoth na tutahakikisha chama chetu kinahifadhi kiti hicho,” akasema Bw Peter Orero ambaye awali alikuwa amelalamika kuhusu udanganyifu katika kura ya mchujo.

Wawaniaji wengine ambao wamewasilisha stakabadhi zao kwa IEBC ni Eliud Owalo wa chama cha Amani National Congress (ANC), Khamisi Butichi wa Ford Kenya, Malaseh Hamida (United Green Movement) Editar Ochieng (Chama cha Ukweli chake mwanaharakati Boniface Mwangi) na Fridah Kerubo Kingara (mwaniaji wa kujitegemea).

KINAYA: Mariga hana deni lako, huwezi kumlazimisha kufanya hisani

Na DOUGLAS MUTUA

HIVI wewe kabwela mzee una nini?

Mbona unamchukia mtoto ilhali unaitwa baba? Watoto wako wakichukiwa utahisije?

Samahani, siutukani uzee ila lazima niujadili hapa, katika muktadha wa udaku wa kisiasa unaoendelea Kenya.

Wazee fulani wanaungulika wakiona vijana wakijitosa ulingoni kuzichapa kisiasa. Watakereketwa sana!

Na wakishindwa wameze nyembe; kwenye siasa hakuna kiti cha mtu, sote tunatafuta. Asiyeangukiwa na bahati aridhike, siku yake itafika na isipofika, basi ole wake.

Siasa za Kenya zina mambo eti. Na wajuaji kibao, wengi wa kiherehere na upungufu wa maarifa. Watazuka waropokwe na maneno kabla ya kuyatafakari, tafakuri ni baadaye eti.

Juzi nimemkabili mjuaji fulani alipozuka kwa fujo kumtaka mwanasoka McDonald Mariga, kabla ya kuingia siasa, atangaze ametumia pesa zake vipi kuifaa jamii.

Hebu tazama kinaya hapa: Kabwela aliyedai maelezo ana umri wa miaka 45 ilhali Mariga ana 32 pekee.

Wala kabwela hana haya akilalamika kwamba hajanyeshewa na neema za Mariga na sifa zote za kucheza kabumbu ya kulipwa.

Nilimuuliza yeye mwenyewe, kwa kuwa amemzidi Mariga kwa umri, alimsaidiaje kufikia upeo wa juu wa soka kutoka mazingira magumu aliyokulia kijana huyo.

Kabwela aliuma mdomo wa chini, akauacha na kuuma wa juu, kisha akasema Mariga ana pesa nyingi kumzidi hivyo basi anapaswa kuwa amemsaidia kwa kiasi fulani.

Nilishikilia kwamba yeye na umri wake mkubwa anapaswa kuwa mlezi na wala si mtegemezi wa kijana huyo.

Niliachana na kabwela huyo nilipoona fikra zake duni za kutaka kusaidiwa haziwezi kubadilika kamwe.

Si ajabu mtoto amempiku kwa kila kitu, mpaka kutamani kuwa mbunge mpya wa Kibra ifikapo Novemba 7, naye kabwela anashiriki umbea tu. Kuna wengi sampuli hiyo.

Ni unafiki kwa watu kuanza kuuliza Mariga – ambaye anatarajiwa kubeba mwenge wa chama cha Jubilee katika kinyang’anyiro hicho – ameisaidia jamii namna gani.

Ni hujuma kumtarajia mtu kutumia mshahara wake binafsi kuisaidia jamii. Hakuna anayepaswa kulazimishwa kutenda hisani kabisa.

Hata walafi tunaoita wabunge hawatumii mishahara yao binafsi, wametengewa mfuko wa kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.

Kwa mtu mzima na ndevu zake, nikidhani anaitwa baba, kumtarajia mdogo wake kwa miaka zaidi ya 10 kuwa mkombozi wake kiuchumi ni kasumba ya kimaskini sana. Ikome!

Kujituma

Kila mtu anapaswa kujituma kivyake kuchuma anachoweza, si kutegemea cha nduguye. Vitabu vitakatifu vinaniambia asiyefanya kazi na asile.

Nguvu nyingi wanazotumia makabwela kulalamika kwamba fulani hajawafaa kwa chochote zinapaswa kutumika katika shughuli za kuzumbua riziki, si kushiriki umbea.

Kwa kuwa mwanasoka wa kwanza kutoka Kenya kusakata kabumbu kwenye ligi ya UEFA, Mariga amewashawishi vijana kiakili wakajua wanaweza kufika mbali pia.

Kina pangu pakavu tia mchuzi watakula huu na hasara juu! Huu ni ulimwengu wa kibepari ambapo unachuma kivyako na kula kivyako; mtegemea cha nduguye afe maskini!

Kwa vyovyote vile, kinyang’anyiro cha Kibra kitakuwa cha kupendeza sana kwani tutawashuhudia ‘Baba’ na Dkt Bill Samoei wakiraruliana magwanda hadharani. Usikose!

 

mutua_muema@yahoo.com

Kutuny, Kamanda na Moses Kuria wapinga uteuzi wa Mariga

Na Samwel Owino

UTEUZI wa McDonald Mariga kupeperusha bendera ya chama cha Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra unaendelea kukumbwa na upinzani ndani ya chama hicho, Mbunge wa Cherangany Joshua Kutuny akiwa wa hivi punde kuupinga.

Mbunge huyo jana alisema mfumo ambao Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya chama hicho ulitumia kumteua mwanasoka huyo wa kimataifa Jumatatu unahujumu demokrasia.

Akiongea katika Majengo ya Bunge, Nairobi, Bw Kutuny alisema alitarajia kwamba bodi hiyo ingehakikisha wagombeaji wote 16 wamepigiwa kura ya moja kwa moja na wanachama wa Jubilee.

“Siasa haitambui jina kubwa, tunahitaji kujisaili upya na kuhakikisha tumerekebisha mambo katika nyumba yetu. Uteuzi ulipasa kufanya kwa njia ya upigaji kura kwa sababu hiyo ndio mbinu ya kipekee ambayo itahakikisha chama chetu kinawasilisha mgombeaji bora,” akaeleza.

Wengine ambao wamepinga uteuzi huo, uliotangazwa na mwenyekiti wa NEB Andrew Musangi, ni mbunge maalum Maina Kamanda na Moses Kuria (Gatundu Kusini).

 

Mikakati ya Dkt Ruto kudhibiti Jubilee

Na CHARLES WASONGA na GEOFFREY ANENE

NAIBU Rais William Ruto ameamua kudhibiti chama cha Jubilee kwa kuhakikisha ameshawishi maamuzi muhimu.

Haya yamebainika huku kukiwepo madai kwamba Dkt Ruto alisukuma Jubilee kudhamini mgombeaji katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra kama sehemu ya mikakati yake wa kukita usemi wake chamani na kufanikisha ndoto yake ya kuingia Ikulu mwaka 2022.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba uongozi wa chama awali haukutaka kudhamini mgombeaji Kibra ili usiathiri uhusiano mzuri uliopo kati ya kiongozi wake, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kupitia handisheki.

Lakini chama hicho kililazimika kukubaliana na uamuzi wa Dkt Ruto ili kuzuia uwezekano wa viongozi wa Jubilee kuunga mkono wagombeaji tofauti katika uchaguzi huo wa Novemba 7 hali ambayo ingepanua zaidi ufa uliopo ndani ya chama tawala.

Mnamo Ijumaa wiki jana, mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEC), Andrew Musangi, alithibitisha kuwa mwanasoka McDonald Mariga, ambaye anapendelewa na Dkt Ruto, ni miongoni mwa watu 16 wangepigwa msasa ili katika harakati za kusaka anayehitimu kuwa mgombeaji wa Jubilee.

Kama ilivyodhihirika katika chaguzi ndogo za Wajir na Embakasi Kusini, Dkt Ruto anataka mgombeaji anayependelea ndiye aibuke mshindi katika uchaguzi mdogo wa Kibra ili kuimarisha nafasi yake ya kuingia Ikulu 2022.

Hata hivyo, saa chache baada ya Jubilee kutangaza Mariga atapeperusha bendera ya chama, kiungo huyu aliyesakata soka yake katika mataifa ya Italia, Uhispania na Uswidi kati ya mwaka 2006 na 2018, amepuuzilia mbali madai hayo.

“Mimi si mradi wa mtu yeyote. Nawania kiti cha ubunge cha Kibra kwa sababu nataka ‘kurudisha mkono’ kwa jamii. Pia, nafahamu maisha ya watu wa eneo hili na kile wanachopitia,” akasema Mariga.

Enzi yake kama mchezaji, Mariga, 32, alichezea Enkopings SK na Helsingborg (Uswidi), Parma, Inter Milan na Latina Calcio (Italia) na Real Sociedad na Real Oviedo (Uhispania). Hajakuwa na klabu tangu Julai 1, 2018, hali ambayo pengine imemsukuma katika siasa kujaribu bahati yake.

Mariga alibwaga watu 15 kupata tiketi ya kupeperusha bendera ya Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra utakaofanyika Novemba 7. Aliwabwaga Morris Kinyanjui, Walter Trenk, Ibrahim Said, Doreen Wasike, Oscar Kambona, Bukachi Chapia, Jane Githaiga, Jack Owino, Omondi Rajab, Daniel Adem, Daniel Orogo, Ramadhan Hussein, Fank Amollo, Timothy Kaimenyi na Geoffrey Mwangi.

Atapambana na mgombea wa ODM, ambaye atajulikana baada ya mchujo utakaofanyika Septemba 7, Eliud Owalo (Amani National Congress) na wagombeaji huru kadhaa.

Kiti hiki kiliachwa wazi baada ya Ken Okoth kuaga dunia Julai 26, 2019 jijini Nairobi baada ya kuugua kansa.

Duru kutoka ndani ya Jubilee zasema Dkt Ruto pia anapanga kudhibiti chama hicho kwa kuhakikisha kuwa wandani wake wanashinda viti vingi katika uchaguzi ambao utafanyika kuanzia Machi 2020. Uchaguzi huo utafanyika kutoka ngazi ya mashinani hadi kitaifa.

Itakumbukwa kuwa alitumia mbinu kama hii kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017, alipoingilia mchujo wa Jubilee na kuhakikisha kuwa wanasiasa wandani wake waliibuka washindi, hasa katika ngome ya Rais Kenyatta ya Mlima Kenya.

Uchaguzi wa chama unapokaribia, wandani wa Dkt Ruto katika matawi ya Jubilee kote nchini sasa wanaamini wana idadi tosha ya wajumbe ambao wataweza kumuondoa Bw Raphael Tuju kutoka wadhifa wake wa Katibu Mkuu.

Dkt Ruto hafurahishwi na jinsi Bw Tuju anaendesha shughuli za chama hicho na Agosti alimtaja kama Katibu Mkuu wa chama tawala ambaye amepoteza mwelekeo na kugeuka mpanga mikakati wa kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.

“Kwa sababu ameonekana kuunga mkono Raila Odinga, tunahisi kuwa Bw Tuju anafaa kuiga mfano wa Bw David Murathe na kujiuzulu mapema. Asipofanya hivyo, tutahakikisha ameong’olewa mamlakani katika uchaguzi wa chama mwaka 2020,” mbunge wa Belgut Nelson Koech alisema juzi.

Hofu

Dkt Ruto anahofia kwamba wanaopinga azma yake kama Bw Murathe wanaweza kusambaratisha chama anachoamini ni maarufu miongoni mwa Wakenya.

Lakini ieleweke kwamba licha ya kutangaza kujiuzulu, jina la David Murathe bado liko katika orodha ya maafisa wa Jubilee, ambapo anaorodheshwa kama Naibu Mwenyekiti.

Inasemekana kuwa Rais Kenyatta alipinga nia yake ya kujiuzulu.

Yapo madai kwamba wafuasi wa Dkt Ruto pia wanapanga kumiliki jina la Jubilee kwa kuunda chama kipya cha Jubilee Republican Party ambacho atakitumia katika safari yake ya kuingia Ikulu 2022.

Hii ni baada ya kubainika kuwa viongozi wa Jubilee wanaounga mkono handisheki wanapanga kukihama kubuni muungano mpya wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 na kukatiza uhusiano kati yao na Dkt Ruto.

Juzi Mbunge Maalum Maina Kamanda alifichua muungano huo utashirikisha chama cha ODM pamoja na “vyama vingine vyenye sera sawa na zetu”.

Jubilee yamtangaza Mariga mgombea wake wa ubunge Kibra

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha Jubilee kimemteua mwanasoka McDonald Mariga Wanyama kuwa mgombea wake katika uchaguzi mdogo katika eneobunge la Kibra mnamo Novemba.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya chama hicho Andrew Musangi alisema Jumatatu kwamba uamuzi huo ulifikiwa baada ya kuwahoji watu 16 waliosaka tiketi hiyo.

“Baada ya kuwahoji kwa makini jumla ya watu 16 waliotuma maombi ya kutaka kuwa wawaniaji wa kiti cha ubunge cha Kibra kwa tiketi ya Jubilee, bodi yangu umemteua Bw McDonald Mariga Wanyama. Hii ni kwa sababu tumeridhika kuwa ana ufahamu wa hali ya eneobunge hilo, ameonyesha bidii, nguvu na kujituma; sifa ambazo Jubilee inahitaji kwa mpeperusha bendera yake,” Bw Musangi akasema kwenye kikao na wanahabari saa moja usiku katika makao makuu ya Jubilee, mtaani Pangani, Nairobi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) Andrew Musangi akimtangaza McDonald Mariga kuwa mgombeaji wa kiti cha ubunge Kibra kwa tiketi ya Jubilee. Hapa ni katika makao makuu ya Jubilee, Pangani, Nairobi. Picha/ Charles Wasonga

Sasa ni rasmi kwamba Bw Mariga atakupambana na mgombeaji wa ODM ambaye atajulika Jumamosi baada mchujo wa chama hicho.

Vilevile, atakabana koo na mgombeaji wa chama cha Amani National Congress (ANC) Eliud Owalo na wagombeaji huru kadhaa.

Kiti cha Kibra kilisalia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge Bw Ken Okoth mnamo Julai 26, 2019 katika Nairobi Hospitali baada ya kuugua kansa ya utumbo.

Umri

Bw Mariga mwenye umri wa miaka 32 amewahi kuichezea timu ya taifa Harambee Stars na miamba wa soka nchini Italia Inter Milan.

Vilevile, amewahi kuchezea timu zingine duniani miongoni mwao ikiwa ni Real Sociedad, Parma, Helsingborge na Real Oviedo.

Wengine waliong’ang’ania tiketi ya Jubilee kwa kinyang’anyiro hiki ni pamoja na Morris Kinyanjui, Walter Trenk, Ibrahim Said, Doreen Wasike, Oscar Kambona, Bukachi Chapia, Jane Githaiga, Jack Owino, Omondi Rajab, Daniel Adem, Daniel Orogo, Ramadhan Hussein, Fank Amollo, Timothy Kaimenyi na Geoffrey Mwangi.

OBARA: Wanakibra wawe makini katika uchaguzi mdogo

Na VALENTINE OBARA

KIVUMBI kimeanza kutifuka katika eneobunge la Kibra kwa maandalizi ya uchaguzi mdogo ambao umetokana na kifo cha aliyekuwa mbunge, marehemu Ken Okoth.

Kinachoonekana kwa sasa ni nafasi ya mahasimu wakuu wawili wa kisiasa nchini kupimana nguvu.

Kwa upande mmoja, kuna Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga na upande wa pili ni Naibu Rais William Ruto wa Chama cha Jubilee.

Katikati ya kimbunga kinachotarajiwa baada ya mchujo wa vyama na hatimaye kampeni zitakapoanza, kuna wakazi wa eneobunge hilo ambalo sehemu yake kubwa ni mtaa wa mabanda.

Kutokana na ushindani unaotarajiwa kati ya Bw Odinga na Bw Ruto, kuna hatari ya wapigakura kupotoshwa na kuishia kuchagua kiongozi asiyefaa.

Wakazi wa Kibra wametatizika kwa miaka mingi kwa kukosa huduma bora za kimsingi ikiwemo afya, usafi, elimu na makao bora.

Juhudi mbalimbali za kubadilisha hali hii katika miaka iliyopita ziligonga mwamba kwa sababu za kisiasa na vilevile ulafi wa kibiashara wa watu wachache wanaonufaika na umaskini wa wenzao.

Marehemu Okoth alifanya mengi kwa dhamira ya kuinua maisha ya Wanakibra lakini kwa bahati mbaya, akatuacha kabla ya kukamilisha mipango mingine aliyokuwa nayo.

Nilipotazama kwenye runinga hivi majuzi, niliona Chama cha ODM kupitia kwa kiongozi wake, Bw Odinga kikisema atakayepeperusha bendera ya chama hicho anafaa kuwa mtu aliye mwaminifu kwa chama hicho.

Ninafahamu fika kwamba kila chama hutaka wale watakaochaguliwa kupitia kwake wawe waaminifu.

Sina haja kueleza mengi kuhusu umuhimu huu kwa chama kwani tumeshuhudia jinsi uasi wa viongozi katika vyama vilivyowaingiza mamlakani unavyoibua misukosuko na kuathiri vibaya mwelekeo wa chama.

Licha ya haya, tumefika katika enzi ambapo uaminifu wa chama pekee haufai kutumiwa kama kigezo cha kumpokeza mtu tikiti ya kuwania uongozi wa kisiasa.

Inahitajika wakuu wa vyama vyote wazingatie umuhimu wa kuwezesha wananchi kuchagua viongozi wenye maono ya kimaendeleo ambayo yataboresha hali yao ya maisha.

Hata kama mgombeaji anachaguliwa kupitia kura ya mchujo, si siri kwamba wakati mwingi wakuu wa vyama huwa na usemi mkubwa kuhusu anayestahili kuchaguliwa na wajumbe.

Kama wakuu wa vyama wanaona vigumu kupigia debe wagombeaji kwa msingi wa uwezo wao wa kuleta maendeleo, basi wito wangu ni kwa wapigakura kujijali wao wenyewe.

Wachague kiongozi anayeweza kuwabadilishia hali ya maisha hata kama ni mgombeaji huru au anayetumia chama kidogo kisicho maarufu.

Chama kisiwe kiini cha kumchagua mtu atakayegeuka kuwa nduli kwa wapigakura pindi aingiapo enzini.

Mariga atetemesha ODM, Kieleweke

Na JUSTUS OCHIENG na CECIL ODONGO

UWEZEKANO wa kuteuliwa kwa mwanasoka McDonald Mariga kuwania kiti cha ubunge cha Kibra umetetemesha chama cha ODM na mrengo wa Kieleweke wa chama cha Jubilee.

Bw Mariga, ambaye aliacha kuichezea Harambee Stars miaka kadhaa iliyopita, ameitwa ‘kutoka benchi’ na mrengo wa ‘Tangatanga’ unaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto ili kuusaidia ‘kushinda kombe’ katika uchaguzi mdogo wa Novemba 7.

Duru za kuaminika ndani ya Jubilee ziliambia Taifa Leo kwamba Dkt Ruto anashinikiza Bw Mariga ateuliwe kupeperusha tiketi ya Jubilee kwa matumaini kuwa ataweza kuzoa kura za jamii ya Waluhya na vijana katika eneo bunge hilo lililo na wapiga kura wengi wenye sifa hizo mbili.

Lakini kwa upande mwingine, upande wa Kieleweke ambao unaegemea mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta kwenye Jubilee, hautaki Bw Mariga apate tiketi hiyo kwa hofu kuwa atakuwa tisho kwa mgombeaji wa ODM.

Hii inatokana na kuwa mrengo wa Kieleweke hauko makini Jubilee kushinda kiti hicho kutokana na handisheki kati ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga.

“Mrengo wa Kieleweke unataka mwaniaji asiyekuwa na ufuasi mkubwa wala pesa za kutetemesha katika kampeni, kama njia ya kuendeleza urafiki uliotokana na handisheki,” akasema afisa wa ngazi ya juu Jubilee.

Akiungwa mkono na Dkt Ruto, Bw Mariga atakuwa na uwezo wa kufanya kampeni inayoweza kuvuruga mpango wa ODM kwenye uchaguzi huo.

Uwezekano wa kuwepo kwa Bw Mariga kwenye kinyang’anyiro hicho ulitajwa jana kama moja ya sababu za ODM kuahirisha mchujo wake uliokuwa umepangwa kufanyika kesho. Sasa uteuzi huo utafanywa Septemba 7 ili kukipa muda wa kuona iwapo Bw Mariga atakuwa debeni kabla ya kuteua mwaniaji wao.

Mvutano

Mvutano ndani ya Jubilee kuhusu mwanasoka huyo aliyecheza kimataifa Italia na Uhispania, pia ulitajwa kuwa sababu ya chama cha Jubilee kukosa kutangaza orodha ya watu tisa ambao kilisema tayari wamewasilisha maombi ya kupewa tiketi ya kuwania ubunge Kibra.

“Upande wa Kieleweke hautaki Bw Mariga. Mrengo wa Dkt Ruto nao unasisitiza ndiye unataka,” zikasema duru za Jubilee.

Chama cha Amani National Congress nacho kinatumia mbinu hiyo hiyo ya kutegemea kura nyingi za Waluhya kwa kumwidhinisha Eliud Owalo apeperushe bendera yake.

Bw Owalo si mgeni Kibra kwani alivurugana na bintiye kinara wa chama cha ODM, Bi Rosemary Odinga kwenye mchujo wa kuwania kiti hicho 2017.

Akizungumza aipozinduliwa rasmi mnamo Jumatano, Bw Owalo alisikitika kuwa wakazi wa eneobunge hilo wamejawa na umaskini mwingi miaka 56 tangu Kenya ijinyakulie uhuru.

“Nimebainisha kwamba tatizo kuu ni namna matatizo yanayowakabili watu wa Kibra yanavyotatuliwa na pia umaskini katika taifa lote. Nina uwezo na mbinu za kubadili mambo,” akasema Bw Owalo.

Huku upande wa ‘Tangatanga’ ukiendelea kumpigia debe Bw Mariga, duru zinaarifu kwamba jamii ya Waluhya walioko ODM inamuunga mkono kiongozi wa vijana Benson Musungu.

Kwa upande wao, Waluo wanamuunga mkono mwalimu mkuu wa Shule ya Dagoretti, Bw Peter Orero.

Jambo hili linamfanya Bw Odinga ajikune kichwa zaidi kuhusu mwaniaji atakayeshinda mchujo na kupata tiketi ya chama.

Jubilee yaruka Mariga katika Kibra

Na CECIL ODONGO

CHAMA cha Jubilee kimekanusha kwamba kiliorodhesha jina la mwanasoka wa kimataifa MacDonald Mariga miongoni mwa wanaotaka tiketi yake ili kuwania ubunge katika uchaguzi mdogo wa Kibra hapo Novemba 7.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju alikanusha Jumanne kwamba aliandika barua yenye jina la Bw Mariga na watu wengine wanne huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikikataa barua hiyo na kuirudisha kwa usimamizi wa Jubilee.

Mwanasoka huyo pamoja na ndugu yake Victor Wanyama waligonga vichwa vya habari nchini mwezi jana baada ya kumtembelea Naibu Rais William Ruto katika ofisi yake wakati wa kupanga mashindano ya soka ya Wanyama Royal Cup yanayodhaminiwa na wawili hao.

Ni kutokana ziara hiyo ambapo barua iliyoorodhesha jina la Bw Mariga ilionekana na wengi kuwa azma yake ya kuwa mbunge wa Kibra inapigwa jeki na Dkt Ruto.

Wengine waliotajwa kama wanaomezea mate kiti cha Kibra kwa tiketi ya Jubilee kwenye barua hiyo tatanishi ni Said Abraham, Morris Peter Kinyanjui, Mukinyingi Walter Trenk na Doreen Nangame Khayanga Wasike.

“Tume ilipokea barua Jumatatu Agosti 26 saa kumi na moja jioni ikipendekeza majina ya wawaniaji wa Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra. Hata hivyo, tume imeelezwa kwamba Jubilee haikuidhinisha barua hiyo. Tume imeandikia chama na kuambatanisha nakala ya barua hiyo ili chama kichukue hatua inayofaa,” ikasema taarifa ya IEBC.

Bw Tuju mnamo Jumatatu jioni alieleza kutofahamu lolote kuhusu barua hiyo iliyochipuka punde tu baada yake kutoa taarifa kwamba chama hicho kitawasilisha mwaniaji kuchuana na mgombeaji wa chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga ili kutafuta mrithi wa marehemu Ken Okoth.

Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Dijitali katika Afisi ya Rais, Dennis Itumbi alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kusambaza barua hiyo na kusema ilikuwa na saini ya Bw Tuju kama thibitisho kwamba aliidhinisha.

“Nasimama na barua niliyosambaza kuhusiana na uchaguzi wa Kibra. Jubilee itaandaa kura ya mchujo. IEBC ina barua ambayo nimeambatanisha hapa,” akaandika Itumbi kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mchujo

Huku hayo yakijiri, Bw Tuju alikanusha kwamba chama hicho kitafanya kura ya mchujo, akisema wenye nia ya kutumia Jubilee kupigania kiti cha Kibra watakaokuwa wamewasilisha vyeti vyao watachujwa Ijumaa hii kisha uamuzi wa mgombeaji wa kupewa tiketi ya moja kwa moja uafikiwe na chama.

Wakati huo huo Bw Tuju alieleza Taifa Leo kwamba hatua ya chama hicho kumwasilisha mwaniaji kukabiliana na ODM Kibra haitavuruga ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga maarufu kama handisheki.

Wanyama na Mariga kucheza pamoja Stars ikilimana na Comoros, CAR

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Stanley Okumbi ametaja kaka ya nyota wa Tottenham Hotspur Victor Wanyama, McDonald Mariga, katika kikosi chake kitakachopimana nguvu dhidi ya Comoros na Jamhuri ya Afrika ya Kati nchini Morocco mwezi Machi 2018.

Mara ya mwisho kiungo Mariga, 30, ambaye anasakata soka yake ya malipo katika klabu ya Real Oviedo inayoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili ya Uhispania, alichezea Stars ni Machi 26 mwaka 2011 dhidi ya Angola.

Mbali na Mariga, Okumbi pia amerejesha kikosini Ismael Gonzalez, ambaye alichezea Stars mara ya mwisho mwaka 2016. Mzawa huyu wa Uhispania anasakata soka katika klabu ya Fuenlabrada inayosiriki Ligi ya Daraja ya Tatu nchini Uhispania.

Vilevile, Paul Were (Kaisar, Kazakhstan), Eric Johana Omondi (Brommapojkarna, Uswidi), Ayub Timbe (Heilongjiang FC, Uchina) na Francis Kahata (Gor Mahia) wamerejea kikosini baada ya kukwekwa pembeni kwa muda mrefu.

Hata Wanyama, ambaye ameshinda taji la goli bora kwenye Ligi Kuu ya Uingereza mwezi Februari, pia amekuwa nje muda mrefu. Alikuwa na jeraha baya mwisho wa mwezi Agosti mwaka 2017 lililomweka mkekani hadi mapema Januari mwaka 2018.

Mvamizi Michael Olunga, ambaye ni Mkenya wa kwanza kufunga mabao matatu kwenye mechi moja ya Ligi Kuu ya Uhispania na winga matata Ayub Timbe pia wamo kikosini.

Sura mpya kikosini ni Erick Kapaito ambaye amekuwa akifanya vyema kwenye Ligi Kuu ya Kenya msimu huu wa 2018.

Baadhi ya majina makubwa ambayo yamekosa namba ni mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Kenya mwaka 2017 Masoud Juma (Cape Town City FC, Afrika Kusini) na mwanasoka bora wa Kenya mwaka 2017, Michael Madoya (Zoo Kericho).

Juma amekuwa akiuguza jeraha naye Madoya bado hajaridhisha Okumbi. Timu itaanza mazoezi Machi 19. Mechi ya Comoros ni Machi 24 nayo ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ni Machi 27. Zote zitapigiwa mjini Marrakech.

Kikosi cha Harambee Stars:

Makipa

Patrick Matasi (Posta Rangers), John Oyemba (Kariobangi Sharks), Faruk Shikalo (Bandari)

Mabeki

Harun Shakava (Gor Mahia), Brian Mandela (Maritzburg United, Afrika Kusini), David Ochieng, (Brommapojkarna, Uswidi), David Owino (Zesco, Zambia), Abud Omar (Slava Sofia, Bulgaria)

Viungo

Patilah Omoto (Kariobangi Sharks), Francis Kahata (Gor Mahia), Duncan Otieno (AFC Leopards), Samuel Onyango (Gor Mahia), Athuman Ismael Gonzales (Fuenlabrada, Uhispania), Anthony Akumu (Zesco, Zambia), Victor Wanyama (Tottenham Hotspurs, Uingereza), McDonald Mariga (Real Oviedo, Uhispania), Johanna Omollo (Cercle Brugge, Ubelgiji), Paul Were (Kaisar, Kazakhstan), Eric Johana Omondi (Brommapojkarna, Uswidi)

Washambuliaji

Ayub Timbe (Heilongjiang FC, Uchina), Cliffton Miheso (Buildcon FC, Zambia), Erick Kapaito (Kariobangi Sharks), Jesse Were (Zesco FC, Zambia), Michael Olunga (Girona FC, Uhispania)