Kaunti yawatengea wavuvi mamilioni

Na WAANDISHI WETU

WAVUVI katika Kaunti ya Mombasa wanatarajia kuvuna pakubwa kwani serikali ya kaunti imetenga Sh250 milioni kuboresha sekta hiyo.

Fedha hizo zitatumika kununua maboti, kujenga vyumba vya kuhifadhi samaki, masoko ya kisasa na kutengeneza maeneo ya wavuvi kuweka vifaa vyao vya kazi na pia sehemu za kuegesha maboti yao.

Kulingana na pendekezo la bajeti ya kaunti ya kipindi cha mwaka wa 2020/2021, serikali ya kaunti hiyo inayoongozwa na Gavana Hassan Joho, itatumia Sh120 milioni kununua maboti hayo, Sh80 milioni kujenga vyumba vya kuhifadhi samaki tani 100, wakati Sh20 milioni zitatumika kuweka soko la kisasa la samaki.

“Kaunti pia itatumia Sh12 milioni kujenga vibanda vya kisasa vya kuuzia samaki na ukumbi wa mikutano katika maeneo ya wavuvi kutua katika maeneo bunge yote,” ilisema ripoti hiyo.

Pia, Sh6 milioni nazo zitatumika katika ujenzi wa mabwawa ya kukuzia samaki.

“Mradi huo unakusudia kuongeza shughuli za uzalishaji wa samaki, kuhakikisha kaunti ina chakula cha kutosha na pia kutoa fursa zaidi za ajira kwa wanawake na vijana,” ikasema.

Angalau maeneo 44 ya wavuvi kutua yatarekebishwa kwa gharama ya Sh10 milioni mara tu bajeti itakapopitishwa. Ununuzi na ukarabati wa maeneo hayo yatafanyika kwa ushirikiano na Halmashauri ya Bandari Nchini (KPA).

Kulingana na ripoti ya mwaka wa 2015 ya shirika la Haki Yetu, kuna maeneo 50 ya wavuvi kutoka Mombasa ambayo yalikuwa yamenyakuliwa.

Wavuvi katika kaunti hiyo walifurahia mpango huo, lakini wakaiomba serikali hiyo iwe ya kusema na kutenda.

“Tunajua kuwa ikiwa mipango yote ambayo imewekwa itatekelezwa, basi tutakuwa na uzalishaji mzuri wa samaki. Tunahitaji msaada wote muhimu ili tasnia yetu istawi,” alisema Khamis Abdallah, mwenyekiti wa wavuvi katika maeneo ya uvuvi katika maeneo ya Old Town.

Kwingineko, Bunge la Kaunti ya Kilifi limepitisha bajeti ya Sh13.3 bilioni ya mwaka wa fedha wa 2020/2021.

Mwenyekiti wa kamati ya bajeti katika bunge hilo Albert Kiraga, alisema bajeti ya mwaka huu imepungua kwa Sh1.4 bilioni ikilinganishwa na ile ya mwaka 2019/2020.

Akiwahutubia wanahabari, alisema wizara ya Afya ndiyo iliyopata mgao mkubwa zaidi wa Sh3.1 bilioni.

 

Ripoti za Diana Mutheu, Mohamed Ahmed na Alex Amani

KURUNZI YA PWANI: Elungata aelezea Wapwani haja ya kushirikiana na maafisa maeneo mpakani yasalie salama

Na WINNIE ATIENO

MSHIRIKISHI wa eneo la Pwani Bw John Elungata na afisa wa uhamiaji Bi Jane Nyandoro wamewaonya wakazi wanaoishi mipakani dhidi ya kuwaruhusu raia wa kigeni kuingia humu nchini kiharamu.

Aidha wamewataka wakazi hasa wa Kwale kuwataarifu maafisa wa usalama kila wanapoona raia wa kigeni wakiingia nchini kwa njia za mkato.

Bw Elungata alisema yeyote anayeingia humu nchini atatakiwa kuwekwa kwenye karantini.

Akiongea huko Kwale, Bw Elungata alisema mtu yeyote anayeingia humu nchini atapimwa ibainike hali yake kiafya hasa ikiwa ana virusi vya corona au la.

“Lakini tunachosema ni kwamba kama unatoka Tanzania, Msumbiji au nchi yoyote ile na unakuja Kenya, lazima upitie sehemu fulani upimwe na ukipatikana una ugonjwa wa Covid-19 unaweza kurudi kwenu. Lakini kama unaingia kwetu lazima uwekwe karantini ukimaliza muda wako unaendelea na shughuli zako,” alisema Bw Elungata.

Hata hivyo, alibainisha kwamba Kenya na Tanzania hazina mgogoro.

Bw Elungata alisema wageni 66 walitiwa mbaroni na polisi walipokuwa wakijaribu kuingia humu nchini wakitumia njia za mpenyo – panya routes – na kuwekwa kwenye karantini.

“Walipomaliza waliachiliwa na kurudi makwao. Tunajua wazee wa mitaa Lunga Lunga wanafanya kazi nzuri sana. Kama kuna ndugu zetu wengine ambao wanashawishika kuwavusha watu, tusiwakubalie kwa sababu ni hatari,” akasema.

Imefichuka kwamba baadhi ya raia wa Tanzania wanaingia humu nchini kupitia Bahari Hindi wakivuka kwa kutumia ngalawa au maboti.

Hata hivyo, Bw Elungata alisema maafisa wa polisi wakishirikiana na wale wa kuchunga bahari – Kenya Coast Guard – wataendelea kushika doria kuhakikisha hakuna raia wa kigeni wanaingia nchini kiharamu.

Aliwaonya wakazi wa Kwale dhidi ya kuwavukisha raia wa Tanzania hadi nchini akisema ni hatari.

“Kuna mtu ambaye anafanya kazi ya kuwaleta Watanzania, usiku wa manane anawatoa, nitamwambia kamishna wa kaunti amkamate na ampeleke karantini. Labda hata kwake kuna mtu amepata ugonjwa,” alisema

Bw Elungata alisema yeyote anayetoroka katika kituo cha karantini katika kaunti za Mombasa, Kwale ua Kilifi, aliyekaa na mgeni ambaye hajamtambulisha na yule aliyekataa kwenda karantini wote watatiwa mbaroni.

“Hatuna shida na hatung’ang’anii mpaka bali tunapigana na ugonjwa pekee. Mtu kama anakuja Kenya na anatoka Tanzania, hatuna shida na yeye sisi ni watu wa Afrika Mashariki tuna mikataba, tunafanya mikakati yetu pamoja hatuna matatizo,” akasema.

Amewataka maafisa wanaolinda mipaka ya Kenya kuwa makini na kuhakikisha watu wanaopita ni wale wanaotakiwa au wanaingia kihalali.

Lakini akasema wazi katika kipindi hiki kigumu ni mizigo pekee ndiyo inayotakiwa kuingia nchini kuepusha watu kutangamana kwa wingi.

Naye afisa wa uhamiaji Bi Nyandoro akasisitiza haja ya kuwakamata wanaotumia njia za kujifichaficha.

“Mkiona watu wanatumia njia za konakona kuingia Kenya tafadhali tujulishe. Tumekwua tukishirikiana na vyombo kadhaa vya usalama kuwakamata wale wanaoingia Kenya kwa njia za mpenyo. Lazima tujilinde,” akasema Bi Nyandoro.

Nairobi yaongoza maambukizi, Mombasa kwa vifo

Na JUMA NAMLOLA

KAUNTI ya Nairobi inaongoza kwa idadi ya maambukizi ya virusi vya corona huku Mombasa ikiongoza kwa watu walioaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Wizara ya Afya ilitangaza kwamba kati ya visa 963 vilivyoripotiwa kufikia Jumanne, Nairobi ina 470.

Aidha, kati ya vifo 50, Mombasa imechangia 27.

Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe aliyetokea kwa mara ya kwanza katika kipindi cha wiki nzima, alisema jana kuwa, kati ya watu 1,933 waliopimwa kuna wanaume 32 na wanawake 19 waliambukizwa.

“Kufikia leo (jana Jumanne), tumepima jumla ya watu 46,784. Tunafurahi kuwa watu wengine 22 wameruhusiwa kurudi nyumbani, na kufanya idadi ya waliopona kuwa 358,” akasema.

Orodha ya kaunti kumi zinazoongoza kwa maambukizi inaonyesha Mombasa inachukua nafasi ya pili kwa visa 331. Maambukizi katika kaunti nyingine ni; Kajiado (43), Mandera (18), Kiambu (17) na Wajir (16). Migori ina visa 14, Kilifi (10), Kwale (7) huku Kitui na TaitaTaveta zikiwa na visa vitano kila moja katika nafasi ya kumi.

Takwimu zinaonyesha kwamba watu wa umri wa kati ya miaka 20 na 39 ndio walioambukizwa zaidi.

Waziri Kagwe alisema kati ya vifo 50, Mombasa kuna watu 27 waliokufa ikifuatwa na Nairobi (20) huku Siaya, Bomet na Kiambu zikiwa na kisa kimoja kimoja.

Alionya kwamba vifo hivyo vinaweza kusababisha maambukizi zaidi iwapo vitatokea nyumbani.

“Idadi kubwa ya waliofariki Mombasa walikuwa nyumbani. Hii inahatarisha maisha ya watu wengi zaidi, ikizingatiwa kuwa huenda watu waliwazika bila kuzingatia kanuni za usalama,” alieleza.

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw Adan Mohamed alionekana kupuuza mzozo uliopo kati ya Kenya na Tanzania kuhusu mipaka yao.

Alisema, kinyume na taarifa kuwa Tanzania imezuia madereva wa matrela kutoka Kenya, magari hayo yanaendelea kusafiri kati ya pande zote mbili.

Siku ya Jumatatu, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bw Martine Shigela, alitoa maagizo kwa walinzi wa mpakani eneo la Horohoro, kwamba wasiwaruhusu madereva kutoka Kenya kuingia Tanzania.

Bw Shigela alisema malori pekee kutoka Kenya yatakayoruhusiwa ni yale yanayopeleka mizigo katika mataifa ya Malawi, Rwanda, Msumbiji na kadhalika.

Lakini Jumanne Bw Mohamed alisema hali iko shwari na madereva wa Kenya wanaendelea kupimwa virusi vya corona na kuvuka mpaka huo.

MJI WA KALE: Serikali yaruhusu shughuli za wafanyabiashara katika bandari ya zamani

Na WINNIE ATIENO

AFUENI kwa wafanyabiashara wanaotegemea bandari ya zamani maarufu Old Port iliyoko Mji wa Kale – Old Town – baada ya serikali kuwaruhusu kuendeleza shughuli zao licha ya kufungwa kwa eneo hilo.

Serikali ilifunga eneo hilo hivi majuzi ili kupunguza maambukizi ya virusi vya corona katika Kaunti ya Mombasa.

Wakazi wa Mji wa Kale wanaongoza kwa maambukizi ya virusi vya corona na kifo kutokana na ugonjwa wa Covid-19 katika Kaunti ya Mombasa.

Mshirikishi wa eneo la Pwani John Elungata na Waziri msaidizi wa Maswala ya Ndani – CAS Interior – Bw Hussein Dado wamewapongeza wakazi kwa kujitolea kupimwa kubainisha hali yao ikiwa wana Covid-19 au la.

Kati ya watu 17 walioaga dunia kufuatia ugonjwa huo Kaunti ya Mombasa tisa wanatoka Mji wa Kale.

“Tumekuja kutathmini mabadiliko tangu serikali ifunge eneo hili; tunafurahi kuona kwamba watu wamekubali kupimwa na wanaendelea kutii utaratibu uliowekwa na hata kukaa nyumbani isipolazimu watoke. Tunaona mafanikio na tukiendelea hivi malengo yetu ya kupunguza maambukizi yaliyokuwa yamekita mizizi yatatimia,” alisema Bw Elungata.

Naye Dado aliwataka ‘wanaojificha’ wajitokeze ili wapimwe.

“Ni vizuri upimwe ujue hali yako. Tumekuja kuangalia changamoto wanazopitia wakazi hapa. Msisikize porojo za watu wa huko nje; tufuate taratibu za serikali,” alisema Bw Dado.

Alisema mzigo iliyokuwa imekwama katika bandari iliyoko Mji wa Kale kufuatia kufungwa kwa eneo hilo itaruhusiwa kupakuliwa.

“Tulipata habari kutoka kwa wafanyabiashara wakisema mizigo yao iko tayari kuondoka katika bandari hii lakini mahamali wamekatazwa. Lakini sasa kupitia kwa Bw Elungata, mahamali watapewa nafasi ya kuingia na kupitisha mizigo ili biashara iendelee,” alisema Bw Dado.

Njia za kukwepa vizuizi

Wakati huo huo, Bw Elungata alisema maafisa wa usalama wamefunga njia zote za mikato ambazo wakazi walikuwa wanatumia kutoka au kuingia kaunti za Mombasa, Kilifi na Kwale.

Hata hivyo, aliwataka wakazi kuwasema wanaoingia na kutoka kaunti hizo.

Uchuuzi marufuku katika mitaa iliyofungwa

VALENTINE OBARA na WACHIRA MWANGI

SERIKALI imezidisha masharti kwa wakazi wa mitaa ya Old Town mjini Mombasa, na Eastleigh katika Kaunti ya Nairobi kwa juhudi za kuepusha ueneaji virusi vya corona.

Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman, alisema Jumamosi serikali imeamua kupiga marufuku uchuuzi katika mitaa hiyo miwili.

Hii ni pamoja na masharti yaliyotolewa awali kwa maeneo hayo ambayo yalifungwa na serikali kwa siku 15, ikiwemo kufunga majengo ya kibiashara, masoko na kuzuia watu kukusanyika eneo moja.

“Tunaomba wakazi wa maeneo hayo waendelee kufuata maagizo yanayotolewa kwao ili kusaidia kurudisha hali ya kawaida,” akasema.

Mitaa hiyo miwili ilifungwa baada ya idadi ya maambukizi kuongezeka kwa kasi katika siku chache zilizopita.

Katika mtaa wa Old Town, maji yalizidi unga wakati wakazi walikataa kupimwa kama wameambukizwa virusi vya corona, na wengine wao wakatoroka.

Jumamosi, hali tofauti na ile ya Old Town ilionekana katika mtaa wa Tudor, eneobunge la Mvita wakazi walipojitokeza kwa wingi kupimwa ikiwa wameambukizwa.

Wakazi wa mtaa huo walisema wanatambua hatari iliyopo na njia ya busara ni kutambua kama wameambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

Walianza kuwasili alfajiri katika Shule ya Msingi ya Marycliff hata kabla maafisa wa Wizara ya Afya kuwasili kwa shughuli hiyo.

Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, alisema shughuli ya kupima watu kwa wingi inaendelezwa pia katika maeneo ya Ganjoni na Majengo.

Maeneo mengine ya kaunti hiyo ambapo kuna idadi kubwa ya maambukizi ni Likoni na Nyali.

Matiang’i azuru Eastleigh kuwatuliza wakazi

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imekanusha madai kuwa amri kufungwa kwa mtaa wa Eastleigh ilitolewa kwa nia ya kuwaadhibu wakazi.

Akiongea Jumamosi alipozuru mtaa huo, Waziri wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i alitaja madai hayo yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa eneo hilo kama propaganda zisizo na msingi wowote.

Dkt Matiang’i aliwaambia wazee na viongozi wa chama cha wafanyabiashara wa Eastleigh kwamba amri hiyo iliwekwa baada ya mtaa huo kuandikisha visa vingi zaidi vya maambukizi ya corona.

“Rais amenituma hapa kuwahakikishia watu wa Eastleigh na raia wote wa Jamhuri ya Kenya, kwamba sisi ni sehemu ya familia moja kubwa. Kwa hivyo, mtu asiseme kwamba kwa kufunga sehemu hii au ile tunalenga kuumiza jamii fulani,” akasema.

Dkt Matiang’i alikuwa ameandamana na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Nairobi Esther Passaris.

Waziri pia alikariri kuwa amri hiyo inalenga kuwakinga wakazi dhidi ya maradhi ya Covid-19 ambayo kufikia sasa yamesababisha vifo vya watu 30.

Visa vilivyothibitishwa kufikia jana Jumamosi ni 649.

“Sielewi ni kwa ni mtu anazunguka akidai kuwa sisi kama serikali tunawabagua. Iweje kwamba tuwabague ilhali nyie ndio huajiri idadi ya raia na hulipa kiwango kikubwa cha ushuru kupitia biashara zenu? Ushuru mnaolipa ndio huchangia kuendesha shughuli katika idara mbalimbali za serikali,” akasema.

“Huu ni ni wakati wa sisi sote kushirikiana kupambana na jinamizi hili. Sio wakati wa kueneza propaganda. Sote ni Wakenya na huwa tunaumia tukipoteza hata mtu mmoja,” Dkt Matiang’i akaongeza.

Eneo la Eastleigh lina maduka makubwa ya kuuza nguo na bidhaa nyinginezo kutoka mataifa ya ng’ambo.

Eneo hilo pia lina mikahawa na vituo vingi vya kubadilisha sarafu za kigeni.

Mnamo Jumatano Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitangaza amri ya watu kutoingia na kutoondoka katika mtaa wa Eastleigh na eneo la Mji wa Kale Mombasa ili kuzuia kuenea kwa Covid-19.

Baada ya kutolewa kwa amri wakazi wa Eastleigh waliibua malalamishi wakidai hatua hiyo itawaathiri zaidi biashara zao zikifungwa.

Baadhi ya wakazi washutumu hatua ya serikali kuufunga Mji wa Kale

Na MISHI GONGO

WAKAZI mjini Mombasa wameshutumu serikali kwa kufunga Mji wa Kale, wakiitaja hatua hiyo kuwa kandamizi na kwamba itasambaratisha biashara zao.

Wakazi katika mji wa Mombasa hutegemea Mji wa Kale kupata bidhaa mbalimbali zikiwemo vyakula na nguo.

Wakizungumza na Taifa Leo Alhamisi, baadhi ya wakazi hao wamesema wanahofia kupata hasara maradufu kupitia mpango huo.

Bi Munira Juma ambaye anafanya biashara ya chakula amesema kufugwa kwa eneo hilo kutamzuia kufanya biashara yake ambayo ndiyo inampatia kipato cha kila siku.

“Ninauza chakula eneo la Bondeni lakini tangu kuwekwa kwa marufuku ya sisi kutoka siwezi kufika eneo hilo; chakula hakiwezi kudumu kwa muda mrefu hivyo nahofia kupata hasara,” amesema.

Wengine wanaouza mavazi wamesema wanachuma zaidi msimu huu, hivyo kufungwa kwa eneo hilo kutaathiri biashara zao.

“Kumi la pili la Mwezi mtukufu wa Ramadhan na la tatu ndio wakati wetu wa kuchuma ambapo watu wengi hununua nguo nyakati hizi na sasa kukatazwa kwao kufika huku kutatuathiri pakubwa,” amesema Mohammad Ahmed muuzaji mabuibui eneo hilo.

Amesema japo kaunti imewaruhusu kutafuta maeneo mengine ya kufanya biashara zao, itakuwa vigumu kupata sehemu nyingine hasa katikati mwa jiji.

Wafanyabiashara hao ambao wengi wao wanahudumu katika soko la Marikiti wamesema kufungwa kwa soko hilo kutaathiri mji wa Mombasa kwa jumla kwani watu wengi hupata bidhaa zao katika soko hilo.

Vitu vinavyouzwa sana katika soko hilo ni mboga, nyama na nguo.

Jumatano, serikali ilitangaza kufungwa kwa Mji wa Kale Mombasa na Eastleigh jijini Nairobi ili kupunguza idadi ya maambukizi ya virusi vya corona miongoni mwa wakazi wa maeneo hayo.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema visa ya maambukizi katika maeneo hayo vilikuwa vinaongezeka kwa kasi mno hivyo serikali iliamua kufunga maeneo hayo ili kupunguza maambukizi au hata kuzima kabisa maambukizi.

Gavana wa Mombasa atishia kuweka ‘lockdown’ Mji wa Kale

MISHI GONGO na WINNIE ATIENO

HUKU maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 yakiendelea kuongezeka katika Mji wa Kale, Kaunti ya Mombasa, gavana wa kaunti hiyo, Hassan Joho ametishia kuweka kafyu ya usiku na mchana katika eneo hilo ili kudhibiti maambukizi.

Gavana Joho ameutaja Mji wa Kale ambao ni kivutio kikuu cha watalii, kuwa kitovu cha maambukizi ya virusi vya corona.

Kufikia Jumamosi, Mombasa ilikuwa imeandikisha visa 118 vya watu walioambukizwa ugonjwa huo. Eneobunge la Mvita linaongoza kwa maambukizi.

“Tunajadiliana kuhusu kuweka kafyu katika eneo hilo iwapo wakazi hawatabadilisha tabia na kufuata maagizo yaliyowekwa na serikali,” amesema Joho.

Ameoneza kwamba ikilazimu watu wa eneo hilo watafungiwa kuepusha kutangamana na watu wengine.

“Tunaelewa huu ni mwezi wa Ramadhani na kuna baadhi yenu mnakula pamoja, lakini tunataka muelewa kuwa hali si ya kawaida, tunafaa kubadili mienendo,” akaeleza.

Akihojiwa na wanahabari, gavana Joho amelalamikia wakazi kudinda kujiwasilisha kupimwa ugonjwa huo hasa waumini wa dini ya Kiislamu kufuatia kuwa ndani ya mwezi wa Ramadhani.

Serikali ya Kaunti ya Mombasa ilianza zoezi la kupima wakazi waliyokatika maeneo yenye maambukizi ya juu siku ya Alhamisi.

“Tumepima watu 53 pekee ambapo baadhi ya wakazi wanasema hawawezi kupimwa kwa sababu ya Ramahani. Mimi si mwalimu wa dini lakini najua iwapo mtu atafanya jambo kwa dharura basi hajavunja saumu,” akasema gavana huyo.

Kulingana na Baraza la Maimamu na Wahubiri Nchini (CIPK) ni kwamba upimwaji huo ni suala nyeti ambalo linahitaji maimamu, viongozi wa dini na maafisa wa afya kulijadili ili kupata mwongozo.

Katibu mtendaji wa CIPK, Sheikh Mohammed Khalifa alisema Ramadhani ni mwezi mtukufu kwa Waislamu.

“Kabla ya kuanzisha kuanzisha zoeza la kupima watu,maafisa wa kaunti walipaswa kuzungumza na viongozi wa dini na maafisa wa afya kujua jinsi ya kutekeleza zoezi hilo kama tulivyofanya na kushughulikia mwili wa maiti aliyekufa na corona,”akasema.

Kulingana na dini ya Kiislamu, waumini hawapaswi kuingiza kitu chochote katika matundu sita miilini mwao.

Matundu hayo ni macho, mianzi ya pua, mdomo na sehemu za siri.

Sheikh Khalifa alisisistiza kuwa kaunti haipaswi kuchukulia sheria za mwezi wa Ramadhani rejareja kwa maana ya kimzaha.

Hata hivyo, gavana Joho amesisitiza kuwa haiwezekani kwa maafisa wa afya kutekeleza shughuli hiyo nyakati za usiku baada ya waumini kufuturu kufuatia marufuku yanayotaka watu wasitoke nje baada ya saa moja za usiku.

Bw Joho amesema kuwekwa kafyu ya usiku na mchana ndiyo njia pekee ya kudhibiti ugonjwa huo.

Amesema inasikitisha kuona wakazi wa eneo hilo wakijumuika kula futari barabarani bila kuzingatia vigezo vilivyowekwa na Wizara ya Afya vya kuvaa maski, kuosha mikono na kutokongamana.

Aidha, amesema baadhi ya wakazi hao wanakataa kupimwa kwa hofu ya kutengwa na jamii wakigundulika kuwa nao, huku wengine wakiona aibu kuhusishwa na ugonjwa huo.