Babu, 93 ashinda vijana kwa mistari, aoa mke wa umri wa miaka 19

Na STEPHEN ODUOR

MWANADADA mwenye umri wa miaka 19, ameshangaza wanakijiji wa Mataarba, kaunti ndogo ya Tana Delta baada ya kuamua kuolewa na babu wa umri wa miaka 93 kwa hiari yake mwenyewe.

Hawaa Roble alifunga pingu za maisha na mzee Abdullah Gardale katika harusi ya kitamaduni iliyofanyika Jumanne.

Licha ya ndoa hiyo kukosolewa na wanakijiji wengi kutokana na tofauti ya umri wa wawili hao, Bi Roble alisema aliamua kuolewa na mzee anayeelewa kutunza mke huku akidai kuwa vijana rika zake hawatoshi mboga.

“Rika zangu ni waoga na hawajali hisia za wengine. Huwa ni vigumu sana kuelewana na mwanamume wa rika yangu ikilinganishwa na jinsi ninavyoelewana na mwanamume mzee,” akasema katika mahojiano na Taifa Leo.

Wawili hao walikutana Kipini ambapo Bi Roble alikuwa akifanya vibarua.

Wakati huo, alikuwa na umri wa miaka 18 na alikuwa amechumbiana na kijana ambaye alitoweka ghafla.

Bi Roble anasema alisubiri kwa muda mrefu kijana huyo arudi ili waoane, lakini akachoka kumngoja.

“Hakutoa sababu yoyote ya kutoroka, wala hakuniaga. Alitoweka tu na nikasikia uvumi kuwa alionekana katika maeneo mengine lakini sijawahi kumwona hadi leo na familia yake pia haijawahi kufichua aliko,” akasema.

Mzee Gardale alianza kumtongoza, na Hawaa akaitikia maneno yake.

Watu wachache waliogundua kuhusu uhusiano wao mapema walijaribu kumkanya, hadi jamaa za mwanamke huyo wakaanza kumgombeza mzee huyo wakimtaka aachane na binti yao.

“Wajomba wangu wengi na hata kaka zangu hawakupendezwa na uhusiano huu lakini mimi nilikuwa nimeridhishwa. Kwa mara ya kwanza nilihisi kupendwa,” akasema.

Jamaa zake waliamini kuwa Bw Gardale alikuwa mzee kupita kiasi na hangetimiza mahitaji ya kihisia ya msichana wa miaka 19.

Walidai kuwa, mwanamume huyo hakufaa kwa sababu aliwahi kutaliki wake zake wawili, na wengine wawili walikuwa wamefariki kwa hivyo hangeishi sana na binti yao.

“Mume wangu ana hekima na nguvu. Wale wanaodhani hana thamani waniulize mimi. Mimi ndiye mke wake, namfahamu ndani na nje,” akasema.

Kwa upande wake, Bw Gardale alisema wanaomkashifu wako huru kufanya hivyo lakini cha muhimu ni kwamba yeye binafsi ana furaha maishani.

“Nimekosolewa na wengi lakini wana haki kutoa maoni yao sawa na jinsi sisi tuna haki ya kuishi kwa furaha,” akasema.

Wawili hao walikuwa wamehamia Malindi kwa muda ili kuepukana na pingamizi hizo.

Jamaa zao walipoona kuwa hawatashinda katika vita hivyo, waliamua kuwaacha wawili hao wafanye watakavyo ndipo wakafunga ndoa Julai 12.

Mwanamke atoroka mumewe na kuolewa na ‘roho mtakatifu’

Na OSCAR KAKAI

MWANAMKE wa umri wa miaka 41 ameshangaza mumewe pamoja na wakazi wa mji wa Makutano, Pokot Magharibi, baada ya kutangaza kuwa ameolewa na roho mtakatifu.

Elizabeth Nalem ambaye ni afisa wa kaunti mjini hapo aliandaa sherehe ya kufunga ndoa na roho mtakatifu katika hafla iliyoandaliwa kwenye hoteli ya Chelang’a mjini Makutano.

Bi Nalem aliandamana na wafanyakazi wenzake wa kaunti pamoja na wafanyabiashara wa kike katika hafla hiyo ambapo alikula kiapo cha kuwa mwaminifu kwa ‘mumewe’ mpya – roho mtakatifu.

Bi harusi alikuwa amevalia mavazi ya harusi na sherehe ilipambwa kwa vigelegele kutoka kwa akina mama huku mumewe, Joshua Nalem, akifuatilia tukio hilo kwa mshangao.

Sherehe hiyo iliongozwa na Kasisi Albert Rumaita wa kanisa la Full Gospel.

“Nimetumikia dunia tangu nilipozaliwa. Lakini sasa roho mtakatifu ameniagiza nitumikie Mungu. Roho Mtakatifu alinituma kwa Pasta Rumaita ambaye alininunulia vazi la harusi, aliandaa hafla hii na akakodisha magari yaliyotuleta haba,” akasema Bi Nalem ambaye ni mama ya watoto sita.

Alisema kwamba kabla ya kuandaa hafla hiyo aliomba ruhusa kwa mumewe, lakini ombi lake likakataliwa.

Jumanne, Bw Nalem aliyeonekana kupigwa na butwaa alishuhudia mkewe ambaye wameishi pamoja kwa miaka 20, akiapa kumpenda na kutoa maisha yake kwa ‘mume’ mwingine asiyeonekana.

“Nimeshangaa sana. Nilitoa mahari; ng’ombe 22 na mbuzi 15 nilipooa mke wangu. Lakini sasa anafunga ndoa na mume mwingine anayedai kuwa roho mtakatifu,” akasema.

Bw Nalem alifichua kuwa ndoa yao imekuwa ikikumbwa na msukosuko kwa miezi kadhaa.

Alisema mvutano baina yao ulianza baada ya mkewe kuanza kubadili mwenendo wake wa maombi.

“Alianza kuamka usiku wa manane kuomba na kila mara nilipomuuliza alikimbia kwa jirani na kuniacha peke yangu,” akasema Bw Nalem.

‘Usilaze damu mwanamke wewe’ 

Na WINNIE A ONYANDO

“MUME wangu anahanya” ni kauli ambayo utasikia kutoka kwa vinywa vya wanawake wengi walio katika ndoa.

Rosey, 25, ni mwanadada mrembo ambaye pamoja na mumewe Paul, wamejaliwa mtoto mmoja wa kiume.

Kipusa huyo anamlaumu mumewe na kumchukia kwa tabia yake ya kuchepuka.

Ingawa si tabia nzuri kidini na kijamii, kuna sababu nyingi zinazoweza kumfanya mwanamume achepuke.

Unaweza ukawa wewe ni mwanamke mrembo kupindukia kama Rosey lakini unashindwa kwa nini mume wako anakuendea kinyume.

Wakati vitendo vya kuchepuka ni vya kulaaniwa, ukweli ni kuwa baadhi ya wanawake hawawajibiki jinsi ipasavyo wakiwa katika ndoa.

Mwanamke hafai kuwa yeye ndiye sehemu ya tatizo huku anamlaumu mume eti ana jicho la nje.

Ukweli ni kwamba baadhi ya wanawake wenyewe wamekuwa chanzo cha waume kurambwa miguu na mbwa.

Wakati wa kuchumbiana, utamuona mwanadada ni malaika, hana shida wala dosari. Mwanamume anashawishika “bila shaka huyu ni mchumba mzuri” na kuanza kuharakisha pilkapilka za kufunga pingu za maisha na kipusa huyo.

Kitumbua kinaingia mchanga wakati mke wa huyo mwanamume anaamua kuwa ‘yeye’ ambapo anatoa rangi yake kamili. Kumbe alikuwa kinyonga sasa amebadilika!

“Simwelewi kabisa mume wangu Paul kwa sababu zamani akinijali na kunifurahisha kipindi tunachumbiana. Sasa amekuwa kigeugeu, simtambui kamwe,” Rosey analalamika.

Rosey anamshuku mumewe kuwa ana ‘mpango wa kando’ ila yeye mwanamke mwenyewe hajajichunguza kutathmini kinachoweza kusababisha mumewe kuwa katika uhusiano wa kimahaba na mwanamke mwingine.

Kuna vijisababu vingi vinavyoweza kuwafanya wanaume kuwa walaghai na kuanza kutoka kimapenzi na wanawake wengine mbali na wake.

Mwanamke pindi tu anapojifungua, analegeza kamba ya usafi na kushughulikia mwili na urembo wake. Anasema kuwa ‘tayari ashapatikana’ ila hajui kuwa wanaume ni viumbe wanaovutiwa na wanachoona au wanayemuona.

Kazi yake katika nyumba ni kumshughulikia mtoto na nyumba, utadhani aliolewa “kuridhisha tu kazi za nyumba” huku akimpuuza mume.

Usilaze damu mwanamke wewe. Mpe mumeo muda mwingi, ukae karibu naye na umdekeze jinsi inavyofaa.

Tengeneza mwili wako, jipambe ili urudishe usichana wako. Mume akirejea nyumbani jioni asije akakupata ukinuka jasho, hujakoga wala hujipamba.

Mpe sababu za kuwa na hamu ya kuja nyumbani.

Mtayarishie chakula katika mazingira safi, mpe chakula kwa njia ya utaratibu. Usimtupie chakula kana kwamba yeye ni mbwa. Hata mbwa wa matajiri hawatupiwi chakula! Ukarimu wako utamtoa ‘ulafi wa fisi’ na kumfanya kuwa na roho ya kutosheka, hata akiwaona warembo wengine nje hana haja.

Unapojitunza kama mwanamke, utampa mume wako hamu ya kutaka kuwa kando yako kila wakati. Hatakuwa na tamaa anapowaona wanawake wengine huko nje.

Mpumbaze na umfunike na blanketi ya mapenzi. Yaani atazama katika bahari ya mapenzi akiona raha ajabu!

Akirejea nyumbani asikutane na nguo zimetapakaa kila mahali, nyumba imechakaa, watoto ni wachafu ilhali wewe kazi yako ni umbea na kurandaranda tu.

Jishughulishe mwanamke ili uweze kuilinda ndoa yako.

CHOCHEO: Jifunze kuomba msamaha ili furaha irejee kwenye ndoa

NA BENSON MATHEKA

Wengi husema kuwa wanaume hawaombi wake zao msamaha wakiwakosea hata wakipatikana peupe wakichepuka lakini sivyo kwa Dan. Inasemekana kuwa wanawake ni wepesi wa kuomba msamaha wakikosea waume wao lakini sivyo kwa Elena. Wawili hawa ni mtu na mkewe na ndoa yao imekuwa yenye patashika nyingi kwa sababu ya tofauti zao.

Tofauti na wanaume wengine, Dan hupenda kuomba mkewe msamaha kila wakati akihisi amemkosea. Hafanyi hivi kwa sababu hawezi kukaa ngumu kama wanaume wengine wenye roho za chuma, ni kwa sababu anampenda mkewe na anatambua mchango wake katika maisha yake. Lakini kwa Elena mambo ni tofauti.

Anachukulia tabia ya mumewe ya kumuomba msamaha kama unyonge.“Mwanamume ngani huyu anayependa kusema “nisamehe” kila wakati. Nimemchoka. Siwezi kuomba msamaha hata akinipata peupe nikichepuka,” asema Elena ambaye amekuwa katika ndoa kwa miaka sita. Kwa George na Cindy, ndoa yao ya miaka 11 imedumu kwa sababu ya kuombana msamaha.

“Tunatambua kwamba binadamu ana mapungufu mengi na kwamba bila msamaha na kunyenyekea kwa mwenzako ndoa haiwezi kudumu. Hii haimaanishi mtu achepuke kwa sababu anafahamu akiomba mwenzake msamaha atamsamehe,” asema Cindy.

Katika maisha ya mapenzi, aeleza, kila kitu hakiwezi kuwa mteremko na inafika wakati vitendo, matamshi na hatua anazochukua mtu zikawa maudhi kwa mwenzake.

“Katika hali hii, kuomba msamaha ndio njia ya pekee ya kurejesha furaha katika ndoa. Hakuna haja ya kununiana kwa sababu ya kukosa kutamka maneno mawili au matatu “naomba msamaha mpenzi” na kutuliza hali,” asema George ambaye pamoja na mkewe ni washauri wa wanandoa katika kituo cha Abundant Life Care jijini Nairobi.

Kulingana na mtaalamu huyu, kuwa na roho ya chuma kunaweza kusababishia mtu mateso makubwa katika maisha ya mapenzi.“Najua mwanadada ambaye ametalikiwa mara tatu kwa sababu ya kuwa na roho ngumu hivi kwamba hawezi kuomba msamaha na kunyenyekea kwa mwanamume.

Najua mwingine ambaye ana cheo kikubwa tu na pesa lakini amekosa mume wa kumuoa kwa kuwa wanaume huwa wanamhepa kwa kuwa hawezi kunyenyekea kwao,” asema George. Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema kwamba dawa ya kukuza mapenzi katika ndoa, ni kuombana msamaha kila wakati mtu akihisi kwamba amemkosea au kumuudhi mwingine.

“Hii ni tiba. Mwanamume, omba msamaha nawe mwanamke usichukulie ombi la mumeo la msamaha kama unyonge. Kwa hakika, mwanamume anayeomba mkewe msamaha ndiye dume kamili na anafaa kuheshimiwa kwa sababu sio wengi wanaofanya hivyo,” asema Joseph Kimani, mtaalamu wa kituo cha Maisha Mema jijini Nairobi.

Sheila Wanjiru, mwanadada mwenye umri wa miaka 25 asema alishtuka mumewe wa miaka mitano alipomuomba msamaha baada ya kumuudhi.

“Sikuamini, nilimkumbatia kwa furaha na kumbusu kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza katika maisha yangu kusikia mwanamume akiomba mwanamke msamaha, na sio mwanamke mwingine, mimi binafsi,” asema Wanjiru. Kulingana na mwanadada huyu, alichukulia hatua ya mumewe kama nguvu na akazidisha mapenzi

.“Tuko sawa, sijawahi kuona mume wangu akiwa na unyonge kwa sababu ya kuniomba msamaha. Ni dume na ninamheshimu sana kwa hilo,” asema. Ingawa Cindy anasema kwamba wanandoa wanafaa kuombana msamaha, anaonya wachumba kuwakosea wenzao makusudi kwa sababu wanafahamu watawasamehe wakiwaomba msamaha.

“Kosa la makusudi linaweza kuzua balaa. Haufai kutumia upole wa mtu wako kumnyanyasa zaidi kwa kurudia kosa ili akusamehe,” asema Cindy. Michael Ndegwa, mkazi wa mtaa wa Loresho, Nairobi asema kwamba alichoka na tabia ya mkewe ya kuhanya na kisha kuomba msamaha akifika nyumbani akiwa amechelewa.

“Ilifika mahali nikakataa msamaha wake. Alikuwa akinitumia vibaya na nikamtaliki,” asema. George asema mtu hafai kusamehe mchumba aliye na tabia zinazoweza kumtumbukiza kwenye hatari. “Kwa mfano, mtu hawezi kuwa anakupiga kila mara kisha akuombe msamaha ilhali amekuumiza,” asema.

Shinikizo mbunge amlipe mpenzi wa zamani Sh200,000 kila mwezi

Na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Ikolomani Bw Bernard Masaka Shinali ameshtakiwa na mwanamke anayedai alipata mtoto naye. Mwanamke huyo Ms Caroline Mutheu Mwakodi amedai kuwa Bw Shinali hamsaidii mtoto huyo.

Anaomba mahakama imshurutishe mwanasiasa huyo kulipa zaidi ya Sh200,000 kila mwezi kugharamia mahitaji ya mtoto huyo aliye na umri wa miaka mitano sasa.

Ripoti ya uchunguzi wa DNA iliyotolewa kortini imebaini kuwa Bw Shinali ndiye baba mtoto kibayolojia. Mahakama ya kuamua kesi za watoto Milimani Naironi imewaamuru mawakili wa Bw Shinali na Bi Mutheu wawasilishe kortini Machi 9 2021 ushahidi wao ndipo uamuzi utolewe.

Mawakili hao ni Bw Majanja Luseno anayemwakilisha Bw Shinali na Bw Katunga Mbuvi anayemwakilisha Mutheu. Katika ushahidi aliowasilisha kortini , Mutheu amedai kuwa walikuwa marafiki na Mbunge huyo hapo 2015 alipopachikwa mimba.

Mutheu, ameeleza kupitia kwa wakili Bw Mbuvi kuwa, alijaliwa kumzaa mvulana Mei 2016. Tangu ajifungue ameeleza kuwa mwanasiasa huyo alikoma kuwasaidia.

Bw Mbuvi anaomba mahakama imshurutishe Bw Shinali awe akimpa Mutheu zaidi ya Sh200,000 kila mwezi kugharamia mahitaji ya mwanawe.

Mama huyo anaomba korti iamuru awe akipewa Sh50,000 za ada ya nyumba, Sh35,000 za matibabu, mshahara wa mjakazi Sh15,000, maankuli Sh35,000, nguo Sh40,000 na ada ya starehe Sh35,000 kila mwezi.

Mama huyo ameeleza mahakama, mshtakiwa hupokea mshahara mnono. Katika ushahidi wake wa kujitetea aliowasilisha mahakamani, Bw Shinali , ameyakana madai kwamba alimpachika mimba , Mutheu kama anavyodai.

“Mimi siyajui kamwe madai kuwa mimi ndiye baba wa mvulana huyo,” Bw Shinali ameeleza katika ushahidi wake kwa mahakama.

Kesi hiyo ilipowasilishwa, Bw Shinali alikataa kata katu kwamba alimzaa mtoto huyo na kuomba mahakama iamuru uchunguzi zaidi ufanywe kubaini madai ya mwanamke huyo.

Mahakama iliamuru uchunguzi wa DNA ufanywe ndipo ukweli ujulikane uwongo ujitenge. Mahakama inayochunguza kesi hiyo iliamuru mnamo Machi 2020 uchunguzi wa DNA ufanywe.

Bw Shinali aliomba kesi isitishwe kusubiri matokeo ya uchunguzi wa DNA kutoka kwa maabara ya Serikali.

Sampuli za kufanyiwa uchunguzi wa maabara zilitwaliwa kutoka kwa Bw Shinani , Mutheu na mwanaye kukaguliwa kiutalaamu wa kisayansi kubaini uzazi wa mtoto huyo.

Mkaguzi katika maabara ya Serikali Bi Pamela Khamala Okelo alipokea sampuli hizo na kuzikagua kwa makini. Uamuzi uliofikiwa katika maabara hiyo ya Serikali na kuwasilishwa kortini ulibaini kuwa Bw Shinali ndiye baba wa mtoto huyo.

“Kulingana na uchunguzi uliofanyiwa sampuli zilizopokewa katika maabara ya Serikali imebainika kwa asilimia 99.99 Bw Bernard Masaka Shinali ndiye baba mzazi wa mtoto wa Caroline Mutheu,” Bi Okelo amesema katika ripoti aliyoiwasilisha kortini mnamo Aprili 7, 2020.

Katika ushahidi wake, Mutheu ameeleza kuwa mnamo Mei 7,2016 walimzaa mwanaye baada ya “ mapenzi kunoga baina yao.”

Lakini ameeleza kuwa, mbunge huyo hawasaidii yeye na mwanawe na “hata hajui tunachokula, kunywa na hata makazi yetu yako na shida.”

Mutheu anaomba mahakama iamuru Bw Shinali awe akigharamia , matibabu ,chakula, makazi, gharama za hospitali na elimu ya mwanaye.

“Mshtakiwa (shinali) ni Mbunge wa Ikolomani iliyoko kaunti ya Kakamega na hupata ndonge nono kila mwezi,” asema Mutheu katika hati zake za ushahidi mahakamani.

Mlalamishi huyo anasema kuwa ndiye anayegharamia mahitaji ya mwanaye na yuahiti “fedha sisizo haba kugharamia mahitaji yake.“

Mutheu amesema mtoto huyo anahitaji maisha mazuri na endapo “ Bw Shinali hatashurutishwa na mahakama kugharamia mahitaji ya mtoto huyo bila shaka ataanza kuishi maisha ya uchochole.”

Mutheu anaomba korti isimame kidete na kuamuru haki za mtoto huyo zilindwe na apewe kile anachohitaji kukua na kuishi maisha yasiokumbwa na bughudha.

Pia anaomba mahakama ipitisha maagizo mengine inayoona yanamfaa , mtoto huyo. Kesi itasikizwa Machi 9,2021.

UMBEA: Mwanamke huridhishwa zaidi na ukarimu na upendo wa mwenzake

NA SHANGAZI SIZARINA

Ipo dhana kwa baadhi ya wanaume kwamba ili umpate mwanamke ama msichana ni muhimu kutunisha msuli wa pesa. Kwamba usambaze noti ili kuimarisha heshima kwa mwanamke ama msichana ambaye anakuvutia.

Imani yao kubwa ikiwa ni kwamba kawaida wanawake hupenda hela, hivyo ili kumpata kwa urahisi muonyeshe kwamba unazo hizo hela.

Mtazamo huu wa baadhi ya wanaume kwamba mwanamke analainishwa na pesa umeleta changamoto nyingi katika mahusiano na ndoa. Kwani baadhi wanadhani unapotimiza haja za mwanamke kifedha inatosha kabisa na hakuna umuhimu wa kutimiza haja zake zingine ambazo ni za kimwili ama kihisia.

Mwenendo huu huleta upweke kwa baadhi ya wanawake wanaojikuta wana kila kitu nyumbani kinachohusiana na mahitaji ya pesa, lakini wanakosa kutimiziwa mahitaji ya kihisia ama kimwili na hao wenzao. Upweke huzaa migogoro isiyokwisha ambayo huweza kufanya baadhi ya wanaume washindwe kuwaelewa wanawake. Kwa tathmini na uamuzi wao, unaweza kuona kwamba ni vigumu kumridhisha mwanamke.

Lakini wanachosahau wanaume wenye mtizamo huu ni kuwa mwanamke kwa asili yake anayo mahitaji ya msingi ambayo yanapopuuzwa, chochote kinachofanyika kama mbadala wa mahitaji hayo hakiwezi kuwa na maana yoyote. Usipoweza kujua mahitaji yake halisi, unaweza kumpa chochote kile unachodhani anakihitaji na bado mambo yasiende kama ulivyotarajia.

Pamoja na hivyo, wapo wanawake ambao lengo kubwa ni kujipatia pesa za mwanaume. Hawa ni wanawake wanaofanya biashara ya mahusiano.

Kwao, hakuna sababu yoyote ya kuwa na uhusiano imara na wenzao isipokuwa mpangilio wa kujipatia vitu na fedha. Hatuzungumzii uhusiano huo wa kibiashara kati ya mwanamume na mwanamke bali uhusiano wa dhati unaojengwa katika misingi ya upendo, uaminifu, kuelewana na ahadi ya kuwa pamoja katika dhiki na raha.

Katika hali halisi, pamoja na fedha, mwanamke huridhishwa zaidi na ukaribu na upendo wa mwenzake.

Mwanamke anahitaji kuambiwa kila mara na kuthibitishiwa kwa vitendo kuwa anapendwa. Hata hivyo, lugha ya mapenzi hutegemea mambo mengi. Kuna athari za utamaduni, desturi na imani zilizopo katika jamii aliyokulia mwanamke. Hata hivyo, yapo matendo yaliyothibitika kuvuka mipaka ya kiutamaduni.

Uelewe kwamba kuna nguvu kubwa kumwambia mwanamke unampenda, na isiwe mara moja bali mara nyingi iwezekanavyo.

Pamoja na kumpenda, mwanamke anahitaji kupata muda wa kutosha na ampendaye, ikiwezekana kutoka naye, kuwa naye nyumbani mara kwa mara pale inapowezekana. Iwapo unataka kuugusa moyo wa mwanamke, akupe heshima unayoihitaji, unawajibika kujua vitu gani mahususi ukimfanyia vinatuma ujumbe wa wazi kuwa unampenda.

Usipoweza kumfanya mwanamke ajisikie kupendwa, anapoteza hamu ya uhusiano. Huchoka kihisia na anaweza kufanya mambo yasiyotarajiwa ili tu kuhujumu mahusiano.

Pamoja na yote, mwanamke hupenda aonekane ni kipaumbele kwa mumewe. Kwamba katika hali ama hatua yeyote, mumewe anampatia kipaumbele kabla ya kufikiria ama kutenda jambo lingine. Kila la heri katika kuboresha mahusiano yako.

sizarinah@gmail.com

MWANAMUME KAMILI: Kila nyumba huwaka moto, muhimu kujenga muamana heshima

NA DKT CHARLES OBENE

Je, ulijua kwamba kutaka kuishi “kama wanavyoishi majirani” ni “uchochezi” unaoweza kuzua rabsha wanandoa wakachaniana nguo sisemi kuvuana heshima hadharani?

Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa katika “nyumba” ya jirani mmoja baada ya vita vikali kuzuka kufuatia “ushauri” wa mke kwa mumewe.

Kwa hakika, sijawahi kusikia wala kuona watu wazima – tena waliokwisha vua soni wakakoga pamoja – wakipigania jambo la kitoto kama lile. Mwanamume mmoja hakusita “kukomesha uchochezi” wa mkewe. Hebu nielezeni nyie mnaojua maana ya “uchochezi!” Alichocha akachochea nini hasa?

Gumegume yule hakuweza kujizuia kiume baada ya “mkewe kumwambia hadharani kwamba ndoa za majirani zilikuwa bora kuliko yao!”

“Majirani walipatana, walipanga mikakati, walifanikisha miradi na kufurahia ufanisi kama familia inavyostahili kufanya!” Isitoshe, mwanamke yule alipendekeza “mumewe kutenga muda na kuwapeleka kujivinjari wikendi” kama “walivyofanya majirani” na “marafiki wa karibu.”

Sijui kama kweli ushauri huu aliotoa “mke kwa mumewe” ulikuwa mbaya ama “ulichochea” kitu. Nijuavyo ni kwamba ndoa za machizi wa leo si ndoa za kujadiliwa kwenye safu ya watu wazima wanaojua maana ya “wawili kuja pamoja na kuwa mwili moja!”

Ndio kwanza tunavuna matunda ya watu kuoa na kuolewa wiki moja baada ya kukutana kwenye dansi za usiku! Hakuna siku mwanga utaoa ama kuolewa na kiza cha maki. Mwanamume kamili anajua tosha vipi na wapi kutuliza mvuke kichwani mwake

Nasisitiza kwamba lililowasha moto wa hamaki watu wazima wakafarakana hadharani lilikuwa jambo la kitoto lisilostahili kuzungumziwa mbele ya watu wazima wenye akili razini.

Lakini kwa kuwa limetishia kuwa chanzo cha vita vya kila siku kwenye nyumba za majahili na machizi wa leo, hatuna budi kulizungumzia na kulikomesha kabla wajuvi wa mitandaoni na kina yakhe kulitilia pilipili. Wajua tena kazi ya wambea wanaopenda mno “kueneza habari” ama kutoa “elimu nasaha” mitandaoni!

Kila nyumba ina siri na kila chumba kimeficha changamoto zake. La muhimu zaidi katika kukuza muamana nyumbani ni kuwepo usuhuba wa dhati na heshima baina ya “mume na mkewe.” Hilo lina maana kwamba wanaooana na kuolewa sharti wazingatie usuhuba kabla ya mapenzi kama kigezo kuu.

Ni jambo la busara mno mwanamume kumchumbia na kuoa rafiki. Vivyo hivyo, mwanamke anastahili kufia rafiki. Mtu unayemjua tena anayekujua nje na ndani katu hawezi kuhamakika ovyo sisemi kutoa ushauri wa kipumbavu katika ndoa. Kuna mambo na tofauti za nyumbani zinazoweza kutatuliwa kwa njia ya “kucheka na kuchekeshana tu!”

Ndivyo maisha yalivyo. Hivyo ndivyo wanavyoishi watu waliotanguliza usuhuba kabla ya mapenzi. Ole nyinyi mliochagua wanawake kwa misingi ya ukubwa wa nyonga! Ole nyinyi mliokimbilia kuolewa na “mastaa tajika katika jamii!”

Usuhuba huu ndio gundi inayoleta watu wazima pamoja wakaona vyema kuweka wazi maisha na siri zao. Usuhuba hauna husuda wala chuki.

Tatizo linalotusibu akina sisi tunaofyatuka kama pomboo ni tabia ya kuoa mashangingi wa vilabuni ama kuolewa na gumegume tunaogutukia kwenye vilabu vya walevi chakari. Kweli, kuoa na kuolewa na mtu usiyejua asili wala fasili yake kama wanavyofanya kina yakhe wa leo ni mwiba unaozidi otesha tende miguuni mwa wanandoa wa leo.

Hakuna na haitakuwepo nyumba ya wawili ambamo hamna zogo japo kidogo. Kutopatana kwa jambo ama wazo miongoni mwa wanandoa ni ubinadamu wala hakuna haja kumaliza kuni kupika na kupakua tofauti hizo mbele ya umma.

Wenzangu watu wazima, msidanganyike kwa hadaa za nyuso za wanandoa zinazometa kama mwezi mkadhani “kwao ndiko peponi!”

Msimalize mate kubishana bure mkitaka kuishi kama “majirani wasiogombana.” Nyinyi mnaoshauriana kupitia arafa za simu ama nyaraka za mitandaoni ndio kwanza “aibu iliyotusibu!” Wanandoa wanaopigania maisha ya majirani wanadunisha mno maana ya ndoa. Hakuna nyumba bora kuliko ya mwingine.

Tofauti ni kwamba “kusikofuka moshi” ni nyumba ya wawili waliokwisha chagua kutumia ubongo kuliko midomo na ulimi. “Majirani wasiogombana” wamechagua wenyewe kujiheshimu na kuzipa hadhi familia zao.

Wamechagua kujenga kuta kuzuia wambea kuchochea maisha ya kwao. Isitoshe, wameekeza kukuza usuhuba na heshima baina yao. Hiyo ndivyo wanavyofanya mwanamke na mwanamume kamili.

obene.amuku@gmail.com

CHOCHEO: Akikuacha kwenye dhiki utamsamehe ukiomoka?

NA BENSON MATHEKA

Miaka minne iliyopita, Rosa* alimuacha mumewe kwa sababu hakuwa na uwezo wa kukimu mahitaji ya familia. Mumewe Alex* hakuwa na kazi na maisha yalipokuwa magumu baada ya kuugua, Rosa aliondoka na watoto wao watatu. Hata hivyo, haikuchukua muda, Alex alipona na akatia bidii hadi akajaliwa kupata mali.

“Baada ya kusikia niliomoka, Rosa amerudi kwangu na kuniomba msamaha. Anataka arudi tujenge ndoa ambayo alibomoa nilipokuwa nikimhitaji zaidi wakati wa ugonjwa. Sidhani ninaweza kumsamehe,” asema Alex.

Kinachomuuma mwanamume huyu ni kwamba Rosa hakurudi kwa wazazi wake alipomuacha akiteseka.

“Japo nilikuwa sijiwezi, nilifuatilia na nikaibaini kwamba hakuenda kwa wazazi wake alipoondoka kwangu akidhani nitakufa kwa sababu ya shida na ugonjwa. Sijui alikokuwa na sitaki anieleze,” asema Alex.

Visa vya wachumba kutema wenzao shida zikiongezeka ni vingi mno hasa wakati huu wa janga la corona.

“Sio kwamba ni jambo geni lakini kipindi hiki cha corona, visa vya waume na wanawake, kuwapiga teke wachumba wao vimeongezeka. Ni mtindo unaoshuhudiwa kote ulimwenguni,” asema Talia Simiyu mshauri wa wanandoa wa kituo cha Big Hearts jijini Nairobi.

Anasema watu wanaowaacha wapenzi wao wakilemewa na shida na kuwarudia wakifanikiwa huwa hawana mapenzi ya dhati.

“Wakati wa harusi hasa za Kikristo, wanandoa huwa wanaapa kuishi pamoja wakati wa faraja na wakati wa dhiki. Kwa hivyo ukimuacha mchumba wako kwa sababu ya kufilisika au kuwa mgonjwa unaenda kinyume na viapo vya ndoa,” asema.

Hata hivyo anasema kuna watu wanaowasamehe waenzao waliowaacha wakiwa na shida na kurejea wakipata pesa.

“Wapo wanaoamua kuwasamehe hasa ikiwa walikuwa wamezaa watoto. Hata hivyo, ni vigumu mtu kusahau kitendo kama hicho na lazima uhusiano wao uwe na misukosuko,” aeleza Talia,Dorcas Kibaya, mwanadada mwenye umri wa miaka 32 anasema kwamba hawezi kumsamehe mumewe aliyeamuacha akiwa mgonjwa mahtuti.

“Mtu ambaye aliniacha nikiwa mgonjwa mahtuti na kuenda kuishi na mwanamke mwingine nimsamehe mimi? Wallahi siwezi!” asema kwa machungu. Mwanadada huyu anasimulia kwamba kama haingekuwa majirani waliomsaidia mumewe alipotoroka, yeye na watoto wake wawili hawangekuwa hai.

“Alijitokeza baada ya miaka sita aliposikia sikufariki, akapata watoto wakiendelea vyema na kudai ni wake. Nilimwambia sikatai watoto ni wake wa kuzaa lakini nikamkumbusha aliwatelekeza nikiwa hoi kwa ugonjwa. Nilimwambia apotelee mbali,” aeleza Kibaya.

Kulingana na Talia, watu wanaweza kuwasamehe wachumba wao wanaowatema wakati wa shida hasa ikiwa walikuwa na watoto lakini wakose kuishi pamoja.

“Msamaha ni muhimu kwa mwanadamu kupata uponyaji wa moyo lakini kwa sababu ya yaliyotokea, napendekeza watu wasipapie kuishi pamoja ikiwezekana,” aeleza.

Peter Kamau alizingatia ushauri huu mkewe aliyemuacha akiwa chumba cha wagonjwa mahtuti aliporejea baada ya kupona na kurudia shughuli zake za kawaida.

“Nilikuwa na uchungu mwingi moyoni lakini nikaumeza kwa sababu niliwapenda watoto wangu. Hata hivyo sikukubali kuishi nyumba moja na mtu aliyeniacha nikiwa ICU na kusomba mali na pesa ambazo ningetumia kulipa bili ya hospitali,” aeleza Kamau.

Kamau ambaye ni mfanyabiashara jijini Nairobi huwa anatenga muda wa kuwa na watoto wake ambao anakidhi mahitaji yao kikamilifu.

“Kutokana na yaliyonipata, nimeamua kwamba hakuna mapenzi ya dhati ulimwenguni. Kuna kinachomfanya mtu kumpenda mwingine na kikikosekana huwa hauna thamani kwake,” aeleza Kamau.

Kulingana na Pasta Isaac Okoth wa kanisa la Reoboth Revival, mtaani Kayole Nairobi, moja ya nguzo kuu za ndoa ni msamaha.“Msamaha ndio nguzo ya ndoa japo ni uchungu kuachwa na mtu wakati unamhitaji zaidi hasa aliyeapa kuishi nawe hadi kifo kiwatenganishe,” asema.

CHOCHEO: Mume si suti, ni ujasiri!

NA BENSON MATHEKA

Faiza alishangaza marafiki wake kwa kumuacha Ali na kumchumbia Abdul ingawa mwanamume huyo alikuwa akimpenda na kumtunza vyema. Kwa mwanadada huyu, hakupata alichotafuta kwa mume katika Ali.

“Ni kweli ana pesa, ni jamala, nadhifu na ananipenda lakini ni mwoga. Siwezi kuishi na mume mwoga katika maisha yangu. Nani atanilinda nikiwa hatarini?” ahoji Faiza.

Mwanadada huyu anasema ingawa Abdul hana pesa kama Ali, ni jasiri. “Ninataka mume ambaye nitahisi kuwa salama sio mwoga atakayeniuliza atakachofanya kunitoa kwenye hatari,” asema.

Sally, mwanadada mwenye umri wa miaka 32 anasema aliolewa na Mwangi kwa sababu ya ujasiri wake. “Nilimuacha mwanamume aliyekuwa akinipatia chochote kwa sababu niligundua alikuwa mwoga.

Ingawa Mwangi ana pesa nyingi, ninajua kitu kimoja, kwamba hakuna anayeweza kunigusa kwa sababu ataona moto,” asema.Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema kwamba hakuna mwanamke anayeweza kukubali mwanamume mwoga.

“Wanawake hupenda wanaume wanaoweza kuwahakikishia usalama wao, sio tu kwa kukidhi mahitaji yao, mbali pia kuwalinda dhidi ya hatari inayoweza kuwakabili. Unaweza kumpa mwanamke kila kitu anachohitaji lakini ikiwa hauwezi kumlinda akikumbwa na hatari, atakuacha,” asema Steven Omboki, mwanasaikolojia wa kituo cha Abundant Life mjini Athi River.

“Kigezo muhimu ambacho wanawake wanazingatia wanapotafuta mume ni ujasiri. Mtu jasiri anaweza kufanikiwa katika mambo mengi. Hata akishindwa anaweza kupigana hadi afaulu,” aeleza.Kulingana na Martha Kawira, mshauri mwandamizi wa shirika la Maisha Mema, wanawake wanaamini kwamba mwanamume mwoga hawezi kuwa mume bora.

“Kwa wanawake, mwanamume mwoga hafai kuwa mume wa mtu. Woga unafanya mwanamume kukosa mke kwa sababu wanawake wanapenda mtu atakayewahakikishia usalama wao na watoto wao,” asema Kawira.

Daisy Mukami, mwanadada mwenye umri wa miaka 32 na mama ya watoto wawili, asema alimuacha mumewe alipogundua alikuwa mwoga.

“Hakuweza kuua hata panya katika nyumba yetu. Hakuweza kukabili majirani wakituchokoza. Hakuweza kutetea mali yake ikitumiwa vibaya na watu wengine. Hivyo niliamua kumtema kwa sababu kuwa naye ni sawa na kuishi katika nyumba bila mlango,” asema Mukami. Kawira asema mume anafaa kuwa mlinzi wa mke, watoto na mali.

“Mume sio suti, mume ni zaidi ya kuwa na gari, sura nzuri na kumnunulia mkewe zawadi. Mume ni ngao ya mkewe na familia. Ukipungukiwa na ujasiri, unajiweka katika hatari ya kukosa mke,” asema Kawira.

Watalaamu wanasema wanawake wanaofahamu vigezo halisi vya mume bora huwa wanachunguza iwapo wanaowachumbia ni jasiri.

“Mwanamume jasiri huwa anajiamini na kwa kufanya hivyo, anaweza kufanikiwa. Mwanamume jasiri anaweza kuwa mfano mwema kwa wanawe,” aeleza Omboki.

Lakini Kawira anashauri wanawake kutofautisha aina za ujasiri akisema wanaweza kudhani mwanamume ni jasiri lakini awe katili.

“Hata unapotafuta mwanamume jasiri, chunga usiangukie katili atakayefanya maisha yako kuwa jehanamu. Wanawake wengi huwa wanakosea na hatimaye kujuta,” aeleza Kawira.Omboki anakubaliana na kauli hii akisema baadhi ya wanawake huwa wanajuta kwa kuolewa na wanaume katili wakidhani wamepata walio jasiri.

“Ni muhimu kufahamu chanzo cha ujasiri wa mtu. Kuna ujasiri unaotokana na elimu, mali, imani ya dini na kuna ujasiri wa kipumbavu pia wa kutumia kifua. Kuna watu jasiri lakini hawana hekima. Hao ni hatari,” aeleza.

Kulingana na wataalamu, mume anafaa kulinda mke lakini sio kuwa tishio kwake. Damaris* mwanadada mwenye umri wa miaka 28 anasema alidhani mumewe angekuwa ngao yake lakini akamkosesha amani kwa kumdhulumu kila wakati.

Shoo ya #WifeMaterial yamtia Eric Omondi matatani

Na SAMMY WAWERU

Mcheshi maarufu Eric Omondi amejipata matatani kutokana na shoo yake ya #WifeMaterial. Shoo hiyo tata imekuwa ikimhusisha na wanawake kadhaa, ambapo amekuwa akionekana akiwabusu na kuwakumbatia hadharani, kupitia video na picha anazopakia kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

#WifeMaterial, kulingana na machapisho ya Erico, imekuwa droo ya mashindano ya “mwanamke bora kwenye ndoa”, na ambayo kilele chake kilikuwa mnamo Jumatano, Desemba 23, 2020 alipotangaza mshindi.

“Na mshindi ni…” mvunja mbavu huyo tajika akachapisha katika kurasa zake za mitandao.

Jumatano hiyohiyo, Omondi alipakia video anayoonekana akiwa na ng’ombe jijini. “Vile tunapeleka mahari kwa kina mshindi wa #WifeMaterial,” yanasema maelezo ya video hiyo.

Shoo hiyo imeonekana kughadhabisha Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Kukagua Filamu Nchini (KFCB), Dkt Ezekiel Mutua, akiitaja kama “iliyooza, potovu na inayochangia utovu wa maadili kwa wasichana”.

“Kuna Corona, lakini huyu ‘mjinga’ amekuwa akibusu wasichana kadhaa, akinasa video kwa madai anaigiza. Msosholaiti mwingine naye, aliyepotoka anarekodi video zaidi akifunza wasichana wadogo jinsi ya kufanya mapenzi na Omondi kupitia programu ya kishetani inayojulikana kama ‘Mombasa Raha’…” ameeleza Dkt Mutua.

Akionekana kukerwa na tabia za Erico, Afisa huyo mwenye msimamo mkali kuhusu masuala ya filamu na uigizaji nchini, anataja studio ya mchekeshaji huyo iliyoko mtaani Lavington, Nairobi, kama ngome ya kudhulumu wasichana kimapenzi na kuwashushia hadhi yao kwa madai ya kuimarisha sekta ya uigizaji.

“Huku mashirika ya kutetea haki za wanawake yakinyamaza na idara ya polisi kutokamata wahusika wa uhalifu huu, ni bayana kama jamii tumepotoka,” Dkt Mutua anasema.

Akiitaka idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) kukamata wahusika, anasema wakati taifa litapevuka kwa maovu hayo, athari ambazo zitakuwa vigumu kurekebisha zitakuwa zimetendeka.

Si mara ya kwanza Dkt Mutua kutofautiana vikali na Eric Omondi, akimtaka kuwa kielelezo na mfano mwema katika jamii kupitia umaarufu wake kwenye uigizaji.

Mitandaoni, kuna baadhi ya wanaosifia shoo ya Erico na wengine wakimkashifu.

“Erico usiombe yeyote msamaha, tuko kwenye dunia huru, hukulazimisha yeyote kushiriki. Wasichana walijitolea kushiriki mashindano kwa hiari yao…” anaeleza Adrian Akasha.

“Tunataka hatua ichukuliwe mara moja, hatutaki mazungumzo,” #Makori Douglas anapendekeza.

“Erico anaonekana kupambana na msongo wa mawazo baada ya mchumba wake wa Kiitaliano kumuacha,” #Chepngeno Benta anadai.

Siombi radhi, Wambua ni dume katili, Nzilani sasa asema

NA PIUS MAUNDU

Kwa mtu aliyejipata katikati ya zogo la kifamilia lililosambaa kote nchini, Jackline Nzilani anaonekana mwenye utulivu mwingi na mwenye roho ya kuwakaribisha watu.

Anaonekana mwenye upole na nafsi yake, hata ingawa ametuhumiwa kumsingizia aliyekuwa mume wake, Julius Wambua huku akimsababishia kufungwa gerezani nusura mwongo mzima.

Akiwa amevalia jaketi nyekundu, blauzi nyeupe na kufunga kitambaa chekundu kichwani, mama huyu mwenye watoto watano anatuongoza kule anakoishi Nairobi kwa ujasiri.

“Siogopi chochote na sijutii kile kilimfanyikia Wambua. Niko tayari kukabili korti na kutoa ushahidi na kuapa kuwa sikumshauri Mwende, mtoto wake adanganye,” asema Bi Nzilani mwenye umri wa miaka 46 anapoketi ili tumhoji.

Mara kwa mara anakatizwa na mwanawe mwenye umri wa miaka mitatu ambaye alimpata na mume aliye naye sasa. Mtoto huyu wa kijana anataka kuwekewa chai na hajui vile maisha ya kale ya mamake yalivyovutia vyombo vya habari.

Bi Nzilani ameshtakiwa kwa kumshauri mwanawe kudanganya kortini kuwa aliyekuwa mumewe alimdhulumu kimapenzi. Bi Nzilani anayejieleza kwa lugha ya Kiswahili iliyo na lafudhi ya lugha ya Kikamba, anasema yaliyo moyoni wake bila kujali huku akiwa haonyeshi hisia zozote za kujuta. Kwake maisha yanaendelea kama kawaida.

Alisimulia Taifa Leo Dijitali kuhusu kadhia za ndoa yake na mumewe Wambua na dhuluma ya kingono kwa bintiye ambayo anasimulia kwa urahisi mwingi kana kwamba yalifanyika jana.

Alisema hajutii hata kidogo kuhusu kufungwa kwa Wambua lakini anajutia hisia ya ‘kusalitiwa’ na watoto wake wawili wa kike; Mwikali na Mwende.

Bi Nzilani ambaye kwa sasa anafanya kazi kama kijakazi, anakumbuka alivyopigiwa simu na mwanawe wa pili, Musyoki ambaye alimweleza kuhusu alivyokiri Mwende.

Musyoki angemletea gazeti, ambalo bado analo, ya alichokiri Mwende huku akisema kuwa, alichokubali Mwende kilitokana na kumkataza kuacha shule ili aolewe.

“Tulikuwa tunaishi karibu. Mwikali na Mwende walikuwa wanaishi pamoja baada ya kumtaliki mume wake wa kwanza. Hapo ndipo mpango ukapangwa na nikagundua wakati ambapo nilianza kupata simu kutoka runinga ya Citizen,” anakumbuka.

Hata hivyo, Nzilani anasema kuwa hata ingawa Bw Wambua ameachiliwa, hataki kumuona tena kwani hakuna mapenzi kati yao.

“Siombi msamaha na hakuna radhi nitaomba kwani ushuhuda niliotoa bado ni wa kweli na alimbaka Mwende. Sikuwahi kumtembelea akiwa gerezani na siko tayari kurekebisha uhusiano baina yetu. Nishaendelea na maisha yangu,” akasema.

Kipande cha uchungu wake kinatokana na uhakika kuwa ndoa yao ilikuwa imegubikwa na mikasa mingi ambako alipigwa mara kwa mara na aliyekuwa mume wake wakati huyo.

Anakumbuka kuwa kile kilichoanza kama mapenzi matamu ya asali ya mwaka wa 1992 kiligeuka ghafla na kuwa shubiri huku vita vikichukua usukani kwa miaka 16 kabla ya kuivunja ndoa hiyo mwaka wa 2008.

Bi Nzilani anaonyesha kuwa Bw Wambua ni mwanamume mwenye matusi mengi, mwenye kutaka kudhibiti watu kwani angeangaza mienendo yake na alipokuwa na tashwishi alimgeukia na kumpiga.

Isitoshe, Nzilani haafikiani na uamuzi wa mahakama kuu ya kumuachilia Wambua kutoka gereza ya Kamiti kule ambako alipaswa kutumikia kifungo cha maisha.

“Korti haingemwachilia bila ya kushauriana nami. Niko tayari kurudi kwenye korti za sheria za Kithimani ili wasimame na ushuhuda wangu wa hapo awali. Sijifichi kutoka mtu yeyote,” akasema.

Kwake, ndoa yake haikuwa kitu angetamani kwa mtu yeyote kwani alikuwa anachapwa bila ya kutenda kosa lolote na hangeruhusiwa kutangamana na watu wowote kwa raha zake hata majirani.

Kwenda kanisa kulikuwa baada ya kuomba ruhusa. Anakanusha madai ya kuuza shamba la familia huku akisema kuwa ni bwana Wambua aliyeuza shamba hilo baada ya kumuoa mwanamke mwingine.

“Tulianza bila kitu hii ni baada yake kufukuzwa kutoka kwa nyumba ya mjomba wake. Tungelala kwa nyumba za majirani kwa kuwa hatukuwa na pahali pa kwenda. Ningevumilia kuchapwa lakini kile kilivunja ndoa yetu ni siku ambayo alinitishia mara kwa mara kuwa angeniua kwa panga. Hiyo ilikuwa mwisho. Niliondoka na sikuangalia nyuma.”

Baada ya kufika Nairobi,  Nzilani alijiunga na kanisa ya Wakorino baada ya kuwacha kwenda kanisa ya New Apostolic alipokuwa akishiriki akiwa mashambani.

Wakati Mwende alitoa ushuhuda wake, alimshtaki mamake kwa kumshauri kumsingizia babake. Bi. Nzilani hata hivyo anakanusha lawama hizo akisema hazina msingi.

“Sikumshauri Mwende kumsingizia babake. Tuliifuata ripoti ya daktari ambayo ilitoka katika hospitali moja ya kibinafsi jijini Nairobi,” akasema  Nzilani. Korti ilisikia kuwa Nzilani alibuni kesi hii ili kulipishia kile alipitia mikononi mwa bwana Wambua alipokuwa ameolewa naye.

Jaji George Odunga wa Mahakama ya Juu alisema kuwa alishawishiwa na ushahidi upya. Alihukumu kuwa kesi ya Wambua haikuhukumiwa vizuri na kuamuru kuwa kesi hiyo kusikizwa upya. Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) amesema kuwa hajaamua kama Wambua atahukumiwa upya kama alivyoagiza hakimu Odunga.

“DPP anapaswa kupitia kesi hiyo yote toka mwanzo na uamuzi uliotolewa kisha kuamua kama kesi hiyo itahukumiwa upya ama la kama alivyoagiza hakimu,” wakili wa DPP aliyejulikana kama Felista Njeru alieleza korti ya Kithimani, Jumatatu 21, 2020.

Jaji alimpa DPP mwezi kufanya uamuzi. Alikubali bwana Wambua kuachiliwa kwa dhamana iliyotolewa na mahakama kuu huku uamuzi wa DPP ukisubiriwa.

Kesi itatajwa Januari 25, 2021.

IMETAFSIRIWA NA WANGU KANURI

Mapenzi au utumwa?

NA BENSON MATHEKA

Kwa miaka saba, Jane amekuwa akimkwamilia Patrick akidai kwamba anampenda ingawa mwanamume huyo hawajibiki kamwe.

“Nampenda tu,” anasema.Mwanadada huyu amekuwa akipambana kivyake na hata kumsaidia Patrick akiwa na shida.“Nimeshindwa kumuacha ingawa hawajibiki.

Ninampenda sana hivi kwamba sidhani ninaweza kuwa au kuishi na mwanamume mwingine katika maisha yangu,” asema.Lakini licha ya kumkwamilia mwanamume huyo, maisha yake yanazidi kuwa magumu mno.

Patrick hajali kamwe na huwa anajigamba kwamba ana mpenzi anayemjali na asiyemsumbua kwa mahitaji ya hapa na pale kama wanavyofanya wanawake wengine.

Tabia ya Jane ni sawa na wanawake wengine wanaokubali kuwa watumwa kwa kuishi na wanaume wasiowajibika wakisingizia mapenzi. Kulingana na wanasaikolojia, wanawake wanaowavumilia wanaume wa aina hii huwa wanajiweka katika shida. “Ikiwa mwanamume hawajibiki, hata kwa masuala madogo, hatoshi mboga.

Kukwama kwa mwanamume kama huyo ni kujipalilia makaa,” asema Dinah Wangui Kamau, mtaalamu wa masuala ya mapenzi wa shirika la Love Care, jijini Nairobi.

Anasema uhusiano wa mapenzi haufai kulemea upande mmoja. “Uhusiano wa kimapenzi na maisha ya ndoa yaliyokolea mahaba hayafai kulemea upande mmoja na hasa mwanamume anafaa kuwajibika kwa mtu wake. Ikiwa hafanyi hivyo au ukiona dalili kwamba mtu wako hana nia ya kufanya hivyo, jinusuru mapema,” asema.

Ivy Kamene, mwanadada mwenye umri wa miaka 28 asema kwamba alipoteza miaka mitatu katika uhusiano na mwanamume ambaye alikuwa kama kupe kwake.

“Nilimpenda lakini hakutambua kwamba kuna mahitaji ya mwanamke ambayo mwanaume anafaa kutimiza bali na burudani chumbani. Hakuwahi kunionyesha dalili za kujiimarisha maishani. Niliamua kumuacha baada ya juhudi za kumshauri abadilike kugonga mwamba,” asema Kamene.Wangui anasema wanaumewasio wajibika, huwa na maneno matamu na vitendo vichache.

“Ninamaanisha wale ambao wana uwezo wa kutimiza majukumu yao na hawafanyi hivyo. Wanapenda raha na starehe lakini hawajali wapenzi wao na hata watoto wao. Huwa ninashauri wanawake kutowavumilia wanaume kama hao hata kama ni magwiji wa kuwapandisha mizuka chumbani,” aeleza Wangui.

Upofu wa mapezi

Kulingana na Dkt Silas Oponyi, mwanasaikolojia wa kituo cha Big Hearts, jijini Nairobi, mwanamume asiyewajibika kwa mpenzi wake au familia yake akiwa na uwezo wa kufanya hivyo, ni hatari mwanamke kumkwamilia akidai anampenda.

“Mapenzi ya aina hii ni upofu wa kiwango cha juu. Ni hatari, yanaweza kuathiri maisha ya mwanamke na kumkosesha raha. Unawezaje kuvumilia mwanamume asiyejali mwonekano wako kwa kukupa pesa za saluni, kununua nguo na chakula? Utavumiliaje mwanamume asiyejali maisha yako ya siku zijazo na watoto wako?” auliza Dkt Oponyi.

Wangui na Dkt Oponyi wanaonya wanawake dhidi ya kusukuma wanaume wapenzi wao kuwajibika kwa mambo yanayopita uwezo wao.

“Kumsukuma au kutarajia mchumba wako akufanyie mambo yanayopita uwezo wake si sawa. Kunaweza kumsababishia mateso ya kisaikolojia na kuvuruga mambo zaidi,” asema Oponyi.

“Uwajibikaji katika uhusiano wa kimapenzi una mipaka kwa kutegemea uwezo wa mhusika. Makosa ambayo baadhi ya watu hufanya ni kuiga wanavyofanyiwa watu wengine na wachumba wao na kulaumu wapenzi wao kwa kutowajibika ilhali hawana uwezo wa kufanya hivyo,” aongeza Wangui.

Wataalamu hawa wanakubaliana kwamba ni jukumu la mwanamume kuonyesha mchumba wake mwelekeo na kuwa na maono ya siku zijazo.

“Hakuna mwanamke anayefaa kuvumilia mwanamume asiye na maono. Hata hivyo, maono yakikosa kutimizwa kwa sababu zisizoweza kuepukika, haimaanishi amekosa kuwajibika,” asema.

Washauri wa masuala ya mapenzi wanakosoa wanawake wanaowatema wanaume uwezo wao wa kuwajibika unapopungua. “Ikiwa mwanamume amepoteza kazi au mapato yake yakipungua, hawezi kufananishwa na bwege asiyetosha mboga,” asema Wangui.

Afunguka jinsi maisha yalimtesa, mama yake akiolewa na wanaume 10 tofauti

Na SAMMY WAWERU

Nicholas Muturi ni mwingi wa tabasamu, furaha na bashasha unapopata fursa ya kutangamana naye.

Ni mkwasi wa ushauri na nasaha hasa kwa wanafunzi na vijana kwa jumla, ujumbe ukiwa; “Licha ya magumu au mazito unayopitia ama kukumbana nayo, Mungu yupo na ipo siku atarejesha tabasamu yako.”

Ni hulka ambazo zimeficha mengi ambayo Nicholas Muturi amepitia, ila sasa ana kila sababu ya kutabasamu na kuwa kielelezo katika jamii.

Yeye pamoja na dadake mdogo, mzawa, ni mayatima, na Muturi anaungama “Mungu ndiye mama na baba wa wasio na wazazi”.

Alizaliwa mnamo Aprili 24, 1992, katika Kaunti ya Kirinyaga, mwaka anaosema kwamba mamake alikuwa angali mdogo sana kiumri. “Alinizaa akiwa na umri mdogo mno, miaka 14,” anasema.

Anafichua, alikuwa katika darasa la saba wakati huo, na alilazimika kuacha masomo, ili kuitika wito wa majukumu ya ulezi.

Hata ingawa kufikia sasa kutambua au kujua babake mzawa imekuwa kitendawili kilichokosa mteguzi, Muturi anasema mamake hakuwa na budi ila kuolekea aliyemtunga ujauzito, yaani babake.

Hata hivyo, Muturi anasimulia kwamba ndoa hiyo haikudumu kwa kile anataja kama “baba kushindwa kutukithi riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi”.

Hatimaye, hakuwa na budi ila kurejea nyumbani, na kwa mujibu wa simulizi yake wakati huo Muturi alikuwa na umri wa miezi kadhaa pekee.

“Baadaye mama aliolewa kwa mwanamume mwingine, ambaye ni baba mzazi wa dadangu. Ndoa hiyo ilidumu muda wa miaka mitatu pekee,” anafichua, akisema wakati wa wawili hao kuachana alikuwa na miaka minne na nusu.

Kulingana na Muturi, utengano huo kwa kiasi fulani uilikuwa wenye sarakasi na drama.

Anasema kilichoanza kama mzaha, mama kutorejea nyumbani siku na wiki kadhaa kwa sababu ambazo hazikiueleweka, kiliishia baba yao kuwapeleka kwa kina nyanya, mama aliyezaa mama yao.

Nicholas Muturi, kijana mkakavu na mcha Mungu aliyepitia mengi maishani. PICHA/ SAMMY WAWERU

Siku iliyofuata, anasema nyanya aliwarejesha kwa baba yao tena, ikawa kana kwamba “wanarushiana watoto”.

Hatimaye, nyanya hakuwa na budi ila kuwaitikia baada ya baba yao kuwarejesha tena, na mara hiyo kuwaacha nyuma ya nyumba ya nyanya usiku. “Kwa huruma, nyanya alituchukua na siku chache baadaye, mama alitujia ambapo tayari alikuwa katika ndoa nyingine, baba wa tatu,” anaelezea.

Baba wa tatu, anamtaja kama “Baba wa ajabu”. “Mchana alikuwa mhudumu wa buchari, na usiku alishiriki uhalifu. Ninakumbuka, nikiwa darasa la pili alikamatwa baada ya kushiriki wizi, na alipofikishwa kortini na kushtakiwa akapatikana na hatia ambapo alihukumiwa kuhudumu kifungo kirefu cha jela,” anafichua.

Ni hatua ambayo ililazimu mamake kuwarejesha kwa nyanya tena, kwa sababu hakuweza kumudu kuwakimu riziki.

Muturi anaendelea kueleza kwamba, maisha humo hayakuwa rahisi. Walilazimika kulalia tandiko la gunia, kwa kuwa mamake asingemudu kununua kitanda na godoro. Ilikuwa hali ngumu kwa watoto wenye umri mdogo, Muturi akidokeza kwamba waliugua Homa mara kwa mara.

“Ndoa iliyofuata, ilikuwa ya mwanaume aliyeonekana kuwa nadhifu, ila iliishia kuwa ya dhuluma kwa dadangu bila ufahamu wa mama. Nikiwa darasa la tano, waliachana,” Muturi anasema.

Ni matukio yaliyoendelea kwa muda, akikadiria kina baba aliopitia mikononi mwao ni zaidi ya 10, watatu kati yao wakiuawa kwa sababu ya kushiriki uhalifu.

Aidha, ni kutokana na maisha magumu Muturi na dadake walipitia, aliamua kukaza kamba masomoni. Nyakati zingine, wawili hao walilala njaa.

Huenda mamake barobaro huyu alichohitaji ni kuwa na familia kamilifu, yaani yenye baba na mama, ili watoto wawe na kielelezo lakini ndoto zake hazikuafikika.

Licha ya magumu maishani aliyopitia, ikiwemo kukosa chakula na karo kukata kiu cha masomo, ameibuka kuwa mshindi. PICHA/ SAMMY WAWERU

Kulingana na Mwinjilisti Janet Esther, ambaye ni mshauri nasaha wa masuala ya ndoa, hakuna kitu muhimu katika malezi ya mtoto ama watoto, kama kuona wana kielelezo cha baba na mama.

“Kwa hakika, ni wachache mno wanaoridhia maisha ya singo fatha au singo matha. Ni matamanio ya mzazi kuona watoto wana mama na baba, ambao ni kioo katika jamii,” Mwinjilisti Janet anaelezea.

Kulingana na mtaalamu huyo, si rahisi kushawishi mtoto, hasa kumweleza kwa nini baba au mama hayupo. “Watoto wanapotangamana shuleni, husifia wazazi wao, mfano ‘utaskia mmoja akisema alicholetewa na baba au mama, ama ahadi alizopewa ikiwa atafanya vyema kwenye mtihani’,” anafafanua.

Huku watoto hao wakiendelea kupitia machungu, Muturi anasema alichokosa maishani ni “mwanamume ambaye angekumbatia kama baba”.

Licha ya lindi hilo la mazito aliyopitia, alitia bidii masomoni. Mwaka wa 2005 alifanya mtihani wa kitaifa darasa la nane, KCPE na kupata alama 313 kwa jumla ya 500, zinazowezekana.

Hata hivyo, mamake aliyetegemea vibarua vya hapa na pale, na ambavyo nyakati zingine vingekosekana, hakuwa na uwezo kumlipia karo kujiunga na shule ya upili.

Isitoshe, nyanya aliugua na familia ambayo angeitegemea kumpiga jeki kimasomo, ilijikakamua kuokoa maisha ya nyanya.

Muturi anasema hakuwa na budi ila kurudia darasa la nane, ambapo mwaka mmoja baadaye alipata alama 365. Mwaka huohuo, 2006, ndio nyanya aliaga dunia.

“Mambo hayakuwa rahisi, mara nyingi nilikosa chakula cha mchana ila matumaini yangu niliyaelekeza kwa Mwenyezi Mungu,” anasimulia.

Anasema licha ya kufanya bora katika KCPE awamu ya pili, hakukuwa na pesa kumuwezesha kujiunga na shule ya upili.

Alikawia kujiunga na kidato cha kwanza, na ni kupitia ukodeshaji wa kipande cha shamba mamake alikuwa amepewa alifanikiwa kuingia shule ya upili. Muturi anasema masomo yake yalifadhiliwa kupitia mgao wa Hazina ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF).

Kiu cha kupata elimu, hakikukatizwa na changamoto chungu nzima alizopitia. “Kidato cha nne, nilifanya KCSE mwaka wa 2010 nikazoa B- na kwa sababu matokeo hayo yasingeniwezesha kujiunga na orodha ya wanaofadhiliwa na serikali kiwango fulani cha karo, niliamua kurudia, kupitia ufadhili wa bodi ya shule nilyosomea,” anaelezea.

Jaribio la pili 2011, Muturi anasema alizoa alama ya B+, na ambapo 2012 alipata nafasi kujiunga na Chuo Kikuu cha Masuala ya Sayansi na Teknolojia Meru, akasomea Shahada ya Hisabati, Kompyuta na Sayansi.

Anasema masomo yalifadhaliwa na wanajamii na walimu wa shule ya upili aliyosomea.

“Wakati huo mama alifanya kazi kama mhudumu wa baa. Nikiwa mwaka wa kwanza chuoni, alipatikana na Saratani, akalazimika kuacha kazi, akaingilia vibarua vya kuchuhuma majanichai,” anadokeza, akisema ni hatua iliyomlazimu kuacha masomo mwishoni mwa mwaka wa pili chuoni, ili kumtunza, hali yake kiafya ilipoanza kudhoofika.

Kijana huyu anasema akiwa chuoni, mamake alikuwa wa msaada mkuu. Hata hivyo, Desemba 2014, alifariki, Muturi na dadake wakaachwa watoto yatima. Aliaga dunia mwaka ambao dadake alifanya KCSE, na kuzoa alama B-.

“Tumeng’ang’ana, na kufikia tulipo ni kwa neema za Mungu,” anaeleza barobaro huyo mcha Mola.

Muturi kwa sasa ni mwalimu wa shule ya upili ya kibinafsi ya St. Joan’s Murang’a Girls. Isitoshe, anasema ni mwanachama wa Shirikisho la Kitaifa la Kikristo la Wanafunzi (KSCF), linalotoa mafunzo ya nasaha na ushauri kwa wanafunzi katika shule mbalimbali nchini.

Barobaro huyu anayehimiza wazazi kupenda watoto wao, licha ya pandashuka wanazopitia, ametunga vitabu vyenye mafunzo na kufariji, na ambavyo anasema anaendelea kuvisambaza katika shule mbalimbali, baadhi yavyo akivitoa bila malipo.

Vitabu hivyo alivyotunga kwa lugha ya Kiingereza, vinajumuisha: God is not done with you yet, Dark pasts brighter tomorrow na Redefining your life.

Ni mtunzi wa vitabu mbalimbali vya kufariji na mafunzo. PICHA/ SAMMY WAWERU

Vingine ni: The Three Pillars of A Believers’ Life, In The Mind of a New Believer pamoja na The Dawn of Salvation, ambapo kufikia sasa amesambaza zaidi ya nakala 5,000.

“Katika shule ya upili, nyakati zingine nililala njaa. Sikufa moyo kuafikia ndoto zangu. Ninalenga kuwapa moyo wanafunzi na vijana wanaopitia changamoto, Mungu ni mwaminifu, hatowaachilia,” anahimiza.

Nicholas Muturi anaungama ameshuhudia ufanisi maishani kupitia neema za Mwenyezi Mungu, kuanzia akiwa kinda hadi kukomaa kwake.

Aidha, anasema malengo yake ya mwaka ujao, 2021, ni kurejea chuo kikuu kuendeleza azma yake kukata kiku cha masomo.

Wakati wa mahojiano na Taifa Leo, alifichua kwamba atajiunga na Chuo Kikuu cha Mt Kenya, kusomea Shahada ya Elimu (Somo la Hisabati na Kemia).

‘Mke wangu mtamu ila tamaa itaniua…’

NA PAULINE ONGAJI

“Nimeshindwa kabisa kutulia na mwanamke mmoja kwani licha ya kuwa nimeoa na napata kila kitu mwanamume anahitaji katika uhusiano, bado najipata nikiwa na msukumo wa kurambaramba vya kando.

“Mke wangu ananifanyia kila kitu, na kusema kweli sipangi kumuacha hata siku moja, kumaanisha kwamba nafanya kila niwezalo kulinda penzi letu. Hata hivyo, nimeshindwa kupunguza kiu ya kuwaonja wanawake wengine huko nje.

“Starehe zangu hizi, mimi huzifanya siku na masaa rasmi ya kazi ili mke wangu asije akanishuku.

“Kwa hivyo, japo nina pesa nyingi, vituko vyangu hivi mimi huviendesha jijini Nairobi, na hasa katika maeneo ya haiba ya chini; sehemu ambazo hakuna anayeweza kunishuku.

“Mbali na hayo, kila ninapoagana na binti kukutana mahali fulani, siwezi enda na gari langu, na badala yake mimi hutumia teksi na kuhakikisha kwamba naacha afisini kila kitu kinachonitambulisha.

“Japo nina wapenzi wa kando, naheshimu nyumba na ndoa yangu ambapo sijawahi kumpa mke wangu nafasi ya kutoniamini.

“Na sio kwamba nataka kuridhishwa na yeyote ninayemuonja. Nia yangu ni kutaka kujua tu iwapo nitampata mwanamke mwingine mwenye uzuri sawa na wa mke wangu; kimaumbile, kitabia na hata kimahaba.

“Lakini katika miaka yangu hii yote ya shughuli hii, sijampata hata anayekaribia robo ya wema na uzuri wa mke wangu.

Kwa hivyo nitazidi kutafuta, na hata nikimpata, sio kwamba nitamuoa au kuwa na uhusiano naye. Nia yangu itakuwa kuwaridhisha marafiki zangu wanaoogopa kuoa wakidai wanawake wema hawapo.”

Polo mtafuna yaya afumaniwa na mke wakati wa corona

KAPKATET, KERICHO

NA NICHOLAS CHERUIYOT

ILIBIDI polo wa hapa akubali kwa haraka kufanya kazi za jikoni ili kuokoa ndoa yake baada ya kufumaniwa akinyemelea yaya.

Tamaa ya jamaa ilivuka mipaka akawa anawatafuna yaya ambao mkewe alikuwa akiajiri.

Semasema za mtaa zaeleza kuwa, tangu kuzuka kwa corona, jamaa alipewa likizo ndefu na kampuni anayoifanyia kazi lakini mkewe akawa bado anaendelea kufanya kazi.

“Mke akienda kazi jamaa alibaki nyumbani pamoja na mtoto wao na meidi. Mkewe alihofia kuwa mumewe alikuwa akimnyemelea meidi ndipo akaanza kuwa mpekuzi wa mambo sana,” mdaku akaarifu.

Juzi mkewe alitoka kazini mapema na kumfumania mume akimpapasa yaya jikoni. Wawili hawa walitengana ghafla nusura wamwage chakula kilichokuwa motoni.

Yaya huyo alipigwa kalamu mara moja na mwingine akachukua nafasi yake siku iliyofuata.

“Nimemtafuta asiye na sura wala mwili wa kuteka hisia za mume wangu lakini bado niko macho,” mrembo alinukuliwa akiambia mashogake.

Mambo yalizidi unga hata zaidi alipofika nyumbani na kuripotiwa na yaya kuwa mumewe alimtongoza mchana kutwa.

“Hakuniacha nifanye kazi leo. Alinifuata akiniambia maneno ya kimahaba lakini nilimpuuza na kudinda kumtimizia tamaa yake,” kidosho alimshtaki jombi.

Mkewe alivunjika moyo sana na baada ya kuwaza na kuwazua, akaamua kuwaita jamaa za mumewe kuokoa jahazi lisizame.

“Iliamuliwa kikaoni kuwa yaya afutwe na mzigo wa kazi za jikoni utwikwe jombi naye akakubali kufanya hivyo ili mke asimtoroke,” mdaku akasema.

Kwa sasa jamaa huonekana akijikaza vilivyo kwa kazi za upishi, kutunza mtoto, kupiga deki na kuosha vyombo kila siku.

Familia yateta chifu kuagiza warudishe mahari

Na MAUREEN ONGALA

FAMILIA katika kijiji cha Muhoni, eneobunge la Ganze imemkashifu chifu wa eneo hilo kwa kuwaagiza kurudisha mahari ya Sh34,000.Familia hiyo imedai chifu wa Ganze, Thaura Mweni alipanga njama na mume wa binti yao kuwahangaisha.

Mnamo Februari, Bi Sanita Kitsao ambaye ni mama wa watoto sita alirudi kwao akidai kupokea vitisho kutoka kwa mume wake.

Kulingana naye, mumewe alimlaumu kuwa mchawi na alipanga kumuua ndipo akaamua kurudi kwao na watoto wake wawili.

“Sitaki kurudi katika ndoa yangu kwa sababu mume wangu anadai nimeingizwa katika kikundi cha wachawi na baadhi ya jamaa zake kwa hivyo anataka kuniua. Pia sitarudisha mahari kwa sababu nimezaa watoto sita na mimi ndiye nimekuwa nikitafutia familia yangu riziki wakati huo wote,” akasema.

Kakake, Bw Lemmy Jefwa alisema chifu aliandaa mikutano mingi kujaribu kuwapatanisha lakini mwanamume akasisitiza arudishiwe pesa alizolipa kama mahari.

Mkutano wa mwisho ulifanywa Ijumaa iliyopita.Alisema waliripoti kuhusu vitisho vya maisha ya dadake kwa kituo cha polisi cha Ganze.

“Ni wazi kuwa chifu ana ubaguzi. Familia inachukulia suala hili kwa uzito. Hatutaki baadaye tuje kusikia dada yetu aliuliwa akimrudia mume wake,” akasema Bw Jefwa.

Hata hivyo, chifu alitetea msimamo wake na kusema ni utamaduni katika jamii za Mijikenda kwamba mahari inastahili kurudishwa wanandoa wakitengana.

Alisema uamuzi wake kuandaa vikao vingi kujaribu kupatanisha wanandoa hao ulikuwa kusudi ili mwanamke husika apate muda wa kuamua kama kweli anataka kuachana na mume wake au atamrudia.

“Mwanamke amekataa kurudi nyumbani kwake. Hatuwezi kuwalazimisha waishi pamoja na desturi ni kuwa anafaa kurudisha mahari ili mume wake aitumie kuoa mke mwingine akipenda, kwani bado angali ni kijana,” akasema Bw Mweni.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kilifi, Bw James Mugera alisema polisi wanachunguza suala hilo.

Kulingana na Bi Jefwa, mumewe amekuwa akimpiga sana katika ndoa na wakati wote visa hivyo vilikuwa vikitatuliwa kwa mashauriano ya wazazi wake ambao walikuwa wakiwapatanisha.

WANDERI: Usiishi katika ndoa isiyo furaha ukihofia jamii, dini

Na WANDERI KAMAU

MOJAWAPO ya hatua kuu katika maisha ya mwanadamu hapa duniani ni ndoa. Ndoa huchukuliwa kuwa hatua muhimu sana kuliko zingine, ambazo ni kuzaliwa, tohara na kifo.

Ndoa huwa na uzito mkubwa kwani huathiri mustakabali wa mwanadamu katika muda wa maisha yake atakayohudumu kama mzazi.

Katika mila za Kiafrika, ndoa ndiyo chemichemi na mwanzo wa ukoo, ambao baadaye hukua na kuwa jamii kubwa iendelezayo uzao wa kizazi husika.

Hivyo, tangu enzi za mababu zetu, ndoa ni taasisi muhimu sana katika jamii za Kiafrika hadi sasa.

Lakini licha ya umuhimu wake mkubwa, taasisi hiyo inaonekana kuingia doa, hasa katika kizazi cha sasa.

Kinyume na ilivyokuwa awali, wanandoa wengi wanashambuliana wao kwa wao, baadhi hata wakiuana kutokana na sababu za mizozo ya kifamilia.

Athari za vitendo hivyo vya kusikitisha ni kuwa vinakatiza ndoto na malengo ya kimaisha ambayo wengi hulenga kuyatimiza.

Bila shaka, matukio hayo ya kuogofya ndiyo yamezua maswali na mdahalo mkali wa ikiwa ni kweli lazima mtu aoe au aolewe ndipo aonekane kuwa “mkamilifu” kwa mantiki ya taratibu ambazo zimewekwa na jamii.

Maswali yanayoibuka ni: Je, ndoa ina umuhimu wowote katika maisha ya sasa? Je, jamii itamkumbatia atakayekiuka kanuni zilizowekwa kuhusu ndoa? Lengo la awali la taasisi ya ndoa limebadilishwa na maisha ya kisasa?

Kulingana na mwanafalsafa Aristotle, lengo kuu la mwanadamu kuishi hapa duniani ni kupata furaha.

Hili ni katika kazi ama shughuli zozote za kimaisha azifanyazo—iwe ni kwenye usomi, uanabiashara, uanahabari, ualimu kati ya mengine.

Lengo kuu ni kupata furaha maishani, ambapo uwepo wa ndoa si jambo la lazima.

Vile vile, lengo lingine kuu ni kuhakikisha kuwa mwanadamu, kama sehemu ya uumba wa Mungu, ametimiza wajibu aliokusudiwa hapa duniani.

Mwanafalsafa Voltaire naye anasema kuwa mkasa mkuu katika maisha ya mwanadamu ni kufariki akiwa hajatimiza yale aliyokusudiwa kuyafanya hapa duniani.

Kwenye maisha yake, Voltaire, aliyeishi Ufaransa, aliamini kuwa ingawa ndoa ni mojawapo ya maagizo makuu aliyopewa mwanadamu na Mungu kuyatimiza ili kuongeza uzao wake duniani, si lazima ijumuishwe kama mojawapo ya mambo makuu anayopaswa kuyazingatia.

Voltaire anashikilia kuwa lengo kuu la mwanadamu linapaswa kuhakikisha kuwa ametumia vipaji alivyopewa na Mungu kama uimbaji, uandishi, usomi, uchezaji kati ya vingine kuhakikisha kuwa wenzake wamefaidika.

Bila shaka, hizi ni baadhi tu ya nadharia kinzani ambazo zimekuwepo kuhusu fasiri kamili ya “ukamilifu” wa maisha ya mwanadamu.

Kinaya ni kuwa, misimamo kama hii inatofautiana vikali na mafundisho ya kidini, yanayosisitiza kuwa lazima mume aoe mke ili kuendeleza uumba wa Mungu.

Haya ni muhimu, lakini lazima tusikubali kutesekea mikononi mwa mtu kwa kisingizio cha “kuheshimu” kanuni za kijamii ama kidini. Haifai hata kidogo kuishi kwa majonzi maisha yako yote eti kwa sababu haya ni mapenzi ya Mungu. La hasha! Ishi maisha ambayo yatakupa furaha.

akamau@ke.nationmedia.com

MILA NA DESTURI: Utoaji mahari na ndoa katika jamii ya Wasomali

Na FARHIYA HUSSEIN

farhiyahusseiny@gmail.com

ILIKUWA fahari kubwa Taifa Leo kupata kupata fursa ya kujumuika na jamii ya Wasomali eneo la Kaskazini Mashariki, Kaunti ya Garissa kushuhudia jinsi harusi zao za kitamaduni zinavyofanywa.

Makaribisho ni mazuri katika uwanja mmojawapo. Shangwe na vigelegele vinahanikiza huku sauti nyororo za kina mama wakiimba nyimbo za kitamaduni zikizidi kunogesha uhondo.

Tunapatana na Bw Deqow Ali na mke wake Bi Barwaqa Adow ambaye anamtayarisha binti yao atakayefunga ndoa siku chache zijazo.

Binti yao karibu ataolewa katika harusi ya kitamaduni.

Bi Adow anasema harusi ni mojawapo ya tamaduni muhimu zaidi kwa jamii ya Wasomali.

“Harusi kwetu huashiria umoja pale nyoyo za wawili wapendanao zinakuja pamoja kutengeneza uhusiano baina ya familia hizo mbili,” anasema Bi Adow.

Bi Barwaqa Adow akitayarisha chakula nje ya nyumba yake ya kitamaduni. Picha/ Farhiya Hussein

Wasomali wanafahamika kwamba wao ni wa Kishiti (cushites) na wanapatikana zaidi Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Asili yao inaelezwa kwamba ni wa kutoka mkoa wa Ogaden, Kusini mwa Ethiopia.

Wasomali zaidi ya 500,000 wanaishi Kaskazini Mashariki, Kenya.

Familia nyingi za Kisomali zinazopatikana nchini Kenya ni zile za Ajuran na Ogaden na lugha yao ni ya Kisomali.

Ingawa hivyo, kunao wengine ambao pia wanazungumza lugha ya Kisomali na wanaitwa Garreh lakini si Wasomali kamili kwa sababu wamechanganya damu ya Borana.

Wasomali hujulikana kuwa ni wafugaji hasa wa ngamia, mbuzi, kondoo, na ng’ombe.

Wakigawanywa katika makundi tofauti ya kikoo – clans – wanapatikana Hawiye, Degoodiya, Ajuuraan, Isxaaq na Ogaadeen .

Wengi wao hupatikana sana jijini Nairobi, Mombasa na sehemu za Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Bw Ali anaelezea kuwa kuna methali katika lugha ya Kisomali inayosema “bahati ni wakati fursa inakutana na maandalizi” na ndivyo huwa wanaashiria wanaoelekea kufunga ndoa.

Bibi arusi kutoka jamii ya Wasomali akivishwa kitambaa na wanawake wa jamii kama njia ya kumpokeza baraka kwenye maisha yake ya ndoa. Picha/ Farhiya Hussein

Anafafanua kwamba katika jamii ya Wasomali, utoaji wa mahari – Meher – hufanyika siku chache kabla ya harusi na wakati mwingine hufanyika siku hiyo ya ndoa.

Ukweli ni kwamba ni jambo linalohitaji mtu kujikusuru na kujitolea kikamilifu. Si rahisi kwa upande wa bwana harusi kwani anapaswa kushughulikia familia ya bi harusi na na kuitunuka zawadi.

Bw Ali (babake biarusi) na ndugu zake walipokea kutoka kwa familia ya bwana harusi zawadi ikiwa ni pamoja na mtoto wa ngamia, hela zilizofunikwa kwa kitambaa ghali na ngamia 20 kama malipo ya mahari.

“Kuna zawadi nne kubwa ambazo bwana harusi anapaswa kutoa. Ya kwanza tunaita, Gabaati ambayo inahusisha nirigi – mtoto wa ngamia – na kawaida huletwa na bwana harusi na baba yake wanapokuja kuomba bi harusi. Ya pili ni Yarad ambayo ni zawadi inatolewa siku ya utoaji mahari ya kuthamini biarusi (Kawaida ni pamoja na pesa zilizofunikwa kwa kitambaa ghali). Tatu, Sooryo; pesa wanazopewa wanaume wa familia ya biarusi ama ndugu au binamu. Na mwishowe, bwana arusi huleta ngamia kama shukrani kwa kuruhusiwa kumuoa yule biarusi,” akaelezea Bw Ali.

Lakini alieleza kadri siku zinavyosonga utamaduni unapotea polepole.

Zama zile, biarusi angetolewa ngamia 100 kama mahari lakini sasa bwana harusi anaruhusiwa kulipa ngamia 10 kama mahari.

Wasomali wana historia pevu ya ufugaji wa ngamia. Picha/ Farhiya Hussein

“Bila malipo ya mahari hakuna arusi ambayo itafanyika na ina maana kwamba biarusi anapaswa kuwa wazi juu ya kile anataka na bila shaka bwana arusi atawajibika na kukitoa,” akasema Omar Abdullahi, mmoja wa wazee wa baraza katika kijiji hicho.

Harusi za Wasomali, nyingi hufanywa kabla ya jua kutua na hufanyika maeneo ambayo kila mtu ambaye huwa amealikwa kwa tarehe iliyowekwa anaweza kufika.

Taifa Leo ilipata fursa ya kushuhudia ndoa ya bintiye Bw Ali.

Wanawake walijitokeza wakiwa wamevalia mavazi yao ya rangi ijulikanayo kama baati. Ni kubwa, na hung’aa (glitters) na hutengenezwa kwa hariri. Nguo hizo ni kubwa kiasi kwamba wanawake hushikilia upande mmoja wakati wa kucheza na kuimba.

Wanawake basi wanamsindikiza biarusi kuelekea kwenye chumba ambacho kimejengwa maalum kwa wanandoa hao wapya huku wakipiga makofi na kucheza wakati wanapiga ngoma.

Bwana arusi anaonekana amesimama kwa umbali nje ya chumba hicho.

Kisha kundi la wanaume linakuja polepole huku wakiimba nyimbo za sifa na kucheza wakielekea kwenye hicho chumba, ambapo bibi arusi yuko.

Ndani ya kile chumba kumetandikwa shuka ndefu chini. Bi arusi amekalishwa katikati huku wanawake wakimzunguka na kuimba.

Wanawake wengine hukusanyika nje ya chumba, wakiacha nafasi ya kutosha kwa wanaume wanaokaribia.

Wanaume kisha hufika pale, wakiongozwa na wazee wa kijiji wanamzunguka bwana arusi kama kundi la nyuki.

Ndani ya chumba hicho, wanandoa hao wapya wanapitia mila kadhaa ikiwa ni pamoja na Todoba Bax, Xeedho, Shaash saar.

Kutumia kitambaa kipepesi wanawake huweka kitambaa juu ya kichwa cha biarusi ambacho huashiria baraka na kumtakia heri katika ndoa yake.

“Hii inategemea na ukoo na mbari ambapo bwana arusi na biarusi hutoka. Wengine huoana kutoka katika familia moja. Kulingana na ukoo, wale wanaofunga ndoa wanaweza kuhusishwa kupitia wazazi wao. Kwa mfano, mama ya bwana arusi na baba ya biarusi wanaweza kuwa wa kutoka kwa tumbo moja,” akabainisha Bw Ali.

Katika jamii zingine nchini, hii inaweza kuonekana kama mwiko yaani taboo.

Utamaduni wa Kisomali pia unaruhusu mwanamume kuoa hadi wake wanne; hasa chini ya sheria za Kiislamu.

Ofisi ya msajili yasimamisha ndoa tena

Na BENSON MATHEKA

NDOA zote za kijamii zinazofanyika katika ofisi za msajili wa ndoa zimesimamishwa tena, siku mbili baada ya ofisi hizo kufunguliwa kwa umma.

Msajili Mkuu Mary Njuya alitangaza kuwa idadi ya watu waliojitokeza kutafuta huduma ilikuwa kubwa na kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona hazikuweza kuzingatiwa.

Huduma hizo zilirejelewa Jumatatu baada ya kufungwa Machi serikali ilipotangaza hatua za kuzuia kusambaa kwa corona.

“Kufuatia kufunguliwa kwa muda kwa baadhi ya huduma za ndoa katika ofisi ya msajili wa ndoa katika jumba la Sheria, idadi kubwa ya watu walijitokeza kinyume na sheria za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona. Kutokana na hilo, ofisi hii imesimamisha kwa muda tena huduma hizo ili kuweka mwongozo wa kuhakikisha kanuni za wizara ya afya kuzuia kusambaa kwa corona zinazingatiwa,” Bi Njuya alisema kwenye taarifa.

Serikali imesimamisha shughuli zote za umma ikiwa ni pamoja na ibada makanisani na arusi ambazo kwa kawaida zilikuwa zikihudhuriwa na watu wengi zimeathiriwa.

Hii inaweza kuchangia idadi ya watu wanaoamua kufanya harusi za kijamii.

Bi Njuya alisema huduma zitarejelewa baada ya hatua za kuzingatia kanuni za afya katika ofisi hizo kuwekwa.

RIZIKI: Hiki kinaweza kuyumba Mungu akakujalia kile

Na SAMMY WAWERU

BI Annitah Njeru ni mtulivu na mwenye tabasamu unapotangamana na kushiriki mazungumzo naye.

Ni mzaliwa wa Kerugoya, Kaunti ya Kirinyaga, na ni huko ndiko anakofanya kazi katika afisi ya usajili na utoaji wa vitambulisho, kazi anayosema aliipata kiurahisi, lakini baada ya kuhangaika kwa muda mrefu.

Mwanadada Annitah na ambaye ni mama wa mtoto mmoja – mwenye umri wa miaka minane – anasimulia kwamba pindi tu baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, 2006, alijiunga na taasisi moja ya mafunzo ya usektretari- uhazili – Nyeri, ambapo alisoma kwa muda wa miaka miwili.

Anasema hata baada ya kufuzu, haikuwa rahisi kupata kazi na hakuwa na budi ila kufanya vibarua vya hapa na pale, angaa kuzimbua riziki.

Vibarua vya kuchuuza nguo na hata kulima, vyote alivifanya, ili kuona analisukuma gurudumu la maisha.

Ni katika pilkapilka hizo, ambapo alikutana na mwanamume mmoja, anayesema kwamba walichumbiana kwa miezi kadhaa, kilele kikawa kuwa mume na mke.

“Nilitamani kuanzisha familia, na kulingana na ahadi zake alionekana mkomavu. Baada ya kujuzana kwa wazazi wa pande zote mbili, tulipata baraka zao tukaanzisha boma,” anaeleza.

Matunda ya ndoa ni kujaaliwa mtoto au watoto, na miaka miwili baadaye, walipata mtoto wa kike.

Annitah, 32, hata hivyo anasema mume wake alitamani kupata mtoto wa kiume, na hapo ndipo mgogoro kati yake na mume ulianza.

Kilichoanza kama mzaha mzee, akimaanisha mume wake, kufika akiwa ameshiba kilitunga usaha.

Kulingana na simulizi ya mama huyo, mavyaa na mashemeji zake walichangia kuchochea mumewe amuache, na hatimaye alimpa talaka. Binti wa wenyewe hakuwa na budi ila kurejea kwao, bila mbele wala nyuma.

Elizabeth Karungari, muuguzi mstaafu na mshauri wa masuala ya ndoa na familia, anasema changamoto za aina hiyo zinashuhudiwa mara kwa mara katika jamii, hasa ikiwa mume hataelewa kuwa huchangia kwa kiasi kikuu katika jinsia, wakati wa kujamiiana kutafuta mtoto.

“Mbegu za kiume kwa kushirikiana na za kike ndizo huamua jinsia ya mtoto. Si kisa kimoja au viwili nimetatua mume akilaumu mke kuzaa jinsia ambayo yeye (mume) hakutarajia,” Elizabeth anasema, pia akiongeza kuwa mume anapohusisha wanafamilia katika ndoa yake haswa masuala yanayoshirikisha mume na mke, uwekezano wa ndoa hiyo kudumu ni wa chini mno.

Kwa mujibu wa simulizi ya Annitah, mashemeji zake hawakutaka kumuona, kiasi cha kutafutia mumewe mke mwingine, tukio ambalo walilifanya hadharani.

“Wazazi wangu walinipokea. Walinisaidia kwa hali na mali,” anasema.

Mwaka mmoja baadaye, Annitah anasema aliingia kwenye ndoa nyingine. Hiyo nayo, hata ingawa hakujaaliwa kupata mtoto, ilijaa dhuluma na mateso, kwa anachotaja “mzee alikuwa mlevi kupindukia”. Aliamua kuondoka, miaka miwili baadaye, akihisi ameshiba vitushi na sarakasi za ndoa.

Mwanadada huyo anaiambia Taifa Leo kwamba 2015 alikumbuka ana vyeti vya usekretari, akaanza oparesheni ya kusaka kazi tena.

Japo halikuwa zoezi rahisi, anasema haikuchukua muda mrefu kupata nafasi ya kazi ya ukarani katika afisi ya usajili na utoaji wa vitambulisho Kerugoya, ambako anafanya kufikia sasa.

“Kila siku nilikuwa namsihi Mungu, asininyime ndoa na kazi. Alinijaalia kazi,” anadokeza, baraka anazosema zilimjia wakati alizihitaji kwa hali na mali, ikizingatiwa kuwa alikuwa na majukumu ya uzazi, kulea bintiye.

Kando na kazi ya kuajiriwa, Annitah ni mkulima eneo la Kirinyaga na pia anasema wikendi na wakati wa likizo hufanya uchuuzi wa nguo. “Huziendea jijini Nairobi, ninazichuuja muda wangu wa ziada kujipa pato la ziada,” anafafanua, akisema anapania kufungua duka, aajiri mfanyakazi atakayemsaidia kujiimarisha.

Isitoshe, mbali na baraka za kazi na biashara, anafichua kuwa amejaaliwa mchumba ambaye hivi karibuni kengele za harusi ‘zitapigwa’, kualika watu kusherehekea wakifunga pingu za maisha na kuonjesha waalikwa keki.

Pasta adinda kuombea polo aliyekataa kuoa bintiye

Na John Musyoki

OTHAYA, Nyeri

Pasta wa kanisa moja eneo hili, alishangaza waumini alipodinda kumuombea jamaa aliyekataa kuoa binti yake.

Penyenye zinasema jamaa alikuwa akimchumbia binti wa pasta huyo lakini kwa sababu ambazo hazikueleweka alikataa kumuoa na akafunga ndoa na mwanadada mwingine wa kijiji chao.

Siku ya kioja jamaa alikuwa ameugua na waumini wa kanisa wakamuomba pasta amtembelee nyumbani kwake akamuombee.

Pasta kusikia hivyo, alichemka na kuanza kulalamika akidai jamaa huyo alikuwa amemkosea sana.

“Maombi yana gharama yake. Nilikuwa na matumaini makubwa kwa jamaa huyo kwamba angemuoa binti yangu ila hilo halikufanyika. Jamaa huyo aliharibia binti yangu muda na simpendi. Kama mnamjali nendeni mkamuombee,” pasta aliwaambia waumini wake.

Waumini wa pasta huyo walishangaa na kumgombeza pasta huyo kwa kukataa kwenda kumwombea jamaa.

“Wewe ni pasta wa sampuli gani kama una wivu na roho ngumu kama chuma. Jamaa huyo alikuwa na haki ya kuoa msichana aliyempenda. Kumbuka wahenga walisema kuwa, kuchumbia sio kuoa,” mwanadada mmoja alimwambia pasta.

Hata hivyo waumini wa pasta huyo waliamini na kufunga safari ya kwenda kumwombea jamaa. Inasemekana baada ya siku chache, jamaa alipata nafuu na kurejelea hali yake ya kawaida.

Aliposikia pasta alikataa kwenda kumuombea, jamaa alisikitika sana na kusema pasta alikuwa akimlazimisha aoe binti yake.

“Nasikitika pasta anaweza kuwa na machungu kwa sababu nilikataa aliponilazimisha kuoa binti yake. Naona jambo la muhimu kufanya ni kuhama kanisa lake ili awe na amani,” jamaa alisema.

Haikujukana ikiwa jamaa huyo alihama kanisa hilo au la.

Demu afichua mumewe amemnyima asali kwa miaka 4

Na TOBBIE WEKESA

WANGURU, KIRINYAGA

Kipusa mmoja kutoka hapa aliwashangaza wengi alipodai ndoa yake haina ladha. Mwanadada huyo alidai kuwa tangu aolewe miaka minne iliyopita mumewe hajawahi kumgusa.

Inadaiwa aliitisha kikao cha dharura na wazee wa kanisa baada ya kugundua kwamba mumewe hakuwa akichangamkia tendo la ndoa.

“Miaka minne sasa imepita lakini hajawahi kunigusa kamwe. Hata kunikaribia kitandani hataki,” mrembo alidai.

Wazee wa kanisa walitulia huku kidosho akiendelea kutoa kauli zake.

“Tulipokuwa tukichumbiana aliniambia tusile tunda kwanza hadi tutakapooana. Sasa tumeoana na bado ananiambia ni mapema sana kula tunda,” kipusa aliendelea kusema.

Wazee wa kanisa walibaki kuangaliana huku wengine wakiangalia chini.

“Mimi nina hisia. Nitangoja hadi lini ilhali natamani raha ya ndoa?” kipusa aliwauliza wazee wa kanisa.

Waliohudhuria kikao hiki walibaki vinywa wazi. “Tulipoenda fungate, nilishangaa sana bwanangu aliponiambia hayuko tayari kuonja asali,” kipusa alisema huku akiketi.

Wazee wa kanisa walimrai polo ajitetee naye akadai mrembo anampeleka mbio.

“Huyu mwanamke aache mbio. Kila mechi huwa na maandalizi. Ningali najiandaa. Makombora yaja,” polo alidai huku vicheko vikishamiri. Duru zinasema kipusa aliinuka na kumshutumu jamaa kwa kutosema ukweli.

“Unajiandaa hadi lini? Ni mechi gani hii unayodai unajiandaa. Wewe sema ukweli,” kidosho alifoka.

Penyenye zinasema wazee wa kanisa waliwarai wanandoa hao kuwa na subira huku wakitafuta suluhisho. Hata hivyo mwanadada alisema hangesubiri na akaapa kumuacha jamaa iwapo wazee hawangesuluhisha suala hilo.

“Subira hadi lini. Mimi naomba kumpa huyu jamaa talaka. Hata kitandani analala na nguo. Sijui anaficha nini,” kipusa alitishia.

 

Afokea pasta kwa kumkataza kuoa kidosho

NA JOHN MUSYOKI

MATENDENI, EMBU

MUUMINI wa kanisa moja hapa alimkemea pasta kwa kukataa kumsaidia kutafuta kidosho mrembo wa kuoa katika kanisa lake.

Duru zinasema jamaa alikuwa amekosa kuoa na akaamua kuomba usaidizi kutoka kwa pasta. Hata hivyo baada ya kumrai pasta amtafutie demu kanisani, mchungaji alikataa na kumkera sana jamaa huyo.

Juzi jamaa alisikika akidai pasta alikuwa na maringo sana. “Sijui pasta huyu wetu ni wa sampuli gani! Nilimwambia kitambo anitafutie demu mrembo kanisani nimuoe lakini amenipuuza tu,” jamaa alisema kwa hasira.

Inasemekana watu walipigwa na mshangao mkubwa na kutaka jamaa huyo awafafanulie ni kwa nini alimtaka pasta amtafutie mwanamke wa kuoa kanisani.

Aliwajibu; “Kabla sijaokoka, pasta aliniambia nikikubali kutubu na kuacha dhambi atanitafutia msichana mrembo kanisani nimuoe. Sasa nimesubiri kwa muda mrefu na sijaona akishughulika. Wasichana wengi wameolewa nikiwa hapa tu na wamepungua sana. Nitasubiri mpaka lini?” jamaa alisema.

Hata hivyo waumini walipomdadisi pasta alidai kwamba jamaa huyo hakuwa amekomaa kuwa na mke. Alisema kuoa kunahitaji mtu kukomaa kiroho na hawezi kupendekeza mwanadada kuolewa na limbukeni katika imani.

“Bado kijana hajakomaa na itabidi asubiri hadi pale Mungu atakapojibu maombi yake,” pasta alisema.

Kulingana na mdokezi, pasta alishuku jamaa alikubali kuokoka ili kupata mke kanisani pekee.

Jamaa aliposikia hivyo alichemka zaidi na kuapa kugura kanisa la pasta huyo kwa kutotimiza ahadi yake.

Waumini walishuku huenda maneno ya pasta yalikuwa ya kweli. Hata hivyo haikujulikana kilichojiri baada ya kioja hicho.

Ataka idhini aoe mke wa nduguye

Na TOBBIE WEKESA

SINOKO, BUNGOMA

Kalameni mmoja kutoka hapa aliwashangaza wengi alipoandaa kikao kuomba idhini ya kumuoa mke wa ndugu yake aliyepotelea mjini kwa miaka mingi.

Inadaiwa polo aliandaa kikao hicho baada ya ndugu yake kupotea kwa boma na kumuacha mkewe akiwa pweke.

Duru zinasema ndugu ya polo hajaonekana kwa boma kwa zaidi ya miaka kumi tangu aondoke kwenda jijini.

Kulingana na mdokezi, polo alidai liandaa hafla hiyo kulingana na mila na desturi za jamii yake.

Inasemekana polo aliwaarifu wazee wa ukoo kuhusiana na mipango yake ya kumuoa mke wa ndugu yake rasmi.

Inadaiwa wazee walipinga mipango ya polo kwani walidai kwamba ndugu yake angali hai.

“Hatujapata habari zozote kuhusu kifo cha ndugu yako. Ni hatia kwako kumuoa mke wake,” mzee wa ukoo alimkashifu polo.

Inasemekana polo hakutaka kumsikiliza yeyote aliyejaribu kupinga mipango yake.

“Huyo jamaa ni kama hana haja na huyu mwanamke. Huyu mke amekaa kwa upweke huku akigongwa na baridi kwa muda mrefu,” polo alidai.

“Wewe tafuta mke wako uoe. Ndugu yako anaweza rudi wakati wowote,” mzee wa ukoo alimkaripia polo.

Polo alisisitiza kwamba mwanamke huyo alikuwa akiumia sana kwa baridi usiku ilhali yeye yuko..

“Huyu ndugu yangu alikuwa ameshapeleka mahari kwao. Mimi sitaki arudi kwao na aolewe kwingine. Ndugu yangu akirudi nitamrejeshea mke wake,” polo alidai huku vicheko vikishamiri.

Wazee walibaki midomo wazi. “Huyu jamaa anasema ukweli. Iwapo mwanamke amekubali kuolewa naye acheni aolewe. Hakuna haja kungoja mtu tusiyejua aliko,” mzee mmoja alisema.

Inadaiwa iliwabidi wazee kuondoka bila kutoa suluhisho.

Mke wa pili kumzika mume aliyefariki Februari

Na ANGELINE OCHIENG’

MJANE mmoja amepoteza haki ya kumzika mumewe wa ndoa baada ya Mahakama ya Kisumu wiki iliyopita kutoa amri mwendazake azikwe kwenye boma la mke wake wa pili.

Bi Siprosa Awino ambaye mumewe aliaga dunia miezi 11 iliyopita, aliwasilisha rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Kisumu akipinga uamuzi wa Hakimu Mkuu Mkazi Winfred Onkunya uliotolewa mwezi Juni wa kumruhusu mkemwenza Grace Were amzike mume wao marehemu Silivanus Nyang’wara Mwanja.

Bi Awino alidai kortini kwamba uamuzi huo haukufaa ikizingatiwa kwamba mashahidi wote walikuwa wamesema mwendazake azikwe kwake mtaani Nyalenda, Kisumu.

Kupitia wakili wake Bi Awino, haikuwa imebainika iwapo marehemu alikuwa na nyumba Kaunti ya Bungoma kulingana na mila na tamaduni za jamii ya Waluo jinsi ilivyokuwa ikidaiwa na mkewe wa pili.

Hata hivyo, Jaji Fred Ochieng’ alikataa ombi lake, akisema uamuzi na korti ya hakimu ilifaa kisha akatoa amri Bi Were aendelee na mazishi ya mumewe.

“Naunga mkono uamuzi uliokuwa umetolewa na korti ya hakimu kwa kuwa uliambatana na ushahidi uliotolewa. Rufaa hii imefeli kwa hivyo imepuuziliwa mbali,” akasema Jaji Ochieng’.

Jaji huyo pia alisema mapenzi na matamanio ya marehemu yanafaa kutimizwa huku akishikilia kwamba alikuwa na maboma mawili; Nyalenda na Bungoma na aliyajenga kwa kutimiza mila ya Waluo ya kubeba shoka, jembe na panga wakati wa kuweka msingi wa nyumba hizo.

“Uamuzi wa marehemu wa kuzikwa nyumbani kwake Bungoma si kinyume cha sheria za Kenya au tamaduni za Waluo,” akaongeza. Mwili wa marehemu Bw Nyang’wara umekuwa ukihifadhiwa kwenye mochari ya hospitali Life Care mjini Bungoma tangu kifo chake Februari 2, 2019.

Wakati wa mauti yake, alikuwa amekosana na Bi Awino na hawakuwa wameishi pamoja kwa muda wa miaka 28.

Kalameni aoa wake wengi ili asifiwe

Na TOBBIE WEKESA

KETEBAT, TESO

Kalameni alishangaza ndugu zake alipowaambia kuwa anataka kuoa wanawake wengi kama babu yake.

Kulingana na mdokezi, jamaa aliaandaa mkutano wa familia na kuweka wazi mipango yake.

Alitoa tangazo hilo na kuwajuza kwamba sababu yake kuu ni kutaka kufata nyayo za babu yake aliyekuwa jogoo kijijini.

“Ninataka kusema hivi. Babu yetu aliheshimiwa sana kwa sababu alikuwa na wake wengi. Hiyo heshima lazima tuidumishe,” alianza kwa kusema.

Ndugu zake walibaki vinywa wazi. “Lazima nimfurahishe babu kwa kufuata nyayo zake. Yeyote atakeyeniletea pingamizi tutakabiliana ipasavyo,” kalameni aliendelea.

Duru zinasema kabla ya kuitisha kikao hicho tayari kulikuwa na lalama kutoka kwa wake zake wa sasa, kwamba amewatelekeza.

“Kwa sasa uko na wanawake watatu, wote wanalalamika. Eti bado unataka kujiongezea wengine ili kufuata nyayo za babu. Utafaulu kweli?” jamaa aliulizwa na kaka yake mmoja.

Alipuuzilia mbali madai hayo. “Kila mwanamke ana shamba lake. Wako na nguvu za kulima ili wajitafutia chakula na mazao mengine ya kuuza sokoni wapate mapeni kidogo.

“Shida yao ni kulalamika tu. Kama babu alifaulu mbona nisifaulu,” kalameni alijibu kwa ukali.

Isitoshe, jamaa aliwakanya dada zake dhidi ya kuungana na wake zake hao watatu kuhujumu mipango yake.

“Ninajua wengine hapa wamesikia juma lijalo ninaleta mke wa nne. Tayari wameshaanza kueneza fitina kwa wake zangu. Komeni kabisa,” jamaa aliwaonya.

Akina dada hawakufurahishwa na vitisho hivyo.

“Ukijitakia sifa kama za babu kutokana na kuwa na wake wengi, sisi hatuna shida. Lakini huu upuzi na ujinga wa kutuzomea peleka kwingine,” walimkemea ndugu yao.

Muda si muda mkutano ukiendelea, wake wa jamaa walifika ghafla kikaoni na kumkabili.

“Anajifananisha na wazee wa zamani bila kujua nyakati zimebadilika. Anajifanya tu lakini hawezi lolote,” wanawake wakamuanika kalameni, lakini alishikilia msimamo wake.

Ulinzi mkali kamanda akizikwa, mke asusia

Na STEVE NJUGUNA

Kamanda wa zamani wa kikosi cha jeshi la angani Kenya, Meja Jenerali Duncan Kireri Wachira, hatimaye alizikwa Ijumaa nyumbani kwake Runda, Nyandarua chini ya ulinzi mkali huku mkewe wa kwanza na watoto wake wakisusia mazishi.

Meja Jenerali Wachira ambaye alikuwa kamanda wa kikosi hicho kati ya 1989 na 1994, alifariki kutokana na ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu katika Hospitali ya Nairobi, maradhi ambayo aliugua kwa zaidi ya miaka mitano.

Kifo chake kilifufua mzozo wa muda mrefu kuhusu mali yake kati ya Bi Margaret Wakonyo, yaya aliyemuoa miaka 19 iliyopita kama mke wake wa pili na wanawe wawili kutoka ndoa ya kwanza.

Baada ya kifo chake mnamo Oktoba 22, mipango ya kumzika marehemu ilisitishwa baada ya Bi Wakonyo na watoto wake wa kambo kuhusika kwenye ugomvi juu ya mali ya Meja Wachira, mali ambayo ni pamoja na shamba la mifugo huko Limuru, kaunti ya Kiambu, nyumba tatu za makazi jijini Nairobi na jengo la kibiashara lililoko Ongata Rongai viungani vya jiji la Nairobi.

Meja Jenerali Wachira alimuoa Bi Wakonyo ambaye aliwahi kuhudumu kama yaya wake miaka mitatu baada ya kumpa talaka mke wake wa kwanza, Ann Wanjiru, mwalimu wa zamani wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Pangani.

Katika ndoa ya kwanza, walikuwa wamebarikiwa na watoto wanne, Marehemu Allan Wachira, Michael Wanjohi, Edward Thiong’o na Sylvia Muthoni.

Kabla ya kifo chake, watoto wake wawili (Wanjohi na Thiong’o) walikuwa wamemshutumu baba yao kwa madai ya kuhamisha umiliki wa mali yake kwa mke wake wa pili jambo ambalo liliwafanya kumshtaki katika Mahakama Kuu.

Lakini mahakama ilimpa Bi Wakonyo agizo la kujumuishwa kama mmoja wa wasimamizi wa mali ya Meja Jenerali Wachira na pia kuwa mwangalizi wa Bw Wachira ambaye wakati huo alikuwa akiugua.

Mwasisi wa wakfu wa kusaidia wale ndoa zao zinayumba

 

Na PETER CHANGTOEK

ALIPOAMUA kuolewa na maridhia wake wa moyoni, matarajio yake hayakuwa mengine, ila ni kuwa na maisha yasiyokuwa na farakano.

Hakujua kuwa mambo yangekuja kuenda segemnege, na maisha yake kumithilishwa na kaka tupu la yai, ambalo halina thamani hata kidogo.

Lakini maisha ya ndoa ya Bi Esther Kisaghu yalipogeuka, na kuwa lindi la machozi na majonzi, aliamua liwe liwalo, na kuondoka katika ndoa, na baadaye ukurasa mpya maishani, ukafunguka.

Aliliasisi Wakfu wa The Rose; shirika lisilokuwa la serikali, ambalo huwasaidia waathiriwa wa dhuluma za nyumbani, ambazo zimekuwa zikikithiri na zinaendelea kukithiri siku baada ya nyingine, si tu nchini Kenya, bali pia katika nchi nyingi duniani.

Anasimulia kuhusu mkasa uliompata, ambao nusra umwondoe duniani, pindi tu alipoolewa na muhibu aliyekuwa akimwamini na kumthamini kwa hali na mali na kwa dhati.

“Nilizipitia changamoto za binafsi. Mimi niliathirika na vita vya nyumbani nilipokuwa ndani ya ndoa. Nilianza kama msichana yeyote yule, ambaye anafurahia kuolewa. Tulipooana tu, kukawa na hali ya mabadiliko,’’ asema Bi Esther, akiongeza kuwa mumewe alianza kumfokea na kutomheshimu. Hapo ndipo masaibu yalipoanza kumwandama.

Mzawa wa Kaunti ya Taita Taveta, awali, Esther alisomea katika Shule ya Msingi ya Kilifi, walikohamia kwa sababu babaye alikuwa mwalimu, kisha akapandishwa cheo kuwa afisa wa elimu.

Kisha, alijiunga na Shule ya Upili ya Alliance, na baada ya hapo, akajiunga na chuo kikuu kimoja kule Marekani, kwa minajili ya kusomea shahada ya Usimamizi wa Biashara.

“Nilipofika katikati, mpenzi wangu akaniambia nirudi tuoane, nikaacha masomo katikati. Nilikuwa nimemaliza miaka miwili….. hiyo shahada haikukamilika,’’ anasimulia huku huzuni ikidhihirika dhahiri shahiri usoni pake.

Hata hivyo, baada ya kuoana, mambo hayakuenda jinsi alivyokuwa akidhani. Lo! Kumbe udhaniaye ndiye siye! Alidhani kuwa alikuwa amempata mpenzi wa dhati, lakini alishangaa ghaya ya kushangaa, alipoanza kudhulumiwa, kuteswa na kubezwa na mumuwe!

“Mwaka wa pili baada ya kuoana, alianza kuninyonga. Mimi nikanyamaza,’’ anasema Esther ambaye aliolewa akiwa na umri wa miaka 27.

Mambo yalipochacha, aliamua ima fa ima, na kujinasua kutoka kwa ulimbo uliokuwa umemnasa na kumbana.

“Nilipoona ndoa yangu imekumbwa na vita zaidi na zaidi, na naendelea kuteseka na mwanangu anaendelea kuteseka, nikatafuta namna ya kuondoka nchini kwa usalama wangu. Kwa vile niliona maisha yangu yalikuwa hatarini mume wangu alipojaribu kunidunga kisu, nikajua nimeona kifo. Katika hali ya kutafuta usalama, nikasema wacha niende chuoni Marekani nisomee shahada yangu ya pili,’’ anasema, akisisitiza kwamba hiyo ilikuwa hali ya kuondokea kifo kilichokuwa kikimkodolea macho!

Hivyo basi, akajiunga na Chuo Kikuu cha Boston, kusudi asomee shahada ya uzamili; Afya ya Umma zingatio likiwa Afya ya Kimataifa (Masters in Public Health – International Health).

Ni katika harakati yake ya kusomea taaluma hiyo ambapo aling’amua kuwa dhuluma za nyumbani zinaweza kuzuiwa.

“Katika hali ya kusoma miaka hiyo minne nilihakikisha nitasaidia watu nyumbani,’’ anadokeza.

Baada ya kukamilisha kusomea taaluma hiyo, Bi Esther, ambaye ni mzazi wa mtoto mmoja wa kiume, alirejea humu nchini, na kuufungua ukurasa mpya maishani kwa kuasisi ‘The Rose Foundation’.

Azma yake ilikuwa kuwahamasisha watu kuhusu uzuiaji wa dhuluma za nyumbani.

“Nikiwa mwanzilishi wa ‘The Rose Foundation’, nimekuwa na huo msukumo kuongea juu ya vita vya nyumbani ili niwasaidie wale waathiriwa wamenyamaza, wanaoogopa kuongea juu ya vita vya nyumbani kwa vile wanaona hakuna usaidizi wowote,’’ asimulia mwasisi huyo.

Amekuwa akiwahamasisha waja, hususani vijana, kuhusu uzuiaji wa dhuluma za nyumbani kupitia kwa mafunzo na warsha mbalimbali. Hali kadhalika, amezipeleka kampeni hizo makanisani, japo anasema kuwa makanisa yamezipokea kampeni hizo kwa mtazamo hasi.

Anasema kuwa watoto wengi huathirika mno kisaikolojia wanapoona dhuluma hizo zikiendelea nyumbani.

“Asilimia 60 ya watoto 10 wa kiume waliokumbwa na dhuluma nyumbani, wakiwa watu wazima, wakioa, pia upo uwezekano watakuwa wa kudhulumu,’’ anafichua.

Msamaha

Anasisitiza kuwa ni jambo aula kwa wale waliodhulumiwa katika ndoa kuwasamehe wale waliowatendea dhuluma hizo. Hata hivyo, anawasihi waliosamehewa kuwajibika ipasavyo.

Mwanzilishi huyo wa shirika hilo lisilokuwa la serikali anasema kuwa ana mipango ya kuzifikisha huduma zake katika kaunti zote nchini.

“Shirika la ‘The Rose Foundation’ limeanza majadiliano na Kaunti ya Taita Taveta…… kwa dhuluma za kijinsia, Taita Taveta ni namba tatu. Halafu tukiona tumeimarika vizuri (hapa) Kenya, tuangalie mataifa jirani….. kufunza mataifa mengine kwamba tunaweza kuzuia vita vya nyumbani,’’ anafichua.