NYS sasa ni safi kama pamba, afisa mkuu asifia mageuzi

Na Kenya News Agency

MKURUGENZI wa Shirika la Kitaifa la Huduma kwa Vijana (NYS) Matilda Sakwa amesema kuwa ufisadi ambao umezingira shirika hilo miaka ya nyuma umetokomea na shirika hilo sasa liko katika mkondo mzuri wa uwajibikaji.

Bi Sakwa alisema kuwa NYS haiwezi kurudia makosa hayo ya miaka ya nyuma kwa kuwa yaliipa shirika hilo dhana mbaya machoni pa umma na pia kuathiri bajeti yake huku lengo lao kuu likiwa kuhakikisha umma unaamini katika utendakazi wao.

“Shirika la NYS limepiga hatua na hakuna sakata tena kama miaka ya nyuma. Kuna mambo mazuri na miradi ya kuvutia inayoendelezwa na shirika hili,” akasema Bi Sakwa mjini Ugunja akiwa ameandamana na mbunge wa eneo hilo Opiyo Wandayi.

Aidha, Bi Sakwa aliwataka wazazi wawe huru kuwaruhusu watoto wao wajiunge na NYS akisema serikali itakuwa ikadhamini ili wasomee kozi za kiufundi baada ya kukamilisha mafunzo yao.

Kwa upande wake, Bw Wandayi aliitaka serikali ibuni sera itakayomlazimu kila Mkenya ambaye ana umri wa miaka 18 kupokea mafunzo ya NYS.

 

Mfumo mpya wa wasaka-kazi kuwafaa vijana

Na MARY WANGARI

VIJANA nchini Kenya huenda wakanufaika pakubwa kutokana na nafasi za ajira katika sekta za umma na za kibinafsi kufuatia kubuniwa kwa mfumo maalum unaohifadhi data za wanaosaka ajira.

Mfumo huo mpya wa kielektroniki unalenga vijana wanaojiunga na kufuzu kutoka Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS).

Akizungumza Jumamosi mjini Gilgil, Kaunti ya Nakuru alipozindua teknolojia hiyo, Rais Uhuru Kenyatta alisema mfumo huo mpya utawezesha kufuatilia, kuhifadhi rekodi na kurahisisha mchakato wa waajiri kuteua waajiriwa miongoni mwa mahafala wa NYS.

“Serikali imejitolea kubuni nyadhifa za kazi kwa vijana katika sekta za umma na za kibinafsi. Kuhusiana na hili, NYS imebuni mfumo unaohifadhi data ya mahafala wake kwa njia inayowezesha waajiriwa kuipata kirahisi,” alisema Rais Kenyatta.

Rais aliyekuwa akizungumza katika hafla ya kufuzu kwa mahafala 7,479 wa NYS, alifafanua kuwa teknolojia hiyo itawezesha waajiri kuteua wafanyakazi wenye ujuzi unaohitajika katika eneo fulani.

ONYANGO: Kukwama kwa ‘Okoa Abiria’ kwazua maswali

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI ilizindua kwa mbwembwe mabasi 27 ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) mnamo Machi 2018 kwa lengo la kurahisisha usafiri na kupunguza msongamano wa magari jijini.

Mabasi hayo yalizinduliwa mara baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukutana na washikadau mbalimbali na kuwataka kuhakikisha kuwa wanashughulikia tatizo la msongamano wa magari jijini kwa haraka.

Mabasi hayo ya NYS yalihudumu katika barabara za kuelekea katika mitaa ya Embakasi, Githurai, Mwiki, Dandora, Kariobangi, Kibera, Kawangware, Kangemi na Kayole.

Mara baada ya kuzinduliwa kwa mradi huo unaojulikana kama ‘Okoa Abiria’, wakazi wa Nairobi walihisi kupata afueni kwani abiria walitozwa nauli ya Sh20 tu bila kujali umbali.

Nauli hiyo ya chini iliwakera wamiliki wa magari ya usafiri wa umma ambao walidai kuwa ilikuwa pigo kwa biashara zao.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NYS wakati huo Richard Ndubai, ambaye sasa anakabiliwa na mashtaka ya kuhusika katika sakata ya wizi wa fedha katika taasisi hiyo, alieleza Wakenya kuwa mabasi hayo yalilenga kutatua tatizo la msongamano wa magari ambalo limekuwa likizonga jiji la Nairobi kwa zaidi ya miongo miwili.

Kadhalika, Bw Ndubai aliambia Wakenya kwamba taasisi hiyo ingeongeza magari mengine 50 zaidi ndani ya kipindi cha miezi miwili ili kuwarahisishia wakazi wa Nairobi usafiri.

Ndubai alinaswa miezi miwili baadaye kabla ya kuongeza magari hayo namna alivyoahidi.

Mwaka mmoja baadaye, ripoti ya Mkaguzi Mkuu iliyotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilionyesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya magari hayo yamekwama.

Mkaguzi wa Hesabu, katika ripoti yake alisema ni magari tisa tu yaliyokuwa yakihudumu kufikia Julai mwaka huu.

Kulingana na ripoti hiyo, serikali haijakuwa ikitengea hela mabasi hayo. Hali hiyo imeyasababisha mabasi hayo kukosa kukarabatiwa.

Ripoti hiyo ilimalizia kwa kusema kuwa “mradi huo wa Okoa Abiria ulikuwa unaelekea kusambaratika”.

Mnamo Aprili mwaka jana serikali iliidhinisha Sh500 millioni zitumiwe na NYS kununua mabasi zaidi.

Magari mengi ya usafiri wa umma jijini Nairobi yanamilikiwa na wanasiasa wenye ushawishi mkubwa serikalini.

Kukwama kwa mabasi ya NYS kunazua maswali tele.

Je, kuna uwezekano kwamba wanasiasa hao wanaomiliki, ndio wamekuwa wakihujumu mradi wa Okoa Abiria wa NYS?

Je, kuna mikono ya wanasiasa katika kukwama kwa mabasi hayo ambayo ni afueni kwa wakazi wa mitaa ambayo wengi wa wakazi ni wenye mapato ya chini?

Je, serikali inalenga kuachana na mradi huo baada ya kubaini kwamba haujafanya lolote kupunguza msongamano wa magari jijini?

Ikiwa kuna mkono wa watu fiche, Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) haina budi kufanya uchunguzi kuwanasa wahusika.

NYS yashindwa kulipia makurutu karo ya vyuo anuwai

DAVID MUCHUI Na BENSON MATHEKA

MAKURUTU zaidi ya 16,000 wa Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), wamefukuzwa katika vituo vya mafunzo anuai nchini baada ya shirika hilo kushindwa kulipa malimbikizi ya karo ya zaidi ya Sh3.3 bilioni.

Haya yanajiri wiki tatu baada ya mkurugenzi mkuu wa NYS, Matilda Sakwa kufichua kuwa linakumbwa na uhaba wa fedha na halitaweza kutekeleza baadhi ya miradi yake.

Kwa wakati huu, shirika hilo linafadhili wanafunzi 16,292 katika vyuo vya mafunzo anuai kote nchini na limechelewa kulipa karo. Kufuatia malimbikizi ya karo, wakuu wa muungano wa vyuo vya mafunzo anuai nchini (Katti) wameamua kuwafukuza wanafunzi.

Kulingana na barua ya mwenyekiti wa muungano huo, Bi Glory Mutungi kwa wakuu wa vyuo vya mafunzo anuai nchini, uamuzi huo ulifikiwa baada ya mkutano kati ya NYS na wizara ya elimu.

“Imeamuliwa kuwa wanafunzi wa NYS hawataruhusiwa kurejea vyuoni hadi NYS ilipe malimbikizi ya karo inayodaiwa na kila chuo,” inasema barua hiyo.

Akiongea na Taifa Leo, Katibu wa mafunzo anuai katika wizara ya elimu, Dkt Kevit Desai alisema vyuo hivyo vilichukua hatua hiyo kwasababu ya matatizo ya kifedha yanayotokana na hatua ya serikali ya kupunguza karo ili kuvutia wanafunzi wengi.

“Kila mwanafunzi wa NYS hulipa Sh109,500 kwa mwaka. Kwa wakati huu NYS inadaiwa na vyuo vyetu Sh3,333,068,637. Kwasababu ya deni hili, vyuo hivyo vinakabiliwa na uhaba wa pesa,” alisema Dkt Desai.

Alisema kupunguzwa kwa karo kumeongeza mzigo wa kifedha wa vyuo hivyo.

“Chuo cha ufundi cha kitaifa kinahitaji wanafunzi 10,000 kiweze kuhudumu vyema ilhali chuo cha mafunzo anuai kinahitaji wanafunzi 5,000. Bila karo, ni vigumu kuendesha shughuli zake,” alisema.

Dkt Desai alisema serikali inalenga kusajili vijana 400,000 kujiunga na vyuo vya mafunzo ya kiufundi kufikia mwaka ujao kupitia mpango wa kupunguza karo.

Mnamo Agosti 24, mwaka huu, Bi Sakwa alisema NYS imelazimika kupunguza idadi ya makurutu kutoka 30,000 hadi 20,000 baada ya bajeti yake kupunguzwa.

Alisema shirika hilo halitaweza kutekeleza baadhi ya miradi yake. “Tunapanga kupunguza idadi ya makurutu tutakaosajili mwaka huu ili kupunguza gharama na kuweka mikakati ya kuongeza mapato,” Bi Sakwa aliambia kamati ya bunge kuhusu Leba.

Alisema NYS ilikuwa imeomba Sh35 bilioni katika bajeti ya mwaka wa 2019/2020 lakini lilitengewa Sh12.7 bilioni pekee.

Kulingana na Bi Sakwa, NYS imetambua miradi ambayo itasitishwa kutokana na ukosefu wa fedha.

“Tumelazimika kusimamisha mradi wa mabasi ya uchukuzi jijini Nairobi kwa sababu hatungeuendeleza kwa sababu ya gharama,” alieleza.

Bi Sakwa aliteuliwa kusimamia shirika hilo wakati ambao lilikuwa limekumbwa na kashfa za mabilioni ya pesa.

Washukiwa kadhaa, wakiwemo wakurugenzi waliotangulia walishtakiwa kortini na kesi zinaendelea.

Waliouzia NYS bidhaa hawajalipwa miaka 4 baadaye

Na BERNARDINE MUTANU

BAADHI ya wanakandarasi halali wa Huduma ya Kitaifa ya Vijana (NYS) kufikia sasa hawajalipwa miaka minne baada ya kutoa bidhaa kwa shirika hilo.

Huku wanakandarasi haramu wakizidi kufurahia mamilioni waliyopora, wale halali waliotoa bidhaa za ujenzi walisahaulika.

Habari zilizoonekana na Taifa Leo Dijitali zilionyesha wafanyibiashara hao walitoa vifaa vya ujenzi, sehemu za magari, sare, vyakula, vitabu na kalamu na vifaa vya mawasiliano miongoni mwa vifaa vingine.

Bidhaa na huduma hizo zilitolewa wakati wa awamu ya mwanzo ya programu ya kuwawezesha vijana na mradi wa taa mitaani.

Baadhi ya wanakandarasi hao waliaga dunia, wengine waliachwa na wachumba, ilhali baadhi yao wanakabiliana na minada, kufurushwa na kufungiwa nyumba, huku wakiorodheshwa kwenye CRB kwa kulemewa kulipa madeni.

Waliozungumza na Taifa Leo Dijitali walieleza kuwa kumbukumbu yao ya NYS ni nyaraka zinazotoa ushahidi kuwa walitoa bidhaa na huduma kwa serikali.

Kulingana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Fedha za serikali Edward Ouko, NYS na wizara inayosimamia huduma hiyo haijalipa watoaji huduma na bidhaa kufikia 800 takriban Sh3 bilioni.

Kwa jumla, wanakandarasi wanadai serikali Sh11.3 bilioni katika biashara zote – halali na haramu.

Ni sakata iliyomfanya Gavana Anne Waiguru wa Kirinyaga kujiuzulu, pamoja na baadhi ya maafisa wa serikali.

Iliibuka kuwa wanakandarasi bandia walilipwa mamilioni baada ya kuwasilisha hewa NYS.

Huku hao wakiburudika, wale halali walipatwa na mshtuko wa moyo na kufa baada ya serikali kusimamisha malipo kwa wanakandarasi wote.

Mwongozo wa kununua bidhaa NYS ulikuwa na dosari, korti yaambiwa

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa masuala ya usimamizi katika Wizara ya Ardhi Bw Julius Kiplagat Kandie Jumatano alikiri kwamba mwongozo uliopewa wakuu wa wizara na mashirika ya Serikali ulikuwa na kasoro.

Akitoa ushahidi katika kesi ya kashfa ya Sh60 milioni dhidi ya katibu wa zamani Lillian Omollo, Bw Kandie alimweleza hakimu mwandamizi Bw Peter Ooko kuwa hakuna njia watekelezaji wa mwongozo huo wangeukwepa.

Bw Kandie aliwaondolea lawama Bi Omollo , aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la huduma ya vijana kwa taifa NYS Bw Richard Ndubai na washkiwa wengine 31 wanaoshtakiwa kwa ufujaji wa Sh60 milioni akisema , “hakuna namna wangeukosoa mwongozo huo.”

Alisema akiwa mwenyekiti wa kamati iliyoteuliwa kubuni mwongozo wa ufunguzi wa zabuni, masharti na sheria za utenda kazi (MTC) aliandaa taarifa iliyopelekewa wizara na mashirika ya Serikali.

“Ilibidi tu makatibu na wakuu wa mashirika ya serikali kutii na kuutekeleza mwongozo huo jinsi ulivyo hata ikiwa ulikuwa na dosari,” alisema Bw Kandie.

Akijibu maswali kutoka kwa wakili Migos Ogamba, Bw Kandie alisema wakuu serikalini na wakurugenzi wa mashirika ya Serikali hawakuwa na budi ila kutekeleza taarifa hiyo pasi kuihoji.

“Kukaidi mwongozo huu ilikuwa sawa na kuhoji na kukosoa mamlaka makuu ya nchi,” Bw Ogamba alimwuliza.

Bw Kandie alisema wanachama wa MTC walikuwa wanateuliwa na Katibu mkuu Wizara ya Ujenzi.

Bw Kandie alisema mwongozo huo ulibuniwa 2012 na waliouteuliwa 2016 waliutumia ukiwa na dosari hizo.

Akitoa ushahidi katika kesi ya kashfa ya NYS ya Sh60milioni, Bw Kandie alisema dosari katika mwongozo ulikuwa tu unarithiwa na wizara zote na wakuu wa mashirika.

Alisema dosari hiyo ilipelekea serikali kupoteza mamilioni ya pesa.

Mawakili walimweleza shahidi huyo makosa aliyofanya na kamati ya MTC ndiyo yalipelekea umma kupoteza viwango vikubwa vya pesa na kwamba ni yeye angelifaa kuwa kizimbani.

Bi Omollo, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa NYS Bw Richard Ndubai  na washukiwa wengine  25 wameshtakiwa kwa kosa la kufanya njama za kuibia NYS Sh60,598,800 kati ya Aprili 6 2016 na Aprili 27 2017.

Bi Omollo ameshtakiwa kwa kosa la kutumia mamlaka ya afisi yake vibaya kwa kuwalipa kimakosa Bi Catherine Njeri kamuyu, Sarah Murungu Andrine na Grace Nyambura Mbare wamiliki wa kampuni ya Erastz Enterprises Sh26,600,000.

Anakabiliwa na shtaka lingine la kuruhusu kampuni ya Arkroad Lrd kulipwa Sh24,866,800.

Bi Omollo na washukiwa hao wengine wamekanusha mashtaka ya utumiaji wa mamlaka yao vibaya. Wako nje kwa dhamana.

Kesi inaendelea kusikizwa.

UFISADI: Kesi ya NYS ilivyowaudhi Wakenya 2018

Na RICHARD MUNGUTI

LICHA ya kuwazingira washukiwa wa kashfa ya shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji alikumbana na mawimbi mazito mazito ambayo yalitishia kuzamisha kesi ya Sh226 milioni dhidi ya washukiwa 35.

Miongoni mwa washukiwa hawa ni aliyekuwa katibu mkuu Wizara ya Jinsia Lillian Mbogo Omollo na aliyekuwa Mkurugenzi wa NYS Richard Ndubai.

Washukiwa hawa wanakabiliwa na mashtaka 82 ya matumizi mabaya ya mamlaka na uporaji wa pesa za umma.

Sio tu watumishi wa umma waliotiwa nguvuni pekee bali pia wafanyabiashara ambao kampuni zao zilitumika kufyonza pesa za umma.

Wakurugenzi wa kampuni nne zinazomilikiwa na watu wa familia moja ya Naivasha walishtakiwa pamoja na Bi Omollo , Ndubai na wengine.

Mshukiwa Anne Wambere Ngirita alidaiwa alilipwa zaidi ya Sh50 milioni pasi kutoa huduma zozote kwa NYS.

Anne, dada zake , ndugu yake na mama yao ni miongoni mwa walioshtakiwa katika kashfa hii ambayo viongozi wa mashtaka waliambia mahakama katika taarifa ya utangulizi kuwa Sh8 bilioni zilitoweka katika kashfa hiyo.

 Pia kutoandaa ipasavyo ushahidi katika kesi hiyo ya Sh226 milioni ilifanya mahakama inayoisikiza kulia hoi.

Hata wakati mmoja ilibidi hakimu mkuu Douglas Ogoti na mawakili wanaowatetea washukiwa hao 37  kwa kufilisi NYS kuuliza , “ ni kwa nini ushahidi huu hauajatayarishwa inavyopasa na washukiwa kupewa nakala zao.”

Hakimu alisema tangu aanze kusikiza kesi hiyo amekumbana na vizingiti sio haba ambazo zimemfanya kuiahirishwa kila mara.

Akasema Ogoti: “Kule nje itasemekana kuwa mahakama inachelewesha kesi.Tunalaumiwa bure. Sio mahakimu wanaochelewesha kukamilika kwa kesi.Ni afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma na ile uchunguzi wa jinai (DCI) zinazoyumbisha kusikizwa kwa kesi hii kwa kutowapa washukiwa nakala za ushahidi.”

Hakimu alidokeza wimbo ambao umekuwa ukikaririwa katika kesi hiyo ni mmoja tu – wa washtakiwa kutopewa nakala za mashahidi.

Washtakiwa na mawakili wao na hakimu wamekuwa wakiuliza swali moja nalo ni hili , “Mbona afisi ya DCI haitaki kuwapa washtakiwa nakala zote za ushahidi uliokusanywa na kurekodiwa kabla ya wao kushikiwa na kufikishwa kortini?”

Ilibainika wazi wazi ni maafisa katika afisi ya DCI ambao wamekawia kuwapa washtakiwa nakala za ushidi waandae utetezi wao.

Katika muda wa zaidi ya mwezi mmoja kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa kila inapoanza kusikizwa hata hakimu akasema DPP anakaidi haki za washtakiwa kwa kuchelewa kuwapa nakala za mashahidi.

Kesi hiyo ilipoahirishwa mara mbili ilibidi Bw Ogoti amwagize afisa anayechunguza kesi hiyo kufika mahakamani kuelezea kilichokuwa kinaendelea.

Afisa huyo alifika na kuahidi kuwapa nakala za mashahidi ifikapo Alhamisi.

Haikuwezekana. Punde tu baada ya Bw Sebastian Mokua, shahidi wa kwanza kuingia kizimbani , alichomoa vocha ya malipo kwa makampuni ya Familia ya Ngirita ambao mawakili walisema “ hawajawahi i ona.”

Akiwa amechemka kwa hasira Bw Ogoti alimwuliza kiongozi wa mashtaka Bi Evah Kanyuira , “ Mbona haujawapa washtakiwa nakala za ushahidi huu?”

Bi Kanyuira hakutoa sababu zozote ila kusema “ naomba ushahidi huu uwekwe kando ndipo washtakiwa wapewe nakala zao.”

Baada ya majimbizano ya muda tena ushahidi mwingine wa malipo ya makampuni Njewanga Enterprises na Ngiwaco Enterprises ulichomolewa.

Tena mawakili na hakimu walishangaa sababu ya DPP kuendelea kutoa ushahidi wa kuwatweza mioyo washtakiwa.

Bw Ogoti hakusita kumkemea DPP akisema anakaidi Kifungu nambari 50(2)(J) cha katiba kinachomtaka awape ushahidi wote washukiwa kwa muda unaofaa ndipo waandae ushahidi wao.

“Ukweli uliopo ndio huu, haki za washtakiwa hawa zimekandamizwan na DPP ikiwa kufikia sasa kuna ushahidi ambao hawajapewa,” alisema Bw Ogoti.

Baada ya uzembe wa DPP na DCI wa kutowapa washukiwa ushahidi kujianika adharani, ilibidi Bw Ogoti atoe maagizo mapya kwamba washtakiwa wote wapewe ushahidi.

Ushahidi uliosababisha tumbo joto ulikuwa wa malipo ya Sh19milioni na Sh5milioni mtawalia kwa makampuni ya Njewanga Enterprises na Ngiwaco Enterprises.

Kampuni hizi zinazmilikiwa na Phyilis Njeria Ngirita na Lucy Wambui Ngirita.

Makampuni ya Familia hii ya Ngirita imedaiwa ilipokea mamilioni ya pesa kutoka NYS bila kutoa huduma.

Walioshtakiwa ni Anne Wambere Ngirita, Lucy Wambui Ngirita, Phyilis Njeri Ngirita na ndugu yao Jeremiah Gichini Ngirita.

Aliyekuwa katibu mkuu wizara ya ugatuzi Bi Lillian Omollo ameshtakiwa kuidhinisha malipo ya Sh54.8 milioni kwa Anne, Sh63.2m kwa Lucy , Sh50.9million na Phyilis  na Sh57.8million kwa Jeremiah kinyume cha sheria.

Kesi itaendelea Machi 2019.

NYS sasa kutegemea mapato yake kujiimarisha

Na CHARLES WASONGA

MSWADA unaolenga kuimaisha usimamizi wa Shirika la Vijana kwa Huduma kwa Taifa (NYS) na kuipa sura mpya baada ya kuzongwa na ufisadi tangu 2015 umetiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Ken Lusaka waliwasilisha mswada huo kwa Rais katika Ikulu ya Mombasa ambapo aliwaongoza Wakenya kualika Mwaka Mpya wa 2019.

Mswada huo maarufu kama “National Youth Service (NYS) Bill” unaibadili sura ya shirika hilo kuwa Shirika la Kiserikali ambalo majukumu yake yatahusisha uendeshaji wa shughuli za uzalishaji mali, utengenezaji bidhaa na shughuli nyinginezo za mapato.

Muhimu ni kwamba, tofauti na hali ilivyokuwa zamani, chini ya sheria hii mpya NYS itakuwa ikizalisha mapato yake badala ya kutegemea, kwa kiwango kikubwa, mgao wa fedha kutoka Serikali ya Kitaifa.

Waziri wa Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Profesa Margaret Kobia alisema chini ya sheria hiyo baraza la watu 12 ambao watasimamia utendakazi wa NYS.

“Vile vile, chini ya sheria hii, mkaguzi wa hesabu atateuliwa kufuatilia matumizi ya fedha katika NYS”, akasema Waziri Kobia ambaye pia alishuhudia kutiwa saini kwa mswada huo.

“Baraza hilo simamizi litasimamiwa na mwenyekiti ambaye atateuliwa na Rais na wajibu wake utakuwa ni kutunga sera na maongozi ya kufanikisha utendakazi wa NYS,” akaongeza.

Awali, usimamizi wa shughuli na utendakazi wa NYS ulikuwa chini ya Katiba wa Wizara ya Utumishi wa Umma na Vijana.

Hii ndio maana kashfa ya wizi wa Sh791 milioni ilipotekea katika shirika hilo aliyekuwa Katibu wa wizara hiyo Peter Mangiti ndiye alielekezewa kidole cha lawama na kutiwa mbaroni.

Na katika awamu ya pili ya sakata ya NYS inakisiwa kuwa Sh9 bilioni ziliibiwa au kufujwa aliyekuwa Katibu Lilian Omollo ni miongoni mwa washukiwa 22 walioshtakiwa kwa uovu huo.

Rais Kenyatta pia alitia saini Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ugavi wa Mapato, ya 2018 ambao unapendekeza kuwa fedha kutoka mashirika ya maendeleo ya nje, yatumiwe kwa miradi iliyokusudiwa pekee.

Chini ya sheria ya awali, serikali za kaunti zimekuwa zikieleleza pesa hizo, ambazo aghalabu huwa ni ruzuku, kwa shughuli zisizokusudiwa.

Kiongozi wa taifa pia alitia saini miswada mingine mitatu ambayo ni: Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Afya, 2018, Mswada wa Masoroveya wa Mijengo, 2017, Mswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, 2018, Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Mashirika ya Akiba na Mikopo (Saccos), 2018 na Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Soko la Hisa 2018.

Maandalizi duni ya kesi ya NYS yafanya mahakama kulia hoi

Na RICHARD MUNGUTI

KUTOANDAA ipasavyo ushahidi katika kesi ya kashfa ya Sh226milioni iliyokumba shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS) kumefanya mahakama inayosikiza kulia hoi.

Hata imebidi hakimu mkuu Douglas Ogoti na mawakili wanaowatetea washukiwa 37 walioshtakiwa kwa kufilisi NYS kuuliza , “ni kwa nini ushahidi huu hauajatayarishwa inavyopasa na washukiwa kupewa nakala zao.”

Bw Ogoti amesema tangu aanze kusikiza kesi hiyo amekumbana na vizingiti sio haba ambazo zimefanya kesi kuahirishwa kila mara.

Akasema Ogoti, “Kule nje itasemekana kuwa mahakama inachelewesha kesi.Tunalaumiwa bure. Sio mahakimu wanaochelewesha kukamilika kwa kesi hii.Ni afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma na ile uchunguzi wa jinai (DCI) zinazoyumbisha kusikizwa kwa kesi hii kwa kutowapa washukiwa nakala za ushahidi.”

Hakimu alidokeza wimbo ambao umekuwa ukikaririwa katika kesi hiyo ni mmoja tu – wa washtakiwa kutopewa nakala za mashahidi.

Washtakiwa na mawakili wao na hakimu wamekuwa wakiuliza swali moja nalo ni hili , “Mbona afisi ya DCI haitaki kuwapa washtakiwa nakala zote za ushahidi uliokusanywa na kurekodiwa kabla ya wao kushikiwa na kufikishwa kortini?”

Imebainika wazi wazi ni maafisa katika afisi ya DCI ambao wamekawia kuwapa washtakiwa nakala za ushidi waandae utetezi wao.

Katika muda wa zaidi ya mwezi mmoja kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa kila inapoanza kusikizwa hata hakimu akasema DPP anakaidi haki za washtakiwa kwa kuchelewa kuwapa nakala za mashahidi.

Wiki hii kesi hiyo iliahirishwa mara mbili hata ikabidi Bw Ogoti kumwagiza afisa anayechunguza kesi hiyo afike mahakamani kueleza kuna ni.

Afisa huyo alifika na kuahidi kuwapa nakala za mashahidi ifikapo Alhamisi.

Haikuwezekana. Punde tu baada ya Bw Sebastian Mokua, shahidi wa kwanza kuingia kizimbani , alichomoa vocha ya malipo kwa makampuni ya Familia ya Ngirita ambao mawakili walisema “ hawajawahi kuuona.”

Tena Bw Ogoti alimwuliza kiongozi wa mashtaka Bi Evah Kanyuira , “ Mbona hamjawapa washtakiwa nakala za ushahidi huu?”

Bi Kanyuira hakutoa sababu zozote ila kusema “ naomba ushahidi huu uwekwe kando ndipo washtakiwa wapewe nakala zao.”

Baada ya majimbizano ya muda tena ushahidi mwingine wa malipo ya makampuni Njewanga Enterprises na Ngiwaco Enterprises ulichomolewa.

Tena mawakili na hakimu walishangaa sababu ya DPP kuendelea kutoa ushahidi wa kuwatweza mioyo washtakiwa.

Bw Ogoti hakusita kumkemea DPP akisema anakaidi Kifungu nambari 50(2)(J) cha katiba kinachomtaka awape ushahidi wote washukiwa kwa muda unaofaa ndipo waandae ushahidi wao.

“Ukweli uliopo ndio huu, haki za washtakiwa hawa zimekandamizwan na DPP ikiwa kufikia sasa kuna ushahidi ambao hawajapewa,” alisema Bw Ogoti.

Baada ya uzembe wa DPP na DCI wa kutowapa washukiwa ushahidi kujianika adharani , ilibidi Bw Ogoti atoe maagizo mapya kwamba washtakiwa wote wapewe ushahidi ambao utawasilishwa dhidi yao ifikapo Desemba 6 2018

Ushahidi uliosababisha tumbo joto ulikuwa wa malipo ya Sh19milioni na Sh5milioni mtawalia kwa makampuni ya Njewanga Enterprises na Ngiwaco Enterprises.

Kampuni hizi zinazmilikiwa na Phyilis Njeria Ngirita na Lucy Wambui Ngirita.

Makampuni ya Familia hii ya Ngirita imedaiwa ilipokea mamilioni ya pesa kutoka NYS bila kutoa huduma.

Walioshtakiwa ni Anne Wambere Ngirita, Lucy Wambui Ngirita, Phyilis Njeri Ngirita na ndugu yao Jeremiah Gichini Ngirita.

Aliyekuwa katibu mkuu wizara ya ugatuzi Bi Lillian Omollo ameshtakiwa kuidhinisha malipo ya Sh54.8milion kwa Anne, Sh63.2m kwa Lucy , Sh50.9million na Phyilis  na Sh57.8million kwa Jeremiah kinyume cha sheria

Washukiwa wa 37 wa NYS walia wanasiasa kudai lazima watafungwa

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA 37 katika kashfa ya Sh226 milioni iliyokumba shirika la huduma ya vijana kwa taifa akiwamo aliyekuwa katibu mkuu Lillian Omollo Jumatano waliomba mahakama iwazuilie wanasiasa wakuu nchini kukoma kuahidi mahakama itawafunga.

Mawakili wakiongozwa na Bw Assa Nyakundi waliteta kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakifanya ziara ng’ambo na humu nchini wakitoa ahadi ambazo hawawezi kuzitimiza.

“Katika siku za hivi punde baadhi ya maafisa wakuu serikalini na wanasiasa wamekuwa wakiahidi washukiwa katika kesi hii ya kashfa ya NYS watafungwa bila shaka,” alisema Bw  Nyakundi.

Wakili huyo alisema, “Ni wewe unasikiza hii kesi mbona wanasiasa wanazugumza kama ni wao watawafunga washukiwa hawa. Naomba hii mahakama iwazime kujadili na kuzugumzia kesi hii katika hafla za umma.”

Bw Nyakundi alimweleza  Bw Ogoti kuwa yapasa wanasiasa na wakuu serikalini wakumbushwe kuwa kuna sheria inayowazuilia watu kujadilia kesi ikiendelea mahakamani.

Hakimu alielezwa kuwa ni yeye anayesikiza kesi na kamwe “ wanasiasa hawapasi kukubaliwa kuendelea na kujadilia kesi hii adharani na midahalo ya kimataifa.”

Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akisema katika hafla mbali mbali kwamba idara ya mahakama itawafunga washukiwa wanaodaiwa waliiba mamilioni ya pesa kutoka NYS.

Wakili Migos Ogamba alisema sheria yapasa kutumiwa kuwalinda washukiwa dhidi ya shutuma kutoka kwa umma.

DPP akubaliwa kuwasilisha ushahidi mpya dhidi ya familia ya Ngirita

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA  imemkubalia Mkurugenzi wa Umma (DPP) Noordin Haji kuwasilisha ushahidi mpya jinsi kampuni za familia ya Ngirita ilivyopokea mamilioni ya pesa katika kashfa ya Sh8bilioni ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS).

Hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti alisema “kumnyima DPP fursa ya kuwasilisha ushahidi huo ni kuilemaza kabisa kesi hiyo ya ufisadi.”

Bw Ogoti alimwamuru DPP awakabidhi washukiwa 37 walioshtakiwa nakala za ushahidi huo mara moja.

Hakimu aliwapa washtakiwa muda wa siku nne kusoma ushahidi huo kabla ya kesi kuanza kusikizwa tena Novemba 21, 2018.

Akikubalia ombi la DPP lililowasilishwa na wakili Caroline Kimiri , Bw Ogoti alisema , “Kifungu nambari 50 (2) (J) cha Katiba kinamtaka DPP awape washukiwa ushahidi wote atakaotegemea kuthibitisha kesi dhidi yao.”

Alisema kukubalia ombi la washukiwa hao 37 ya kumzuia DPP kuwasilisha ushahidi huo mpya ni kukubali kuvunja katiba na sheria ambazo mahakama inatakiwa kutekeleza na kuhakikisha imetekelezwa.

Alisema kesi hii dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu Bi Lillian Mbogo Omollo , aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa NYS Richard Ndubai na washukiwa wengine 37 sio ya kawaida.

Alisema mashtaka ni 82 , washukiwa ni 37 na mawakili ni zaidi ya 30.

Bw Ogoti alisema kifungu nambari 25 cha katiba kimeagiza kila mshukiwa apewe fursa ya kujitetea na kutendewa haki.

Hakimu aliwakubalia viongozi wa mashtaka Bw Gitonga Riungu , Evah Kanyuira, Caroline Kimiri , Jalson Makori na Hellen Mutellah kuwasilisha ushahidi huo mpya.

Ushahidi huo unajumuisha nakala za malipo kwa Bi Phyillis Njeri Ngirita na kampuni ya Njewanga

Pia washtakiwa watapewa nakala za taarifa za Benki ya Kenya Commercial (KCB) tawi la Naivasha.

Na wakati huo huo , hakimu alifahamishwa Bi Anne Wambere Ngirita anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Mater.

Pia alipokea ripoti ya uchunguzi aliofanya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai kuhusu hospitali Anne alidai alihudhuria Naivasha.

Bw Riungu alisema ripoti za madaktari waliomtibu Anne Wambere Ngirita zilisema anaweza kuendelea na kesi huku akitumia madawa.

Wakipinga kuwasilishwa kwa ushahidi huo, washukiwa hao walimweleza hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti , kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) alikiuka kifungu nambari 50 cha katiba kinachomtaka afichue ushahidi wote kabla ya kesi kuanza kusikizwa.

“Ni jukumu la DPP kutimiza vipengee vyote vya Kifungu nambari 50 (2) (c) na (J) cha katiba kinachomtaka amkabidhi kila mshukiwa ushahidi kabla ya kuanza kusikizwa kwa kesi,” Bw Ogoti alifahamishwa.

Mawakili Assa Nyakundi, Migos Ogamba na  Stephen Ligunya walisema hatua ya DPP kuwasilisha ombi la kuwasilisha kwa ushahidi baada ya kesi kuanza kusikizwa ni ukandamizaji wa haki za washtakiwa.

Washukiwa hao wamekanusha mashtaka 82 dhidi yao. Wako nje kwa dhamana.

KASHFA YA NYS: Malumbano mahakamani

Na RICHARD MUNGUTI

KULIZUKA malumbano makali baina ya mawakili wanaowatetea washukiwa 37 katika kashfa ya Sh8bilioni ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS) na viongozi wa mashtaka hata ikabidi hakimu aahirishe kesi kwa muda wa dakika 15.

Kizaazaa kilizuka pale wakili Assa Nyakundi alipomtaka kiongozi wa mashtaka Caroline Kimiri awache kuwasilisha tetezi mpya katika ombi la kupinga ushahidi mpya ukiwasilishwa katika kesi hiyo.

Mawakili kadhaa walimuunga mkono Bw Nyakundi wakisema ,” upande wa mashtaka wapasas kuzingatia tu sheria na wala sio kuwasilisha ushahidi mpya.”

Lakini Bi Kimiri alipandwa na mori na kumweleza hakimu mkuu Douglas Ogoti kuwa “mawakili hao wa kutetea washukiwa wako na njama ya kuhakikisha hakamilishi ushahidi wake.”

Hakimu alimtaka Bi Kimiri asisikize madai ya mawakili wa washukiwa kisha aendelee akamilishe ushahidi wake.

Shambulizi hilo dhidi ya Bi Kimiri liliingiliwa na viongozi wengine wa mashtaka Bi Evah Kanyuaira , Bi Hellen Mutellah, Bw Jalson Makori na Bw Joseph Gitonga Riungu.

“Lazima mawakili wa kutetea washtakiwa watupe muda wa kuwasilisha ushahidi wetu. Hatukuwavuruga walipokuwa wanatoa tetezi zao,” alisema Bw Makori.

Mkinzano ulitokotoka hata Bw Makori akaomba mahakama iamuru aliyekuwa katibu wa ugatuzi Bi Lillian Mbogo Omollo arudi kukaa kizimbani ahame viti vya mawakili wanaomwakilisha kwa vile ndiye anazua vurugu na kuwataka mawakili wapinge ushahidi wa Bi Kimiri.

Upande wa mashtaka uliomba mahakama ikubali ushahidi mpya ulioguduliwa na mkurugenzi wa kuchunguza jinai (DCI).

Lakini washtakiwa wanaomba mahakama ikatae kupokea ushahidi mpya unao onyesha jinsi mamilioni ya pesa yalivyolipwa  mmoja wa familia ya Ngirita kati ya 2008 na 2016.

Wakipinga kuwasilishwa kwa ushahidi huo, washukiwa hao walimweleza hakimu mkuu Bw Ogoti , kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) alikiuka kifungu nambari 50 cha katiba kinachomtaka afichue ushahidi wote kabla ya kesi kuanza kusikizwa.

“Ni jukumu la DPP kutimiza vipengee vyote vya Kifungu nambari 50 (2) (c) na (J) cha katiba kinachomtaka amkabidhi kila mshukiwa ushahidi kabla ya kuanza kusikizwa kwa kesi,” Bw Ogoti alifahamishwa.

Mawakili Assa Nyakundi, Migos Ogamba na  Stephen Ligunya walisema hatua ya DPP kuwasilisha ombi la kuwasilisha kwa ushahidi baada ya kesi kuanza kusikizwa ni ukandamizaji wa haki za washtakiwa.

Mawakili hao walisema ufichuzi wa DPP kwamba Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) hakuwa amepata nakala za malipo ya zaidi ya Sh50milioni kwa Bi Phyilis Njeri Ngirita washukiwa waliposhtakiwa sio sababu tosha ya kukubaliwa kwa ushahidi huo.

Bw Ligunya alisema inaeleweka kwa DCI kusema alisahau kuambatanisha ushahidi huo alipowashtakiwa washukiwa hao kutokana na wingi wa hati za ushahidi zilizopo.

Hata hivyo alisema, viongozi saba wa mashtaka wakiongozwa na Bw Riungu Gitonga, walikosea kutowaarifu washtakiwa kwamba kuna ushahidi uliokuwa umesahaulika na kwamba utawasilishwa.

“Shida kubwa ya DPP ni kunyamaza na kumbe kuna ushahidi muhimu uliokuwa umeachwa nje,” alisema Bw Ligunya.

Bw Ligunya anayemwakilisha aliyekuwa katibu mkuu Bi Lillian Mbogo Omollo anayeshtakiwa kwa kutumia mamlaka yake vibaya na kufanya njama za kuibia NYS zaidi ya Sh226milioni.

Mahakama ilifahamishwa kuwa Fomu nambari1340 na 1341 zilizoidhinishwa kumlipa Bi Lucy Njeri Ngirita hazikuwa katika seti ya nakala za mwanzo.

“Kutokabidhiwa nakala hizi kumetutatiza kuandaa utetezi wetu,” Bw Ligunya alisema.

Alipinga kuwasilishwa kwa ushahidi huo.

Bw Ogamba aliambia mahakama DPP alikuwa amekimya kama maji ndani ya mtungi kwamba ushahidi wote haukukabidhiwa washtakiwa.

“Kesi zinazowakabili washtakiwa hawa ni tatu na hati hizi za ushahidi  ni muhimu sana kwa washukiwa kuandaa ushahidi,” alisema Bw Ogamba.

Alisema Phyillis Njeri Ngirita ambaye ni mmiliki wa kampuni ijulikanayo kwa jina Njewanga Enterprises anakabiliwa na mashtaka ya kupokea mali ya umma na ulanguzi wa pesa.

Alisema mshtakiwa huyo pamoja na wenzake 36 wamekosewa na akaomba korti ikatalie mbali ushahidi huo akisema utaathiri pakubwa utetezi wao. Washtakiwa hao 37 wanakabiliwa na mashtaka 82.

Wamekanusha wakishirikiana na wengine ambao hawako mahakamani walifanya njama za kuilaghai Serikali zaidi ya Sh226milioni.

Bi Omollo amekana alimruhusu mfanya biashara Bi Anne Wambere Wanjiku Ngirita kupitia kwa kampuni yake Annwaw Investment Sh54,848,750.

Pia ameshtakiwa kwa kuruhusu dada wa Anne, Bi Lucy Wambui Sh 63,254,008 na Phyillis Njeri Sh50,970,500.

Mahakama yamkubalia Anne Ngirita kwenda kutibiwa

Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA mkuu katika kashfa ya NYS Bi Anne Wambere Wanjiku Ngirita Jumanne aliruhusiwa kwenda hospitali na mahakama inayosikiza kesi za ufisadi wa Sh8bn.

Hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti alimkubalia Bi Ngirita kwenda hospitali ya Mater kupokea matibabu baada ya kuugua.

Mshukiwa huyo pamoja na mama yake  na dada zake wawili wameshtakiwa kupokea zaidi ya Sh900 milioni kutoka kwa NYS.

Yadaiwa hawakutoa huduma zozote ndipo wapokee pesa hizo.

Bw Ogoti alimkubalia Bi Ngirita kwenda hospitali huku akisubiri ripoti ya Mkurugenzi wa uchunguzi wa Jinai (DCI)  kuhusu ripoti za hospitali alizowasilisha Bi Ngirita.

Bw Ogoti Jumatatu alimwamuru DCI Geoffrey Kinoti achunguze ripoti hizo kubaini ikiwa ni za kweli. Bw Ogoti alimtaka DCI awasilishe ripoti ya rekodi hizo katika muda wa siku tatu.

Atawasilisha ripoti hiyo Jumatano kubaini ikiwa Bi Ngirita ni mgonjwa. Bi Ngirita aliwasilisha rekodi tata za hospitali

Hakimu alitoa agizo hilo alipokataa kuahirisha kesi dhidi ya washukiwa 37 wanaoshtakiwa pamoja na Bi Ngirita kumwezesha kwenda hospitali.

Bi Ngirita aliomba kesi hiyo iahirishwe kumwezesha kwenda hospitali Mater kwa alikuwa mgonjwa na hangeweza kuketi mwa muda mrefu.

SAKATA YA NYS: Kesi yaanza rasmi

Na RICHARD MUNGUTI

KESI ya kashfa ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) dhidi ya washtakiwa 37 iliyopelekea zaidi ya Sh11bilioni kupotea ilianza kusikizwa Jumatano.

Shahidi wa kwanza Bw Sebastian John Mokua alianza kutoa ushahididi dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu Bi Beatrice Mbogo Omollo na aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa NYS Bw Richard Ndubai miongoni mwa wengine.

Bw Mokua aliambia mahakama kuwa makampuni 36 yalipeleka maombi ya kutoa huduma mbali mbali kwa NYS.

Katika ya huduma zilizopelekewa maombi ni uuzaji wa vyakula , makaratasi na bidhaa nyinginezo.

Bw Mokua alisema kuwa Bi Lucy Wambui Ngirita , mamayake Bi Anne Wambere Ngirita alikuwa amepewa zabuni ya kuuzia NYS vyakula katika kampi ya Gigiri.

Kutokana na mauzo hayo ya chakula , Lucy Njeri anashtakiwa alipokea ShSh63,254,008 kupitia kwa kampuni yake-Ngiwaco Enterprises.

Malipo hayo yaliidhinishwa na Bi Omollo.

Bw Mouko alisema kati ya makampuni hayo 36 ni manne tu yaliyoteuliwa.

Bw Mouko ni mmoja wa mashahidi 43 waliorekodi taarifa dhidi ya washtakiwa hao 37.

Jumatatu wiki hii washtakiwa hao walifunguliwa mashtaka mapya 82 ya matumizi mabaya ya mamlaka na kulipwa kwa huduma ambazo hazikutolewa

Katika kesi hiyo yenye mashtaka 82 , Bi Omollo , aliyekuwa mkurugenzi mkuu Bw Richard Ndubai na washukiwa wengine 28 akiwamo Bi Anne Wambere Ngirita wameshtakiwa kuifuja Serikali kupitia kwa NYS Sh226,945,258.

Bi Omollo amedaiwa alitumia mamlaka ya afisi yake vibaya kwa kuidhinisha malipo ya Sh54,848,750 kwa Bi Anne Wambere Ngirita kupitia kwa kampuni yake ijulikanayo kwa jina Annwaw Investment Limited.

Pia Bi Omollo ameshtakiwa kuidhinisha malipo ya Sh63,254,008 kwa Bi Lucy Wambui Ngirita kupitia kwa kampuni yake-Ngiwaco Enterprises.

Pia alimlipa By Phyilis Njeri Ngirita Sh50,970,500 kupitia kwa kampuni yake –Njewanga Enterprises.

Mbali na hao dada Bi Omollo alishtakiwa kwa kumlipa baba yao Bw Jeremiah Gichiri Ngirita Sh57,872,000 kupitia kwa kampuni yake-Jerrycathy Enterprises aliomiliki pamoja na mkewe (njeri).

Bw Ndubai , aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa NYS ameshtakiwa kwa kuidhinisha malipo ya Sh16, 590,000 kwa Bi Phyilis Njeri Ngirita kupitia kwa kampuni yake Njewanga.

Bi Anne Wambere Ngirita ameshtakiwa kwa kuifuja NYS Sh54,848,750 bila ya kutoa huduma zozote.

yake Anne, Bw Jeremiah Gichini Ngirita alikana alipokea Sh57,872,000 kutoka kwa NYS bila ya kutoa huduma zozote.

Lucy na mama yake Njeri Ngirita walikana walitia kibidoni zaidi ya Sh114m kutoka kwa NYS bila ya kutoa huduma zozote.

Washtakiwa walikanusha mashtaka mapya yaliyowasilishwa dhidi ya wafanyakazi hao wa zamani wa NYS na wafanya biashara hwa wa familia ya Ngirita.

Kesi inaendelea.

Mswada mpya jikoni kuruhusu NYS kuhudumu KDF

Na VALENTINE OBARA

BARAZA jipya litakalobuniwa kusimamia Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS), litapewa mamlaka ya kuamua kuwatuma vijana wakahudumu katika kikosi cha Jeshi la Taifa (KDF) wakati wa vita ikiwa Mswada wa NYS 2018 utapitishwa bungeni na kuidhinishwa kuwa sheria.

Kwa sasa, Sehemu ya 17 kwenye Sheria ya NYS (2012) imempa rais mamlaka moja kwa moja kuagiza vijana wa NYS wakatumikie KDF endapo nchi itakumbwa na vita, mapinduzi au hali ya tahadhari ya kiusalama.

Lakini mswada uliopendekezwa na Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia na ukakubaliwa katika baraza la mawaziri wiki iliyopita, umemwondolea rais mamlaka hayo.

Mswada huo unasema kutakuwa na baraza ambalo limekabidhiwa majukumu makubwa ikiwemo kuamua kutuma NYS wakatumikie katika vikosi vya jeshi.

Uamuzi wa kuwatuma vijana vitani utatolewa baada ya mashauriano kati ya Baraza la NYS na Baraza la Usalama wa Kitaifa ambalo rais ndiye mwenyekiti wake huku naibu rais akiwa mmoja wa wanachama.

“Endapo sehemu yoyote ya NYS itaagizwa kuhudumu katika KDF au kwa njia nyingine katika ulinzi wa taifa ndani au nje ya Kenya, sehemu hiyo ya NYS itachukuliwa kuwa sehemu ya KDF na itasimamiwa kwa msingi wa sheria zote zinazohusu KDF,” mswada huo unaeleza.

Baraza la NYS litasimamiwa na mwenyekiti atakayeteuliwa na rais.

Wanachama wake watajumuisha Mkuu wa KDF, Mwanasheria Mkuu, katibu wa wizara inayosimamia masuala ya NYS, katibu wa Wizara ya Usalama wa ndani na katibu wa Wizara ya Fedha. Wote watakuwa huru kuteua maafisa kuwawakilisha katika baraza hilo.

Zaidi ya haya, kiapo cha vijana wanaohitimu katika NYS pia kitabadilishwa ili kifanane na cha wanajeshi kwa kuapa kuwa waaminifu na wazalendo kwa rais aliye amiri jeshi mkuu.

Kiapo cha sasa kilicho kwenye Sheria ya NYS kina aya moja pekee ambapo vijana wanaohitimu huapa kuwa waaminifu kwa shirika hilo.

Lakini kiapo kilicho kwenye mswada unaosubiriwa kuwasilishwa bungeni kina aya nne zinazofanana na kiapo cha wanajeshi. Aya mbili za kwanza zinahusu uaminifu kwa rais wa taifa.

, cha tatu kinahusu heshima kwa sheria za NYS na cha nne ni kuhusu utoaji huduma inavyohitajika bila uoga, mapendeleo wala nia mbaya.

Serikali imekuwa ikihamasisha umma kuhusu mswada huo mpya kwa msingi kuwa ukipitishwa utasaidia kuboresha huduma za NYS na usimamizi wake ili kukabiliana na sakata za ufisadi ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika shirika hilo kwa miaka kadhaa sasa.

Mswada wa NYS kuwasilishwa bungeni

Na BERNARDINE MUTANU

BARAZA la Mawaziri limeidhinisha mkataba kutoka Wizara ya Vijana na Huduma za Umma. Mkataba huo ulibuniwa kwa lengo la kuwasilishwa kwa Mswada wa Shirika la Kitaifa la Vijana (NYS) 2018.

Mswada huo una mikakati kadhaa inayolenga kuimarisha operesheni na usimamizi wa NYS miongoni mwa kuleta mabadiliko katika idara hiyo kuifanya shirika la kiserikali.

Zaidi, mswada huo unalenga kuambatisha malengo ya NYS na ajenda nne za maendeleo serikalini (Big 4 Agenda) pamoja na Ruwaza ya 2030.

“Unalenga kukabiliana na udhaifu uliobainishwa katika muundo wa NYS ambao umefanya vigumu utekelezaji mkamilifu wa wajibu wake,” ilisema taarifa kutoka kitengo cha uchapishaji cha rais (PSCU).

Pia, mswada huo unalenga kuziba nyufa katika usimamizi na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya NYS kwa lengo la kudhibiti ufisadi na uhalifu ndani ya shirika hilo.

Katika mkutano ulioendeshwa na Rais Uhuru Kenyatta Ikulu, Nairobi, na uliohudhuriwa na Naibu wa Rais William Ruto Baraza la Mawaziri pia liliidhinisha mwongozo wa utekelezaji wa mradi wa nyumba za bei ya chini, moja ya ajenda nne za maendeleo za serikali ya Jubilee.

Kesi ya tatu ya sakata NYS kuanza Februari 2019

Na RICHARD MUNGUTI

MOJA ya kesi tatu dhidi ya waliokuwa maafisa wa shirika la huduma ya  vijana kwa taifa ya sakata ya Sh469 milioni itaanza kusikizwa Februari 7, 2019.

Kesi hiyo ilitengewa siku hiyo washukiwa 44 walipofika kortini. Baadhi ya walioshtakiwa ni aliyekuwa katibu mkuu Bi Lilian Omollo , aliyekuwa mkurugenzi mkuu NYS Dkt Richard Ndubai na washukiwa wengine 41..

Kiongozi wa mashtaka Bw Gitonga Riungu alieleza Bw Ooko kuwa atatayarisha cheti kingine cha mashtaka kitakachowashirikisha washukiwa wote 47.

Faili tatu zimeunganishwa kuwa kesi moja baada ya hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti kumwamuru Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji agawanye kesi 10 zinazowakabili washukiwa hao wanaojumuisha wafanyabiashara wa Naivasha wa Familia ya Ngirita kuwa tatu.

“Kufuatia maagizo ya Bw Ogoti nimeunganisha kesi tatu kusikizwa kwa pamoja kwa vile mashahidi ni wamoja,” alisema Bw Riungu.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema kuwa kuna washukiwa watatu ambao hawajajibu mashtaka.

Mawakili wanaowatetea washtakiwa wakiongozwa na wakili Migosi Ogamba walisema wamepokea nakala za mashahidi kutoka kwa afisa anayechunguza kesi hiyo.

Mahakama ilifahamishwa kuwa nakala za usahidi ambazo hazijapokewa zitachukuliwa katika afisi ya Mkurugenzi wa Jinai (DCI).

SAKATA YA NYS: Kesi kuanza kusikizwa Januari 2019

Na RICHARD MUNGUTI

KESI ya sakata ya Sh469 milioni katika Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu Bi Lilian Omollo , aliyekuwa mkurugenzi mkuu NYS Dkt Richard Ndubai na washukiwa wengine 41 itaanza kusikizwa Januari 7, 2019.

Kesi hiyo itaanza kusikizwa na hakimu mwandamizi Bw Peter Ooko.

Kiongozi wa mashtaka Bw Gitonga Riungu alieleza Bw Ooko kuwa atatayarisha cheti kingine cha mashtaka kitakachowashirikisha washukiwa wote 47.

Faili tatu zimeunganishwa kuwa kesi moja baada ya hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti kumwamuru Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji agawanye kesi 10 zinazowakabili washukiwa hao wanaojumuisha wafanyabiashara wa Naivasha wa Familia ya Ngirita kuwa tatu.

“Kufuatia maagizo ya Bw Ogoti nimeunganisha kesi tatu kusikizwa kwa pamoja kwa vile mashahidi ni sawa,” alisema Bw Riungu.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema kuwa kuna washukiwa watatu ambao hawajajibu mashtaka.

Mawakili wanaowatetea washtakiwa wakiongozwa na wakili Migosi Ogamba walisema wamepokea nakala za mashahidi kutoka kwa afisa anayechunguza kesi hiyo.

Mahakama ilifahamishwa kuwa nakala za usahidi ambazo hazijapokewa zitachukuliwa katika afisi ya mkurugenzi wa jinai (DCI).

Bw Ooko aliamuru kuwa kesi hiyo itaendelea kila siku kuanzia Januari 7, 2019 bila kuahirishwa.

Naye Bw Ogoti ataanza kusikiza kesi tano ambazo zimeunganishwa kusikizwa pamoja kuanzia Oktoba 29 mwaka huu.

Bw Ogoti alimwamuru Bw Haji Jumanne atenganishe kesi dhidi ya washukiwa hao wote ndipo sisikizwe na kuamuliwa kwa haraka.

“Kesi hizi zitasikizwa kila siku pasi kuahirishwa,” aliagiza Bw Ogoti.

Aliagiza washtakiwa wanaotaka kusuluhisha kesi dhidi yao na DPP wafanye hivyo na kuwasilisha makubaliano mahakamani.

Pia aliwaonya mawakili dhidi ya kuzembea katika kazi zao za kuwatetea washtakiwa akisema , “kesi hizi hazitacheleweshwa na kutokuwako kwa mawakili.”

Mahakama iliwatahadharisha mawakili na washtakiwa dhidi ya kufanya njama za kuahirisha kesi.

Katika kesi hiyo, washtakiwa watano kutoka kwa familia moja (Ngirita) wamefunguliwa mashtaka.

NYS: Agizo DPP atenganishe kesi kumi mara tatu

Na Richard Munguti

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Haji Jumanne aliamriwa atenganishe mara tatu kesi kumi za kashfa ya Sh469milioni zilizoibwa kutoka kwa Shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS) dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu Bi Lilian Omollo na washukiwa wengine 50.

Hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi (ACC) Bw Douglas Ogoti alimwamuru DPP awasilishe ushahidi pasi na kuchelewa katika kesi hii iliyo na umuhimu wa kitaifa.

Bw Ogoti aliagiza DPP aanze kuwasilisha ushahidi Oktoba 29 2018 na kuendelea pasi kusitishwa hadi Desemba 7 2018. Hakimu alimwamuru DPP atenganishe kesi hizo ziwe tatu na kumtaka awasilishe mashtaka mapya dhidi ya washukiwa katika kesi hizo.

“ Kesi hii imeahirishwa mara tatu ili DPP awe na muda wa kuwapa washukiwa ushahidi lakini hili limeshindikana.Lazima nichukue msimamo kama korti na kutoa mwelekeo. Lazima kesi ianze kusikizwa Oktoba 29, 2018,” akasema Bw Ogoti.

Pia alimtaka DPP aendelee na kupokea ushahidi mpya na mapendekezo ya washukiwa wanaotaka kesi zao zilisuluhishwe nje ya mahakama.

Hakimu alisema ikiwa kuna makubaliano yoyote kati ya DPP na washtakiwa yanapasa kuwasilishwa kortini kwa njia ya maandishi.

“Sitapinga washtakiwa kufika kwa DPP kuungama waliyotenda kuhusu kashfa hii, lakini hili halitamzuia DPP kuwasilisha ushahidi.” Bw Ogoti.

Alimtaka DPP awashtaki washukiwa ambao hawajafika kortini. Hakimu alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamishi makali kutoka kwa mawakili wanaowatetea Bi Omollo, aliyekuwa mkurugenzi wa NYS Bw Richard Ndubai pamoja na washukiwa wengine kuwa “DPP hana pupa tena ya kuendelea na kesi hiyo kinyume cha kasi washtakiwa walivyokamatwa na kufikishwa kortini.”

Mawakili Cliff Ombeta, Kirathe Wandugi na Assa Nyakundi waliongoza mawakili 39 kulalamika kuwa DPP “anakandamiza haki za washtakiwa waliofikishwa kortini pasi kupewa nafasi ya kupumua walipotiwa nguvuni.”

“Washtakiwa walikuwa wanatiwa nguvuni kwa sarakasi ambayo wao wenyewe hawakufahamu kwani walikuwa wanaona kama ni filamu wanatazama filamu,” alisema Bw Wandugi. Wakili huyo alisema vyomba vya habari vya humu nchini na kitaifa zilifurika mahakamani na kupeperusha kushikwa na kushtakiwa kwa washukiwa hao 50.

Bw Ombeta alimweleza hakimu kuwa jambo la kushangaza ni kuwa afisi ya DPP haijawapa nakala za mashahidi licha ya wao kupeleka makaratasi rimu 10 kutengeneza nakala za mashahidi.

Bw Ombeta alisema kuwa kuna kesi kumi dhidi ya washukiwa miongoni mwao familia ya watu watano wa Mzee Ngirita waliofikishwa kortini wote mama na bintize watatu na mwanao.

“Bado hatujapewa nakala za mashahidi. Kuna mashtaka 147 na faili za kesi hii ni 10. Kila faili inatakiwa kutenganisha ndipo kila kesi iendelee kivyake,” alisema Bw Ombeta.

Alilalamika kuwa kesi hiyo imetajwa mara tatu lakini viongozi wa mashtaka Bi Emily Kamau na Bw Alexander Muteti wameshindwa kuwapa nakala za mashahidi na “ hata kuna washukiwa watano bado kushikwa na kushtakiwa kortini.”

Bi Kamau aliomba muda wa siku 21 kukamilisha uchunguzi na kuwakabidhi washtakiwa ushahidi akiongeza , “baadhi ya washtakiwa wanaomba muda wasikizane na DPP ndipo kesi dhidi yao ziondolewe.”

Mashahidi 43 kuitwa kwenye kesi ya NYS

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa mashtaka ya umma (DPP) Jumatano alisema ataita mashahidi 43 kutoa ushahidi katika kesi inayowakabili washukiwa 47 wa sakata ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa NYS.

Washukiwa wamekanusha mashtaka ya wizi wa zaidi ya Sh468milioni , matumizi mabaya ya mamlaka na kutozingatia kwa sheria za ununuzi wa bidhaa zilizowekwa na Serikali.

Kiongozi wa mashtaka alimweleza hakimu mkuu , mahakama ya kesi za ufisadi katika mahakama ya Milimani Nairobi Bw Douglas Ogoti kuwa kila shahidi atachukua muda wa masaa mawili kutoa ushahidi dhidi ya washukiwa hao 47.

“Kila mmoja wa mashahidi hawa 43 atachukua muda wa masaa mawili kutoa ushahidi kisha ahojiwe na mawakili 40 wanaowatetea washtakiwa,” hakimu alifahamishwa.

Walioshtakiwa ni pamoja katibu mkuu Bi Lillian Omollo na aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa NYS Richard Ndubai.

Mawakili walisema watachukua muda sawa na huo kila mmoja kuwahoji mashahidi.

Washtakiwa wote 47 walikanusha mashtaka dhidi yao na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh8milioni kila mmoja.

Miongoni mwa wale ambao hawajalipa dhamana ni pampja na Bi Anne Wambere Ngirita Bi Anne Wambere Ngirita , baba yake na dada zake wawili.

Mama yao Bi Lucy Ngirita alifaului kumpata mtu wa kumsimamia dhamana.

Wengine wa familia hiyo ya Ngirita hawajalipa dhamana na wanaendelea kuzuiliwa katika gereza la viwandani na Kamiti.

Familia ya Mzee Ngirita iliyoshtakiwa kwa ufisadi huo wa zaidi ya Sh468milioni ingali katika magereza ya Viwandani na Langata mtawalia.

Walioshtakiwa ni pamoja na Bi Anne Wambere Ngirita aliyshtakiwa kupokea Sh60milioni.

Shtaka lilisema kuwa hakuwa ametoa huduma zozote kwa shirika hilo ndipo alipwe pesa hizo.

Washtakiwa hao wamekaa gerezani kwa zaidi ya mwezi mmoja huku wakijikakamua kulipa dhamana hiyo.

Bi Omollo na Bw Ndubai  aliyekuwa mkurugenzi aliondoka siku chache baada ya Jaji Hedwiq Ong’undi kuwapa dhamana  mnamo Juni 19.

Washukiwa 47 wa sakata hiyo ya NYS walishtakiwa kwa makossa mbali mbali.

Kesi inaendelea.

Hamtawahi kusikia wizi tena NYS, serikali yaahidi Wakenya

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imewahakikishia Wakenya kuwa Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) halitakumbwa na kashfa nyingine baada ya uongozi mpya kuchukua usukani.

Waziri wa Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Profesa Margaret Kobia Jumatano alitoa hakikisho hilo alipomjulisha rasmi Mkurugenzi Mkuu mpya Bi Matilda Sakwa kwa Wakenya, katika hafla fupi iliyofanyika katika makao makuu ya shirika eneo la Ruaraka Nairobi.

Bi Sakwa ambaye kabla ya kuteuliwa kwake alikuwa Kamishna wa Kaunti ya Machakos anakuwa mahala pa Richard Ndubai ambaye mwezi Juni alikamtwa kuhusiana na sakata ya wizi wa Sh9 bilioni katika shirika hilo.

Bw Ndubai, ambaye alikamatwa pamoja na Katibu wa Wizara hiyo Bi Lilian Omollo, aliachiliwa kwa dhamana baada ya kuzuiliwa kuziuzini kwa mwezi mmoja.

“Kwanza ningependa kuomba msamaha kwa Wakenya kufuatia kutokea kwa sakata mbili katika NYS ambazo zimetoa picha mbaya kuhusiana na kazi tunayofanya hapo.

Kwa hivyo, tunaposimama hapa kumkaribisha Mkurugenzi Mkuu mpya ningependa kuwahakikishia Wakenya sakata nyingine sawa na hiyo haitatokea tena katika shirika hili,” Profesa Kobia akasema.

Aidha, Waziri huyo, ambaye aliteuliwa kusimamia wizara hiyo mapema mwaka huu, alisema chini ya uongozi wa Bi Sakwa pesa za NYS hazitafujwa wala kuibiwa, bali zitatumika kwa shughuli zilizokusudiwa.

Akaongeza: “Na madeni yote ambayo hayajalipwa ya kima cha Sh5.6 bilioni yaliyolimbikizwa kuanzia mwaka wa 20013 hadi 2017 hayatalipwa. Tunataka kuendesha uchunguzi kubaini uhalali ya madeni hayo, ili kuzuia visa vya malipo kutolewa kwa wafanyabiashara walaghai.”

Akiongea katika hafla hiyo, Bi Sakwa aliwaomba Wakenya kumpa muda ili aweze kujifahamisha na majukumu ya afisi yake katika wadhifa wake mpya.

Hata hivyo, aliihakikishia serikali kuwa atafanya kila awezalo ili kuleta mabadiliko katika shirika hilo kanda na “kuleta uthabiti katika usimamizi wa rasimali zake zote.

“Kwa hivyo, nawaomba Wakenya na wafanyakazi wote wa NYS kuniunga mkono ili niweze kufanyakazi kwa manufaa ya wote.”

SAKATA YA NYS: Dhamana ya Lillian Omollo yakubaliwa,aondoka gerezani

Na RICHARD MUNGUTI

KATIBU mkuu Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Bi Lillian Omollo alikuwa wa kwanza kuruhusiwa kuondoka gerezani baada ya dhamana alizowasilisha kukubaliwa na mahakama.

Bi Omollo na washukiwa wengine wawili watapumua hewa safi wakiwa huru baada ya kukaa gerezani siku 26 tangu Mei 28, 2018 walipozuiliwa baada ya kushtakiwa kwa sakata ya NYS iliyopelekea zaidi ya Sh460milioni kupotea.

Bi Omollo ataondoka gereza la Langata anakozuiliwa baada kutupiliwa mbali kwa ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kwamba dhamana zote watakazowasilisha washtakiwa zikaguliwe na kuidhinishwa na shirika la urejeshaji mali ya umma iliyoibwa ARA.

Katika barua aliyokuwa ameandikia mahakama Alhamisi Bw Haji alikuwa ameitaka korti iruhusu ARA iidhinishe dhamana hizo  alizosema huenda zilinunuliwa na pesa zilizoibwa NYS.

Ombi hili lilipingwa vikali na mawakili wanaowatetea washtakiwa wakisema Bw Haji anajaribu kuhujumu maagizo ya korti.

Akitupilia mbali ombi hilo la Bw Haji hakimu mwandamizi Bw Lawrence Mugambi ni mahakama tu iliyo na mamlaka ya kukataa dhamana na kuruhusu zoezi la ukaguzi liendelee.

Bw Mugambi alisema DPP hana mamlaka kisheria kuweka masharti mapya katika utaratibu wa kuwahoji wadhamini na uhalali wa dhamana walizowasilishwa washtakiwa.

Alisema kuwa Bw Haji atakiuka sheria ikiwa ataruhusiwa kuvuruga maamuzi ya mahakama kuu iliyoweka masharti ya kuachiliwa kwa dhamana kwa washukiwa hao wa sakata ya NYS ambapo zaidi ya Sh400milioni zillibwa kwa kulipia huduma ambazo hazikutolewa.

Mahakama kuu iliwaachiliwa washtakiwa hao Juni 19 2018.

Akiwaachilia kwa dhamana Jaji Hedqig Ong’udi aliamuru kila mshukiwa awasilishe dhamana ya Sh5 milioni na mdhamini wa Sh2 milioni pamoja na dhamana ya pesa tasilimu Sh1milioni.

Bw Mugambi alisema suala alilozua DPP ni nzuri katika jitihada za kupambana na ufisadi lakini halikuwa moja ya masharti ya Jaji Ong’undi.

Alisema kama DPP angelitaka ARA ishirikishwe katika ukaguzi wa dhamana , angeliomba Jaji Ong’undi atoe agizo kwamba dhamana zote ziidhinishwe na shirika hili la urejeshaji mali ya umma iliyoibwa.

“Sitamruhusu DPP awe kizingiti katika utekelezaji wa maagizo ya Mahakama kuu katika ukaguzi wa dhamana na mahojino na wadhamini,” alisema Bw Mugambi.

Hakimu huyo alisema Jaji Ong’undi alikuwa ameamuru wadhamini wakaguliwe na mahakimu wa mahakama zinazosikiza na kuamua kesi za ufisadi.

Wakipinga masharti hayo mapya aliyowasilisha DPP, mawakili Dunstan Omari, Cliff Ombeta, Kirathe Wandugi walisema kinara huyu wa mashtaka anavuruga utenda kazi wa mahakama akiwa na nia “ washtakiwa wote 47 washindwe kulipa dhamana waliyopewa.”

Bw Omari aliomba korti imwekee muda Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI)  muda wa siku tatu au wiki moja akamilishe kukagua uhalali wa dhamana walizowasilisha washtakiwa na kutoa ripoti kwa mahakama.

“Tutakaa hapa muda wa miezi mitatu au minne na hata mwaka ikiwa Polisi na DPP wataruhusiwa kuvuruga utaratibu wa kuidhinisha dhamana zilizowasilishwa na washtakiwa hawa 47,” alisema wakili Assa Nyakundi.

Lakini mahakama iliamuru shughuli ya kukagua wadhamini iendelee na ikiwa kutaimbuka suali kuhusu dhamana yoyote ile basi DPP atakuwa huru kuapa Afidaviti akiomba ARA ichunguze dhamana husika.

“Kila mshtakiwa atakaguliwa kivyake. Ikiwa kutazuka swali kuhusu dhamana zitakazowasilishwa na washtakiwa basi DPP kupitia afisa anayechunguza kesi hiyo Bw Paul Waweru atahoji stakabadhi hiyo,” Bw Mugambi aliamuru.

Mlima wa nakala za ushahidi kwenye kesi ya wizi NYS

Na RICHARD MUNGUTI

HAKIMU anayesikiza kesi ya ufisadi dhidi ya washukiwa 41 wa sakata ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa NYS wanaoshtakiwa kwa ubadhirifu wa mamiloni ya pesa alimwamuru mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP Noordin Haji awape washukiwa nakala za ushahidi ifikapo Juni 25, Jumatatu .

Bw Douglas Ogoti anayesikiza kesi dhidii ya  katibu mkuu wizara ya umma , jinsia na vijana Bi Lillian Wanja Muthoni Mbogo Omollo anayeshtakiwa pamoja na aliyekuwa kinara wa NYS Richard Ndubai na washukiwa wengine 39 akiwamo mwanamitindo Ann Wambere Ngirita aliagiza wapewe mabunda ya ushahidi waanze kuandaa ushahidi.

Mawakilii Cliff Ombeta alimweleza Bw Ogoti kuwa wamechoka kuomba DPP awape nakala za mashahidi. “Naomba hii korti iamuru tupewe nakala za mashahidi. Washukiwa hawa wameanza kuingiwa na woga kwamba ushujaa ninaosifika kuwa nao haupo.”

Ombi hilo liliungwa mkono na mawakili wengine 34 wakisema upande wa mashtaka umeorodhesha mashahidi 36 katika kesi moja tu na kuna kesi kumi..

“Hatuwezi kuwashauri washtakiwa na kuandaa tetezi zao. Hatujapewa nakala za ushahidi,” alisema Bw Ombeta.

Bw Ogoti aliamuru kesi hiyo itajwe tena Julai 17 2018 ndipo mawakili waeleze ikiwa walipokea nakala za usahidi kisha waeleze muda watakaochukua kuwahoji mashahidi.

Kiongozi wa mashtaka alisema amewasilisha nakala zaidi ya 100 kortini na kuwa mawakili wako huru kwenda kuzichukua kwa afisa anayechunguza kesi hiyo Inspekya Paul Waweru.

Washtakiwa walirudishwa rumande katika magereza ya Viwandani na Langata baada ya kueleza ugumu waliokumbana nao kulipa dhamana ya Sh8milioni.

Washukiwa wa NYS wanyimwa dhamana tena

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA wote41 wa sakata mpya ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa NYS wanaodaiwa walifuja zaidi ya Sh9 bilioni wataendelea kukaa gerezani baada ya hakimu kukataa kubatilisha masharti ya dhamana yaliyowekwa na Jaji Hedeiq Ong’undi Jumanne.

Hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti alisema kamwe “hawezi ng’o kuvuruga amri ya Mahakama kuu licha ya tetezi washtakiwa hawawezi kulipa dhamana hiyo kwa vile wako na mapato ya viwango mbali mbali.”

Badala ya kubatilisha Bw Ogoti alitoa maagizo mapya. Jaji Ong’undi alikuwa amewaamuru washtakiwa walipe dhamana ya Sh8milioni.

Akiwaachilia kwa dhamana Jumannne , Jaji Ong’undi aliwaamuru washtakiwa walipe kila mmoja dhamana ya pesa tasilimu Sh1milioni , wawasilishe dhamana ya Sh5milioni na mdhamini wa Sh2milioni atakayeidhinishwa na hakimu mkuu.

Kupitia kwa mawakili wao washtakiwa wote walimlilia Bw Ogoti awabatilishie masharti waliyopewa wakisema “ itakuwa vigumu kuyatimiza.”

Akasema Bw Ogoti , “Hii mahakama haiwezi kamwe kuvuruga au kugeuza maagizo ya Jaji Ong’undi. Hii korti haina mamlaka kamwe kuingilia maamuzi ya Mahakama kuu.”

Bw Ogoti alisema kuwa jukumu ambalo Jaji huyo aliwapa mahakimu ni kuwahoji wanadhamini watakaofika kortini kuwasimamia dhamana washtakiwa.

Bw Ogoti aliwaamuru washtakiwa hao wawasilishe barua zinazoidhinisha uhalali wa hati za umiliki mashamba ama vyeti vya umiliki wa magari.

Pia aliwataka washtakiwa wawsilishe ripoti ya msajili endapo watategemea vyeti vya umiliki wa magari.

Pia aliwataka kila mmoja awasilishe kitambulisho chake cha kitaifa.

“Mbali na kitambulisho cha kitaifa kilichoidhinishwa na msajili ,,mtawasilisha hapa kortini barua iliyoandikwa na afisa anayechunguza kesi hii akihidhinisha stakabadhi zote mtakazowasilisha kama dhamana sio ghushi,” alisema Bw Ogoti.

Hakimu alisema kusikizwa kwa kesi kwapasa kung’oa nanga lakini kizingiti ni “afisi ya DPP ambayo haijawapa washtakiwa nakala za mashahidi waandae tetezi zao.”

Alitenga Julai 17 iwe siku mawakili kueleza muda watakaochukua kuwahoji mashahidi.

Mawakili zaidi ya 30 wakiongozwa na Mabw Cliff Ombeta . Kirathe Wandugi, Assa Nyakundi , Migos Ogamba na Kimani wa Wakimaa walimweleza hawajapewa nakala hizo na jitihada zao za kuzipata zimegonga mwamba.

Bw Ogoti aliamuru mmoja washtakiwa Bi Lucy Ngirita , mama ya Ann Wambere Ngirita na nduguze apelekwe kutibiwa katika hospitali kuu ya Kenyatta iwapo haridhiki na huduma anazopokea katika Kliniki cha Gereza la Langata anakozuiliwa pamoja na Katibu mkuu Wizara ya Umma , Jinsia na Vijana Bi Lillian Wanja Muthoni Mbogo Omollo.

Wabunge wamkemea Waiguru kuwatisha kwa kumhusisha na ufisadi NYS

Na CHARLES WASONGA

Mbunge wa Shinyalu Justus Kizito amemkaripia Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru kwa kutisha kuwashtaki wabunge ambao walimhusisha na sakata ya wizi wa mabilioni ya pesa za umma katika Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS).

Akiongea na wanahabari Jumatano katika majengo ya bunge Bw Kizito alisema wabunge ambao walilengwa na Bi Waiguru hawatamwomba msamaha jinsi alivyotaka kwani walikuwa wakifanyakazi kazi yao ya kulinda mali ya umma na? kupambana na ufisadi.

“Waiguru anafaa kuelewa kuwa Katiba ya Kenya inawapa wabunge mamlaka ya kuchunguza masuala yenye umuhimu kwa taifa. Na wizi wa Sh9 bilioni na Sh791 milioni katika NYS sio masuala mepesi.

Kwa hivyo, Waiguru hafai kuwatisha wabunge wanapofanya kazi yao ya kutaka yeye na watu wengine waliosimimia shirika hilo wachunguzwe,” akasema Mbunge huyo wa ODM huku akimhakikishia Rais Uhuru Kenyatta kuwa wanaounga mkono vita dhidi ya ufisadi.

“Waiguru anafaa kutisha Wakenya wanaolalamikia wizi wa pesa zao chini ya usimamizi wake wala sio sisi. Wakenya wamepoteza jumla ya Sh10 bilioni kupitia NYS na wahusika wote wanafaa kuadhibiwa bila huruma,” akaongeza Bw Kizito.

Aliandamana na wabunge; Justus Kizito (Shinyalu, ODM), Alpha Miruka (Bomachoge Chache, KNC), Tindi Mwale (Butere, ANC) na mbunge maalum Sammy Saroney (Wiper).

Mnamo Jumanne Bi Waiguru alitoa makataa ya siku saba kwa Bw Ali, na wenzake, kumwomba msamaha, kwa maandishi, la sivyo, awafungulie mashtaka mahakamani kwa kumharibia jina.

“Tumepewa agizo kwamba ikiwa hautaondoa matamshi hayo na kuomba msamaha ndani ya muda wa siku saba tutaanzisha mashtaka dhidi yako, na wenzako,” wakili wa Bi Waiguru Mohammed Muigai alisema Jumanne kwenya taarifa.

Kulingana na Waiguru maneno yaliyotumiwa na Bw Ali dhidi yake yaliashiria kuwa yeye ni mwizi na mnyakuzi wa pesa za umma, kando na kutostahiki kushikilia afisi ya umma.

Wabunge wengine aliowalenga ni; Mbw Mwale, Caleb Amisi (Saboti, ODM) na Kuria Kimani (Molo, Jubilee).

 

Wanaofaa kuchunguzwa kwa wizi NYS

Wabunge hao walikuwa wamedai kuwa Bi Waiguru, aliyekuwa Mkuugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) Ndegwa Muhoro, Waziri wa Afya Sicily Kariuki na mwenzake Mwangi Kiunjuri (Kilimo) wanapasa kuchunguzwa kuhusiana na wizi wa Sh9 bilioni katika NYS.

Bi Waiguru alikuwa waziri wa Ugatuzi na Mipango sakata ya kwanza ya kupotea kwa Sh791 milioni katika NYS. Bw Kinjuri na Bi Kariuki pia waliwahi kushikilia wadhifa huo baada Waiguru kujiuzulu kutokana na shinikizo za umma.

Wabunge hao pia walipendekeza kuchunguzwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NYS Nelson Githinji na naibu wake Sam Michuki, Inspekta wa Polisi Julius Muia, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Petro Kenya Oil Gor Semelang’o pamoja na wafanyabishara Ben Gethi na Peter Gathecha.

Akiongea kuhusu vitisho vya Bi Waiguru Bw Ali, maarufu kama “Jicho Pevu” alisema: “Tunamwogopa Mungu pekee. Hatumwogopi Waiguru. Vitisho vyake ni bure… aende mahakamani alivyotisha. Hatuwezi kusuluhisha awamu ya pili ya sakata ya NYS bila kuangazia sakata ya kwanza. Ikiwa Waiguru ni msafi mbona anaingiwa na wasiwasi?”

“Nimetumwa bungeni na watu wa Nyali kutetea wizi wa pesa wanazolipa kama ushuru kwa serikali. Kwa hivyo, sitaogopa vitisho kutoka kwa mtu yeyote na sitaomba msamaha kwa kutaja majina ya watu wakubwa kama Waiguru na wengineo katika sakata hii ya NYS,” akaongeza mbunge huyo ambaye hakuchaguliwa kwa tiketi ya chama chochote bungeni.

Waiguru atisha kumshtaki Jicho Pevu kwa kumhusisha na wizi NYS

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru ametisha kumshtaki Mbunge wa Nyali Mohammed Ali kwa kumhusisha na sakata ya wizi wa Sh9 bilioni NYS.

Bi Waiguru ametoa makataa ya siku saba kwa mbunge huyo awasilishe msamaha kwa maandishi la sivyo amfungilie mashtaka.

Bw Ali, maarufu kama Jicho Pevu, pia alipendekeza kuwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) Ndegwa Muhoro pia achunguzwe kuhusiana na sakata hiyo.

Mbunge huyo aliorodhesha kampuni 40 ambazo alisema zinapasa kuchunguzwa kwa kuhusika moja kwa moja na sakata hiyo

“Tumepewa agizo kwamba ikiwa hautaondoa matamshi hayo na kuomba msamaha ndani ya muda wa siku saba tutaanzisha mashtaka dhidi yako ambayo yatakugharimu pakubwa,” wakili wa Bi Waiguru Mohammed Muigai alisema Alhamisi kwenye taarifa Jumanne.

Kulingana na Waiguru maneno yaliyotumiwa na Bw Ali yaliashiria kuwa yeye ni m mwizi na mnyakuzi wa pesa za umma, kando na kutostahiki kushikilia afisi ya umma.

“Mteja wetu amesema maneno ambayo yalitumiwa yalilengwa kumharibia sifa na kumwondolea heshima ilhali yeye ni afisa wa umma anayeheshimika,” taarifa hiyo ikaongeza.

Kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Jumanne Bw Ali pia aliwaambia mawaziri Mwangi Kiunjuri, Sicily Kariuki na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa Samsom Muchuki wajitokeze waelezee kile wanachojua kuhusu sakata hiyo.

“Kiunjuri na Kariuki wamewahi kuhudumu katika Wizara hii ambayo inasimamia NYS. Kwa hivyo, wanafaa kujitokeza na kuelezea kile wanachojua kuhusu sakata hii,” akasema Bw Ali ambaye alikuwa ameandamana na wenzake, Tindi Mwale (Butere) na Caleb Amisi.

Wabunge hao waliwataja washukiwa waliokamatwa kuhusiana na sakata hiyo kama samaki wadogo.

“Tungetaka papa na nyangumi pia wakamatwe ili tuwe na matumaini kwamba serikali inajituma katika vita hivi dhidi ya ufisadi,” akasema Bw Amisi ambaye ni Mbunge wa ODM.

Wabunge hao walisema hayo saa chache baada ya Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Utumma, Vijana na Jinsia Lilian Mbogo Omollo, Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai na washukiwa wengine 41 kuachiliwa huru kwa dhamana ya Sh1 milioni kila mmoja.

Hii ni baada ya wao kukaaa korokoroni kwa zaidi ya wiki tatu.

Uamuzi kuhusu dhamana kwa washukiwa 47 wa NYS kutolewa Juni 19

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA wote 47 wanaoshtakiwa kwa sakata ya mamilioni ya pesa katika Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) Jumanne waliwasilisha maombi ya kuachiliwa kwa dhamana katika Mahakama kuu.

Washukiwa hao kupitia kwa mawakili zaidi ya 30 wakiongozwa na Mabw  Cliff Ombeta, Kirathe Wandugi,  Assa Nyakundi , Migos Ogamba na  Kimani wa Wakimaa walimweleza Jaji Hedwig Ong’undi (pichani) “haki za kimsingi za kuachiliwa kwa dhamana zilikiukwa na hakimu mkuu Douglas Ogoti aliyeamuru wasalie gerezani hadi kesi isikizwe na iamuliwe.”

Na wakati huo huo, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupitia kwa wakili Bw Duncan Ondimu alisema “ dhamana katika kesi zote zinazohusu hujuma za kiuchumi zitakuwa zinapingwa vikali.”

Bw Ondimu alisema kesi zote za ufisadi na hujuma za kiuchumi zitakuwa zinasikizwa kwa siku chache.

Bw Ondimu alisema ushahidi wote dhidi ya washukiwa wote wa NYS wanaokabiliwa na  mashtaka ya matumizi mabaya ya mamlaka uko tayari na “ kesi inaweza kuanza kusikizwa  wakati wowote.”

Akipinga washukiwa wakiachiliwa kwa dhamana , Bw Ondimu alisema washtakiwa watawafuruga mashahidi.

“Mashahidi wengi katika kesi hii walikuwa wadogo wa washukiwa hawa kazini na ni rahisi kuwavuruga,” alisema Bw Ondimu.

Wakili Assa Nyakundi awasilisha tetezi mahakamani. Picha/ Richard Munguti

Lakini msimamo huo wa DPP ulikumbana na upinzani mkali kutoka kwa mawakili wanaowatetea washtakiwa.

Mabw Ombeta , Nyakundi , Karathe , Wa Kimaa na Ogamba walisema idara ya mahakama imethibitiwa kabisa na watu wenye ushawishi mkubwa serikalini.

Wakilaani matamshi ya afisa wa Polisi anayechunguza kesi hii Inspekta Paul Waweru kuwa “ atahakikisha  kesi hii imesikizwa kwa upesi na hata ikibidi masaa ya kuisikiza na kuiamua yaongezwe.”

“Je,  afisa huyu wa polisi ametoa wapi mamlaka ya kuwasimamia mahakimu na majaji. Matamshi haya yana maana kuwa mahakimu na majaji wameanza kuthibitiwa ,” alihoji Bw Nyakundi.

Mahakama iliombwa isipitoshwe na matamshi ya DPP kuwa kesi itaendelezwa kwa upesi.

“Ikiwa ombi la dhamana dhidi ya washukiwa 22 ilichukua muda hadi saa nane unusu usiku je kesi hizi 10 zitachukua muda gani?” Bw Nyakundi alimwuliza Jaji Ong’udi.

Washukiwa hao 47 ni pamoja na aliyekuwa Meneja Mkurugenzi wa NYS Bw Richard Ndubai , Katibu wa Wizara  Bi Lilian Omollo, mfanyabiashara Bi Ann Wambere waliomba korti iwaachilie kwa dhamana.

Jaji Ong’udi atatoa uamuzi wa dhamana mnamo Juni 19, 2018.

Awali malumbano makali kati ya mawakili wa washukiwa na Bw Ondimu kuhusu agizo la Bw Ogoti kwamba washukiwa wapeanze robota 10 za makaratasi ya kufanyia nakala za ushahidi.

“Agizo hili halifai. La fedhehesha Serikali. Kwani Serikali haina pesa. Ni sheria washukiwa wapewe nakala za mashahidi na afisi ya DPP.

SAKATA YA NYS: Wabunge wa Jubilee na Nasa wataka Waziri Kariuki ang’atuliwe

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE watano Alhamisi walimtaka Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki ajiuzulu la sivyo watamtimua afisini kuhusiana na sakata ya Sh9 bilioni katika Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS).

Wakiongozwa na Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro wabunge hao kutoka mirengo ya Jubilee na NASA, pia walimtaka Rais Uhuru Kenyatta kumsimamisha kazi Bi Kariuki la sivyo waanzishe mchakato wa kumng’oa mamlakani kwa kupitisha hoja ya kutokuwa na imani naye bungeni.

Huku wakipendekeza kushtakiwa kwa waziri huyo, wabunge hao walidai kuwa washukiwa 43 waliokamatwa juzi, wakiwemo Katibu wa Wizara Lilian Omollo na Mkuregenzi wa NYS Richard Ndubai, “ni samaki wadogo”.

Pesa hizo zilipotea katika mwaka wa 2016, Bi Kariuki akiwa mamlakani kama waziri aliyesimamia NYS.

“Kitendawili cha sakata ya NYS hakiwezi kuteguliwa ikiwa Bi Sicily Kariuki hataondoka afisini kisha afunguliwe mashtaka. Haiwezekani kwamba Sh9 bilioni zinaweza kupotea au kuibiwa bila waziri kujua,” Bw Osoro, ambaye ni Mbunge wa chama cha Kenya National Congress (KNC), alisema jana kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

Aliandamana na wabunge Moses Kirima (Imenti ya Kati, Jubilee), Tindi Mwale (Butere, ANC), Abdikarim Osman (Fafi, Kanu) na Meja Bashir Abdulahi (Mandera Kaskazini, Jubilee).

Wabunge hao walisema wanamuunga mkono Rais Kenyatta pamoja na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kutokana na kujitolea kwao kupambana na ufisadi, wakiahidi kupiga jeki mchakato huo kwa kupitisha sheria husika bungeni.

Washukiwa 43 wa sakata hiyo wangali kwenye rumande baada ya Hakimu Mkuu Douglas Ogoti kuwanyima dhamana.

Wito wa jana ni wa pili kutolewa na wabunge mwaka huu kumtaka Waziri Kariuki kuondoka afisini. Shinikizo za kwanza zilianzishwa Machi mwaka huu.

wabunge 170 walipotia saini hoja ya kumtaka ajiuzulu kwa kumsimamisha kazi aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) Bi Lily Koros.

Hoja hiyo ilifeli kuwasilishwa bungeni baada ya Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto kuingilia kati.