SENSA: Kuna wakulima milioni 6.4 pekee nchini

Na DIANA MUTHEU

Kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa letu lakini kulingana na ripoti moja, kati ya watu milioni 47.9  nchini, ni milioni 6.4 pekee ambao ni wakulima.

Kulingana na matokeo ya Sensa ya 2019, mimea maarufu inayopandwa nchini ni mahindi na maharagwe.

“Watu 5.1 milioni walijihusisha na kilimo cha mahindi na wengine 3.6 milioni walipanda maharagwe,” ikasema ripoti.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Sensa iliyoandaliwa na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS), watu 4.7 milioni walifuga wanyama.

Akizungumza na Taifa Leo, Naibu Waziri wa Kilimo Prof Hamadi Boga alisema asilimia 60 ya wakulima nchini hupanda mahindi na maharagwe kwa kuwa watu wengi nchini hula bidhaa za mahindi kama vile ugali na Githeri.

“Kila wakati nchi inapokua, watu wachache hujihusisha moja kwa moja na kilimo shambani kwa kuwa hali ya maisha hubadilika, majengo mapya yakajengwa na watu wakahamia katika miji mikubwa.

“Tunahitaji wakulima wachache ambao watapanda mimea katika vipande vikubwa vya ardhi na wengine wajiunge na sekta ya kuboresha vyakula,” akasema Prof Boga.

Naibu waziri huyu alisema kuwa tatizo kubwa ni kuhakikisha kuwa nchi inapata mazao ya kutosha.

“Umri wa wastani wa mkulima ni 51 kwa kuwa wengi wana shamba na uwezo wa kulima. Vijana wengi uhamia katika miji mikubwa ambapo hawajihusishi na kilimo cha moja kwa moja ilhali wao ni asilimia 75 ya watu wote nchini,” akasema naibu waziri.

Katika sekta ya samaki, ripoti hii ilisema kuwa familia 109,640 ilijihusisha na uvuvi. Ufugaji wa samaki ulionekana kuwa wa chini sana huku watu 29,325 pekee wakijihusisha nao.

Prof Boga alisema jamii zingine hapo awali zilidhania samaki ni aina ya nyoka lakini walipofunzwa, wakajua ni chakula bora.

“Wakenya wengi hawali samaki sana lakini wameanza kujifunza. Kampeni za kuhamasisha watu kula samaki zitaendelea kwa kuwa ni chakula ambacho kina protini ya kutosha,” akasema.

Naibu waziri huyu alisema kuwa ufugaji wa samaki ni sekta ambayo vijana wanaweza kujitosa ili watumie talanta, ujuzi wao na teknolojia pia.

“Jamii inapoendelea kukua, watu wengi hupendelea kula vyakula vya protini ikilinganishwa na ulaji wao wa nafaka. Kilimo cha samaki ni kati ya bishara zenye pesa nyingi ambayo vijana wanafaa waingilie,” akasema Prof Boga.

SENSA: Wakenya milioni 7 hawajasoma

Na DIANA MUTHEU

WATU 7.1 milioni hawajawahi kuhudhuria shule hata siku moja, ripoti moja imeeleza.

Kulingana na matokeo ya Sensa ya mwaka wa 2019 yaliyotolewa Ijumaa iliyopita, kati ya watu 47.6 milioni humu nchini, asilimia 16.3 hawajawahi kuenda shuleni.

“Watu 7.1 milioni hawajawahi kuhudhuria shule,” ikasema ripoti hiyo ya Sensa iliyoandaliwa na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS).

Katika ripoti hiyo watu wengi ambao hawajapata elimu, asilimia 19.6 walikuwa mashambani ambao ni 5.9 milioni huku na kwa jumla walikuwa 1.1 milioni.

Ripoti yenyewe ilieleza zaidi kuwa idadi ya wanawake ambao hawajawahi kuhudhuria shule ilikuwa juu zaidi kuliko ya wanaume na ile ya watu wenye jinsia mseto. Wanawake walikuwa asilimia 17.6 ilhali wanaume walikuwa asilimia 14.9.

“Idadi ya wanawake ambao hawana elimu ni 3.8 milioni na wanaume ni 3.2. Watu wenye jinsia mseto walichukua asilimia 20.7 kwa kuwa 207 miongoni mwao hawajawahi kuenda shuleni,” ikasema ripoti.

Vile vile, ripoti hii ilifafanua kwa undani zaidi kuwa watu wengi ambao hawana elimu wanatoka katika kaunti za Garissa, Wajir na Mandera. Kaunti hizi zinapatikana katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa nchi.

Kaunti ya Garissa inaongoza kwa idadi ya watu 5.8 milioni (asilimia 75.2) ambao hawana elimu, ikifuatiwa na Mandera ambao ni 5.5 milioni (asilimia 71.9) na kisha Wajir,5.4 milioni (75.2).

Kulingana na KNBS, katika kaunti za Garissa na Wajir, idadi ya wanaume ambao hawana elimu ni juu zaidi kuliko ya wanawake. Kaunti ya Garissa ni 311,556 (asilimia 73.2) na Wajir ni 285,684 (asilimia 75.3).

“Wanawake ambao hawajawahi kuhudhuria shule katika kaunti ya Garissa ni 273,149 (asilimia 77.5) ilhali katika kaunti ya Wajir ni 263,682 (79.4),” ikasema ripoti.

Katika kaunti ya Mandera, idadi ya wanawake ambao hawana elimu ni juu zaidi kuliko ya wanaume.

Wanawake ni 284,543 (asilimia 74.1) na wanaume ni 271,252 (asilimia 69.3).?Ripoti hii ilisema kuwa watu 18,750 nchini wanahudhuria elimu ya ngumbaru. Hata hivyo, wengi wao walikuwa wa mashinani.

“Watu walio katika miji na wanasoma ngumbaru ni 3,780 ilhali wale wa mashinani ni 14,970. Wanaume ni 9,561 na wanawake ni 9,187,” ikasema.

SENSA: Simu nyingi nchini zinamilikiwa na wanawake

Na DIANA MUTHEU

WANAWAKE wengi nchini Kenya wana simu za mkono kuliko wanaume, ripoti iliyoandaliwa na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS), imeonyesha.

Kulingana na ripoti hio ya Sensa iliyotolewa Ijumaa wiki jana, kwa jumla, idadi ya watu wanaomiliki simu za rununu nchini ni 20.6 milioni.

“Watu hawa ni kutoka umri wa miaka mitatu na zaidi,” ikasema ripoti.

Hata hivyo, ripoti ilithibitisha kuwa idadi ya wanawake wanaomiliki rununu iko juu zaidi kuliko wanaume.

“Idadi ya wanawake wanaomiliki simu ni 10.4 milioni na wanaume ni 10.2 milioni,” ikasema ripoti.

Rununu ni mojawapo ya chombo ambacho hutumika sana katika mawasiliano. Miundo ya simu hizi za mkono imekuwa ikibadilika mara kwa mara kadri teknolojia inapoendelea kukua.

Pia, simu hizi zimekuwa vifaa muhimu vya kuendeleza teknolojia kwa kuwa mitandao maarufu kama vile Whatsapp, FaceBook, Twitter na nyinginezo hupatikana kupitia rununu za kisasa.

Pia, ripoti hii ya Sensa ilielezea zaidi kuwa kufikia mwaka wa 2019, kati ya watu wa umri wa miaka mitatu na kuendelea, asilimia 22.6 walitumia intaneti na wengine asilimia 10.4 walitumia kompyuta.

Ripoti pia ilisema kuwa asilimia 4.3 ya Wakenya wa umri wa miaka 15 na zaidi walitafuta na kununua bidhaa na huduma mtandaoni.

SENSA: Kina mama 180,000 hujifungulia nyumbani

Na PETER MBURU

LICHA ya mpango wa serikali wa afya kwa wote na kuondoa mfumo wa kulipisha kina mama wanaotafuta huduma za kujifungua hospitalini, bado kuna wanawake wengi wanaojifungulia nyumbani.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS), kati ya wanawake 1,340,468 waliojifungua kwa kipindi cha mwaka hadi sensa ilipofanywa Agosti 2019, 189, 464 hawakupata huduma hizo katika vituo vya afya.

Vilevile, kati ya idadi hiyo, kina mama wapatao 2,297 waliripoti kuwa hawakuwa wakijua walipojifungulia.

Takwimu za KNBS aidha zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita watoto wapatao 763,452 wamezaliwa mahali ambapo si katika vituo vya afya, huku watu 9,590 wakikosa kufahamu walijifungulia wanao wapi.

Maeneo yaliyoadhirika na hali hii zaidi ni mashambani, ambapo watoto 173,847 hawakuzaliwa hospitalini kwa kipindi cha mwaka hadi Agosti, 2019 na watu 2,031 hawakufahamu walipojifungulia.

Kaunti ya Mandera inaongoza kwa idadi ya watu ambao hawajifungulii katika vituo vya afya kwani kwa miaka mitano iliyopita, watoto wapatao 41,071 wamezaliwa nje ya vituo vya afya. Kwa mwaka mmoja, watoto 12, 463 walizaliwa nje ya vituo vya afya, kati ya idadi jumla ya watoto 26,639 waliozaliwa.

Kulingana na idadi ya watoto waliozaliwa kwa mwaka mmoja, Kaunti ya Nairobi iliongoza kwa kurekodi watoto 135,229, ikifuatwa na Kiambu kwa watoto 69,596.

Katika kaunti hizo mbili, watoto 2,206 na 1,705 mtawalia walizaliwa nje ya mahospitali.

Kaunti za Lamu na Isiolo nazo zilirekodi idadi ndogo zaidi ya watoto waliozaliwa, kwa visa 4,235 na 8,037 vya kujifungua mtawalia. Watoto 756 Lamu walizaliwa nje ya vituo vya afya, nako Isiolo watoto 2,333 wakazaliwa bila huduma za hospitali.

SENSA: Walemavu wengi ni wanawake

Na PETER MBURU

WANAWAKE wengi wako na ulemavu ikilinganishwa na wanaume, kulingana na ripoti ya sensa iliyofanywa 2019.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kati ya watu 918, 270 wa zaidi ya miaka mitano waliorekodiwa kuwa na ulemavu wakati wa sensa Agosti mwaka jana, wanawake ni 523,883.

Wakazi wa mashambani pia walichangia idadi kubwa ya walemavu kwa visa 738,778, nao wa mijini wakijumuisha 179,492. Mashambani, wanawake 422,678 waliripoti kuwa na ulemavu, wanaume wakiwa 316,071.

Mijini nako kati ya walemavu 179,492, idadi ya wanawake ilikuwa juu, wakiwa 101,205.

Kaunti iliyoripoti visa vingi vya ulemavu Kenya ni Kakamega kwa visa 47,919, kati ya idadi hiyo wanawake wakiwa 27,546.

Kaunti ya Nairobi ilifuata kwa walemavu 42,703, ambapo wanawake walikuwa 23,322. Katika kaunti hiyo, eneo la Embakasi ndilo limeathirika zaidi kwa visa 7,137, likifuatwa na Kasarani kwa visa 6,719, nalo la Makadara likiwa na visa vichache zaidi, 1,955.

Kitaifa, eneo la Kibwezi katika Kaunti ya Makueni lilikuwa na walemavu wengi zaidi wakiwa 7,962, ambapo wanawake walijumuisha 4,693.

Aina za ulemavu zilizoripotiwa zaidi ni wa kutembea, kuona, kusikia, wa akili, uwezo wa kujitunza na mawasiliano.

Wakenya 385,417 wana ulemavu wa kutembea, 333,520 wana ulemavu wa macho, 212,798 wa akili, 153,361 ulemavu wa kusikia, wengine 139,929 shida za kujitunza na wasioweza kuzungumza vyema ni 111,356.

Katika Kaunti ya Nairobi, ulemavu ulioathiri watu wengi ni ule wa macho ambapo kuna watu 18,790 kisha wa kutembea kwa visa 14,551.

Katika aina zote za ulemavu, ni katika ule wa mawasiliano pekee ambapo idadi ya wanaume inazidi ya wanawake, zikiwa 60,701 na 50,641 mtawalia.

Idadi ya mazeruzeru (albino) pia ilirekodiwa kuwa 9,729, kati yao wanaume wakiwa 4,467 na wanawake 5,261. Kaunti ya Kakamega ilirekodi kuwa na idadi ya juu zaidi ya mazeruzeru wakiwa 568, ikifuatwa na ya Meru ambapo wako 563. Kaunti za Lamu na Isiolo zilikuwa na visa vichache zaidi, kwa mazeruzeru 17 na 20 mtawalia.

Jumla ya watu 7,652 hawakueleza ikiwa walikuwa ama hawakuwa na ulemavu, kati yao wanaume wakiwa 3,821 na wanawake 3,827.

SENSA: Wakenya 20,000 hulala nje penye baridi kila siku

Na PETER MBURU

WATU wapatao 20,101 hulala nje penye kibaridi kila siku kwa kukosa makao, kulingana na takwimu zilizotolewa na Shirika la Takwimu (KNBS), kutokana na sensa iliyofanywa 2019.

Kati ya idadi hiyo, wanaume wanajumuisha 17,747 nao wanawake wakiwa 2,348 huku wanaoishi mijini wakiwa wengi kwa idadi ya 14,581, na wanaoishi mashambani ambao ni 5,520.

Kaunti ambayo haikurekodi kisa cha mtu anayelala nje ni Isiolo pekee, huku Nairobi ikiwa na visa vingi zaidi, vikiwa watu 6,743. Kati ya idadi hiyo, wanaume walikuwa 6,064 nao wanawake 679.

Takwimu za ripoti hiyo zimeonyesha kuwa wanaume wengi ndio wanalala nje, maeneo ambako wanawake wengi walirekodiwa kuwa wakilala nje yakiwa Nairobi (679), Mombasa (230), Kisumu (136) na Migori (103).

Takwimu hizi zimeripotiwa wakati serikali inaendeleza mpango wa kutengeneza nyumba za gharama nafuu, kwa lengo la kuhakikisha kuwa kila Mkenya anaishi katika mazingira nadhifu.

Vilevile, zimetolewa wakati tatizo la familia za mitaani limekuwa likisumbua mashirika ya serikali na serikali nyingi za kaunti.

, huku washikadau wakijaribu mbinu za kumaliza familia hizo.

Wakati wa kufanya hesabu hiyo, watu ambao walikuwa katika vituo vya matibabu ama kuelimishwa hawakuhesabiwa, ila ni waliokuwa mitaani pekee waliohesabiwa.

SENSA: Wakenya 14,000 wana umri wa zaidi ya miaka 100

Na PETER MBURU

KENYA ilikuwa na wazee 14,040 wanaozidi umri wa miaka 100 kufikia Agosti 2019, wakati hesabu ya watu kote nchini ilifanywa.

Kulingana na matokeo ya sensa yaliyotolewa na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS), asilimia 72.4 ya idadi hiyo ilikuwa wanawake.

Ripoti ya KNBS ilionyesha kuwa hadi wakati wa sensa, kulikuwa na wanaume 3,876 waliokuwa na zaidi ya miaka 100, na wanawake 10,164.

Hata hivyo, hakukuwa na mtu yeyote aliyeripoti kuwa katika sehemu ya watu wa jinsia mbili.

Vilevile, watu ambao hawakuwa wanafahamu umri wao walikuwa 687, kati yao wakiwa wanaume 385, wanawake 297 na watano walioripoti kuwa na jinsia mbili.

Katika sensa ya 2009, idadi hiyo haikurekodiwa, kwani waliohesabiwa walikuwa wa kati ya kuzaliwa hadi miaka 95 pekee.

Sensa hiyo ilirekodi jinsi viwango vya maisha vimepanda miongoni mwa Wakenya kwa mambo ya kimsingi kama mahali pa kuishi, kupata maji safi na kuboreshwa kwa hali ya afya.

Hayo yakiongezwa na hali kuwa serikali imekuwa ikiwapa wazee wa zaidi ya miaka 65 pesa za kiinua mgongo kila mwezi, huenda ndiyo sababu ya kuwepo kwa idadi kubwa ya wazee wakongwe.

Katika ugawaji wa umri kwa makundi, lililoongoza ni la watoto wa kati ya miaka 10 na 14, ambao walikuwa milioni 6.3.

Walifuatwa na wale wa kati ya miaka mitano na tisa waliokuwa milioni 6.2.

Matokeo hayo ya mwaka 2019 pia yalionyesha kuwa idadi ya watoto ambao hawakuwa wametimu mwaka tangu kuzaliwa ilikuwa 105,074, kati yao wakiwa wasichana 552,528, wavulana 552,508 na 38 wa jinsia mbili.

TAHARIRI: Idadi ya watu isizidi maendeleo ya nchi

Na MHARIRI

KILA mara ripoti kuhusu takwimu za watu nchini zinapotolewa, suala linaloibuka miongoni mwa wananchi wengi ni kuhusu siasa.

Utakuta midahalo inayosheheni mitandao ya kijamii na maeneo mengine ambapo watu hujumuika ni kuhusu makabila yaliyo na idadi kubwa ya watu, yale yaliyo na upungufu wa watu na jinsi idadi hizo zitakavyotumiwa kisiasa uchaguzini.

Si vibaya kutabiri mkondo wa kisiasa kwa kutumia takwimu hizi, lakini inafaa mambo yanayohusu maendeleo yapewe uzito zaidi.

Ni nadra sana kupata watu wakijadiliana kuhusu jinsi takwimu za idadi ya watu zinavyoweza kutumiwa kutabiri mkondo wa maendeleo na uchumi wa nchi.

Hata wakati baadhi ya vyombo vya habari vitakapojizatiti kufanya uchanganuzi wa kina katika kulinganisha idadi ya watu na maendeleo, ni wananchi wachache sana ambao watatilia maanani masuala hayo.

Hivi sasa, kuna wengi wanaosherehekea jinsi idadi ya makabila yao ilivyoongezeka. Hakika, kwa jumla idadi ya watu imeongezeka kitaifa.

Kile tunachofaa kujiuliza ni ikiwa kweli tuna rasilimali za kutosheleza mahitaji ya idadi hii ya watu inayoongezeka.

Hivi sasa, nchi hii inakumbwa na changamoto tele katika uzalishaji wa chakula cha kutosha, utoaji huduma bora za afya kwa bei nafuu, na huduma bora za elimu.

Ilivyobainika kwenye ripoti ya Idara ya Takwimu za Kitaifa (KNBS), hata hali ya makao ni mbovu mno kwa mamilioni ya Wakenya.

Imebainika, ni wananchi wachache sana wanaoishi katika nyumba nadhifu, huku mamilioni wakitegemea nyumba zilizojengwa kwa nyasi na udongo.

Tunaweza kulaumu wanasiasa kwa kufanya raia waamini kuwa ni muhimu kuzaana kwa wingi, eti kwa vile hiyo ni njia ya kuongeza kura za jamii na kupeleka mmoja wao hadi Ikulu.

Wanasiasa wetu wengi ni wabinafsi, na kamwe hawajali kuhusu mahitaji ya umma.

Wametelekeza majukumu yao ya kuhudumia wananchi vyema ilhali wangali wanapigia debe watu wazaane kwa wingi.

Kuna mataifa ambayo kweli yameimarika kwa kutumia idadi yao kubwa ya watu kujiletea maendeleo, lakini tujiulize, je, Kenya imefikia uwezo wa kuhitaji idadi kubwa ya watu kuendesha uchumi wake au ongezeko hili litakuwa ni laana?

Matokeo ya sensa kaunti yangu yanaogofya – Lonyangapuo

Na Oscar Kakai

GAVANA wa Kaunti ya Pokot Magharibi, Profesa John Lonyangapuo amepuuzilia mbali matokea ya sensa ya kaunti hiyo akidai kinyume na matokeo, kaunti hiyo inaongoza kwa ongezeko la idadi ya watu.

Kulingana na ripoti ya sensa, kaunti hiyo ina watu 621,241. Gavana huyo ambaye alihudhuria sherehe ya kufuzu kwa walimu katika chuo cha walimu cha West Pokot alisema matokeo hayo ni ya kuogofya na atachukua hatua kali dhidi ya Idara ya Takwimu za Kitaifa Kenya (KNBS).

Alisema anaamini idadi ya watu wa kaunti hiyo ni kati ya 830,000 na milioni 1.2 kwa sababu ilikuwa ikiongoza kwa idadi ya watoto wanaozaliwa miaka iliyopita.

“Kwani nani waliua watu wetu? Nani anafanya kina mama wetu kutozaa?” aliuliza Prof Lonyangapuo.

“Inamaanisha wanawake wa Pokot Kaskazini ni tasa na wamekataa kuzaa kwa miaka kumi na wanaume wamekauka,” akaendelea kusema.

Viongozi wa maeneo mengi wamekuwa wakilalamika kuhusu matokeo hayo ya sensa na wengine wakitishia kushtaki KNBS ili ifafanue ilivyofikia takwimu hizo wakidai huenda kuna ulaghai ulifanywa.

Lakini KNBS imeshikilia kwamba ilifuata kanuni zote za kitaifa na kimataifa zinazosimamia sensa, na kwamba imejitolea kueleza kinaga ubaga ilivyofanya kazi yake kama itatakiwa kufanya hivyo.

Wanaopinga ripoti hiyo wanadai kuna njama ya kuwapunguzia mgao wa rasilimali, huku pia kukiwa na wasiwasi kwamba ripoti hiyo itatumiwa kuamua kama baadhi ya maeneobunge yanastahili kuendelea kuwepo au yaondolewe.

 

JAMVI: Matokeo ya sensa kuzaa miungano mipya ya kisiasa

Na BENSON MATHEKA

Matokeo ya sensa, yaliyotolewa Jumatatu wiki hii, yameanza kuzua joto huku wanasiasa wakitilia shaka idadi ya wakazi wa maeneo yao.

Hata hivyo, wadadisi wanasema matokeo hayo yatabadilisha siasa za Kenya kabla ya 2022 huku wanasiasa wakiyatumia kubuni miungano ya kisiasa hasa wale wanaomezea mate kiti cha urais.

“Wanasiasa sasa watatumia idadi ya wakazi wa maeneo wanayotaka kujipigia debe. Miungano ya kisiasa itategemea idadi ya wakazi wa eneo ambalo mwanasiasa anatoka.

“Tusidanganyane, ushirika wa siasa huwa unategemea idadi ya kura ambazo mwanasiasa anaweza kuweka kikapuni,” asema mdadisi wa siasa, George Odongo.

Anatoa mfano wa miungano ya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2013 ambayo ilizaa Jubilee na Cord na kisha chama cha Jubilee na muungano wa NASA akisema ililenga maeneo yaliyo na watu wengi.

“Jubilee ilipata nguvu kutokana na kura za maeneo ya Rift Valley na Mlima Kenya wanakotoka viongozi wao Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Wake William Ruto, NASA ilikuwa na nguvu maeneo ambayo vinara wake wanne walitoka na yote ni maeneo yaliyo na watu wengi,” asema.

Kulingana na matokeo ya sensa, takriban nusu ya Wakenya wanaishi ngome za chama cha Jubilee ya Mlima Kenya, Rift Valley na Kaskazini Mashariki.

Maeneo hayo yana jumula ya watu 22.4 milioni miongoni mwa watu 47 milioni waliohesabiwa.Wadadisi wanasema hii inaweza kuzidisha mgogoro katika chama hicho tawala huku wanaomezea mate kiti cha urais wakitaka kukithibiti.

“Hata kama kitavunjika, wanasiasa watawania kushirikiana na vigogo wa kisiasa wa maeneo hayo kubuni miungano itakayochipuka kabla ya 2022,” aeleza.Ngome za muungano wa NASA ambao pia inakumbwa na mizozo, ina zaidi ya watu 20 milioni ishara kwamba vinara wake wakiutia nguvu unaweza kuitoa jasho Jubilee kwenye uchaguzi mkuu ujao ilivyokuwa 2017.

“Lakini dalili zinaonyesha kuwa miungano iliyo kwa wakati huu itavunjika na wanasiasa kutumia matokeo ya sensa kujipanga upya. Kuanzia sasa, itakuwa ni wanasiasa kujadili miungano huku wanaotoka maeneo yaliyo na watu wengi wakiwa na nafasi ya kujinadi,’ aeleza Bw Simon Kamau, mchanganuzi wa siasa.

Anasema kuna uwezekano mkubwa wa wawaniaji wa kiti cha urais kubadilisha mbinu na kulenga kaunti zilizo na watu wengi.Katika ngome za kiongozi wa ODM Raila Odinga aliyekuwa mgombeaji urais wa muungano was NASA, hali inaweza kubadilika iwapo muungano huo utavunjika.

Kuna juhudi za viongozi wa eneo la Magharibi kuungana na kushirikiana na wanasiasa wengine kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Katika eneo la Ukambani ambako kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka anatoka sensa ilionyesha kuna watu 3.5 milioni na tayari kuna minong’ono kuwa huenda akatema NASA na kuungana na kushirikana na wanasiasa wengine kubuni muungano mpya wa kisiasa.

Wadadisi wanasema kuna uwezekano mkubwa wa Bw Musyoka, Mudavadi, Wetangula wakaungana na Bw Ruto kabla ya uchaguzi huku mrengo mmoja wa Jubilee, ukiungana na Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Baadhi ya wanasiasa wa chama cha Jubilee wamekuwa wakisema kutakuwa na muungano mkubwa wa kisiasa kabla ya 2022 na wadadisi wanasema matokeo ya sensa yatachangia pakubwa muundo wake.

“Nguvu za siasa ni idadi ya watu na kwa vyovyote vile, mtu hawezi kutenga siasa na idadi ya watu katika demokrasia kama ya nchi yetu.

“Ikizingatiwa vyama vya kisiasa nchini ni vya kimaeneo na mtu hawezi kushinda urais kwa kutengemea eneo lake au jamii yake pekee, matokeo ya sensa yatatoa mwelekeo kwa miungano ya kisiasa kuanzia sasa,” alisema Bw Odongo.

Kulingana na viongozi wa chama cha Amani National Congress za Musalia Mudavadi, eneo la magharibi lina watu 6 milioni na linafaa kutumia idadi hiyo kuhakikisha litakuwa kwenye serikali ijayo.

Naibu Rais William Ruto ambaye ametangaza azma yake ya kugombea urais amekuwa akijaribu kupenya eneo hilo lililopigia NASA kura kwa wingi na kuna tetesi kwamba huenda akaungana na baadhi ya viongozi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kulingana na seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, matokeo ya sensa yatabadilisha mkondo wa siasa nchini. Kaunti ya Nairobi ina watu 4.5 milioni. “ Wanaojipanga kuwania urais lazima walenge Nairobi,” alisema.

Kiraitu, Linturi kulinda Meru ‘isivamiwe’ kisiasa

Na DAVID MUCHUI

VIONGOZI wa kisiasa katika Kaunti ya Meru wameapa kulinda eneo hilo dhidi ya ‘uvamizi’ wa wapinzani wao, huku wakiahidi kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022.

Wakihutubu Ijumaa kwenye mahafala katika Taasisi ya Kitaifa ya Kiufundi ya Meru, Gavana wa Meru Kiraitu Murungi na Seneta Mithika Linturi, waliwaomba wanasiasa ambao wametangaza kuwania urais kuwaheshimu viongozi wa eneo hilo ili kuwapa nafasi ‘kukamilisha kazi zao’.

Dkt Ruto alikuwa mgeni wa heshima katika hafla hiyo ambapo wanafunzi 1,125 walifuzu kwenye taaluma mbalimbali.

Kwenye kauli zilizoonekana kupinga ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI), wawili hao walisema kwamba watawashinikiza viongozi wengine kubuni msimamo thabiti kuhusu utatuzi wa changamoto zinazoathiri eneo hilo.

Wakirejelea matokeo ya uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra, walisema kuwa kuna haja ya viongozi kuheshimu mwelekeo wa kisiasa wa eneo hilo.

Data za sensa

Bw Linturi alisema kuwa kulingana na matokeo ya Sensa yaliyotolewa majuzi, ni dhahiri kuwa kaunti hiyo ina idadi kubwa zaidi ya watu katika eneo hilo.

“Kama tunavyoheshimu misimamo ya kisiasa ya maeneo mengine, msimamo wetu pia unapaswa kuheshimiwa. Tunapaswa kupewa nafasi ya kufanya maamuzi yetu kwa njia huru ili kujua vile tutafanya kazi na viongozi wengine. Kwa kuwa Naibu Rais huwa anazuru eneo hili sana, tutakubaliana kuhusu mwelekeo wa kisiasa tutakaochukua,” akasema Bw Linturi.

Bw Murungi aliunga mkono kauli hiyo, akisema kuwa atawashinikiza viongozi wa eneo hilo kubuni msimamo huru kuhusu ripoti hiyo.

MBURU: Viongozi watakao wakazi wazaane wamejaa ubinafsi

Na PETER MBURU

MATOKEO ya sensa yaliyotolewa na serikali wiki hii yameanika hila za baadhi ya viongozi wa kisiasa nchini tena, ambao wamekuwa wakiwapotosha wananchi kuwa na familia kubwa, hata bila kujali uwezo wao wa kukimu mahitaji yao.

Punde baada ya Shirika la Takwimu Kitaifa (KNBS) kutangaza matokeo ya hesabu ya watu iliyofanywa Agosti, jambo kuu ambalo viongozi wengi wamekuwa wakilalamikia ni kuwa, idadi ya watu ambao kaunti zao zilitangazwa kuwa nao ni ndogo mno.

Viongozi hawa wamelalamika kuwa haiwezekani kuwa wakazi wa maeneo yao wameongezeka kwa kiwango kidogo tangu matokeo ya sensa ya miaka kumi iliyopita mnamo 2009, wengi wao wakipinga uhalali wa matokeo hayo.

Cha kushangaza ni kuwa, viongozi waliojitokeza kulalamika hadi sasa ni wale maeneo yao yalikuwa na wakazi wachache. La kustaajabisha ni kwamba, hakuna yeyote aliyejitokeza kufikia sasa, kulalamika kuwa wakazi wa eneo lake ni wengi kupita kiasi.

Hakuna kiongozi ambaye ameshauri wakazi wa eneo lake kuwa na idadi ya watoto wanaoweza kulea bila changamoto za kiuchumi.

Lakini kinaya ni kwamba, kuna baadhi yao wengine ambao hata wamejitokeza kuwahimiza wakazi wao kutoshiriki mbinu za upangaji uzazi, ili wawe na watoto wengi, kuongeza idadi yao wakati wa sensa.

Ni ubinafsi ulioje kwa kiongozi kuwashauri watu kujifungua watoto wengi kwa ajili ya sensa na kuongeza idadi ya kura pekee, bila kujali jinsi mahitaji ya kila siku ya watoto hao yatakidhiwa wala mazingira watakamoishi.

Vilevile, hila kubwa kwa viongozi- ambao wana familia ndogo licha ya mapato yao makubwa inaonyesha jinsi viongozi wetu bado hawajali maslahi ya wananchi, ila kila mara wao husukuma ajenda zitakazowanufaisha tu na kuwakweza kisiasa.

Miaka ya nyuma, taifa lilishuhudia matukio ya kutamausha, ambapo viongozi walijitokeza wazi kusifia hali ya watu kujifungua watoto wengi, wakati wengi wa wanaopotoshwa hivi huwa ni maskini wasio na mapato.

La kuudhi zaidi ni kuwa, viongozi wa kike pia wamekuwa wakihusika katika upotoshaji huu wa watu, licha ya kuwa ndio wanatarajiwa kuwa mstari wa mbele kushauri kina mama na wazazi kwa jumla, kujifungua watoto ambao wana uwezo wa kuwalea na kuwasomesha ipasavyo.

Takwimu za sensa ni feki sana – Magavana

Na WAANDISHI WETU

MATOKEO ya Sensa yaliyotolewa Jumatatu yameibua joto huku baadhi ya wanasiasa na wataalamu wakitilia shaka uhalisi wake na kutaka shughuli hiyo irudiwe.

Magavana kutoka kaunti zilizoorodheshwa kuwa na idadi ndogo ya watu walidai kuwa matokeo hayo yalilenga kutimiza maslahi ya kisiasa hasa wakati huu mjadala unatarajiwa kuhusu ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) lililobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga.

Kulingana na viongozi hao, matokeo hayo yalikarabatiwa ili kunyima baadhi ya maeneo haki ya uwakilishi na mapato kutoka serikali ya kitaifa.

Viongozi wa kaunti ya Tharaka Nithi waliojawa na hasira, walitilia shaka matokeo hayo yaliyoonyesha kuwa kaunti yao ina watu 393,177 ikilinganishwa na 365, 847 kwenye sensa ya 2009 kuonyesha kuwa katika kipindi cha miaka kumi ni watu 27,330 waliozaliwa.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, kaunti hiyo ilikuwa na wapigakura 213,156 ambao ni zaidi nusu ya wakazi wote.

Gavana wa kaunti hiyo Muthomi Njuki, wabunge Kareke Mbiuki (Maara), Patrick Munene (Chuka Igambang’ombe) na Gitonga Murugara (Tharaka) walisema kwamba hawataruhusu matokeo hayo yatumike kwenye mgao wa rasilimali kwa kaunti yao, wakiyataja kuwa feki.

“Ni jambo la wazi kwamba matokeo sio ya kweli na tunayahusisha na ripoti ya BBI kwa kuwa ni ajenda inayosukumwa kisiasa na watu wasiotakia watu wetu mema,” alisema Bw Munene.

Akikosoa matokeo hayo, Bw Njuki alishikilia kwamba haiwezekani wakazi waliongezeka kwa watu 27,000 ilhali ripoti ya idara ya usajili inaonyesha watoto waliozaliwa katika kipindi cha miaka saba iliyopita ni 53,930 huku watu walioaga dunia wakiwa 10,411.

“Tunakataa takwimu hizi kwa kuwa zinatumiwa kutimiza malengo ya kisiasa hapo 2022. Haiwezekani kamwe idadi ya watu wazima izidi ya watoto. Tutaelekea mahakamani iwapo KNBS haitarudia sensa eneo letu,” alisema Gavana Njuki.

Wanasiasa hao walidai kwamba dalili zote zilionyesha kuwa idadi ya wakazi wote wa Tharaka-Nithi ilikuwa imefika zaidi ya watu 480,000.

Bw Mbiuki alisema matokeo hayo yamewashangaza hata Wakenya wengine ambao wanafahamu kwamba eneo hilo liliokoa serikali ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki kwenye uchaguzi wa 2007 kwa kura nyingi ilhali sasa linaonewa ikilinganishwa na maeneo mengine ya Mlima Kenya.

Gavana Kiraitu Murungi wa kaunti jirani ya Meru, Francis Kimemia wa Nyandarua na Wycliff Wangamati na Naibu Gavana wa Samburu Bw Julius Leseeto pia walitilia shaka uhalisi wa matokeo hayo.

Bw Kimemia alisema haiwezekani kuwa wakazi wa Nyandarua waliongezeka kwa watu 40,000 katika kipindi cha miaka kumi.

Kwa upande wake, Bw Wangamati alisema ingawa kaunti yake iliorodheshwa ya tano kwa wingi wa watu, ilishikilia nafasi hiyo miaka kumi iliyopita.

“Kaunti yetu inajulikana kwa kuwa na watu wengi na tuko na bidii kuzaa. Tunashangaa ni nini kilichofanyika,” alisema Bw Wangamati.

Aliyekuwa seneta wa Kakamega, alitilia shaka takwimu za KNBS kwamba idadi ya wakazi wa eneobunge la Ikolomani alilowahi kuwakilisha bungeni lilipungua kutoka watu 143,153 mwaka wa 2009 hadi 111,743 mwaka huu.

“Wacheni zenu. Hakukuwa na mkurupuko wa maradhi Ikolomani! Haya matokeo ni feki na yanalenga kunyima baadhi ya sehemu na jamii mgao wa mapato ya kitaifa,” alisema Bw Khalwale.

Naye aliyekuwa mbunge wa Gem Jakoyo Midiwo alisema matokeo hayo yanaonyesha kuna tatizo na akatoa mfano wa kaunti ya Tharaka Nithi.

“Miaka kumi na miwili iliyopita, Tharaka Nithi ilikuwa na wapigakura 216,000 na sasa watu wote ni 393,000. Kuna jambo lisilo la kawaida,” alieleza.

Kulingana na aliyekuwa seneta wa Mandera, Billow Kerrow, matokeo hayo sio ya kuaminiwa.

“Eneo la Kati ya Kenya lililo na kiwango cha chini kupata watoto sasa lina watu wengi. Kaskazini Mashariki ambalo wanawake wanapata watoto wengi na familia kubwa lina kiwango cha chini cha ongezeko la watu. Hii ni sensa ya vifaranga,” Bw Kerrow aliandika kwenye Twitter.

Aliyekuwa spika wa bunge la taifa Farah Maalim alisema sensa nchini Kenya hutumiwa kutimiza maslahi ya kisiasa naye Fatuma Gedi akahusisha kupungua kwa idadi ya wakazi wa baadhi ya maeneo ya Kaskazini Mashariki na maisha yao ya kuhamahama.

“Baadhi ya watu wametilia shaka matokeo ya sensa katika eneo la Kaskazini Mashariki, watu ni wafugaji wa kuhamahama. Nafikiri baadhi yao huenda walikuwa wamehama sensa ilipofanywa,” alisema.

Kulingana na mtaalamu wa masuala ya uchumi Bw Tony Watima, kuna masuala yanayohitaji ufafanuzi zaidi katika ripoti ya sensa hasa kuhusu kaunti za Kiambu na Mandera.

“Kiambu ina ongezeko la asilimia 49 ya watu ilhali Mandera imepungua kwa asilimia 15 ilhali kiwango cha idadi ya watoto wanaozaliwa hakiungi hali hii. Na haiwezi kuwa wakazi wengi wa Nairobi wamehamia Kiambu,” asema Bw Watima.

Wengine waliokosoa matokeo hayo ni gavana wa Meru Kiraitu Murungi ambaye alitisha kushtaki KNBS akisema idadi ya watu 1.5 milioni ni ya chini, mbunge wa Kandara Alice Wahome aliyedai wakazi wa Murang’a ni zaidi ya 1,056,640 na seneta wa kaunti ya Kisii Profesa Sam Ongeri aliyesema kuwa takwimu kwamba wakazi wa Kisii ni 1.26m na Nyamira ni 605, 576 sio za kuaminiwa.

Ripoti Za: Benson Matheka, Cecil Odongo, Waikwa Maina na Samuel Baya

PWANI: Wanawake waombwa kukubalia waume kuoa wake wengi

Na MOHAMED AHMED

WANAWAKE wa Pwani wamehimizwa kuwakubalia waume zao kuoa wake zaidi ya mmoja ili kuwezesha kuongezeka kwa idadi ya watu eneo hilo.

Baraza la Maimamu na Wahubiri Nchini (CIPK) lilisema jana kuwa upanuzi wa ndoa ndio utakaowezesha idadi ya watu Pwani kuongezeka.

CIPK ilitoa pendekezo hilo kwa wanawake baada ya matokeo ya idadi ya watu yaliyotolewa Jumatatu kuonyesha kuwa kaunti tatu za Pwani zipo miongoni mwa zile zenye idadi ndogo zaidi ya watu.

Katibu mtendaji wa CIPK, Sheikh Mohammed Khalifa alisema pia kuna haja ya wakazi wa Pwani kuhimizwa kuoa wake zaidi.

“Tukiongeza ndoa ndipo tutapata watoto na kufanya idadi yetu kuwa ya juu zaidi. Tumekuwa tukiacha mafunzo ya dini na tamaduni zetu na kufuata mienendo ya wazungu kwa kuzaa watoto wachache,” akasema Sheikh Khalifa.

Alisema wanawake wakilegeza misimamo kwa waume wao kuhusu kuoa zaidi ya mke mmoja, na vijana nao watie juhudi za kuoa na kupata watoto basi idadi ya wakazi wa Pwani itaongezeka pakubwa.

Sheikh Khalifa alizungumza baada ya Taifa Leo kutoa kichwa cha habari katika gazeti lake la jana lililoeleza kuwa eneo la Pwani huenda likawa limelegea chumbani.

Kichwa hicho cha habari kilizua hisia tofauti nchini hususan kanda ya Pwani huku wakazi wa eneo hilo wakishinikiza wanaume kuwacha utumizi wa dawa za kulevya ambazo zinalemaza katika uzazi.

“Utumizi wa miraa na muguka umekuwa juu, jambo ambalo limechangia Wapwani kupata watoto wachache na ndiposa idadi yetu iko chini,” akasema Bw Khamis Omar, mkazi wa Mombasa.

Kulingana na takwimu za matokeo hayo, Kaunti ya Lamu ndiyo yenye watu wachache zaidi nchini kwa kuwa na watu 143,920 ikifuatwa na Isiolo ambayo ina watu 268,002.

Kaunti ya Samburu iliibuka na watu 310,327, huku Taita Taveta ikiwa na watu 340,671 nayo Tana River ikiwa na watu 315,943.

Wakazi wa Kiambu wafurahia Sensa ya 2019

Na LAWRENCE ONGARO

HUKU watu wengi wakilalamika kuhusu hesabu kamili ya sensa, iliyotangazwa na serikali, wakazi wengi wa Kaunti ya Kiambu wanaishabikia.

Mfanyabiashara mjini Thika, Bw Elius Ngaru Mwaura anasema matokeo hayo ya Kiambu yanaridhisha na kwa hivyo wanatarajia kupata mgao wa fedha ipasavyo.

Kwa mfano takwimu za sensa zinaeleza kuwa kaunti ndogo ya Ruiru ina idadi ya watu 371,111.

Thika Magharibi na Mashariki, ina watu 324,776. Halafu Juja inajivunia kuwa na watu jumla 300,949.

“Maeneo hayo matatu yanastahili kukatwa mara mbili kila moja ili yawe na uwakilishi ufaao wa uongozi,” alisema Bw Mwaura.

Alisema kulingana na jinsi mambo yalivyo, maeneo hayo yamepata idadi kubwa ya watu kwa sababu ya barabara kuu ya Thika Superhighway ambayo imesambaza hali ya biashara kwa maeneo mengi.

Wakati huo pia kuna vyuo vikuu kadha katika miji hiyo na kwa hivyo idadi ya watu ni ya juu.

“Hata ingawa mji wa Kiambu ndiyo makao makuu ya Kaunti ya Kiambu, ukweli wa mambo ni kwamba biashara kubwa na fedha za mapato nyingi zinatoka mjini Thika,” alisema Bw Mwaura.

Alisema ni wazi sasa kila eneo litapata mgao wake wa kifedha kulingana na jinsi idadi ya watu inavyoeleza.

Bw Daniel Mwangi ambaye ni Mfanyabiashara na pia mkazi wa Thika mjini alisema Jumanne kwamba ameridhishwa na matokeo hayo.

Alisema maeneo ya Thika na Ruiru yanastahili kukatwa mara mbili ili kupata uwakilishi unaofaa.

“Kwa mfano, miji ya Thika na Ruiru inahudumia watu wengi na biashara ni nyingi katika maeneo hayo,” alisema Bw Mwangi.

Kulingana na takwimu kamili zilizotolewa, Kaunti ya Kiambu ina idadi ya watu wapatao 2,417,735 milioni.

Maeneo mengine ni kaunti ndogo ya Gatundu Kaskazini  109,870. Gatundu Kusini 122,103. Githunguri ,165,232. Kabete 199,653. Kiambaa 236,400. Kiambu Mjini 145,903. Kikuyu 187,122. Lari 135,303 halafu Limuru ni 159,314.

Katika eneo pana la Kati, Kaunti ya Kiambu imezipiku kaunti kadha katika sehemu hiyo.

Kwa mfano, huku Kiambu ikiwa na watu 2,417,735 milioni, Nyeri ina 759,164. Kirinyaga ina 610,411. Halafu Nyandarua ina idadi ya watu 631,281.

Halafu inadaiwa kuwa idadi kubwa ya watu wanaoishi Kiambu wanafanya kazi jijini Nairobi na kwingineko. Wengine nao wamejinunulia vipande vvya ardhi huko kutoka kwingineko.

SENSA: Kila Mkenya anadaiwa Sh124,000

Na LEONARD ONYANGO

MATOKEO ya Sensa yaliyotangazwa Jumatatu yamethibitisha kuwa kila Mkenya anadaiwa kiasi cha Sh124,000 ili kulipa jumla ya Sh5.9 trilioni ambazo Kenya inadaiwa.

Kulingana na matokeo hayo yaliyotangazwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Takwimu nchini (KNBS), Bw Zachary Mwangi, katika Ikulu ya Nairobi, Kenya ina jumla ya watu 47,564,296.

Kati yao wanawake ni 24,147,016 na wanaume 23,548,056 huku watu walio na jinsia mbili wakiwa 1,524.

Ripoti ya Hazina Kuu iliyowasilishwa katika Bunge la Kitaifa mwezi uliopita ilionyesha kuwa deni ambalo Kenya inadaiwa na wakopeshaji wa humu nchini na mataifa ya kigeni kama vile China, limefikia Sh5.902 trilioni.

Deni hilo likigawanywa kila Mkenya atatakiwa kulipa Sh124,084.

Matokeo ya Sensa pia yanaonyesha kuwa Wakenya wameongezeka kutoka milioni 37.7 hadi milioni 47.6 kati ya 2009 na 2019.

Hiyo inamaanisha kwamba Wakenya milioni 9.9 wameongezeka ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Hiyo inamaanisha kwamba watoto 2,710 huzaliwa humu nchini kwa siku. Hiyo ni sawa na watoto 225 kwa saa na watoto watatu kwa kila dakika.

Itahitajika viwanja 793 vyenye uwezo wa kubeba watu 60,000 kama vile Uwanja wa Kasarani ili kila Mkenya kupata nafasi.

Matokeo hayo ya sensa pia yamefichua kuwa takribani Wakenya milioni tisa hawakujisajili na Huduma Namba.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia (ICT), Bw Joe Mucheru, mnamo Mei alisema kuwa Wakenya milioni 38 walijisajili na Huduma Namba.

Kulingana na matokeo ya sensa, kaunti 18 zina watu milioni moja na zaidi.

Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu milioni 4.4 ikifuatiwa na Kiambu watu milioni 2.4 milioni.

Kaunti nyingine zilizo na zaidi ya watu milioni moja ni Nakuru (milioni 2.2 milioni), Kakamega (milioni 1.8), Bungoma (milioni 1.6), Meru (milioni 1.54), Kilifi (milioni 1.45), Machakos (milioni 1.4), Kisii (milioni 1.26) na Mombasa (milioni 1.2).

Nyingine ni Uasin Gishu (milioni 1.16), Narok (milioni 1.15), Kisumu (milioni 1.15), Kitui (milioni 1.13), Homa Bay (milioni 1.13), Kajiado (milioni 1.1) , Migori (milioni 1.1), Murang’a (milioni 1.05).

Kaunti sita zilizo na watu chini ya 400,000 ni Tharaka-Nithi , Taita/Taveta , Tana River, Samburu, Isiolo na Lamu.

“Wastani wa watu wanaoishi katika nyumba moja imepungua kutoka watu 4.2 mnamo 2009 hadi watu 3.9 mwaka huu,” akasema Bw Mwangi.

“Hiyo ni ripoti ya kwanza na shirika la KNBS litatoa ripoti nyingine zitakazoto ufafanuzi wa kina kuhusu idadi ya watu kuanzia katika ngazi ya lokesheni, shughuli za kiuchumi kati ya taarifa nyinginezo,” akaongezea.

Sensa hiyo iliyofanyika usiku wa Agosti 24 na Agosti 25, mwaka huu, ndiyo ya kwanza kufanyika chini ya Katiba ya 2010.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo ya sensa, Rais Uhuru Kenyatta aliagiza wizara na mashirika ya umma kuzingatia takwimu za KNBS katika mipango ya miradi ya maendeleo.

“Ninaagiza wizara na mashirika yote ya serikali na hata serikali za kaunti kutumia takwimu zilizotolewa na KNBS katika mipango yote ya maendeleo,” akasema Rais Kenyatta.

SENSA: Mbona serikali inatudharau?, Tharaka-Nithi yawaka

NA CECIL ODONGO

VIONGOZI kutoka kaunti ya Tharaka-Nithi wameapa kwenda mahakamani baada ya miezi sita ili kupinga matokeo ya idadi ya watu yaliyotolewa Jumatatu na kuonyesha kuwa kaunti hiyo ina watu 393,177.

Wakihutubia wanahabari jijini Nairobi Jumanne, Gavana wa kaunti hiyo Bw Muthomi Njuki, mbunge wa Tharaka, Bw Gitonga Murugara, mwenzake wa Chuka-Igambang’ombe Bw Patrick Munene na  yule wa Maara Bw Kareke Mbiuki walitishia kwenda mahakamani ili zoezi la kuhesabiwa kwa watu eneo hilo lirudiwe.

Walisema kaunti hiyo inaonewa kutokana na siasa za jopokazi la maridhiano (BBI) ilhali kura zake ziliokoa utawala wa Rais mstaafu Mwai Kibaki mwaka wa 2007.

“Tunakataa takwimu hizi kwa kuwa zinatumiwa kutimiza malengo ya kisiasa hapo 2022. Haiwezekani kamwe idadi ya watu wazima iwe kubwa kuliko ya watoto. Tutaelekea mahakamani iwapo KNBS haitarudia sensa eneo letu,” akafoka Gavana Njuki.

Kutoka kushoto: Mbunge wa Tharaka Bw Gitonga Murugara, Gavana wa kaunti hiyo Bw Muthomi Njuki, mbunge wa Maara Bw Kareke Mbiuki mwenzake wa Chuka-Igambang’ombe Bw Patrick Munene walipohutubia wanahabari jijini Nairobi, Jumanne. Picha/ Cecil Odongo

Bw Njuki aliongeza kuwa kulingana na matokeo ya idadi ya mwaka 2009, kaunti hiyo ilikuwa na watu 365,330 hivyo basi ni makosa kusema kuwa kwa muda wa miaka 10 ni watu 27, 847 ambao wameongezeka.

Alisema hilo ni kinyume na matarajio yao kuwa dalili zote zilionyesha kuwa idadi hiyo itakuwa imefika 480,000.

Kwa upande wake, Bw Mbiuki aliishangaa serikali kudharau eneo hilo kwa kukosa kutoa hesabu kamili ya watu kama maeneo mengine.

“Hazina Kuu inafaa kutoa fedha za kugharamia zoezi lingine la sensa kwa kuwa kaunti hii inatapata mgao wa chini na pia kubaguliwa katika utoaji wa ajira serikalini,” akasema.

Bw Munene naye alisema eneobunge lake limo hatarini kuvunjwa kwa kuwa kulingana na sheria inayopendekezwa, halifikishi watu 130,000.

Bw Murugara alitaja takwimu hizo kuwa feki na kuikejeli KNBS maanake wanaishi maisha sawa na wenzao wa Meru na Embu ambao idadi yao imeongezeka pakubwa.

SENSA: Kaunti 14 zaongoza kwa idadi kubwa ya wanaume

NA MWANDISHI WETU

JUMLA ya Kaunti 14 zina idadi kubwa ya wanaume kuliko wanawake, kulingana na matokeo ya sensa yaliyotolewa jana na Shirika la Takwimu nchini (KNBS).

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kaunti zote za ukanda wa Kaskazini Mashariki na baadhi za Pwani zina idadi ndogo ya wanawake ikilinganishwa na wanaume.

Hii ni licha ya takwimu za KNBS kuonyesha kuwa kuna idadi kubwa ya wanawake (milioni 24.0) ikilinganishwa na wanaume (milioni 23.5) nchini Kenya. Kaunti ya Garissa, ina wanaume 76,000 zaidi ya wanawake.

Kaunti nyingine katika ukanda wa Kaskazini Mashariki mwa Kenya zilizo na idadi kubwa ya wanaume ikilinganishwa na wanawake ni Wajir ambayo ina wanaume 49,534 zaidi, Mandera, Marsabit, Isiolo, Pokot Magharibi na Samburu.

Katika eneo la Bonde la Ufa, Kaunti za Baringo na Elgeyo Marakwet zina idadi ya juu ya wanaume ikilinganishwa na wanawake.

Kaunti ya Baringo ina wanaume 336,322 ikilinganishwa na wanawake 330,428. Kaunti ya Elgeyo-Marakwet inayoongozwa na Gavana Alex Tolgos, ina wanaume 227,317 ikilinganishwa na wanawake 227,151.

Kaunti ya Laikipia ndiyo ya pekee katika eneo la Mlima Kenya iliyo na uhaba wa wanawake.

Katika ukanda wa Pwani, Mombasa ina wanaume 610,257 ikilinganishwa na wanawake 598,046.

Hiyo inamaanisha kuwa jiji la Mombasa lina wanaume 12,000 zaidi ya wanawake.

Kaunti nyingine za Pwani zilizo na idadi ndogo ya wanawake ikilinganishwa na wanaume ni Tana River na Taita Taveta.

Kaunti ya Tana River ina wanaume 158,550 ikilinganishwa na wanawake 157,391.

Kaunti ya Taita Taveta ina wanaume 173,337 huku wanawake wakiwa 167,327.

Ripoti ya KNBS pia ilifichua kuwa kuna watu 1,524 walio na maumbile ya jinsia mbili. Kati yao 245 wanaishi jijini Nairobi na 135 katika Kaunti ya Kiambu.

Ripoti iliyotolewa na jopokazi lililobuniwa na Mkuu wa Sheria mnamo 2017 kuchunguza watu walio na jinsia mbili na kutoa mapendekezo kuhusu sera, ilikadiria kuwa watu walio na maumbile hayo ni 800.

Ni jopokazi hilo lililoongozwa na Bw Mbage Ng’ang’a lililopendekeza kuhesabiwa kwa watu walio na jinsia mbili katika sensa ya Agosti mwaka huu.

SENSA: Idadi kubwa ya Wakenya huishi Rift Valley na Mlima Kenya

Na JUMA NAMLOLA

ENEO la Rift Valley limo kifua mbele kupata mgao mkubwa wa maendeleo na usemi wa kisiasa baada ya kuandikisha idadi kubwa zaidi ya watu kwenye sensa iliyofanyika Agosti.

Kulingana na matokeo hayo, Rift Valley inaongoza kwa watu 12,442,639 wanaotoka kaunti 13. Idadi hii ni robo ya Wakenya wote.

Eneo la Mlima Kenya linafuata kwa jumla ya watu 8,029,729 wengi wao wakiwa wa kutoka Kiambu (2,417,735), huku wachache zaidi wakitoka Kaunti ya Tharaka Nithi (393,177).

Tayari viongozi wa Tharaka Nithi, ambayo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2007 ilidhaniwa kuwa na wapiga kura wengi zaidi nchini, wamelalama na kuapa kwenda kortini iwapo Baraza la Takwimu Nchini (KNBS) halitahesabu upya watu wake.

Nyanza ikiwa na watu 6,269,579 ni ya tatu ikifuatwa na Magharibi (5,021,843), Nairobi (4,397,073), Pwani (4,329,474) na Ukambani (3,545,772).

Maeneo ya jamii za wafugaji katika uliokuwa mkoa wa Mashariki pamoja na wenzao wa kaunti tatu za Kaskazini Mashariki, wanafikia idadi ya watu 3,528,187.

Katika siku za majuzi viongozi wa Mlima Kenya wamekuwa wakisisitiza mfumo wa ugawaji raslimali za nchi ufanywe kulingana na idadi ya watu badala ya ukubwa wa eneo.

Viongozi wanasema watakataa ripoti ya Jopo ya Maridhiano (BBI) iwapo haitaangazia maeneo yao ya uwakilishi.

Eneo hilo ambalo kwa miaka mingi limekuwa na uwakilishi serikalini, hasa katika ngazi ya urais, linataka BBI ipendekeze kugawanywa na kusambazwa kwa maendeleo kulingana na idadi ya watu.

Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri amekuwa mstari wa mbele kuwataka watu wa eneo hilo wakatae BBI kwa misingi kuwa itawapa watu walio na idadi ndogo uwezo sawa na wao katika maamuzi muhimu ya kitaifa.

Ijapokuwa kimsingi Laikipia anakotoka Bw Kiunjuri ipo Rift Valley, anaamini iwapo kila kura itaheshimiwa, basi watu wa Mlima Kenya watapata manufaa ya mageuzi ya Katiba yanayotarajiwa.

Wadadisi wa masuala ya siasa na uchumi wanahisi kuwa iwapo mfumo wa idadi ya watu utatumiwa kama kigezo cha kupeleka maendeleo, watu walio maeneo yaliyotengwa wataendelea kubaki nyuma kwa miaka mingi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Pwani, Profesa Halim Shauri anaamini kuwa mbali na idadi ya watu, ukubwa wa maeneo wafaa kuzingatiwa.

“Pendekezo la kugawa maeneo bunge kuwa mengi zaidi halina mashiko. Kinachofaa kuangaliwa ni iwapo uchumi wa nchi yetu unaweza kuhimili uzito wa mahitaji yetu ya kifedha,” anasema Prof Shauri.

Kwa msingi huo, anapendekeza kwamba mfumo bora zaidi wafaa kuwa ule ya kuyagawa maeneo kwa kuzingatia idadi ya watu hasa kwa wastani wa kati ya milioni 3 na 4 ili kuwe na maeneo yasiyozidi 15.

SENSA: Familia kubwa Mandera, Wajir, Marsabit na Garissa

Na VALENTINE OBARA

KAUNTI zilizo Kaskazini Mashariki ya nchi zinaongoza kwa idadi ya watu wanaoishi katika nyumba moja.

Ripoti ya sensa iliyotolewa Jumatatu ilionyesha katika Kaunti ya Mandera, takriban watu saba huishi katika nyumba moja.

Hii ilifuatwa na Wajir, Garissa, Turkana na Marsabit ambazo huwa na takriban watu sita kwa kila nyumba.

Maeneo ya Kati na Mashariki yanayojumuisha Kaunti za Meru, Tharaka-Nithi, Embu, Kitui, Machakos, Makueni, Nyandarua, Nyeri, Murang’a na Kirinyaga familia nyingi zina kati ya watatu na wanne kwa kila nyumba.

Kila nyumba Pokot Magharibi, Samburu, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Nandi, Baringo, Laikipia, Nakuru, Narok, Kajiado, Kericho na Bomet zilizo Rift Valley huwa na watu kati ya wanne na watano.

Kwa wastani kitaifa, kila nyumba huwa na watu wapatao wanne isipokuwa Kaunti ya Nairobi ambapo imebainika kwamba nyumba nyingi hazina watu zaidi ya watatu.

Katika eneo la Magharibi, kaunti za Kakamega, Vihiga, Homa Bay, Kisii na Nyamira zina watu wasiopungua wanne kwa kila nyumba. Bungoma na Busia zina karibu watu watano kwa kila nyumba, huku nyumba za Siaya na Kisumu zikiwa na watu wasiozidi wanne.

SENSA: Pwani walegea chumbani

Na MOHAMED AHMED

ENEO la Pwani limo kwenye hatari ya kuendelea kubaki nyuma kimaendeleo na kisiasa kutokana na wakazi wake kukosa kutia bidii ya kuzaa watoto wengi.

Hii ni baada ya takwimu za hesabu ya watu zilizotolewa jana kuonyesha kuwa kaunti tatu za Pwani ni kati ya tano ambazo zinavuta mkia kwa kuwa na idadi ndogo zaidi ya watu.

Hii inamaanisha kuwa Pwani itaendelea kupata mgao wa chini wa fedha za maendeleo, na pia usemi wake utazidi kuwa hafifu katika masuala ya kisiasa.

Lamu inashika mkia kote nchini, Tana River imo katika nafasi ya 44 huku Taita Taveta ikitosheka kuwa nambari 43.

Kaunti za Isiolo na Samburu kutoka Mashariki zinafuatana katika nafasi za 46 na 45.

Kulingana na takwimu za matokeo hayo, Kaunti ya Lamu ina watu 143,920 pekee, Tana River 315,943 na Taita Taveta 340,671.

Baadhi ya wakazi wa Pwani waliohojiwa na Taifa Leo walitilia shaka matokeo hayo wakisema kuna wengi ambao hawakuhesabiwa.

Mkazi mmoja wa Taita Taveta naye alisema wazaliwa wengi wa kaunti hiyo hasa wanawake wameolewa nje ya kaunti hiyo ndiposa idadi ya wakazi iko chini.

Hata hivyo kaunti za Kilifi na Mombasa zilijizatiti ikilinganishwa na kaunti nyingine za Pwani baada ya matokeo hayo kuonyesha kuwa kuna watu milioni 1.4 Kilifi na milioni 1.2 Mombasa.

Kuwepo kwa idadi ndogo ya watu katika kanda ya Pwani kumepelekea viongozi kueleza hofu ya eneo hilo kukosa kuendelea maendeleo.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na maendeleo katika kanda ya Pwani, Hassan Mwakimako alisema kuwa matokeo hayo yatarudisha nyuma eneo hilo iwapo serikali itakumbatia mfumo wa kugawa fedha kulingana na idadi ya watu.

“Kunaweza kuwa na sababu tofauti za kuwepo kwa matokeo hayo ya chini katika kaunti za Pwani lakini suala kuu ni kuwa kanda ya Pwani itaendelea kutengwa kimaendeleo kama ambavyo ilivyokuwa siku za nyuma,” akasema Prof Mwakimako.

Kwa upande wake, Katibu mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri (CIPK), Sheikh Mohammed Khalifa alisema kuwa kuna uwezekano kuwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo hawakuhesabiwa.

Kwa upande mwingine, kaunti za Nairobi, Kiambu, Nakuru, Kakamega na Bungoma ndizo zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu.

Kulingana na matokeo hayo yaliyotolewa jana, Kaunti ya Nairobi ambayo ndio jiji kuu la nchi ina watu milioni 4.3 ikifuatwa na Kiambu yenye watu 2.4 milioni.

Kaunti ya Nakuru yenye watu 2.1 milioni inashikilia nafasi ya tatu, huku kaunti mbili kutoka eneo la Magharibi – Kakamega (1.8 milioni) na Bungoma (1.6 milioni) zikishikilia nafasi za nne na tano mtawalia.

Viongozi wa Tharaka Nithi walalama kuhusu matokeo ya sensa

Na CECIL ODONGO na LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI wa Kaunti ya Tharaka Nithi sasa wanadai kwamba siasa zinazohusiana na Jopo la Maridhiano (BBI) ndizo zimesababisha eneo hilo ‘kuchezewa shere’ kwenye matokeo ya Sensa ambayo ripoti yake ilitolewa rasmi kwa umma Jumatatu.

Haya yanajiri huku mbunge wa Thika akitaka BBI iwe ni ya kuleta umoja na wala sio kupalilia siasa za chuki.

Mwanasiasa Kareke Mbiuki amedai eneo hilo sasa sasa linadharauliwa ikilinganishwa na maeneo mengine.

“Kura za eneo hili ndizo ziliokoa utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki mwaka 2007,” amesema Bw Mbiuki.

Jana Jumatatu Gavana wa Kaunti ya Tharaka Nithi, Muthomi Njuki pamoja na mbunge wa Tharaka, George Murugara walipinga matokeo yaliyoonyesha kwamba kaunti hiyo ina idadi ya watu 393,177 ambapo walitishia Shirika la Takwimu Nchini (KNBS) wakilitaka kufanya upya tathmini yake.

Sensa ya mwaka 2019 ilionyesha kwamba Kenya ina idadi jumla ya watu 47,564,296 wanaume wakiwa ni 23,548,056 nao wanawake wakiwa ni 24,014,716 ya sehemu ya idadi jumla.

Viongozi wa kanisa wamehimizwa kuwa mstari wa mbele kuchambua na kutathmini yale yameandikwa na jopokazi la maridhiano (BBI), ili kuwapa Wakenya mwongozo. Ripoti hiyo haijatolewa rasmi kwa umma kufikia sasa.

Ilidaiwa kuwa wakati wa kuunda katiba ya sasa mwaka wa 2010, ilisemekana kuwa asilimia 20 ilikuwa sio kamilifu na kwa hivyo huu ndiyo wakati wa kuipiga msasa.

Mbunge wa Thika, Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina ametoa changamoto kwa viongozi wa makanisa kutoka madhehebu mbalimbali kujitokeza wazi na kuichambua na kuitathmini kwa undani ripoti ya BBI ili kuwapa Wakenya mwonngozo unaoweza kuaminika.

“Huu ndiyo wakati wa viongozi wa makanisa kote nchini kujitokeza wazi kuwa mstari wa mbele kuzungumzia maoni ya BBI ili nao wananchi wawe na mwelekeo utakaowafaa kwa umoja wa nchi,” alisema Bw Wainaina.

Aliyasema hayo katika kanisa la Makongeni Full Gospel Church, mjini Thika, wakati wa kutawazwa kwa Askofu Mpya wa kanisa hilo Bw John Chege.

Alisema huu ndiyo wakati wa kanisa kuhesabiwa na kuonekana wako mstari wa mbele kuwapa wananchi mwelekeo utakaowafaa katika maisha ya sasa na ya baadaye.

“Wakati wa hapo awali kanisa lilikuwa mstari wa mbele kuhusu Katiba ambapo kama wananchi wangefuta yote waliyoelezwa wakati huo pengine wakati huu hatungepata matatizo kadha tunayoyapitia,” alisema Bw Wainaina.

Alisema kwa wakati huu, uchumi wa Kenya unayumbayumba ambapo ikiwa misukumo kama Punguza Mizigo, BBI na nyinginezo haitakuwa tayari kuangazia maslahi ya wananchi, basi haitakuwa ya manufaa kwa yeyote.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina (kushoto) na askofu mpya wa jimbo la Thika Magharibi, Bw John Chege (katikati). Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema hali mbaya ya uchumi ni kutokana na katiba mbaya na kwa hivyo viongozi wa kanisa wanastahili kuwa mstari wa mbele kutaja mazuri na mabaya huku akisema viongozi wa kisiasa wengi wanaangazia uongozi wa viti.

Alisema mambo muhimu zaidi katika maoni ya BBI yanastahili kuzungumzia maswala ya ufisadi ambao umeathiri uchumi wa nchi pakubwa.

Askofu mpya, Chege aliyetawazwa kinara wa jimbo la Thika Magharibi, alisema angetaka kuona maoni ya BBI yakizungumzia umoja, amani, na maridhiano kwa wananchi wote ili wawe kama Kenya moja.

Alisema kanisa liko mbioni kutathmini maoni ya ndani ya BBI ili baadaye waweze kuwapa mwongozo Wakenya.

Aliwashauri wanasiasa kuachana na siasa za migawanyiko na kuhubiri umoja na utangamano wa pamoja kama Wakenya.

“Sisi wachungaji tunataka kuona Wakenya wakiishi kwa amani ambapo kila nmoja anaweza ishi mahali popote bila kutatizwa na yeyote. Pia tungetaka kuona ushirikiano wa viongozi wa siasa katika kila pembe ya nchi,” alisema mchungaji Chege.

Maafisa walioshiriki sensa walalamikia kukosa malipo

Na MARY WANGARI

KUNDI la maafisa wapatao 50 walioshiriki shughuli ya kuhesabu watu Agosti liliandamana Alhamisi kulalamikia dhidi ya kukosa kulipwa ujira wao baada ya kufanya kazi.

Maafisa hao wakiongozwa na Bw Gerald Nandwa walisema kuwa walikuwa wamechoka kuzungushwa na maafisa wa Shirika la Kitaifa kuhusu Takwimu (KNBS), ambao wamekuwa wakiwakwepa kila wanapoulizia pesa zao.

“Hatujalipwa tangu shughuli ya kuhesabu watu ilipoisha. Wamekuwa wakituzungusha huku na kule. Wengine wao wamezima simu huku wengine wakitueleza wao si wafanyakazi wa KNBS. Hatujui sasa tumwendee nani,” alisema Bw Nandwa.

Kulingana na Bw Nandwa, waandamanaji hao walihusisha maafisa kutoka kaunti mbalimbali nchini walioshiriki kazi hiyo na ambao bado hawajapokea malipo yao hadi sasa.

“Watu wa Nairobi walilipwa kitambo lakini kuna baadhi ambao bado hawajapokea hela zao. Maeneo ya Kakamega unapata kwa mfano Kakamega Kusini wamelipwa lakini maeneo mengine bado hawajapata mishahara yao hadi tunashangaa wanafanya mambo haya vipi,” akalalama.

Hata hivyo, tuliwasiliana na Mkurugenzi wa KNBS Bw Zachary Mwangi aliyekanusha madai hayo akisema ni kaunti tano pekee ambazo hazikuwa zimelipwa ambapo watakuwa wametuma pesa kufikia Jumanne wiki ijayo.

“Tunaendelea kulipa watu, tumebakisha kaunti tano ambazo kufikia Jumatatu au Jumanne watakuwa wamepokea pesa zao. Wanaosema hawajapokea pesa Kaunti ya Nairobi ni wale walioandika akaunti ambazo hazifanyi kazi ambapo tukituma pesa zinakosa kwenda. Pia kuna wale ambao hawakurejesha vifaa tulivyowapa,” alisema Bw Mwangi akiongeza kuwa maafisa wake walikuwa wakishughulikia suala hilo.

Kwa upande wake, Bw Nandwa alieleza kuwa suala la kupoteza au kutorejesha vifaa halikuwa hoja maadamu tayari walikuwa wameafikiana jinsi ya kusuluhisha jambo hilo.

“Ikiwa kuna kifaa kilichopotezwa walikuwa wakate kiasi fulani cha pesa. Kama ni tarakilishi walikuwa wakate Sh15000 kutoka kwa mshahara au kama ni kuvunja kioo chake ungekatwa Sh5000. Lakini kuna waliorejesha kila kitu na bado hawajapokea malipo yao,” alilalama.

SENSA: Hofu ya wanasiasa Mlima Kenya

Na MWANGI MUIRURI

HAIJULIKANI hasa ni kwa msingi gani ambapo wanasiasa wengi wa Mlima Kenya hukesha wakilalamika kuwa “idadi zetu – jamii za Gema (ushirika wa Gikuyu, Embu na Ameru) – zinapungua kila uchao.”

Ingawa wanasiasa wengi katika eneo hilo huwa na kati ya watoto wawili na watatu katika ndoa zao au ulezi wao, bila kuzingatia wa nje ya ndoa, wao husukuma kampeni kali wakiwataka wenyeji wazaane.

Ni hali mbaya kiuchumi kuwataka raia wa kipato cha chini wazae kwa sababu tu za kisiasa bali sio kwa msingi wa uwezo wa malezi.

Siasa ni mchezo mchafu.

Hata somo la sayansi ya siasa lililemewa na kuipa maana dhana ya “siasa” na ikaafikiana kuwa “sisi wote ni wanasiasa katika hali zetu zote za kimaisha.”

Ni kauli anayopenda kutumia mhadhiri Gasper Odhiambo.

Ni katika hali hiyo ambapo Seneta wa Kiambu, Kimani wa Matangi alisema anaomba Mungu sensa ya mwaka 2019 isije ikathibitisha huenda “tumepitwa kwa idadi na jamii kama ya Akamba na Abaluhya.”

Analia kuwa katika eneo la Mlima Kenya, kumekuwa na maandamano tele ya wanawake wakiteta kuhusu kupotea kwa nguvu za kiume miongoni mwa wanaume wa eneo hilo hivyo basi kupunguza uwezo wa kuzaa.

Aidha, mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria anateta kuwa ulevi umekuwa tisho kuu kwa wenyeji.

“Hapa kwetu shule za msingi zinafungwa kwa kukosa watoto wa kusajiliwa kama wanafunzi,” akasema Kuria.

Anasema kuwa ulevi huo pamoja na utumizi wa dawa za kupanga uzazi miongoni mwa wanawake wa eneo hilo kumesababisha kukosa kuafikia malengo ya kuongezeka kwa takriban watu milioni moja kwa mwaka.

Gavana wa Nyandarua, Francis Kimemia anasema kuwa hesabu ya watu na nyumba iliyofanywa 2009  ilionyesha upungufu wa watu 1.8 Milioni kwa kuwa ilitarajiwa wafike  zaidi ya Millioni nane lakini wakawa 6.3 milioni.

“Tukaze tukiomba sensa hii ya sasa itupe matumaini ya kesho yetu katika siasa,” asema.

Ni hali ambayo imewaelekeza wengine wa wanasiasa wa eneo hilo kutangaza zawadi za pesa taslimu kwa walevi wote ambao watatema uraibu wao na watunge wanawake wao mimba, zawadi hiyo ikiwa kati ya Sh500 na Sh1,000!

Aidha, Bw Kimemia alidai kuwa pombe haramu zilielekezwa katika jamii hizo miaka ya 80 kwa misingi ya siasa ambapo nia ilikuwa kuwamaliza kizazi.

“Ni lazima watu wa jamii hizi wajiulize mbona ni kwao tu pombe hizi zilikubaliwa ziuzwe bila ya kuthibitiwa. Na tangu maeneo yenu yafanywe kuwa kiwanda na pia soko ya pombe hizi, hamuzai na serikali inaashiria kuunganisha baadhi ya mashule kwani mengi hayana idadi ya kuhudumiwa na walimu 10,” akasema.

Katika hali hiyo, wanawake wa eneo hilo wameshawishiwa walegeze kinga dhidi ya kupata uja uzito kupitia utumiaji dawa za kupanga uzazi na washirikiane na waume zao ili kupambana na upungufu wa watoto katika eneo hilo.

Mshirikishi wa kitaifa wa Shirika la Wanawake Waelimishaji (Fawe) Bi Cecilia Gitu anasema kuwa utumiaji wa dawa za kupanga uzazi bila ya kuwahusisha waume zao unasababisha upungufu wa watoto katika eneo hilo.

Alisema idadi ya watoto wanaozaliwa kila mwezi eneo hilo imepungua hadi wane kwa sasa ikilinganishwa na watoto saba waliokuwa wakizaliwa mwaka wa 1998.

Ripoti ya Shirika la Kenya Demographic Health Survey (KDHS) 2018 ilionyesha kuwa asilimia 67 ya wanawake wa Mlima Kenya hutumia dawa za kupanga uzazi na huwa hawaelezei waume zao kuhusu hali hiyo.

“Ukiambatanisha na idadi ya wazee wanaokunywa pombe kupindukia hivyo basi kulemewa na majukumu muhimu ya ndoa, utaona hali ya hatari kuhusu vizazi vijavyo kwani idadi yao itakuwa chache mno,” akasema.

Alilalamika kuwa kwa sasa hospitali nyingi hata hazipati waja wazito wa kuhudumia na shule nyingi za nasari imefungwa kwa kukosa watoto wa kusajili.

“Nyakati tulikuwa tunasikia shule moja ya msingi iko na watoto zaidi ya 2,000 zimeisha na sasa hata serikali inawaza kujumuisha shule kadhaa pamoja kwani hakuna idadi ya kufundishwa na walimu zaidi ya 10,” akateta.

Karani wa sensa aliyechafua makazi ya mtu atozwa faini

Na WAANDISHI WETU

KARANI wa sensa aliyekamatwa baada ya kwenda kuwahesabu watu katika nyumba moja akiwa mlevi katika Kaunti ya Murang’a amekubali kukiuka kanuni za kazi yake.

Samson Ndirangu alikubali mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Violet Ochanda, aliyemwachilia kwa dhamana ya Sh20,000 ama kifungo cha miezi minne gerezani.

“Nimemwachilia karani huyo kwa faini ya Sh20,000 ama kifungo cha miezi minne,” akasema kwenye uamuzi wake.

Karani huyo alifika katika makazi hayo katika eneo la Mukuyu Alhamisi usiku akiwa mlevi. Baadaye, alianza kukojoa ndani ya nyumba hiyo, bila kujali uwepo wa watoto.

Vilevile anadaiwa kula chakula cha watoto hao.

Karani hakuwa na vifaa vya kuwahesabu watu wakati huo.

Katika Kaunti ya Nyeri, viongozi wa kisiasa na kidini wamewataka watu kuhakikisha kuwa wamehesabiwa kabla ya shughuli ya sensa kukamilika leo Jumamosi.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Nyeri, Bi Rahab Mukami, aliwasihi wakazi wa kaunti hiyo ambao hawajahesabiwa kuwatafuta makarani na kuhakikisha kwamba wamehesabiwa kabla ya zoezi kukamilika.

“Ikiwa haujahesabiwa au makarani hawajafika nyumbani kwako, tafadhali, watafute na uhakikishe wamekuhesabu. Haupaswi kukaa tu na kusema kwamba hawakuja,” akasema Bi Mukami.

Aliwakumbusha kuwa rasilimali za nchi hugawanywa kulingana na idadi ya watu akisema kuwa kaunti zingine zinaweza kuunganishwa kwa sababu ya kuwa idadi ndogo ya watu.

Asilimia 90

Katika kaunti ya Nyandarua asilimia 90 ya wakazi walikuwa wamehesabiwa kufikia Ijumaa.

Katibu wa wizara ya uchukuzi Prof Paul Maringa na mwenzake wa mafuta Bw Andrew Kamau walisema walitarajia wakazi wote watahesabiwa kabla ya zoezi kukamilika.

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Gibert Kitiyo alisema asilimia 80 ya wakazi walikuwa wamehesabiwa kufikia Ijumaa licha ya visa vya ukosefu wa usalama vilivyohudiwa eneo hilo.

Katika Kaunti ya Lamu, serikali ya kitaifa imetuma makarani zaidi wa kuhesabu watu eneo la Lamu ili kusaidia kuharakisha zoezi la sensa masaa machache kabla ya shughuli hiyo kukamilika.

Shughuli hiyo ya kuhesabu watu ilianza rasmi kote nchini mnamo Agosti 24 na imepangwa kukamilika Jumamosi Agosti 31.

Akizungumza Ijumaa na wanahabari mjini Lamu, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia, alithibitisha kuongezwa kwa makarani 15 zaidi ambao tayari wamesambazwa kwenye baadhi ya maeneo ambayo yameshuhudia kujikokota kwa zoezi hilo la kuhesabu watu.

 

Ripoti za NDUNG’U GACHANE, MERCY MWENDE, WAIKWA MAINA na KALUME KAZUNGU

Itikadi ya kutohesabu watoto yatatiza sensa Narok

Na GEORGE SAYAGIE

ITIKADI ya jamii ya Wamaasai inayopiga marufuku kuhesabiwa kwa watoto na mifugo unaonekana kuwa kikwazo cha shughuli ya kuhesabu watu katika Kaunti ya Narok.

Tangu shughuli hiyo kung’oa nanga siku tano zilizopita, ni asilimia 37 pekee ya wakazi ambao wamehesabiwa.

Jamii ya Maasai inaamini kuwa kuhesabu watoto au mifugo kunaweza kuleta laana, maafa au majanga.

Wachungaji wa mifugo wamekuwa wakihama kutoka eneo moja hadi jingine kuepuka mifugo yao kuhesabiwa, hivyo kuwapa makarani wa sensa kibarua kigumu kutekeleza majukumu yao.

Kamishna wa Kaunti ya Narok, Samuel Kimiti jana alilazimika kufanya kikao na wasimamizi wa sensa kutoka wilaya zote za kaunti hiyo, ambapo walianzisha kampeni inayolenga kuwahimiza wakazi kujitokeza na kuhesabiwa kabla ya shughuli hiyo kufungwa kesho.

“Tunawaomba wakazi kujitokeza na kuhesabiwa. Ikiwa bado hujahesabiwa tafadhali nenda kwa chifu na makarani watakuja nyumbani kwako,“ Bw Kimiti akawaambia wakazi wakati wa kampeni hiyo.

Kulingana na Msimamizi wa Sensa katika Kaunti ya Narok, Bi Leah Wambugu, kaunti hiyo ina jumla ya makarani 2,700, wasimamizi 800 na wasimamizi wakuu 81.

Kupitwa na wakati

Gavana wa Narok Samuel Tunai aliwataka wakazi kutupilia mbali itikadi hiyo ya kuogopa kuhesabiwa akisema kuwa utamaduni huo umepitwa na wakati.

Gavana Tunai aliyekuwa akizungumza katika Hospitali ya Narok alipozindua shehena ya dawa za thamani ya Sh39 milioni zitakazosambazwa katika hospitali zote katika kaunti hiyo, alisema kuwa kuhesabu watoto na mifugo hakuleti laana kama inavyoaminika miongoni mwa wakazi.

“Nahimiza jamii ya Wamaasai kuruhusu serikali kuwahesabu. Utamaduni wa kutohesabu watoto na mifugo umepitwa na wakati,” akasema Gavana Tunai.

Bw Tunai alisema kuwa takwimu zitakazokusanywa na serikali ni muhimu katika ugawaji wa rasilimali kwa kaunti.

Muda maalum wa sensa wakaribia kutamatika baadhi wakihofia kukosa kuhesabiwa

Na SAMMY WAWERU

ZIMESALIA siku mbili pekee kukamilika kwa muda uliotengwa maalumu kwa shughuli ya kitaifa ya kuhesabu watu, sensa 2019.

Hata hivyo, baadhi ya Wakenya wameelezea hofu yao kwamba huenda wakakosa kuhesabiwa.

Kulingana na msemaji wa serikali Kanali Cyrus Oguna, shughuli hiyo iliyoanza Jumamosi Agosti 24 itatamatika Jumamosi Agosti 31.

Kwenye kikao na waandishi wa habari Jumatano, Kanali Oguna alisema wale ambao hawatakuwa wamehesabiwa baada ya Agosti 31 watatakiwa kuripoti katika afisi ya chifu au kamishna wa kaunti.

Kufikia Jumatano, baadhi ya wananchi walilalamikia kutoona makarani wa taasisi ya takwimu za kitaifa (KNBS) katika maboma yao, wakihofia kufungiwa nje katika shughuli hiyo.

Awali Bw Oguna alikuwa amesema watu wasiwe na wasiwasi, akihakikisha kwamba kila Mkenya atashirikishwa.

Edwin Kabeti ambaye ni mkazi wa Nairobi anasema kufikia sasa maafisa wa KNBS hawajaonekana katika jengo analoishi.

“Nimekuwa nikiwasubiri kuanzia Jumamosi na sioni dalili yao kunihesabu,” Bw Kabeti ameambia Taifa Leo.

Shughuli hiyo ya kitaifa iliendeshwa mnamo Jumamosi na Jumapili kati ya saa kumi na mbili za jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi.

Jumapili, Kanali Oguna alisema baada ya Agosti 24 na 25, shughuli hiyo itafanyika hata wakati wa mchana.

Bi Annitah Wairimu kutoka Kiambu anapendekeza ili kuhesabu kila Mkenya maafisa wa KNBS waruhusiwe kuzuru maeneo ya kazi kujua wale ambao hawajashirikishwa.

“Nina wasiwasi huenda muda uliotengwa ukaisha kabla sijahesabiwa. Ninaomba serikali iamuru KNBS maafisa wake wazuru watu katika maeneo yao ya kazi, wale ambao pamoja na jamaa zao hawajahesabiwa data zao zichukuliwe. Baadhi yetu tunafanya ajira za juakali zinazotulazimu kuamkia alfajiri na mapema na kutoka kama tumechelewa,” anasema Annitah.

Kauli ya mfanyabiashara huyo pia inaungwa na Bw Simon Kagombe anayelalamikia kukawia kwa maafisa hao.

Naye Bi Mary Wanjiru ambaye ni mmoja wa makarani wanaoendesha shughuli hiyo eneo la Zimmerman, amesema kwamba katika mengi ya majengo wanayozuru mchana, wanakaribishwa na kufuli mlangoni.

Atupwa ndani kwa kukataa kuhesabiwa, 3 wakamatwa

NA WAANDISHI WETU

MWANAMUME amefungwa miezi sita gerezani kwa kuzuia afisa wa sensa kumhesabu. Abraham Cheruiyot kutoka Kesses, Kaunti ya Uasin Gishu alihukumiwa katika mahakama ya Eldoret Jumamosi.

Katika Kaunti ya Tharaka Nithi, watu watatu walikamatwa katika lokesheni ya Kathangacini, kaunti ndogo ya Tharaka Kaskazini kwa kukataa kuhesabiwa kutokana na imani yao ya kidini.

Watatu hao ni wa dhehebu la Kabonokia na wanaendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Marimanti baada ya kutoroka boma lao wakisema dini yao haiwaruhusu kushiriki mambo ya dunia kama sensa.

Dhehebu la Kabonokia pia limekataza waumini wake kwenda shuleni au kutibiwa hospitalini.

Katika kijiji hicho hicho, mwanaume mwingine alikamatwa baada ya kuchapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba angewakatakata maafisa wa sensa iwapo wangefika kwake kutokana na machungu ya kukosa kupewa kazi hiyo ya kuhesabu watu.

Katika Kaunti ya Homa Bay, mwanaume alimuua nduguye ambaye alirejea nyumbani kuhesabiwa kufuatia mzozo wa ardhi.

Marehemu Joseph Olale, 56, alirejea nyumbani kwao katika kijiji cha Kamato Punde, wadi ya Lambwe kutoka mji wa Ahero anakofanya kazi ili ahesabiwe, lakini wakashiriki ugomvi na kakake kuhusu shamba la familia ndipo akauawa.

Kamanda wa polisi eneo hilo Charles Mwangi alisema mnshukiwa amekamatwa.

Katika Kaunti ya Vihiga, mwanaume alikamatwa Jumanne jioni baada ya kupanda juu mti asihesabiwa na maafisa wa sensa.

Bw Elias Asige kutoka kijiji cha Itumbi, lokesheni ndogo ya Givogi anaendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Serem huku mwanamke ambaye alipatikana kwenye boma lake bado akiandamwa na polisi baada ya kutoroka.

Kamishina wa Vihiga, Sammy Waweru alithibitisha kisa hicho na kusema maafisa wake wanamsaka mama aliyetoweka.

Ripoti za Alex Njeru, George Odiwuor, Derick Luvega na Titus Ominde