Ruto adai kumiliki kura za eneo la Mlima Kenya

Na STEVE NJUGUNA

NAIBU Rais William Ruto amepuuzilia mbali juhudi za kiongozi wa ODM Raila Odinga kupenya Mlima Kenya.

Dkt Ruto alisema kuwa tayari anamiliki eneo hilo lililo na wapiga kura wengi.

Dkt Ruto ameonekana kuwa kwenye njia panda kisiasa akijitahidi kudumisha ushawishi wake Mlima Kenya wakati huu ambapo Bw Odinga amezindua kampeni kali eneo hilo.

“Kuna watu wamejua leo ati kuna mlima na sasa wameanza kutafuta google map ili waanze kupanda mlima. Ningetaka kuwaambia kuwa mimi ndiye mwenye mlima,” alisema.

“Walipokuwa kwingineko, nilizuru mara kadhaa eneo hili, tukajenga barabara Mlima Kenya na kuanzisha miradi mingine ya maendeleo. Ninawakaribisha mlimani lakini wanapokuja acha wajue kwamba kuna wenyeji kwa mlima,” alisema Naibu Rais katika Shule ya Msingi ya Nyahururu DEB, Kaunti ya Laikipia.

Wakati huo huo, Dkt Ruto pamoja na wabunge wanaoegemea kambi yake walipuuzilia mbali mkutano uliofanyika kati ya kiongozi wa ODM na viongozi wa kibiashara kutoka eneo la Mlima Kenya.

“Kuna watu wanaoandaa mikutano Nairobi kupanga jinsi ya kuja kuuza mtu ambaye amegundua leo kwamba kuna mlima unaopatikana mahali fulani. Msiruhusu watu wengine wanaoandaa mikutano Nairobi kuja kuwafanyia uamuzi kuhusu ni nani atakayekuwa rais wenu mpya,” alisema.

Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua alisema hawatampa nafasi Bw Odinga kuwashinda katika kinyang’anyiro cha urais.

“Vuguvugu la walalahoi haliwezi kuzimwa. Naibu Rais amekuwa sehemu ya jamii ya Mlima Kenya kwa miaka mingi sasa na katika muda huo, amegeuka kipenzi cha watu,” alisema.

Ruto, Muturi wasuta mabwanyenye wa MKF kwa kudai ndio wenye ufunguo wa kura za Mlima Kenya

Na SAMMY WAWERU

SIKU mbili baada ya wakfu wa wafanyabiashara kutoka Mlima Kenya – Mount Kenya Foundation (MKF) – kukutana na vinara wa One Kenya Alliance (OKA), baadhi ya viongozi na wanasiasa wamejitokeza na kukashifu kauli ya mabwanyenye wa muungano huo kwamba “wao ndio wenye ushawishi na maamuzi ya kura za eneo la Kati”.

MKF ikiongozwa na mwenyekiti wake, Bw Peter Munga na naibu, Titus Ibui, Alhamisi ilifanya kikao na Mabw Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (Kanu), katika mkahawa wa kifahari wa Safari Park, jijini Nairobi, na kuahidi itajua mgombea itakayeunga mkono 2022 kuwania urais.

Aidha, MKF ilisema itatathmini manifesto ya kila mwaniaji na kufanya maamuzi ya nani itaunga.

Wakfu huo wiki iliyopita pia ulikutana na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Kufuatia mikutano hiyo, baadhi ya viongozi na wanasiasa wamejitokeza na kukashifu MKF wakisema haina ufunguo wa kura za jamii ya Mlima Kenya.

Wakiongozwa na naibu wa rais, Dkt William Ruto, wamesema Wakenya ndio wana kura ila si “mabwanyenye wachache wanaokongamana hotelini kwa sababu zao za kibinafsi”.

“Ni wao wataamua au ni nyinyi Wakenya wenye kura?” Bw Ruto akataka kujua akihutubia umati wa watu Laikipia mnamo Jumamosi.

Naibu wa rais ni kati ya wanasiasa ambao wametangaza nia yao kuwania urais mwaka ujao.

Naye Spika wa Bunge la Kitaifa, Bw Justin Muturi akionekana kusuta MKF alisema wanaomezea mate kiti cha urais wanapaswa kujituma mashinani ili kujua mahitaji ya wananchi.

“Mkikaa hotelini na kupanga urithi wa serikali mtajuaje mahitaji ya Wakenya? Acheni wananchi wajiamulie wanayetaka awaongoze,” Bw Muturi akasema.

Spika huyo pia ametangaza kuwa debeni, katika kinyang’anyiro kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.

Wakfu wa wafanyabiashara kutoka Mlima Kenya unajumuisha wafanyabiashara tajika na wenye ushawishi mkuu eneo la Kati na nchini kiuchumi.

Mumewe mbunge amlaumu Ruto vikali

Na STANLEY NGOTHO

MUME wa mbunge wa Kajiado Mashariki, Peris Tobiko, Bw Kishanto Ole Suuji, amemlaumu Naibu Rais William Ruto kwa kufanyia mkutano katika boma lake bila idhini yake.

Bw Suuji alimshutumu Ruto kwa kupanga mkutano wa kisiasa na mkewe bila kumwarifu.

Mkutano huu ulifanyika nyumbani kwake IIporosat, kaunti ndogo ya Kajiadio Mashariki.Bw Suuji alisema kuwa alikasirishwa na njama ya kuwaleta wajumbe nyumbani kwake bila ya kumwarifu.

Ijumaa, Bw Ruto alikuwa nyumbani kwa Bi Tobiko kwa mkutano ambao ungemwezesha Bi Tobiko kuhamia chama cha United Democratic Alliance kutoka Jubilee.

Wanasiasa wanaounga mkono UDA walisafirishwa nyumbani kwake Bi Tobiko kuanzia saa moja asubuhi.

Wajumbe pamoja na Naibu Rais walipokuwa wakiwasili nyumbani kwao, Bw Suuji alikuwa akizunguka kwenye vituo vya polisi ili kulalamikia ‘njama’ ya mkewe na Ruto.

Bw Suuji alikutana na Bi Ancent Kaloki, Mkuu wa Polisi (OCPD) Isinya, kabla ya kuhutubia wanahabari kumlaumu mkewe na Naibu Rais.

“Walivamia nyumba yangu bila kunifahamisha. Wameharibu mimea yangu na kuwachinja mifugo wa familia yangu. Nimesikitika sana,” akasema Bw Suuji.

Bw Suuji ambaye ni Kamishna katika Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) alisema kuwa yeye kama afisa wa serikali hafai kuwa na mkutano kama huo nyumbani kwake.

Bw Suuji ambaye anaunga azima ya urais ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga, alitishia kumshtaki Naibu Rais na mbunge Tobiko kwa kuvamia nyumba yake.

Mkutano huo wa IIpolosat unatamatisha mvutano kati ya Bi Tobiko na mbunge wa Kajiado Kusini, Katoo Ole Metito ambaye alikuwa akimezea mate tikiti ya UDA.

Washauri wa Naibu Rais walimshauri kutomuunga mkono Bw Metito na badala yake akumbatie Bi Tobiko kugombea ugavana ili aweze kumenyana na gavana wa sasa Joseph Ole Lenku kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Raila kukita kambi ngome yake Ruto

ONYANGO K’ONYANGO na BARNABAS BII

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga wiki ijayo anatarajiwa kukita kambi katika ngome ya Naibu Rais William Ruto eneo la Bonde la Ufa katika juhudi za kujitafutia uungwaji kwenye eneo hilo lililo na wapigakura 4.5 milioni.

Bw Odinga ataanzia katika Kaunti ya Turkana na kisha kufululiza hadi mjini Eldoret (Kaunti ya Uasin Gishu) na kumalizia ziara yake Kaunti ya Nakuru.

Mjini Eldoret, Bw Odinga atakutana na wajumbe kutoka Kaunti za Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet, Baringo, Uasin Gishu na Nandi.

“Baada ya kutoka Eldoret, nitaelekea Nakuru ambapo nitakutana na wajumbe kutoka Kaunti za Nakuru, Kericho na Bomet,” Bw Odinga alisema Jumatano.

Dkt Ruto na mwenyekiti wa Kanu, Gideon Moi – wote kutoka eneo la Bonde la Ufa – wametangaza azma yao ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.

Baada ya kutoka katika eneo hilo ambalo ni ngome ya Dkt Ruto, Bw Odinga ataelekea Meru ambapo atakutana na wajumbe kutoka kaunti za Meru, Embu na Tharaka Nithi.

Bw Odinga ambaye amekuwa akizunguka katika maeneo mbalimbali kutafuta wafuasi kupitia vuguvugu lake la Azimio la Umoja, ataelekea Ukambani baada ya kutoka Meru.

Kulingana na ODM, Bw Odinga atazindua rasmi azma yake ya kuwania urais mwanzoni mwa mwaka ujao baada ya chama chake kukamilisha shughuli ya kusajili wanachama wapya.

Baada ya Meru, Bw Odinga ataelekea katika eneo la Mlima Kenya Magharibi na kisha kumalizia ziara zake jijini Nairobi.

“Azimio la Umoja lilizinduliwa katika Kaunti ya Nakuru na linalenga kuhimiza Wakenya kuungana na kusahau tofauti zetu za kikabila. Nchi haiwezi kuendelea kukiwa na ubaguzi wa kikabila. Ninazuru kila eneo nchini Kenya na kuwaeleza Wakenya kwamba tunaweza kushirikiana kupambana na ukabila,” akasema Bw Odinga na kuongeza kuwa tayari ameidhinishwa na wajumbe kutoka Nyanza, Magharibi, jamii ya Wamaasai, Pwani na Kaskazini Mashariki.

Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna alithibitisha kuwa Bw Odinga Alhamisi atazuru Kaunti ya Turkana kabla ya kuelekea Eldoret.

Bw Odinga ameahidi kuwasaidia wakazi wa Bonde la Ufa kupata mapato zaidi kutokana na mazao yao kama vile mahindi, chai, maziwa na miwa.

Ruto amlima Uhuru

WANDERI KAMAU na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto alitumia ziara yake katika eneo la Kisii kumshambulia Rais Uhuru Kenyatta – hatua inayodhihirisha kwamba urafiki baina ya viongozi hao wawili hauwezi kufufuliwa tena licha ya wito wa maaskofu kutaka kuwapatanisha.

Akihutubu wikendi kwenye kikao cha faragha na viongozi wanaomuunga mkono katika Kaunti ya Kisii, Dkt Ruto alisema kwamba serikali ya Rais Kenyatta ilipoteza dira ya maendeleo tangu 2018 alipotangaza kushirikiana na kiongozi wa ODM Raila Odinga kupitia kwa handisheki.

Alimkosoa Rais Kenyatta na Bw Odinga kwa akisema kwamba handisheki haikuleta amani nchini. Badala yake, Dkt Ruto alidai, ilivuruga amani ndani ya chama cha Jubilee.

“Kuna wageni (Bw Odinga na viongozi wengine wa uliokuwa muungano wa NASA) waliotutembelea. Walikuja na mapepo kwani walivuruga kila ajenda tuliyokuwa nayo kubadilisha maisha ya Wakenya. Walikuja na mapepo ambayo yalisababisha wakuu wa chama kutimua wanachama wake huku wabunge wakipokonywa nyadhifa Bungeni. Je, hiyo ndiyo amani iliyoletwa na wageni?” akauliza.

Kwenye kikao hicho, Dkt Ruto alisema moja ya mipango iliyovurugika ni ule wa ujenzi wa nyumba 500,000 walizolenga kumaliza kufikia mwaka 2022 ili kuwasaidia Wakenya kupata makazi bora kwa bei nafuu.

Alisema kwamba kufikia sasa, serikali imefaulu kujenga nyumba 3,000 pekee.

Aidha, aliongeza kwamba serikali imefeli kutimiza ahadi yake ya kuboresha sekta nyingine muhimu kama vile afya na kilimo.

“Ikiwa huu ungekuwa mtihani, ni wazi serikali imefeli kabisa. Tatizo kuu ni kwamba tuliacha masuala muhimu na kuegemea shughuli za Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI),” akaeleza.

Alisema kuwa kutokana na mvurugiko uliotokana na handisheki, Chama cha Jubilee (JP) kilisambaratika kabisa na kuanza kuwahangaisha wanachama wake.

Aliongeza kwamba baada ya uchaguzi wa 2017, chama kilikuwa na karibu wabunge 170, lakini sasa kimebaki na wabunge kati ya 20 na 25.

“Tulipoanzisha Jubilee, tulikuwa na lengo la kukifanya kuwa chama cha kitaifa, kinyume na hali ambayo imekuwepo ambapo vyama vingi hubuniwa kwa misingi ya kikabila. Ni kwa ahadi hiyo ambapo Wakenya walituunga mkono kikamilifu na kuwachagua wabunge wengi zaidi ikilinganishwa na vyama vingine. Hata hivyo, chama kiligeuka kuwa jukwaa la vitisho na usaliti. Matunda ya handisheki yalikuwa ni kufukuzwa kwa viongozi chamani na wengine kutolewa katika kamati za Bunge na Seneti,” akasema Ruto.

Alipuuzilia mbali juhudi zinazoendeshwa kuunganisha Jubilee na ODM, akikitaja chama cha Jubilee kama kisicho na ushawishi wowote.

Licha ya mpango wa BBI kuanzishwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga, Dkt Ruto aliutaja kuwa “ulaghai mkubwa zaidi wa kisiasa kuwahi kushuhudiwa nchini.”

Kauli hiyo ni licha ya Rais Kenyatta kusisitiza kwamba mpango huo ulilenga kuwafaidi Wakenya kwa kuongeza mgao wa fedha unaotumwa katika serikali za kaunti.

“BBI ilikuwa njama ya kuturudisha katika enzi ya Rais mwenye mamlaka kupindukia. Hii ni licha ya Wakenya kupinga hilo kupitia harakati za kushinikiza mageuzi ya kikatiba kwa zaidi ya miaka 30,” akasema.

Hapo Jumapili, Dkt Ruto pia alijitetea vikali dhidi ya lawama za kukataa kushiriki mazungumzo ya kutafuta muafaka kati yake na Rais Kenyatta yaliyoitishwa na maaskofu wa kanisa Katoliki.

Kwenye ujumbe alioweka kwenye mitandao ya kijamii, Dkt Ruto aliambatanisha barua aliyowatumia maaskofu hao, akisema amekuwa tayari kushiriki mazungumzo bila masharti yoyote.

Kauli yake ilionekana kumwelekezea lawama Rais Kenyatta kama ndiye aliye kizingiti kikuu kwa mazungumzo hayo.

Ruto atua Nyanza akitaka Uhuru, Raila waunge mkono azma yake

Na MWANDISHI WETU

NAIBU Rais William Ruto, Jumamosi aliwataka Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuunga mkono azma yake ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Dkt Ruto alisema alipohudumu kama naibu kiongozi wa ODM alimuunga mkono Bw Odinga katika uchaguzi mkuu wa 2007, hatua iliyomsaidia kuteuliwa Waziri Mkuu.

Vile vile, alisema alimsaidia Rais Kenyatta kushinda urais kwa mihula miwili kwa tiketI ya chama cha Jubilee.

“Inasikitisha kuwa watu hawa wawili wamekuwa wakinishambulia licha ya kwamba niliwasaidia kupata nyadhifa hizo kubwa. Sasa nawaomba waniunge mkono ili niwezeshe Wakenya wa tabaka la chini kupata kazi na maisha mazuri,” Dkt Ruto akasema.

Alisema hayo mjini Awendo, Kaunti ya Migori alipokaribishwa na Gavana wa Kaunti hiyo, Bw Okoth Obado na viongozi wengine wa eneo hilo alipofika huko kuvumisha azma yake ya urais.

Dkt Ruto alitoa mchango wa Sh1 milioni kufadhili ujenzi wa Kanisa la Kiadventisti la Awendo Central, Sh1.4 milioni kwa makundi ya bodaboda na Sh500,000 kwa akina mama wafanyabiashara mjini Awendo kama hatua ya kupiga jeki makundi hayo.

Wapuuza Uhuru

VITALIS KIMUTAI na BENSON MATHEKA

WANASIASA wamedhihirisha kuwa kamwe hawako tayari kutii amri ya Rais Uhuru Kenyatta aliyepiga marufuku mikutano ya kisiasa na mingineyo kwa lengo la kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Polisi nao wamempuuza Rais Kenyatta kwa kuonyesha ubaguzi katika utekelezaji wa kanuni alizotoa, ambapo wanawaacha wanasiasa kuzivunja, huku wakiwawinda raia wa kawaida kwa visingizio vya kutekeleza sheria hizo.

Wanasiasa na maafisa wakuu serikalini wamepuuza bila kujali masharti ya kupambana na ueneaji wa ugonjwa wa Covid-19, hali inayotoa picha kuwa kanuni hizo zinaendeleza tu ubaguzi dhidi ya raia wa kawaida.

Utekelezaji wa sheria za kukabiliana na virusi vya corona umeanika ubaguzi ambao serikali imekuwa ikiendeleza dhidi ya wananchi.

Naibu Rais William Ruto, waziri mkuu zamani Raila Odinga, aliyekuwa makamu wa rais Kalonzo Musyoka na mwenzake Musalia Mudavadi, ni miongoni mwa wengine ambao wamekuwa wakimwonyesha Rais Kenyatta ‘dharau’ kubwa kwa kuandaa mikutano ya halaiki licha ya kuipiga marufuku.

Cha kutamausha ni kuwa polisi, ambao wanafaa kutekeleza maagizo ya Rais Kenyatta, wamekosa kufanya lolote kuzuia mikutano hiyo inayochochea usambazaji wa Covid-19. Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i na katibu wa wizara ya afya Susan Mochache ambao wanafaa kuwa msitari wa mbele kutekeleza sheria hizo wamekuwa wakizivunja.

Mnamo Septemba 11 wawili hao waliongoza hafla kadhaa kaunti za Nyamira na Kisii walikohudhuria umati wa wakazi.

Polisi pia wamekuwa wakilenga wananchi wa kawaida katika utekelezaji wa kafyu, uvaaji barakoa na kufungwa kwa kilabu za pombe.

Lakini ubaguzi unazuka inapohusisha wananchi wa kawaida, ambapo polisi hutumwa kutekeleza kanuni kwenye hafla za kidini, mazishi, harusi, kufungwa kwa mabaa ifikapo saa moja jioni pamoja na kukamata wasiovaa barakoa na kuwa nje baada ya saa nne za usiku.

Wakati polisi wanapokabiliwa na raia kwa kuwadhulumu wanatumia nguvu. Mnamo Agosti 2 polisi walilaumiwa kwa kuwaua ndugu wawili waliowakamata wa kukiuka kafyu eneo la Kianjakoma, Kaunti ya Embu. Maafisa sita wameshtakiwa kwa mauaji ya kaka hao waliokuwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Wikendi iliyopita katika Kanisa Katoliki la Tegat, kikosi cha polisi kilitumwa kuhakikisha idadi ya waumini haikupita 100 kwenye ibada iliyoongozwa na Askofu (Kanali Mstaafu) Alfred Rotich.

Wiki mbili kabla ya kisa hicho, polisi walifutilia mbali hafla ya kidini katika Kaunti Ndogo ya Bomet kwa visingizio vya kutekeleza sheria za Covid-19.

“Utekelezaji wa sheria za Covid-19 unaonyesha ubaguzi mkubwa. Polisi wanahakikisha wananchi ikiwemo katika maeneo ya ibada hawapiti idadi iliyotangazwa, lakini wanaruhusu mikutano ya wanasiasa inayohudhuriwa na maelfu, wengi wakiwa hawajavaa barakoa,” akasema Rolex Kiprotich Sirmah, mwanasiasa kutoka Bomet Mashariki.

Kwenye mikutano ya wanasiasa pamoja na hafla zingine wanazohudhuria kama vile mazishi na ibada makanisani, polisi wamekuwa wakitazama tu sheria alizotangaza Rais Kenyatta zikivunjwa.

Kulingana na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Nyeri ya Kanisa Katoliki Antony Muheria, tatizo kubwa katika utekelezaji wa kanuni za kuzuia corona ni wanasiasa.

“Ninaambia wanasiasa wetu wapende nchi yao, waache kuandaa mikutano ya kisiasa ambayo imetambuliwa kama kichocheo kikuu cha maambukizi ya corona,” asema.

Wanasiasa hao wamekuwa wakiandamana na washirika wao maeneo tofauti nchini wanakoandaa mikutano kujipigia debe hata kabla ya msimu wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 kutangazwa rasmi.

Bw Odinga ameandaa mikutano kaunti za Kakamega, Kisii, Homa Bay na Mombasa kuvumisha kampeni yake ya Azimio la Umoja mbali na kukutana na makundi kadhaa ambako kanuni za kuzuia corona hazizingatiwi.

kt Ruto amekuwa akipuuza kabisa kanuni hizo akikutana na jumbe kutoka maeneo yote ya nchi katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi, pamoja na kuandaa mikutano ya kisiasa maeneo tofauti.

Mwishoni mwa wiki, Dkt Ruto alizuru maeneo ya Kajiado na Makueni alikohutubia mikutano kadhaa siku moja baada ya kuongoza washirika wake kuendeleza kampeni yake ya hasla kaunti ya Kiambu.

Katika kile kinachodhihirisha kuwa sheria ni za watu wa matabaka ya chini, polisi wamekuwa wakiwanyima Wakenya wakiwemo viongozi wa kidini kibali cha kuongoza hafla zinazokiuka kanuni za wizara ya afya za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona huku wakiwarusu wanasiasa.

Kuhusu takwimu za maambukizi zilizotangazwa jana, watu 317 walipatikana kuambukizwa na virusi hivyo baada ya watu 6,129 kupimwa, huku wengine 27 wakiaga dunia na kufikisha jumla ya walioangamizwa na ugonjwa huo kuwa 5045.

Mlima wateleza kwa Ruto, Raila

Na BENSON MATHEKA

NDOTO za Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Raila Odinga kujinyakulia ufuasi mkubwa katika eneo la Mlima Kenya zimeanza kuyumbishwa na hekaheka za wanasiasa wa eneo hilo wanaojaribu kujiweka katika nafasi nzuri ya kushinda viti mbalimbali, kibinafsi na kieneo, katika uchaguzi hapo 2022.

Viongozi wa eneo hilo wamezidisha mikakati ya kuungana na kuamua mwelekeo ambao litakaochukua kabla na kwenye uchaguzi mkuu ujao huku wito ukitolewa lisimamishe mgombeaji wa urais.

Tayari, Spika Justin Muturi, anayetoka eneo hilo ametangaza kuwa atagombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Ingawa viongozi wa eneo hilo wamekuwa wamegawanyika, juhudi za kuungana kutetea maslahi ya wakazi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuondoka mamlakani zimeshika kasi, hatua ambayo wadadisi wanasema inaweza kuwa pigo kwa Dkt Ruto na Bw Odinga.

“Kuungana kwa eneo la Mlima Kenya kunafaa kuwapa Dkt Ruto na Bw Odinga wasiwasi kwa kuwa wimbi linaweza kubadilika hasa likiamua kuunga mmoja wao kugombea urais,” asema mdadisi wa siasa Peter Njogu.

Rais Kenyatta amekuwa akimuunga Bw Odinga kuwa mrithi wake ingawa washirika wake wanadai ni vigumu kwa waziri mkuu huyo wa zamani kuungwa mkono na wapigakura eneo la Mlima Kenya.

Katika siku za hivi punde, viongozi wa eneo hilo waliokuwa upande wa Dkt Ruto na Bw Odinga wamekuwa wakionyesha dalili za kujitenga nao na kuunga wanaopigania umoja wa jamii za Gema.

Mnamo Jumatano, Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru ambaye alikuwa akimsifu Bw Odinga wakati wa kampeni za Mpango wa Maridhiano (BBI) alisema kuwa ataamua mwelekeo wa kisiasa baada ya kushauriana na wakazi wa kaunti yake na eneo pana la Mlima Kenya.

Bi Waiguru alikiri kwamba ni vigumu kumpigia debe Bw Odinga na kwamba chama cha Jubilee kimepoteza umaarufu eneo la Mlima Kenya kwa sababu ya BBI.

“BBI haikuwa maarufu mashinani na ni wakati wa kutafakari mwelekeo wa kisiasa. Nitaelekea upande ambao watu wa Kirinyaga wataamua. Pia tunashauriana kama eneo,” Bi Waiguru alisema wiki hii.

Kauli yake ilijiri baada ya mbunge wa Gatundu Kusini pamoja na aliyekuwa waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri, ambao kwa miaka mitatu wamekuwa washirika wa Dkt Ruto, kujitenga naye na kuanzisha juhudi za kuunganisha eneo hilo kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Bw Kuria, Bw Kiunjuri na kiongozi wa chama cha Narc Kenya, Bi Martha Karua wamezidisha juhudi za kuunganisha eneo hilo kuchukua mwelekeo mmoja wa kisiasa. Wiki jana, waliwaleta pamoja viongozi kutoka mirengo yote ya kisiasa eneo la Mlima Kenya kujadili hali ya baadaye.

Bw Kiunjuri na Bw Kuria wamekataa wito wa Dkt Ruto wa kuvunja vyama vyao ili kuunga United Democratic Allliance (UDA).

Bw Kuria anaongoza Chama Cha Kazi naye Bw Kiunjuri anaongoza The Service Party of Kenya.

Viongozi wa vyama 20 vilivyo na mizizi eneo hilo walipanga kukutana kesho katika Kaunti ya Embu ili kuamua mwelekeo ambao watachukua, lakini baadaye ripoti zikasema kuwa mkutano huo umepanguliwa.

Dkt Ruto na Bw Odinga wamekuwa wakiashiria kuwa watateua wagombea wenza kutoka eneo hilo.

“Kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga, hakuna anayeweza kusema amevuta Mlima Kenya upande wake kwa wakati huu. Linaendelea kujipanga bila Rais Kenyatta na sio ajabu viongozi wakaamua kuunga mmoja wao,” asema.

Bi Karua anasema kuwa juhudi za kuunganisha vyama vya kisiasa vilivyo na mizizi eneo la Mlima Kenya zinalenga kongamano la tatu la Limuru ambalo litaamua mwelekeo wa kisiasa. Jamii za Gema zimekuwa zikikutana Limuru uchaguzi mkuu ukikaribia kuamua mwelekeo na kuteua msemaji wao ambaye kwa kawaida huwa ni mgombea urais.

Kulingana na Naibu Gavana wa Meru, Titus Ntuchiu eneo hilo halikuamua kumuunga Bw Odinga ilivyoripotiwa na viongozi wa kaunti hiyo walipokutana na kiongozi huyo wa ODM.

“Hatutaunga ODM au UDA moja kwa moja. Tutajadiliana kupitia chama chetu cha kisiasa cha kieneo,” alisema.

Alisema kwamba Gavana Kiraitu Murungi ambaye aliongoza ujumbe wa wasomi kutoka kaunti hiyo kukutana na Bw Odinga atazindua chama cha eneo la Mlima Kenya Mashariki.

Mbunge wa Kieni, Bw Kanini Kega, alisema japo walipanga kukutana, hawatajadili mgombea urais watakayeunga kama eneo kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Mkakati wangu ni wa kuleta maendeleo na amani – Ruto

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amesisitiza ataendelea kutekeleza ajenda za maendeleo nchini licha ya shutuma anazoelekezewa na baadhi ya maafisa wa serikali.

Akiongea Jumanne alipopokea viongozi wa mashinani kutoka eneobunge la Gatanga katika makazi yake rasmi ya Karen, Nairobi, Dkt Ruto pia alisema ataendelea na kampeni yake ya urais huku akipalilia umoja nchini.

“Nitaendelea kutekeleza miradi ambayo tulianzisha na Rais Uhuru Kenyatta huku tukiwaunganisha Wakenya,” akasema.

Dkt Ruto aliongeza tayari amewaleta pamoja zaidi ya wabunge 150 ambao watasaidia katika utekelezaji wa ahadi ambazo serikali ya Jubilee iliwapa Wakenya.

“Hatutavunjika moyo. Na hatutarudi nyuma,” Dkt Ruto akasisitiza.

Miongoni mwa wabunge waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Rigathi Gachagua (Mathira), Kimani Ichungwa (Kikuyu), George Theuri (Embakasi Magharibi), Isaac Mwaura (Seneta Maalum aliyepokonywa wadhifa wake) na Bw Edward Muriu anayewania kiti hicho cha ubunge cha Gatanga 2022.

Dkt Ruto alitoa kauli hiyo siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Amos Kimunya kumwonya vikali.

Wakihutubu katika makao makuu ya chama cha Jubilee mtaani Pangani, Nairobi, wawili hao walioandamana na wabunge wengine wa Jubilee walimtaka Dkt Ruto kuwakanya wandani wake dhidi ya kuikosea heshima familia ya Rais Uhuru Kenyatta.

Aidha, walimtaka kujiuzulu kutoka serikalini badala ya kuendelea kuihujumu na kupinga misimamo na sera zake ilhali yeye ni mshirika ndani ya serikali.

Majemedari wa Raila sasa waanza kumnadi Magharibi

Na SHABAN MAKOKHA

WANDANI wa Kinara wa ODM Raila Odinga wameanza kampeni kali ya kumuuza Magharibi mwa nchi na wikendi iliyopita walitua katika Kaunti ya Busia ambapo walimtaja kama anayefaa zaidi kuingia ikulu 2022.

Naibu Kiongozi wa ODM, ambaye pia ni Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya pamoja na Wabunge Raphael Wanjala (Budalang’i), Kizito Mugali (Shinayalu), Godfrey Osotsi (maalum) na mbunge wa zamani wa Funyula Paul Otuoma, walimtaja Bw Odinga kama mwanamageuzi ambaye anastahili kuchukua uongozi wa nchi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu mwakani.

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula ambao wanatoka Magharibi mwa nchi pia wametangaza kuwa watawania kiti cha Urais 2022.

Siogopi vitisho vya serikali

LEONARD ONYANGO na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto amepuuzilia mbali hatua ya serikali kumpokonya walinzi wa GSU na baadhi ya madereva huku akiitaja kama vitisho vya muda.

Dkt Ruto aliwataka wandani wake ambao pia wamekuwa wakihangaishwa na serikali kuwa wavumilivu kwani ‘vitisho mnavyopata kutoka kwa serikali ya Jubilee ni vya muda mfupi na vinapita’.

Naibu wa Rais aliyekuwa akizungumzo katika eneo la Mariashoni, Molo, Kaunti ya Nakuru, wakati wa mazishi ya aliyekuwa Seneta Maalumu Victor Prengei aliyeaga dunia katika ajali ya barabarani, alisema hatishwi na hatua ya Inspekta Jenerali Hillary Mutyambai kuondoa maafisa wa GSU katika makazi yake mtaani Karen, Nairobi, na kijijini Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu.

Alhamisi, Dkt Ruto alipigwa na butwaa Bw Mutyambai alipoagiza maafisa wa GSU waliokuwa wakilinda makazi yake kuondoka na mahala pao kuchukuliwa na maafisa wa Polisi wa Utawala (AP) kutoka Kitengo cha Kulinda Majengo ya Serikali (SGB).

Maafisa wa GSU waliondolewa katika makazi ya Dkt Ruto siku mbili baada ya Rais Kenyatta kumtaka kujiuzulu ikiwa hajaridhika kuwa serikalini.

“Wale wanaoshughulika na masuala ya mamlaka na askari, mimi sitakuwa na nafasi ya kujibizana na nyinyi kwa sababu ninashughuli nyingi za kupanga mambo ya uchumi. Sitajibizana nanyi kuhusiana na maneno ya usalama. Kabla ya kujadili suala la usalama wetu viongozi, tunafaa kujadili usalama na maslahi ya Wakenya wa kawaida kwanza,” akasema Dkt Ruto huku akionekana kurejelea Bw Mutyambai na waziri wa Usalama Fred Matiang’i.

Dkt Ruto alisema chama cha Jubilee kimegeuka kuwa chama cha vitisho na fujo hadi viongozi waliomo hawajui wasimame wapi.

“Ukiona baadhi ya wanasiasa wakinipinga si makosa yao bali inatokana na vitisho na vurugu zilizomo ndani ya Jubilee,” akasema.

Msimamo huo wa Dkt Ruto unakinzana na kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na wandani wake ambao wameshikilia kuwa maafisa wakuu wa usalama watawajibika endapo ‘chochote kitatokea kwa Naibu wa Rais’.

Mkuu wa Wafanyakazi katika Ofisi ya Naibu wa Rais, Ken Osinde, Alhamisi aliandikia barua Inspekta Jenerali wa Polisi Mutyambai akidai kuwa maisha ya Dkt Ruto yako hatarini.

Bw Osinde pia alitilia shaka maafisa maafisa wa AP waliotumwa katika makazi ya Dkt Ruto.

“Tunashuku kwamba maafisa wa AP wametumwa katika makazi ya Naibu wa Rais kutekeleza jambo ovu ambalo maafisa wa GSU walikataa kutekeleza. Utawajibika endapo kitu chochote kibaya kitatokea kwa Naibu wa Rais au mtu yeyote wa familia yake,” akasema Bw Osinde kupitia kwa barua yake kwa Bw Mutyambai.

Jumamosi, wandani wake wakiongozwa na maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Susan Kihika (Nakuru), Aaron Cheruiyot (Kericho), wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Rigathi Gachagua (Mathira), walishutumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kumhangaisha Dkt Ruto, ilhali alimsaidia kufanya kampeni 2013 na 2017 na kuibuka washindi.

Bw Murkomen alisema ni wakati Rais Kenyatta ajitokeze wazi na kuwaleleza Wakenya kosa lolote ambalo Dkt Ruto aliwahi kumfanyia au jukumu lolote alilokataa kutekeleza.

“Baada ya Mahakama ya Juu kutupilia mbali matokeo ya urais ya uchaguzi mkuu wa 2017, nilikuwa pamoja na Rais Kenyatta. Tulipitisha kauli ya pamoja kumsaidia kufanya kampeni licha ya maamuzi hayo. Dkt Ruto alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa kwenye mstari wa mbele kumsaidia Rais. Swali langu ni; alikufanyia nini ili kuelekezewa dhuluma hizi zote?” akashangaa Bw Murkomen.

Bw Nyoro na Bi Kihika walimtaka Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli kuandikisha taarifa kwa polisi kuhusu ikiwa anafahamu lolote kuhusu njama zinazoendelea dhidi ya Dkt Ruto.

Hilo linafuatia kauli ya Bw Atwoli kuwa huenda Dkt Ruto asiwepo debeni 2022.

Licha ya Bw Atwoli kujitetea Ijumaa kuwa hafahamu lolote kuhusu yanayoendelea, wawili hao walisema ni lazima awafafanulie Wakenya kiwazi.

“Bw Atwoli hawezi kutoa baadhi ya kauli bila kufahamu ukweli kuzihusu. Ikiwa ana ukweli kuhusu haya, basi anapaswa kujitokeza wazi,” akasema Bi Kihika.

Ruto ataka majibu kuhusu ulinzi wake

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto sasa anamtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Hilary Mutyambai kujibu maswali kuhusu hali zilizomfanya kuwabadilisha maafisa wa GSU waliokuwa wakilinda makazi yake katika mtaa wa Karen, Nairobi.

Kufuatia mabadiliko hayo Alhamisi, makazi ya Dkt Ruto sasa yatakuwa yakilindwa na maafisa wa Polisi wa Utawala (AP) kutoka Kitengo cha Kulinda Majengo ya Serikali.

Lakini kwenye barua aliyomwandikia Bw Mutyambai jana Ijumaa, Msimamizi Mkuu wa Wafanyakazi katika afisi ya Dkt Ruto, Balozi Ken Osinde, alisema afisi hiyo inataka maelezo kamili kuhusu kile kilichochangia mabadiliko hayo.

“Tunataka majibu kuhusu uhusiano wa mabadiliko hayo na kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya watu kwamba Dkt Ruto hatakuwa debeni kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Je, ni makosa yapi maafisa wa GSU waliokuwa wakilinda makazi ya Dkt Ruto walifanya ili kubadilishwa? Huenda hizi ni njama za kuwatumia watu wanaojifanya kuwa polisi kufuatilia mienendo ya Dkt Ruto, ambazo maafisa hao walikataa kuunga mkono?” akauliza Bw Osinde kwenye barua hiyo.

Kutokana na hilo, alisema wamekataa mabadiliko hayo, kwani yalifanywa bila kuzingatiwa kwa taratibu zifaazo kisheria.

Vile vile, alisema wanataka maafisa hao kurejeshwa, ili kuendelea na majumuku yao ya awali.

Bw Osinde pia alisema Bw Mutyambai ndiye ataelekezewa lawama, ikiwa Dkt Ruto ama jamaa yake yeyote yule atakumbwa na mkosi wowote.

Kauli yake inajiri huku Idara ya Polisi ikiendelea kushikilia kuwa hatua hiyo ni “mabadiliko ya kawaida.”

Hali hiyo iliendelea kuzua hisia mseto Ijumaa, huku watu mbalimbali wakijitokeza kukosoa uamuzi huo.

Katika hali isiyo kawaida, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli, alikosoa mabadiliko hayo akiyataja kuwa yasiyofaa.

Kwenye taarifa, Bw Atwoli alisema kuwa licha ya tofauti za kisiasa zilizopo, usalama ni haki ya msingi ya kila Mkenya.

“Hatua hiyo haifai kwani huenda ikageuzwa kuwa kisingizio kwa mkosi wowote ambao huenda ukamkumba Dkt Ruto,” akasema.

Watu wengine ambao wamekosoa hatua hiyo ni maseneta Johnson Sakaja (Nairobi), Ledama Ole Kina (Narok) kati ya viongozi wengine.

Ruto akataa talaka ya Uhuru

VALENTINE OBARA na LUCY MKANYIKA

MAJIBIZANO makali yameibuka upya kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, Dkt William Ruto huku rais akimshinikiza Dkt Ruto kuondoka serikalini.

Kwenye mahojiano katika Ikulu ya Nairobi, Jumatatu, Rais Kenyatta alilalamikia jinsi ambavyo Dkt Ruto amekuwa akikaidi misimamo ya serikali kuu tangu alipoamua (kiongozi wa nchi) kushirikiana na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kupitia ‘handisheki’ mnamo 2018.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Rais kuhojiwa na wanahabari, tangu arejee mchini kutoka Uingereza Julai 30, na tangu Mahakama ya Juu idumishe uamuzi wa Mahakama Kuu na kuharamisha marekebisho ya Katiba kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI).

“Katika jamii watu wasipoelewana, jambo la heshima kiongozi anafaa kufanya ni kusema, “sikubaliani na sera za serikali hii kwa hivyo nataka kujitenga nayo”, kisha awasilishe barua ya kujiuzulu. Natamani sana watu wangekuwa wanafanya hivi. Huwezi kuishi ndani ya nyumba kisha uwe unaibomoa wakati huo huo,” akasema Rais Kenyatta.

Hata hivyo, Dkt Ruto, Jumanne alipuuzilia mbali wito wa kumtaka ajiuzulu na kusisitiza ataendelea kumenyana na wakosoaji wake akiwa serikalini.

Alikuwa akizungumza katika mazishi ya Ronald Habel Sagurani, ambaye alikuwa diwani wa Wadi ya Mahoo, Kaunti ya Taita Taveta hadi kifo chake wiki iliyopita.

“Kwa wale wanaoona nimewakosea, nawomba msamaha. Lakini nimeamua ya kwamba sina nafasi ya kurudi nyuma wala starehe ya kusalimu amri. Nawaomba wanielewe kuwa niko na kazi maalumu ya kutekeleza kwa sababu tumeamua tutabadilisha uchumi,” akasema.

Tangu 2018, Naibu Rais amekuwa akilalamika kuwa ushirikiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga ulitatiza utekelezaji wa mipango ya serikali ya Jubilee kufanikisha maendeleo nchini, akidai muda na rasilimali nyingi za serikali zilitumiwa kwa kampeni za BBI.

Mivutano kati ya viongozi hao wawili wakuu serikalini ilifikia kiwango cha kuwa, Naibu Rais alionekana kama mwanaharamu asiyependwa nyumbani.

Licha ya kuwa baadhi ya majukumu yake yalikabidhiwa Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i, huku pia mawaziri, makatibu wa wizara na Bw Odinga wakitumwa kumwakilisha Rais katika hafla mbalimbali, Rais Kenyatta alisisitiza huwa anashirikisha viongozi wote katika maamuzi yake.

“Nimejaribu kadri ya uwezo wangu kuhusisha kila mtu serikalini ikiwemo wale wanaoikosoa. Kama hupendezwi na ajenda yangu niliyochaguliwa kutekeleza, ondoka uachie wengine nafasi kisha wewe utapata nafasi yako baadaye utekeleze yako. Huwezi kutuambia huondoki na wakati huo huo hatuelewani, ni lazima uamue,” alisema Rais Kenyatta.

Kulingana na Dkt Ruto, mipango ya kurekebisha katiba ambayo iliharamishwa na Mahakama Kuu kisha katika Mahakama ya Rufaa wiki iliyopita, ilikuwa imelenga kuwanufaisha viongozi wachache na kumsaidia Bw Odinga kushinda urais kwa urahisi 2022.

Hata hivyo, Rais Kenyatta alipohojiwa Jumatatu alirejelea msimamo wake kuwa BBI ililenga kuleta mabadiliko ambayo yangemfaa raia wa kawaida, na hivyo basi maamuzi ya mahakama ni pigo kubwa kwa wananchi.

Alitoa mfano wa pendekezo la kuongeza idadi ya maeneobunge, ambapo, kulingana naye, lingepelekea maeneo yaliyo na idadi kubwa ya watu kugawanywa na hivyo basi ugavi wa fedha za Hazina ya Kitaifa ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF) kufanywa kwa njia ya usawa.

Rais alipuuzilia mbali kuwa BBI ilinuiwa kumwezesha Bw Odinga kuingia Ikulu, wala yeye mwenyewe kuongeza kipindi chake cha uongozi.

Lakini kama mwanandoa asiyetaka kujibizana na mwenzake ana kwa ana wanapozozana, Dkt Ruto alitumia fursa mazishini Taita Taveta kusisitiza msimamo wake kwamba BBI ilijali masilahi ya vigogo wa kisiasa.

Imani ya Naibu Rais na wandani wake kuhusu msimamo huu wa BBI imekuwa ikitiliwa nguvu katika siku za hivi majuzi, ambapo Rais aliandaa vikao mara mbili katika Ikulu ya Mombasa na Bw Odinga, pamoja na vinara wa Muungano wa OKA.

Mfumo wa kuinua uchumi bottom-up umetajwa kwenye Biblia – Ruto

Na SAMMY WAWERU

NAIBU wa Rais William Ruto ameendelea kutetea mfumo wa bottom-up kuboresha uchumi, anaotumia kama mojawapo ya sera kutafuta kura kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.

Dkt Ruto amesema mfumo wa kuinua uchumi kutoka chini kuenda juu, anaohoji unalenga maskini, mwananchi wa kawaida na vijana umetajwa kwenye Biblia.

“Wakati mnaskia tunasema kuhusu mfumo wa kuboresha uchumi wa bottom-up, umetajwa kwenye Biblia agano la Zaburi sura ya 113 mlango wa 7 na 8,” Dkt Ruto akasema.

Alisema hayo Jumapili, alipohudhuria ibada ya misa katika Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Francis Assisi, Gatina, eneo la Kawangware, Nairobi.

“Mungu aliye juu mbinguni anasema atamwinua fukara kutoka mavumbini, amnyanyue maskini kutoka unyonge wake na kumketisha na wafalme, pamoja na viongozi wa watu wake,” Naibu Rais akanukuu mafungu hayo.

Huku baadhi ya wapinzani wake wakimkosoa na kudai ahadi zake ni hadaa tupu kwa wananchi, Ruto alisema endapo atakuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya, mfumo wa bottom-up atautumia kutafutia ajira wasio na kazi, kina mama mboga na kundi la mahastla, kauli anayotumia kuashiria na kujihusisha na “watu wa kiwango cha chini kimaendeleo”, kuboresha maisha yao.

Aidha aliendelea kusuta wapinzani wake, akisema wanatumia Mpango wa Ripoti ya Maridhiano (BBI) ambao hatma yake i mikononi mwa mahakama ya rufaa, kubuni nafasi za uongozi kujinufaisha.

“Nyinyi watu wa Kawangware mtakubali tuwe na mjadala wa kugawana mamlaka?” akahoji wakati akihutubia waumini wa Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Francis Assisi, akionekana kuelekeza matamshi yake kwa kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

“Utulivu na umoja wa taifa utakuwa wa manufaa endapo mjadala hautaegemea kubuni nafasi za viongozi. Uwe wa kuimarisha maisha ya wananchi…Hapo ndio tutakuwa tunatembea pamoja kama taifa na Wakenya,” akasema.

Naibu Rais ni kati ya viongozi na wanasiasa walioeleza azma yao kuwania urais mwaka 2022.

Juhudi za Naibu Rais kupenya Ukambani zapata pigo kubwa

Na PIUS MAUNDU

JUHUDI za Naibu Rais William Ruto kupenya katika Kaunti ya Kitui ziligonga mwamba baada ya madiwani 15 waliokutana naye wiki hii kubanduliwa katika kamati za bunge la kaunti.

Spika wa bunge la Kaunti ya Kitui, George Ndotto aliwasuta madiwani hao walioandamana na aliyekuwa naibu gavana wa Nairobi, Jonathan Mueke kukutana na Dkt Ruto katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi.

“Tunatenga Bunge la Kaunti ya Kitui na vitendo vya madiwani waliokutana na Dkt Ruto,” Bw Ndoto alisema kwenye taarifa na kuongeza kuwa Naibu Rais hatapenya katika ngome hiyo ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

“Tunataka ifahamike kwamba sisi wawakilishi wa Kaunti ya Kitui tuko nyuma ya mgombea urais wetu Stephen Kalonzo Musyoka kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Hakuna kitakachotufanya tubadilishe msimamo wetu. Tunataka Wakenya wajue kuwa Kalonzo Musyoka anaungwa mkono kikamilifu katika kaunti yake ya nyumbani na tunawahimiza wampe heshima anayohitaji kuongoza nchi hii.”

Sababu za Ruto kutia miamba 5 tumbojoto

Na WANDERI KAMAU

UJASIRI mkubwa alio nao Naibu Rais William Ruto kwamba atamrithi Rais Uhuru Kenyatta, licha ya vizingiti vilivyoko mbele yake, ni miongoni mwa sababu kuu zinazomfanya kuogopwa na vigogo wengine wa siasa nchini.

Kufikia sasa, Dkt Ruto hajaelezea nia yoyote ya kubuni muungano wa kisiasa na vigogo wengine.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio wiki iliyopita, Dkt Ruto alisema “hataunda miungano ya kikabila” akisisitiza huo si mkakati wa mrengo wake wa ‘Hustler Nation.’

Hata hivyo, wadadisi wa siasa wanasema tatizo kuu linalomwandama Dkt Ruto ni ahadi aliyotoa Rais Kenyatta kwamba, atamuunga mkono kuwa mrithi wake kwa miaka kumi atakapomaliza kipindi chake 2022.

Mnamo 2016, Rais Kenyatta alisema baada ya kumaliza kuhudumu kwa miaka kumi, angemuunga mkono Dkt Ruto kuiongoza nchi kwa miaka 10 pia.

“Dkt Ruto anaonekana kushikilia kuwa lazima Rais Kenyatta atimize ahadi yake kama alivyosema. Anaamini Rais anastahili ‘kumrudishia mkono’ kwa kumfanyia kampeni mnamo 2013 na 2017,” asema mdadisi wa siasa Mark Bichachi.

Anasema imani hiyo ndiyo imemfanya kuunda kundi la ‘Tangatanga’, lengo kuu likiwa kuonyesha ana uwezo wa kujitafutia wafuasi bila uungwaji mkono wa Rais.

“Anaporejelea kuwa mrengo wake una wananchi na Mungu, ni ishara ya kupoteza imani kabisa kupata uungwaji mkono wa serikali, kinyume na ilivyokuwa kabla ya uhusiano wao na Rais Kenyatta kudorora. Ni msimamo huu ambao pia unaakisi masaibu ambayo baadhi ya washirika wake wa kisiasa wamekuwa wakipitia,” asema Bw Bichachi.

Wadadisi wanasema sababu nyingine ya Dkt Ruto kuogopwa na vigogo wengine wa kisiasa ni kwa sababu anawachukulia kama wasaliti.

Ruto atawezana?

Na WANDERI KAMAU

UFANISI wa jitihada za Rais Uhuru Kenyatta kubuni muungano wa vigogo wakuu wa siasa za kimaeneo utakuwa pigo kubwa kwa ndoto ya Naibu Rais William Ruto kuongoza Kenya mwaka 2022.

Wachanganuzi wa siasa wasema ikiwa waliokuwa vinara wa NASA watakubali kubaki pamoja hadi uchaguzi wa mwaka 2022, basi Dkt Ruto atakuwa na nafasi ndogo sana ya kuingia Ikulu.

Kulingana na mchanguzi wa siasa, Javas Bigambo, muungano wa Moses Wetangula (Ford-Kenya), Gideon Moi (Kanu), Kalonzo Musyoka (Wiper), Raila Odinga (ODM) na Musalia Mudavadi (ANC) chini ya udhamini wa Rais Kenyatta utakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kutwaa madaraka 2022.

Wadadisi wanasema kwa kuwaunganisha vigogo hao, Rais Kenyatta analenga kubuni dhana kuhusu uwepo wa “mrengo wa kisiasa unaoshehenii sura kamili ya Kenya.”

Rais Kenyatta anaonekana kuwakilisha eneo la Mlima Kenya, Bw Odinga eneo la Nyanza, Bw Musyoka eneo la Ukambani, Mabw Mudavadi, Wetang’ula na Oparanya eneo la Magharibi huku Moi akiwakilisha ukanda wa Bonde la Ufa.

“Manufaa makubwa ya kisiasa walio nayo ni kuwa, wanajenga dhana kuwa wanawakilisha kila sehemu ya Kenya. Ikiwa watabuni muungano wa kisiasa wenye nguvu, itakuwa rahisi kwao kuwashinikiza wafuasi wao kuwaunga mkono. Hili ni ikilinganishwa na Naibu Rais William Ruto, ambaye atahitaji kuwa na washirika zaidi wa kisiasa katika maeneo hayo,” asema Bw Bigambo.

“Ukitazama uungwaji mkono kwa sasa, unaweza ukasema Ruto ana asilimia 95 ya kura za Wakalenjin na takriban asilimia 44 hadi 55 za Wakikuyu, ambazo zinaweza kupungua kadri uchaguzi unavyokaribia ikitegemea masuala tofauti ikiwemo uteuzi wa naibu wake.

“Kwa upande mwingine, vigogo wa NASA wanadhibiti hizo kura nyingine pamoja na zilizosalia za Wakikuyu ukiongeza Uhuru kwenye hesabu hiyo. Hii ina maana kuwa muungano wa waliokuwa Nasa pamoja na Uhuru uko kifua mbele,” mchanganuzi Mark Bichachi alidokezea Taifa Leo katika mahojiano.

Muungano huo pia unatajwa kuwa katika nafasi nzuri ya kufaidika kutokana na raslimali za serikali.

“Vigogo hao wana nafasi ya kufaidika kutokana na raslimali za serikali. Rais ana ufahamu kuhusu matumizi ya raslimali hizo kujisaidia na kujiendeleza kisiasa,” akasema Bw Bigambo.

Mnamo Agosti 2020, kakake Bw Odinga, Dkt Oburu Oginga, alisema anaamini kigogo huyo ana nafasi nzuri kuibuka mshindi wa urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, kwani atakuwa na uungwaji mkono wa serikali.

Wadadisi wanataja uungwaji mkono wa serikali iliyopo kama jambo muhimu kwa mgombea urais yeyote yule, kwani hilo humpa imani kubwa ya kisiasa.

Wanataja hilo kama moja ya vikwazo vilivyowaandama baadhi ya vigogo hao kwenye azima ya kuwania urais katika miaka ya awali.

“Kiuhalisia, serikali huwa na ushawishi mkubwa kwa taasisi muhimu kama Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Idara ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS), Idara ya Polisi, Jeshi la Kenya (KDF), Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kati ya nyingine ambazo huwa muhimu katika mchakato mzima wa uchaguzi,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Marais wa awali kama marehemu Daniel Moi walikuwa wakikosolewa kwa kutumia asasi hizo vibaya kwenye chaguzi kuu.

Rais Kenyatta pia amekuwa akikosolewa na wapinzani wake kwa kutumia taasisi hizo kuwahangaisha washirika wa kisiasa wa Dkt Ruto.

Lengo lingine la Rais Kenyatta, kulingana na wadadisi, ni kubuni dhana kuwa vigogo hao wana uwezo mkubwa kuwashinikiza wafuasi wao katika maeneo wanakotoka kujitokeza pakubwa kuwaunga mkono.

Wanasema chini ya mpangilio huo, vigogo hao wataonekana kama ‘wawakilishi’ wa makabila yao, hali itakayoifanya vigumu kwa Dkt Ruto kupenya katika ngome zao.

“Ikizingatiwa siasa za Kenya hujikata kwenye ukabila, kuna uwezekano mkubwa jamii zitakimbilia mrengo ulio na ‘mmoja wao’, hivyo kuupa muungano huo uungwaji mkono mkubwa katika karibu maeneo yote nchini,” asema Bw Bigambo.

Wanasema uhalisia huo umeshuhudiwa kwenye chaguzi zote kuu nchini kuanzia 1992, wakati mfumo wa vyama vingi ulipoanza nchini.

Hata hivyo, wakosoaji wa muungano huo wanautaja kuchangiwa na “hofu ya umaarufu” wa Dkt Ruto.

Wanasema pasingekuwepo na umaarufu wa Dkt Ruto, huenda kila mmoja angewania urais kivyake.

“Wakati vigogo hao sita wanapoungana dhidi ya Dkt Ruto, inamsawiri Ruto kama aliye na umaarufu mkubwa kuwaliko. Hili linajenga taswira kuwa lengo lao kuu ni kupata mamlaka, kwani wengi wao hawajaelezea waziwazi manifesto zao,” asema Bw Bigambo.

Ruto akita kambi Nakuru kupigia debe mfumo wa kumuinua mwananchi wa kipato cha chini

Na RICHARD MAOSI

NAIBU Rais William Ruto alikita kambi katika eneo la Elementaita, Kaunti ya Nakuru, Jumatatu kupigia debe muundo wa kuimarisha uchumi unaolenga kumtoa mtu wa kipato cha chini katika lindi la umaskini hadi katika viwango vya maisha bora.

Muundo huo anauita ‘bottom -up economy’ na umezua mjadala kote nchini.

Ruto alihudhuria kikao hicho ambacho kiliwaleta pamoja washikadau, wasomi pamoja na viongozi wa kutoka eneo la Nyanza kuzungumzia maswala muhimu ya kiuchumi na biashara.

Akiwahutubia wanahabari, Ruto alieleza kuwa kuna haja ya kuboresha teknolojia ya uzalishaji wa mimea na mifugo, kama nia mojawapo ya kupiga jeki maendeleo.

Aidha aliwashtumu viongozi wanaopinga muundo wa Bottom-Up, akisema wengi wao walikuwa na nia ya kujitengenezea nyadhifa za uongozi.

Ni katika hafla hiyo ambapo washikadau na viongozi waliweka mikakati ya kufanikisha mambo matatu muhimu, katika hatua ya kukwamua raia kutokana na hali ngumu ya maisha, hususan wakati huu taifa likiendelea kupigana na janga la Covid-19.

Alisema kuwa uwekezaji katika sekta ya umma na binafsi utasaidia kuboresha miundomisingi ya nchi na hatimaye kutengeneza nafasi nyingi za ajira miongoni mwa vijana, ikizingatiwa kuwa asilimia kubwa hawana kazi.

Pili alisema kuwa serikali imeanzisha mikakati ya namna ya kuimarisha uzalishaji katika sekta ya kilimo kuanzia miwa, parachichi, ndizi, mahindi na mihogo.

“Ninatumai wale wanaopinga mapendekezo haya wataitikia wito tuandae kikao cha majadiliano ambayo yataleta mapendekezo muhimu kuhusu namna ya kumfaa raia wa kawaida,” akasema.

Aidha aliwataka wakome kuhepa kila mara mjadala kuhusu namna ya kukwamua uchumi wa nchi unapojadiliwa.

Raila amsuta Ruto kulialia ndani ya serikali

Na WAANDISHI WETU

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amemsuta Naibu Rais William Ruto kwa kulalamika jinsi rafiki yake, Bw Harun Aydin, alikamatwa na maafisa wa kupambana na ugaidi.

Bw Odinga alisema ni kinaya kwamba wanaolalamika wako ndani ya serikali na wanajua yanayojiri, ilhali wanataka kulaumu wengine.

Bw Aydin alikuwa aandamane na Naibu Rais kuelekea Uganda wiki iliyopita; lakini Dkt Ruto alizuiwa kusafiri, ikidaiwa kuwa amri ya kutaka asiondoke nchini ilitolewa na mamlaka za juu serikalini.

Raia huyo wa Uturuki alikamatwa na polisi Jumamosi katika uwanja wa ndege wa Wilson jijini Nairobi, akitokea Kampala, Uganda.

“Serikali inashughulikia mambo ya uhalifu na kadhalika. Wale ambao wako serikalini lakini wanapiga kelele ndio wanajua kinachoendelea na sababu zake. Mimi siwezi kujua kama sijaelezwa maana siko serikalini,” alisema Bw Odinga.

Alikuwa ameandamana na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi, kwa ibada katika kanisa la ACK Mombasa.

Dkt Ruto na wanasiasa wanaoegemea upande wake jana waliendelea kulalamika kuhusu kisa hicho, wakidai ni sehemu ya mbinu za kumhangaisha katika safari yake ya kuwania urais mwaka 2022.

Akiongea baada ya kuhudhuria ibada katika kanisa Katoliki la St Joseph mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru, Dkt Ruto alisema wanaompiga vita kisiasa watumie nguvu zao kuunganisha Wakenya na kuuza manifesto zao.

“Mipango yetu ya maendeleo haikupiga hatua kubwa kwa sababu ya migogoro ya kisiasa. Sasa wanataka kutisha Wakenya kwamba, ukiwa rafiki wa Ruto utapelekwa mahakamani. Kama wewe ni mwekezaji unayejuana na Ruto utapelekwa mahakamani,” akaeleza.

Mbunge wa Kikuyu, Bw Kimani Ichung’wa, alishutumu baadhi ya maafisa katika Ofisi ya Rais akidai wanahusika kumdhalilisha Dkt Ruto.

Akisema ni ofisi hiyo ambayo hushughulikia suala la kuwapa raia wa kigeni idhini ya kuingia nchini, alishangaa vipi Mturuki huyo alikubaliwa kuingia Kenya na kuondoka mara kadhaa hapo awali.

Bw Ichung’wa alionya kwamba kisa cha hivi majuzi kitafukuza wawekezaji nchini, huku akimsihi Naibu Rais kusimama kidete na kutotishwa na mipango ya wapinzani wake.

“Walianza na viongozi wanaoegemea upande wa Naibu Rais. Lakini sasa wamehamia wawekezaji na wafanyabiashara mpaka wawekezaji sasa wanatoroka nchi,” alihoji.

Duru zilisema Bw Aydin anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo; na polisi wataomba kumzuilia kwa muda zaidi ili wakamilishe uchunguzi kuhusu madai kwamba anahusika katika kufadhili ugaidi.

Mwaka huu 2021, inasemekana Mturuki huyo amesafiri Kenya mara sita kutoka Istanbul (Uturuki), Cairo (Misri) na Addis Ababa (Ethiopia).

Wakili wake, Bw Ahmednassir Abdullahi, Jumapili alisema bado hajakubaliwa kumwona.

“Kwa siku ya pili nimekatazwa kumwona Harun Aydin. Sababu bado ni ile ile…“amri kutoka juu”. Kwa bahati nzuri, hawana budi ila kumfikisha mahakamani kesho (leo Jumatatu) kama inavyotakikana kikatiba,” akasema kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.

Afisa katika ubalozi wa Uturuki jijini Nairobi alisisitiza kuwa, Bw Aydin hana rekodi yoyote ya uhalifu nchini kwao na ni mfanyabiashara. Hata hivyo, hajasema hufanya biashara gani.

Ripoti za Winnie Atieno, Mary Wambui na Macharia Mwangi

Ruto hatimaye afafanua mfumo wa ‘Bottom-up’

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto hatimaye amejitokeza kutetea mpango wake wa kiuchumi wa kuwainua watu maskini maarufu kama Bottom Up Model baada ya wandani wake kadhaa kuonekana kushindwa kuufafanua inavyofaa.

Baadhi ya washirika wa Dkt Ruto wamejipata matatani, wakishindwa kueleza kwa kina maana halisi ya mfumo huo.

Miongoni mwa wale waliojipata katika hali hiyo ni mbunge Alice Wahome (Kandara) na Kimani Ichung’wa (Kikuyu).

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni mapema wiki hii, Bi Wahome alionekana kushindwa kabisa kufafanua jinsi mpango huo utakavyowasaidia Wakenya ikiwa Dkt Ruto atachaguliwa kuwa rais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Ichung’wa pia alijipata katika hali iyo hiyo majuzi, alipoelezwa kutofautisha mfumo huo na ule wa ugatuzi, kwani utaratibu wake ni kuelekeza fedha mashinani.

Lakini jana, Dkt Ruto alisema kuwa mpango huo unalenga kuwasaidia wananchi wa kiwango cha chini, kuwawezesha kuendesha biashara zao bila kuchukua mikopo kutoka kwa wakopeshaji wa kibinafsi na mashirika mengine ya kifedha yanayowatoza riba ya kiwango cha juu.

“Lengo letu ni kuwainua wananchi wa kiwango cha chini kwa namna ambayo wataweza kujisimamia kifedha kwa kupata mikopo ya riba ya kiwango cha chini. Tutaafikia hili kwa kubuni hazina maalum kushughulikia mahitaji yao ya kifedha,” akasema Dkt Ruto.

Baadhi ya viongozi wamekuwa wakikosoa mfumo huo kama unaokosa kueleza kwa kina jinsi utakavyowainua Wakenya.

Hapo awali Naibu Rais alikuwa ameahidi kutenga takribani Sh200 bilioni kutoka kwa mgao wa maendeleo kwenye bajeti ili kuinua biashara za kiwango cha chini.

Mbinu za kuzima Ruto Mlimani zaanza kusukwa

Na BENSON MATHEKA

WASHIRIKA wa Rais Uhuru Kenyatta kutoka eneo la Mlima Kenya wameanza kusuka mikakati ya kupunguza umaarufu wa Naibu Raise eneo lao na kumvumisha kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Mikakati hiyo inadhamiria kumsawiri Bw Odinga kama rafiki wa eneo hilo ambaye serikali yake itajali na kulinda maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya.

Mnamo Jumanne, baadhi ya washirika wa Rais Kenyatta waliahidi Bw Odinga kwamba watamuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu ujao wakimtaja kama rafiki wa jamii hiyo kwa miaka mingi.

Duru zinasema kwamba kwa baraka za Rais Kenyatta, wanasiasa wanaounga handisheki wataendesha kampeni kutumia vyombo vya habari hasa vituo vya redio vya lugha za jamii za eneo hilo kumjenga Bw Odinga.

“Tuna mikakati yetu na wakati huu, wanaodhani ni jogoo wa kuwika Mlima Kenya watajua kwamba tunamtambua Bw Odinga kama jamba,” alisema mbunge mmoja ambaye aliomba tusitaje jina lake asionekane kumwaga mtama mapema.

Alisema kwamba wamepanga kuhakikisha kuwa Bw Odinga atamrithi Rais Kenyatta kwa kuwa amedhihirisha hana kisasi au chuki na jamii yoyote Kenya.

Mnamo Alhamisi, baraza la watu mashuhuri katika Kaunti ya Murang’a ambalo lina ushawishi mkubwa katika kaunti hiyo na Mlima Kenya kwa jumla lilikutana kujadili hali ya siasa.

Ingawa waliyojadili hayakubainika mara moja, duru zinasema walijadili athari za siasa kwa eneo lao na anayeweza kulinda maslahi ya wakazi.

Mkutano wao ulijiri siku mbili baada ya mfanyabiashara SK Macharia, mmoja wa wanachama wa baraza hilo, kuwa mwenyeji wa Bw Odinga katika hafla aliyoandaa eneo la Ndakaini ambapo waliozungumza walimsifu Bw Odinga na kuahidi kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Duru zinasema kuwa miongoni mwa mikakati ya washirika wa Rais Kenyatta ni kuondoa hofu ya wakazi kumhusu Raila ambayo imeenezwa na kukita mizizi kwa miaka mingi na uongo ambao washirika wa Naibu Rais wamekuwa wakieneza kumhusu.

“Wapinzani wetu wamekuwa wakitangatanga eneo letu kwa miaka minne na kudanganya watu wetu kwamba Raila ni hatari kwa eneo lao ilhali ‘Baba’ hajawahi kufanya lolote baya. Tunataka kuondoa uongo huu,” alisema mbunge wa kuteuliwa Maina Kamanda.

Kulingana na mbunge huyo, moja ya mikakati yao ni kufuta uongo wa Naibu Rais, Dkt Ruto na washirika wake na kuleta ‘pumzi’ mpya katika siasa za eneo la Mlima Kenya.

Alisema wakati umefika wa kuondoa propaganda na kueleza wakazi ukweli.

Ijumaa, washirika wa Rais Kenyatta walitarajiwa kukutana kusuka mikakati kuanzia madiwani, wabunge, magavana na viongozi wa kijamii wenye ushawishi.

Lengo la washirika na wanamikakati wa Rais Kenyatta ni kufuta kauli-mbiu ya Hasla ambayo Dkt Ruto ametumia kupenya na ‘kuteka’ eneo hilo kwenye safari yake ya kuelekea ikulu 2022.

Ujumbe wao kwa wakazi utakuwa ni kwamba Bw Odinga ametekeleza wajibu mkubwa kwa nchi hii si tu kuanzia handisheki yake na Rais Kenyatta mnamo Machi 2018 bali kuanzia 1963 baba yake aliposaidia Mzee Kenyatta kuachiliwa huru na wakoloni, kupigania demokrasia wanayofurahia na kumwezesha Mwai Kibaki kushinda urais 2002.

Uchaguzi: Mrengo wa Ruto watishia kushtaki Kenya UN

Na WAANDISHI WETU

MJADALA kuhusu tarehe ya Uchaguzi Mkuu 2022 umeibua cheche za maneno, huku wanasiasa wanaomuegemea Naibu Rais William Ruto wakitishia kuishtaki serikali kwa Umoja wa Mataifa (UN).

Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali, na aliyekuwa Seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, walisema Chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho Dkt Ruto anatarajia kutumia kuwania urais 2022, hakitakubali uchaguzi uahirishwe.

“Tutapinga hilo na hata kuandika barua kwa Baraza la Usalama katika Umoja wa Mataifa (UN) kueleza kuwa Kenya haiko vitani, na hivyo serikali inafaa kuweka mipango ya kuhakikisha uchaguzi utafanyika jinsi ilivyopangwa,” akasema Bw Omar.

Wiki iliyopita, Mahakama ya Afrika ilichapisha maoni kwa mataifa ya Afrika ambayo hayatakuwa na uwezo wa kuandaa uchaguzi kwa sababu ya janga la corona, yazingatie kuahirisha; japo ikiwa tu kuna sheria za kitaifa zinazoruhusu uahirishaji wa Uchaguzi Mkuu.

Katiba inahitaji Uchaguzi Mkuu kufanyika mwaka wa tano baada ya kila uchaguzi, katika Jumanne ya pili ya mwezi Agosti.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) tayari ilitangaza uchaguzi utafanyika Agosti 9, 2022.

“Janga kuu zaidi litakuwa kuendelea kuishi chini ya serikali hii iliyojaa ubaguzi katika utoaji huduma kwa Wakenya.

“Hatutakaa kitako tukitazama uchaguzi uahirishwe kinyume cha Katiba. Wale wanaoshinikiza hilo wanajua wamepoteza umaarufu mashinani na sasa wanataka muda zaidi wajiandae kwa uchaguzi,” alisisitiza Bw Omar.

Naye Bw Ali aliongeza: “Kuna viongozi wa kaunti na wengine katika serikali kuu ambao wamekuwa wakijaribu kuninyamazisha. Sitanyamaza wakati watu wachache wanata kunufaika huku wananchi wakiteseka.”

Wawili hao walikuwa wakizungumza katika kikao cha wanahabari mjini Mombasa, baada ya kuzindua upya shughuli ya kusajili wanachama katika UDA.

Akizungumza katika eneo la Ruriri, Kaunti ya Nyandarua, Mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro alisema hawatakubali tarehe hiyo ibadilishwe.

“Ushauri uliotolewa na Mahakama ya Afrika haujaipa Kenya kibali cha kuahirisha uchaguzi. Sisi tarehe yetu inalindwa na Katiba,” akasema mbunge huyo katika hafla ambapo Dkt Ruto alikuwa ameenda kuwashukuru wakazi kwa kuchagua MCA wa chama cha UDA.

Gavana wa Pokot Magharibi Prof John Lonyangapuo alionya kuwa uvumi kuhusu njama ya kuairisha uchaguzi mkuu unaweza kutumbukiza taifa katika machafuko. Alisema siasa za aina hiyo ni hatari kwa nchi.

“Tunafaa kukomesha uvumi na propaganda kuhusu suala hilo. Hata kama ni ukweli, wacha ije. Tupunguze joto la kisiasa na kuhudumia Wakenya,” akasema Prof Lonyangapuo mjini Kanyarkwat alipokagua miradi.

Naye kinara wa Narc Kenya, Bi Martha Karua, akizungumza Jumamosi katika kijiji cha Riandira, Kaunti ya Kirinyaga, alisema tarehe ya chaguzi inaweza tu kubadilishwa iwapo Kenya iko katika vita na taifa lingine.

“Kwa sasa, Kenya ina amani; tarehe ya chaguzi inapaswa kusalia ilivyo,” waziri huyo wa zamani wa masuala ya Katiba alieleza na kuwataka Wakenya kusimama kidete kukataa njama zozote za kuahirishwa kwa uchaguzi.

“Tunafaa kujiandaa kukataa njama zozote za serikali kuahirisha tarehe ya uchaguzi. Ni sharti kura ifanyike kuambatana na Katiba,” alisema.

Ripoti za ANTHONY KITIMO, JOSEPH OPENDA, MARY WANGARI, OSCAR KAKAI na GEORGE MUNENE

Dkt Ruto afichua alichomnong’onezea Rais katika ukumbi wa Bomas

Na SAMMY WAWERU

NAIBU Rais Dkt William Ruto amefichua yaliyojadiliwa kwenye manong’onezano kati yake na Rais Uhuru Kenyatta Oktoba 26, 2020 wakati wa uzinduzi rasmi wa Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) katika ukumbi wa Bomas of Kenya.

Wakati wa hafla hiyo, Rais Kenyatta akianza kuhutubu, kwa utani alitumia fumbo la riadha za masafa mafupi kupokezana vijiti, kuashiria muafaka kati yake na Dkt Ruto kumuunga mkono aingie Ikulu 2022.

Alisema badala ya Naibu wake kusubiri apokezwe kijiti, alikirejelea nyuma, anayemkabidhi akiwa mbali.

Rais Kenyatta alisema hayo, kufuatia msimamo wa Dkt Ruto hadharani kuhusu BBI, akitaka kuelezwa mswada huo maarufu na ambao kwa sasa uko mikononi mwa mahakama ya rufaa baada kuharamishwa, utakavyoleta uongozi jumuishi na kusaidia Mkenya wa kawaida kujiimarisha.

Dkt Ruto alipasua mbarika Jumanne, akisema alimsaili Rais kwa nini maagano yake aliyaelekeza kwa mpinzani ama wapinzani wa Jubilee.

“Najua watu wamekuwa wakitaka sana kujua tulichonong’onezana. Nilimueleza Rais ‘mbona wewe katika harakati zetu, kile kijiti cha chama chetu unataka kumpa mwingine’,” akasema.

Maelezo ya Dkt Ruto yakionekana kutegua kitendawili cha alichomueleza Rais, yanafasiriwa kulenga kuchanganua usaliti unaoendelea kushuhudiwa katika chama tawala cha Jubilee.

Wakati wa kampeni za 2013 na 2017, Rais Kenyatta alinukuliwa mara kadha akiahidi naibu wake kwamba atamuunga mkono 2022 ili kuingia Ikulu.

Handisheki kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo Machi 9, 2018, ambapo viongozi hawa walitangaza kuzika tofauti zao za kisiasa, imeonekana kuharibu mpango kabambe wa Ruto.

Ruto aahidi wapiga kura bondeni uhuru wa kuamua

Na GEORGE SAYAGIE

NAIBU Rais William Ruto ameahidi wa wakazi wa kaunti za bondeni kwamba hataingilia uamuzi wao kuhusu viongozi watakaowachagua kuwania nyadhifa mbalimbali kwenye uchaguzi wa 2022.

Mapema wiki hii, Dkt Ruto aliwaahidi wakazi wa Kaunti ya Narok kwamba, licha ya kuwa mkazi wa Narok baada ya kununua ardhi katika eneo la Transmara Magharibi, hataingilia demokrasia yao kwa kuwachagulia kiongozi.

“Hakuna mtu anayepaswa kutoka nje na kuchagua au kuwalazimishia kiongozi kama wakazi wa Narok au katika sehemu zozote za taifa hili. Tumieni haki zenu kidemokrasia na kuchagua viongozi mnaotaka kwa nyadhifa tofauti 2022,” alisema Dkt Ruto.

Dkt Ruto amejitahidi kunasa tena eneo la Narok, ambalo Rais Uhuru Kenyatta alipoteza kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga katika chaguzi za 2013 na 2017.

Amezidisha shughuli za kisiasa katika kaunti za Narok na Kajiado katika wiki za hivi majuzi akinuia kudhibiti kisiasa jamii ya Wamaasai.

Naibu Rais tayari anakabiliwa na kitendawili kigumu kisiasa kwa sababu wandani wake kadhaa wanamezea mate viti vya ugavana katika eneo la Bonde la Ufa.

Kizungumkuti kinachomsubiri Dkt Ruto kinatokana na hali kwamba, idadi kubwa ya wagombea watawania tiketi ya chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) na huenda wanategemea usaidizi wake kupata uteuzi kwa kinyang’anyiro hicho.

Tayari, makabiliano makali kisiasa yanatokota huku vikosi vya Naibu Rais vikijiandaa kuwabwaga viongozi wa kaunti hizo huku wengine wakijitayarisha kuwarithi wale waliokamilisha hatamu zao mbili za uongozi.

Kufikia sasa, wagombea wanaomezea mate tiketi ya (UDA) ili kutwaa kiti cha Gavana Samuel Tunai anayehudumu kipindi chake cha mwisho afisini ni wabunge watatu na waziri msaidizi mmoja.

Miongoni mwa vigogo walio mbioni kumrithi Gavana Tunai, ni Waziri Msaidizi katika Wizara ya Leba Patrick Ntutu na Mwakilishi Mwanamke Narok Soipan Tuya, wabunge Gabriel Tongoyo (Narok Magharibi), Korei ole Lemein (Narok Kusini).

Wengine ni Katibu wa Wizara ya Ugatuzi Charles Sunkuli, ambaye hajataja chama atakachokitumia kuwania kiti hicho.

Uchaguzi 2022 ni lazima – Ruto

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto amepuuza wito wa kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu ujao, akitaja pendekezo hilo kama kelele zitakazopita, na uchaguzi mkuu ujao ufanyike kwa amani.

Dkt Ruto alisema kwamba wanaopendekeza uchaguzi mkuu uahirishwe wanaharibu wakati kwa sababu ni lazima uchaguzi mkuu ufanyike Agosti 9, 2022 ilivyopangwa.

“Ninataka kuwaambia Wakenya msiwe na wasiwasi, msitishwe. Kenya hii ni ya Mungu. Tutakuwa na amani kutoka sasa hadi 2022. Hizi kelele mnazosikia zitapita na uchaguzi wa 2022 utafanyika kwa amani,” akasema Dkt Ruto.

Dkt Ruto alisema kwamba Mungu ataipa nchi hii viongozi watakaochukua usukani 2022.

“Maneno haya mengi ni mipango tu ya siasa. Na nyinyi si wageni kwa mambo ya siasa. Itapangwa hivi na vile na mambo yataenda sawasawa kwa sababu tuko na Mungu,” alisema.

“Msitutishe eti huenda kukaenda vingine na kuharibika. Hakutaharibika kwa sababu tunaamini Mungu na ni Mungu wa amani,” alisema.

Dkt Ruto alisema Mungu ni wa mipango na hivyo basi ni lazima Kenya isonge mbele kwa kuzingatia mipango iliyowekwa. Baadhi ya wanasiasa wanaounga Mpango wa Maridhiano (BBI) wamekuwa wakipendekeza uchaguzi mkuu ujao uahirishwe hadi kura ya maamuzi ya kubadilisha katiba iliyosimamishwa na Mahakama Kuu itakapofanyika.

Waandalizi wa mchakato huo wamekata rufaa wakitaka uamuzi huo ubatilishwe huku baadhi yao wakijitokeza wazi kusema kuwa iwapo rufaa haitaamuliwa kwa wakati, itabidi uchaguzi mkuu uahirishwe hadi refarenda ifanyike.

Mswada wa marekebisho ya katiba wa 2020, unapendekeza kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wake wawili na kubuniwa kwa maeneobunge mapya 70 miongoni mwa mabadiliko mengine ya kikatiba na usimamizi.

Dkt Ruto amekuwa akipinga mchakato wa kubadilisha katiba akisema Wakenya wanahitaji kuwezeshwa kiuchumi na si marekebisho ya katiba yenye madhumuni ya kubuni nafasi kwa wanasiasa wachache.

Wiki mbili zilizopita, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya wafanyakazi nchini (Cotu), Francis Atwoli alisema kuwa itabidi uchaguzi mkuu uahirishwe kwa mwaka mmoja au miwili hadi katiba irekebishwe kupitia Mswada wa BBI.

Akizungumza akiwa katika kanisa la AIC Bomani, Kaunti ya Machakos jana, Dkt Ruto alisema baadhi ya kauli zinazotolewa na wanasiasa zinalenga kutia hofu Wakenya.

“Kutakuwa na amani Kenya kabla na kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Msibabaishwe na kelele hizi mnazosikia,” alisema Dkt Ruto.

Katika kauli inayoonekana kumlenga kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga aliyekemea viongozi wa kidini na kuwataka wakome kuingilia masuala ya siasa, Dkt Ruto aliwaambia serikali inatambua wajibu wao.

Viongozi wa kidini wamepinga wito wa kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu ujao.

“Serikali ya Kenya inatambua na inajihusisha na ushirikiano kati ya kanisa na serikali. Kuna mambo mengi ambayo kanisa hufanya kusaidia yale ambayo serikali inapaswa kufanya,” alisema Dkt Ruto.

“Kwa sababu hiyo, viongozi wa kanisa wanafaa kufahamu kwamba kama serikali tunatambua mnayofanya,” akiongeza Dkt Ruto.

Aliwataka viongozi wanaokosoa kampeni yake ya kuwawezesha maskini almaarufu ‘Hustler’, kwa kupanga miungano ya kisiasa kumkabili kwenye uchaguzi mkuu wasaidie wanyonge hao kwanza.

“Ninataka kuwaomba wanasiasa, na nimesikia wengi wakipanga miungano ya kukabili wapinzani wao, hata tunapounda miungano ya kumenyana na wapinzani, tusisahau wasiojiweza,” alisema.

Alisema kwamba wanasiasa wanafaa kufahamu kwamba wananchi ni muhimu kuliko viongozi.

Wenyeji watumai kuzima mzozo na wasimamizi wa ‘shamba la Ruto’

Na LUCY MKANYIKA

MZOZO kati ya jamii za Kaunti ya Taita Taveta na wasimamizi wa shamba linalohusishwa na Naibu Rais William Ruto, umepata matumaini kutatuliwa.

Hii ni baada ya wasimamizi wa shamba hilo kukubali shughuli za kuzibua mikondo ya mito inayoingiza maji katika Ziwa Jipe ziendelee.

Wasimamizi hao wa shamba la Kisima wakiongozwa na Bw Aries Dempers, wamekubali shughuli hiyo ianze ndani ya shamba hilo la ekari 1,000.

Wakazi kwa muda mrefu walikuwa wamelalamika kuwa shamba hilo linasababisha uwezekano wa ziwa kukauka kwa vile mikondo inayoelekeza maji ziwani ilikuwa imezibwa.

Mnamo Jumapili, kamati iliyojumuisha Diwani wa Wadi ya Mata, Bw Chanzu Kamadi, wakulima, wavuvi na wasimamizi wa shamba hilo walikutana na kuelewana kuhusu jinsi shughuli hiyo itatekelezwa.

“Tumeelewana kazi ianze Jumatatu (jana) asubuhi. Wasimamizi wameturuhusu kwa hivyo kwa sasa hakuna changamoto zimeibuka,” akasema Bw Kamadi.

Serikali ya kaunti kupitia kwa Hazina ya Ustawishaji Wadi ilitenga Sh5 milioni kuzibua mikondo ya mito ya Sombasomba, Sembike, Lesesia na Maloja ili kuongeza kiwango cha maji ziwani.

Shughuli hiyo ilichelewa kwa sababu ya mzozo kati ya wasimamizi wa shamba na wenyeji, iliposemekana wasimamizi hao walifunga sehemu zilizotakikana kufanyiwa ukarabati.

Bw Kamadi alisema shughuli hiyo inatarajiwa kukamilishwa baada ya siku 14.

Dkt Ruto amekuwa akitembelea shamba hilo mara kwa mara na hata kufanya mikutano hapo na viongozi wa kijamii.

Zamani lilikuwa likimilikiwa na aliyekuwa mbunge wa Taveta, Bw Basil Criticos.

Bingwa wa ukaidi

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto ameonyesha ujasiri na ubingwa wa kipekee wa kukaidi mkubwa wake Rais Uhuru Kenyatta bila kuogopa, hulka ambayo imemfanya atengwe serikalini.

Dkt Ruto amekuwa akiepuka hafla anazohudhuria Rais Kenyatta licha ya kuwa msaidizi mkuu wa kiongozi wa nchi, hali ambayo imefanya uaminifu wake kwa serikali kutiliwa shaka.

Ingawa anasisitiza kuwa hajawahi kumkosea heshima Rais Kenyatta, wadadisi wa siasa wanasema matamshi yake na ya washirika wake wa kisiasa pamoja na vitendo vyao vinaonyesha ukaidi wa hali ya juu.

Baadhi ya vitendo hivyo ni kuanzisha mpango mbadala wa uchumi licha ya kuwa serikalini, kujitambulisha na kufadhili vyama tofauti vya kisiasa na kukwepa majukumu yake kama msaidizi rasmi wa rais kwa kutohudhuria hafla za mkubwa wake.

Wanasema kwamba, japo dalili za ukaidi zilianza pindi alipokataa kukumbatia handisheki kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, zilijitokeza wazi wakati wa kuzinduliwa kwa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi mnamo Oktoba 26, 2020.

Katika hafla hiyo, Dkt Ruto alitofautiana hadharani na Rais Kenyatta kwa kukosoa vikali ripoti hiyo akisema, haikuwa suluhu kwa ukosefu wa ushirikishi nchini. Tangu wakati huo, alianza kususia hafla za Rais Kenyatta na kukosoa mipango ya serikali, hatua ambayo wadadisi wanasema ni kilele cha ukaidi na kudunisha mkubwa wake.

“Kile Ruto anafanya sasa ni ukaidi wa wazi na hii amekuwa akifanya hadharani kana kwamba anatoa tangazo kwa umma la vita dhidi ya Rais na washirika wake serikalini,” asema mchanganuzi wa siasa Samuel Omwenga.

Dkt Ruto amewahi kutisha kukabiliana na watu wenye ushawishi serikali wanaopanga kuzima azima yake ya kuwa rais kwenye uchaguzi wa 2022.

Mnamo Septemba 28, alikosa kuhudhuria kongamano la taifa kuhusu janga la corona katika ukumbi wa Bomas na ikabidi kiti chake kuondolewa Rais Kenyatta alipowasili. Dkt Ruto alijitetea akisema hakuwa amealikwa, kauli ambayo haikuridhisha Wakenya, wakiwemo wachanganuzi wa siasa.

Kwa kawaida, akiwa naibu rais na msaidizi mkuu wa rais, Dkt Ruto anatarajiwa kuzungumza kwa sauti moja na mkubwa wake na kutetea maamuzi na mipango ya serikali.

Hata hivyo, Dkt Ruto amekuwa akilaumu Rais Kenyatta waziwazi kwa kutelekeza ajenda za serikali na kuzingatia handisheki yake na Bw Odinga.

Alizunguka kote nchini akifanya mikutano ya hadhara kukosoa handisheki na mageuzi ya katiba.

“Kila wakati tunazungumza kuhusu kubadilisha katiba lakini wakati huu tutabadilisha mjadala na kuanza kuzungumza kuhusu kubadilisha maisha ya masikini nchini,” Dkt Ruto alisema Oktoba 16, 2020 akiwa Kisii.

“Wakati wa kubadilisha mdahalo umefika, hatutazungumzia tena kubuni nafasi za uongozi kwa watu wachache lakini tutajadili siasa za watu wadogo. Tutazungumzia kuhusu waendeshaji wa boda boda na biashara ndogo ndogo,” aliongeza.

Huo ulikuwa mwanzo wa kuanzisha vuguvugu lake la hasla, ambalo Rais Kenyatta alionya lililenga kuchochea vita vya matabaka.

Jumamosi, aliendeleza kampeni yake ya kuvumisha ajenda mbadala ya uchumi katika eneo la Pwani.

Licha ya onyo la Rais, Dkt Ruto aliendelea na kampeni yake huku akikaidi kanuni za kuzuia corona. Kulingana na mchanganuzi wa siasa Geff Kamwanah, Dkt Ruto amejitenga na ajenda ya uchumi ya Rais Kenyatta na kuanzisha yake ya hasla.

Dkt Ruto pia amekuwa akikaidi maamuzi ya serikali na chama tawala na kujihusisha na shughuli za chama kingine cha United Democratic Alliance (UDA).

Kulingana na sheria, kiongozi aliyechaguliwa hafai kujihusisha na shughuli za chama tofauti. Hata hivyo, Dkt Ruto amekuwa akiunga na kufadhili shughuli za vyama vingine.

Wiki hii, alitangaza wazi kwamba, alikuwa akiunga wagombeaji wa UDA katika chaguzi ndogo za maeneobunge ya Bonchari, kaunti ya Kisii, Juja Kaunti ya Kiambu na wadi ya Rurii kaunti ya Nyandarua.

Dkt Ruto akiungana na Raila, kipi kitarajiwe Mlima Kenya 2022?

Na MWANGI MUIRURI

HABARI kuwa Naibu Rais Dkt William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanaweza wakaungana kusaka urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 zimezua hisia mseto Mlima Kenya.

Hofu ni kuwa, ikiwa hilo litafanyika, eneo hilo ambalo limekuwa katika uongozi wa taifa hili katika serikali tatu tangu uhuru (Hayati Mzee Jomo Kenyatta 1963-1978, Mwai Kibaki 2002-2013 na Uhuru Kenyatta 2013 hadi sasa) litatengwa na lijipate katika upinzani.

Mchanganuzi wa kisiasa Bw Gasper Odhiambo anasema Dkt Ruto akiungana na Bw Odinga, basi itakuwa ni njia ya uhakika ya kuadhibu upande wa Rais Kenyatta iwapo kiongozi wa nchi atasaliti ahidi ya ‘Yangu Kumi na ya Ruto Kumi’.

“Ni hali inayoweza kuitupa jamii ya Rais katika pipa la giza kisiasa,” asema Bw Odhiambo.

Hata hivyo, anasema muungano wa Dkt Ruto na Bw Odinga unaweza ukasambaratishwa na Mlima Kenya nao wakiamua kujipanga upya na kusaka muungano wao kwa kuwa naye Bw Odinga anatengwa na Musalia Mudavadi wa ANC, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Moses Wetang’ula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa Kanu.

“Ukiangalia mpangilo huo, utapata kwamba Dkt Ruto na Bw Odinga wakiungana halafu Mlima Kenya ijitenge nao kabisa, basi huenda wasifaulu,” asema.

Anasema kuwa ule muungano hatari kwa Mlima Kenya ni ule ambao utawaleta pamoja Mudavadi, Kalonzo, Moi na Wetang’ula kisha Bw Odinga na Dkt Ruto waungane nao akisema kuwa hali kama hiyo itawaacha wapigakura wa Mlima Kenya wakiwa peke yao dhidi ya Wakenya wengine wote.

“Hao wote wakija pamoja dhidi ya Mlima Kenya na wapate mbinu ya kukubaliana kuhusu mwaniaji mmoja ambaye atakuwa ama Dkt Ruto au Bw Odinga na hawa wengine wote watii, basi hapo ndipo taharuki ya Gema kutengwa itaibuka, lakini sio katika hali nyingine yoyote ya miungano,” aeleza.

Hata hivyo, walio katika mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao hufuata Dkt Ruto wamepuuzilia mbali muungano huo wakisema hata ukiibuka na utekelezwe, kile kitafanyika hakitaathiri uwezo wa Mlima Kenya kuwa ndani ya serikali.

“Habari hizo zilitokana na mahojiano ya Dkt Ruto na kituo cha Radio Citizen ambapo alikuwa muwazi kwamba ikiwa ataungana na Bw Odinga, itakuwa ni ODM ije ndani ya ‘Tangatanga’ wala sio sisi tuwaendee. Ina maana kuwa atakuja kwa masharti yetu,” akasema Mbunge wa Mathira Bw Rigathi Gachagua.

Bw Gachagua anasema kuwa msimamo wa ‘Tangatanga’ ni kuwa hata muungano wa kisiasa uwe wa nani kati ya mwingine nani au chama gani na kingine kipi, ni lazima iwe Dkt Ruto ndiye atakuwa mgombea wa urais.

Ikiwa Bw Odinga atajiunga na Dkt Ruto basi “aridhike na nafasi ya Waziri Mkuu na hilo itabidi kwanza BBI ipitishwe katika referenda na kisha awanie ubunge, ashinde ndipo ateuliwe kuwa Waziri Mkuu.”

Pendekezo la wadhifa wa Waziri Mkuu katika BBI ni kwamba atakayeteuliwa ni lazima awe mbunge.

Bw Gachagua alisema kuwa ikiwa Dkt Ruto ataingia kwa muungano wa kisiasa na Bw Odinga na akubali kutowania urais (Dkt Ruto) “basi sisi tutajitoa na tupange upya mikakati yetu ya kisiasa kwa kuwa Bw Odinga kamwe hawezi kuwa chaguo letu la kisiasa na hakuna vile tutamuunga mkono kama Mlima Kenya ndio awe rais.”

Seneta wa Murang’a Bw Irungu Kang’ata alisema huo muungano unaosemwa sio mbaya ila tu eneo la Mlima Kenya “limeamua kuwa mwaniaji wao wa urais ni Dkt Ruto wala sio mwingine yeyote na ikiwa hilo litasambaratika kupitia mikakati yoyote ile itaibuka katika miungano ya kisiasa, basi tuko tayari kuanza kujipanga upya.”

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Peter Kenneth alisema kuwa uwezekano huo wa Dkt Ruto na Bw Odinga ni kiini cha kuwatuma wanasiasa wote wa Mlima Kenya kwanza waungane na wapange mikakati yao ya 2022 wakielewa kuwa “hata kina nani waungane Kenya hii, sisi tukiwa na umoja wetu wa kura na tukatae katakata kuzigawa katika debe, tutawatatiza pakubwa.”

Alisema kuwa hali ya siasa ni sawa na jinsi mto mkubwa hupewa maji na mito midogo katika safari ya kujaza bahari.

“Hii ina maana kuwa sisi kama walio na asilimia 35 ya kura zote hapa nchini, ikiwa tunatumbukiza katika kapu moja kisiasa, tunahitaji tu asilimia 16 ya nyongeza ya kura ili tuibuke na ushindi. Hakuna sheria imeundwa Kenya hii ya kutuzuilia kuwania urais na ikiwa mito midogo hupea maji mto mkubwa, hata wakiungana, kinga yetu ni umoja wetu,” akasema Bw Kenneth.

Bw Kenneth alisema kuna haja kubwa ya wanasiasa wa Mlima Kenya sasa kutupilia mbali tofauti zao na kwanza wavunje mirengo yao hasidi ya kisiasa na cha maana kama hali ya dharura, waungane na waanze kuongea kwa sauti moja ili uzito wao wa kura utambulike na uheshimiwe.

Alisema kuwa “tukiungana, liwe liwalo tutakuwa ndani ya serikali ya baada ya 2022 tukiwakilishwa na mtu wa eneo hili ama katika wadhifa wa rais, naibu wa rais au waziri mkuu.”

Kwa mujibu wa Seneta wa Nyeri Ephraim Maina, “nimekuwa nikionya kuwa tunapelekwa mbio isiyofaa na baadhi ya wanasiasa wetu ambao tangu 2013 wamekuwa wakituchuuza kwa mirengo fulani ya kisiasa bila kuzingatia athari za kutokuwa na subira darubini ya kisawasawa ipigwe kujua tunaelekezwa wapi na ni wapi kunatufaa zaidi.”

“Rais Kenyatta amekuwa akihofia hilo la kutengwa kufanyika na ndipo amekuwa akisisitiza umuhimu wa BBI ambayo inaunda serikali pana inayojumuisha maeneo hapa nchini kulingana na kura zao na kisha kugawa rasilimali kulingana na idadi ya watu,” akasema Bw Maina.

Bw Maina ameambia Taifa Leo “hii ndiyo hali ambayo Rais amekuwa akijaribu kuzima na ndiyo hali wale ambao wanatuchuuza kwa mrengo wa Dkt Ruto wamekuwa wakipinga bila kuzingatia kwamba kiongozi wa nchi huwa na ufahamu zaidi wa mitindo na njama za wanasiasa kupitia habari za ujasusi.”

Akasema: “Rais alijua haya yalikuwa na uwezekano wa kutokea na ndipo akazindua mpango wa kuhakikisha eneo la Mlima Kenya huwa linapangiwa njama za kulitenga kisiasa kutokana na wingi wa kura zao na mtindo wao wa kupendelea mwaniaji wao katika uchaguzi wa urais.”

Aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau naye akasema kuwa “sasa ni wazi kuwa busara ya Rais Kenyatta ya kuwataka watu wa Mlima Kenya waunge mkono mchakato wa BBI ilikuwa na kiini cha kumulika uwezekano wa kutengwa kwa Mlima Kenya.”

Hata hivyo, mchanganuzi wa kisiasa Prof Ngugi Njoroge anauliza: “Hili la kutiwa hofu kuwa huenda Mlima Kenya wakatengwa kisiasa na waingie upinzani lina mashiko kweli? Kuna ushahidi kuwa wapigakura wa eneo hilo wana tamaa ya kuwa ndani ya serikali?”

Anauliza pia: “Wakati wenyeji wa Mlima Kenya walianza kuonyesha nia ya kuunga mkono mwingine katika wadhifa wa urais 2022, ilikuwa ni ishara kuwa wamechoka kuhusishwa na serikali haswa baada ya kuibuka kuwa wadhifa huo huwa hauwasaidii sana kumaliza shida zao?”

Anasema kuwa hata miungano iundwe kwa msingi upi, Wakenya watafanya maamuzi yao “na sioni ule msukumo mkubwa wa jadi Mlima Kenya wa kupambana kufa kupona kuwa ndani ya serikali kama upo kwa sasa.”

“Wenyeji wamechoka kujumuishwa ndani ya ukabila wa kuwindia mtu binafsi ukubwa na hatimaye kuachwa kwa mataa kila mmoja wao akipambana na hali yake,” akasema.