Makala

TUONGEE KIUME: Dada, usiolewe mikono mitupu

Na BENSON MATHEKA July 25th, 2024 2 min read

AKINA dada sikizeni. Ikiwa unataka kuolewa, jihami. Sio kwa bunduki, mkuki na simi. Jihami kwa mali na mapato yako. Kumbuka barobaro anayetaka mke anatafuta msaidizi.

Kuwa na uwezo wa kuongeza thamani katika ndoa.

Ikiwa hauongezi thamani yoyote kwa ndoa yako zaidi ya ngono, usiwazie ndoa.

Kabla ya kuwazia ndoa, jifunze jinsi ya kutengeneza pesa. Usiruhusu mzigo kuwa mzito sana kwa mwanaume.

Hii pia huongeza kujiamini kwako. Hakuna mwanamume anayedharau mwanamke anayejitegemea. Hakuna mlofa na kabwela anayethubutu kurushia mistari demu aliyejihami kwa uwezo wa kujitengeneza pesa.

Na usikubali mwanamume wa aina hiyo kukukaribia, isipokuwa uwe umegundua ana kitu cha kipekee unachoweza kutumia kujiendeleza. Kitu hicho, dada, kisiwe ngono.

Nenda shule kaka. Soma ujiwezeshe. Kuna kozi nyingi za muda na hata zinazotolewa wikendi. Kuna kozi nyingi za mtandaoni ikiwa hali karibu na wewe sio nzuri kuhudhuria za kawaida.

Kuwa na ujuzi kutasaidia kujihami kabla ya kuingia katika ndoa. Tumeona ndoa nyingi zikivunjika mwanamume akigundua mkewe ni tupu kichwani. Dada, jaza kichwa chako na maarifa na ufahamu kwa manufaa yako binafsi na ya ndoa yako.

Na usiwe kipofu uingie katika ndoa na mwanamume usiyejua anatoka au kukumbatia utamaduni wa aina gani.

Jua unakoenda kabla ya kuelekea huko. Usiolewe na uanze kupigana na kila takwa la kitamaduni kutoka kwa mumeo na jamii yake.

Na usikubali kuzaa idadi ya watoto ambao hauwezi kuwatunza.

Akina dada, nyakati zimebadilika. Chukua jukumu kuhusu idadi ya watoto unaoweza kushughulikia.

Usidanganyike kuwa mapenzi ni upofu. Hakuna kitu kama hicho. Ingia kwa ndoa ukiwa na hakika ya unachofanya. Ipange ndoa yako kabla ya kuifunga. Kutokuwa na mpango ni uzembe unaozaa majuto.

Ndoa inapaswa kuwa muungano kati ya watu wawili wenye akili, sio muungano wa kihisia usio na mpango.

Usimlaumu mtu yeyote kwa chaguo lako. Una kila haki ya kuolewa au kubaki bila kuolewa. Ikiwa umechagua kuolewa, lazima uwajibike kwa chaguo lako.

Usimwache Mungu katika kila hatua unayopiga. Ukigundua mtu wako hapendi Mungu, hautakosea  kubadilisha nia kumhusu.

Epuka janga ambalo akina dada wengi hujitumbukiza. Kujiingiza katika shimo la kina cha madeni wakitaka kuolewa. Usikope kufadhili harusi, usijaribu.

Kwa ufupi, usijiingize katika gharama zizokuwa na maana ukitaka kuolewa kupitia harusi la kukata na shoka.

Nakupa onyo; gharama ya harusi sio sawa na ufahari wake. Wengi wamegharamikia harusi kisha ndoa inabadilika kuwa balaa. Ukiwa na uwezo, sawa, ukikosa usikope au kukausha akaunti zako za benki kwa sababu ya harusi.