Jamvi La SiasaUncategorized

Matiang’i achelea kutaja azma yake

Na MERCY SIMIYU, BENSON MATHEKA April 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ALIYEKUWA Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, alirejea nchini Alhamisi usiku huku kukiwa na minong’ono kuhusu uwezekano wake wa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2027.

Dkt Matiang’i aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa ndege ya Qatar Airways kutoka Washington, DC.

Waziri huyo wa zamani, ambaye alihudumu chini ya utawala wa Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta, alipokelewa na baadhi ya wandani wake na jamaa wa karibu, akiwemo Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee Jeremiah Kioni, Seneta wa Kisii Richard Onyonka, na Seneta mteule Gloria Orwoba.

Dkt Matiang’i hakuzungumza na wana habari kudokeza azma yake ya kumpinga Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027. Na ingawa hakuzungumza na vyombo vya habari uwanjani humo, kurejea kwake baada ya kukaa kwa muda Amerika kumechochea mjadala mpya wa kisiasa.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja, Dkt Matiang’i aliishi maisha ya faragha ughaibuni, akiepuka umaarufu na kutoa matamshi machache kwa umma.

Kurejea kwake, ikiwa ni zaidi ya miaka miwili kabla ya uchaguzi, kumefufua mijadala kuhusu mustakabali wake wa kisiasa za humu nchini huku akisalia kimya.

Ni chama cha Jubilee kinachoongozwa na Uhuru Kenyatta ambacho tayari kimetangaza kuwa kitamuunga mkono Dkt Matiang’i, huku Katibu Mkuu wa chama hicho Jeremiah Kioni akithibitisha kuwa kinapanga kupigia debe azma yake ya kuwania urais 2027.

“Hakuna tena kusubiri. Kila kitu kiko tayari,” Jubilee ilichapisha kwenye kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.Wakati wa mkutano wa wajumbe wa chama hicho uliofanyika Aprili 6 katika eneo la Keumbu, Kaunti ya Kisii, Kioni alisisitiza kuwa waziri huyo wa zamani ameidhinishwa rasmi kupeperusha bendera ya chama.

“Tunaposema ni Matiang’i, tunamaanisha uongozi unaojua kuhudumia raia. Aliwahi kuongoza wizara muhimu za serikali na kuhakikisha utekelezaji wa mipango ya kitaifa. Yeye si mgeni kwa majukumu,” alisema.

Bw Kioni alilinganisha rekodi ya utendakazi wa Matiang’i na viongozi wa sasa, akishutumu baadhi yao kwa kuweka siasa mbele ya uongozi.

“Hata kabla ya 2017, Ruto tayari alikuwa ameanza kampeni. Hakuwa na muda wa kazi ya ofisi. Lakini Matiang’i anajua maana ya utawala. Ana msimamo thabiti, na ni kiongozi aliyethibitishwa.”

Mnamo Aprili 6, Kioni alithibitisha kuwa Dkt Matiang’i amepata idhini ya kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Jubilee katika uchaguzi wa 2027.

“Nimesikia watu wakija hapa wakihubiri umoja, lakini wao ndio wale wale wanaosambaza migawanyiko kwa sababu wametumwa kuleta mpasuko katika jamii. Wanaweza kusema Matiang’i anashtakiwa, lakini idadi ya kesi wanazoweza kumsingizia si hoja yetu. Hata wakimfungia jela, bado sisi tutamchagua,” alisema Kioni.

Lakini Dkt Matiang’i, ambaye alipanda ngazi katika utawala wa Uhuru Kenyatta na kupata sifa kwa msimamo wake thabiti kuhusu utoaji huduma kwa umma na usalama wa taifa hajasema iwapo atagombea au la.

Lakini anachukuliwa huenda akajitokeza kama mpinzani mkuu wa Rais William Ruto katika kinyang’anyiro kinachotarajiwa kuvutia vigogo wengine wa upinzani akiwemo Raila Odinga (ikiwa atawania) Kalonzo Musyoka na wanasiasa wengine chipukizi.

Jina lake limetajwa pia na vinara wa upinzani akiwemo aliyekuwa naibu Rais Rigathi Gachagua ambao wanasema wako tayari kuungana naye iwapo atajitosa katika kinyang’anyiro cha urais.

“Tunanuia kuanzisha serikali mpya ili kusaidia taifa letu. Tunafanya haya kwa kushirikiana na kiongozi wenu Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa, George Natembeya na Fred Matiang’i. Mimi, Riggy G, nitafanya kazi nyuma ya pazia, nikisaidia kufanya maamuzi muhimu. Nataka kuwahakikishia Wakenya kwamba, tuna mbinu ya kuwapatia uongozi bora,” Gachagua alisema akiwa Machakos wikendi iliyopita.

Kulingana na mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki, hatua ya Dkt Matiang’i kuchelewa kutangaza azima yake inatokana na mseto wa masuala kadhaa.

“Inaweza kutokana na mikakati ya kisiasa au kutofanya uamuzi kuhusu chama atakachotumia tiketi au hata hadhi yake kama Waziri wa Usalama wa Ndani.Kuna vyama viwili vinavyommezea mate- United Progressive Alliance (UPA) na Jubilee na hii inaweza kumfanya achelewe kimkakati kufanya mashauriano zaidi,” asema na kuongeza kuwa dalili zote zinaonyesha Matiang’i atajibwaga katika uchaguzi wa urais.