Habari za Kitaifa

Uwezekano wa mpango wa elimu bila malipo vyuo vikuu


HUENDA mpango wa elimu bila malipo ukatekelezwa katika kiwango cha chuo kikuu endapo serikali itazingatia ushauri wa wabunge na kuunda sera ya kuunganisha hazina zote za kufadhili masomo katika ngazi hiyo. 

Wakiongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, wabunge walisema uwepo wa hazina nyingi za kutoa basari hauna faida yoyote na hutoa mwanya wa kuingizwa ufisadi katika mpango huo.

Bw Wetang’ula Jumanne, Agosti 20, 2024 alisema hamna mantiki yoyote kwa Madiwani (MCA), Wabunge, Wabunge Wawakilishi, Serikali za Kaunti, Hazina ya Kufadhili Masomo ya Vyuo Vikuu (UF), Bodi ya Kufadhili Elimu ya Juu (HELB), Wizara ya Elimu na mashirika ya kibinafsi kuendesha mipango sambamba ya utoaji basari ya masomo.

“Ikiwa mwaweza kuunda sera ya kuweka pamoja hazina hizi, Bunge hili litakuwa tayari zaidi kuigeuza kuwa sheria ili tuwe na mpango wa elimu bila malipo katika kiwango cha Chuo Kikuu,” Bw Wetang’ula akasema.

“Shida yetu itasuluhishwa mara moja,” Bw Wetang’ula akaongeza, akitoa ushauri kwa Katibu katika Idara ya Elimu ya Juu Beatrice Inyangala.

Spika huyo alisema hayo wakati wa kikao kisicho rasmi cha wabunge (Kamukunji), kufuatia pendekezo la Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi kwamba hazina zote za serikali za kutoa basari za masomo ziwekwe pamoja.

Bi Inyangala alikuwa amealikwa katika kikao hicho, katika majengo ya bunge, kufafanulia wabunge kuhusu mpango mpya wa kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka familia maskini.

Hii ni baada ya wabunge kukosoa mfumo unaotumiwa kubaini wanafunzi wenye uhitaji mkubwa kufuatia kukithiri kwa visa ambapo wanafunzi kutoka jamii maskini walipata ufadhili mdogo kinyume na hitaji lao.

Wabunge pia waliilaumu Idara ya Elimu ya Juu inayoongozwa na Bi Inyangala kwa kutotoa ufafanuzi kamili kuhusu mfumo mpya wa ufadhili wa masomo waliosema unabagua wanafunzi kutoka familia maskini.

Walimlaumu afisa huyo kwa kumwachia Rais William Ruto wajibu wa kufafanua utendakazi na umuhimu wa mfumo huo mpya wa ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu.

Wazo la wabunge la kuundwa kwa hazina moja ya kufadhili masomo katika vyuo vikuu linajiri baada ya Wizara ya Elimu kuandaa mswada wa kufanikisha lengo hilo.

Mswada huo unaojulikana kwa kimombo kama “Basic Scholarships and Bursaries Bill, 2024” unalenga kuunganisha ufadhili unaotolewa na serikali na basari na kuziweka chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu.

Hatua hii itaondoa usimamizi wa hazina hizo mikononi mwa wanasiasa, kama vile madiwani, wabunge na magavana.

Vile vile, wiki jana, Mbunge Mwakilishi wa Nairobi Esther Passaris alitoa notisi ya hoja kuhusu mageuzi katika utoaji basari nchini.

Bi Passaris pia anapendekeza kuwekwa pamoja kwa misaada ya masomo inayotolewa na serikali na basari na kuziweka chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu.

Jopo kazi la Rais kuhusu Mageuzi katika Elimu pia lilipendekeza kuvunjwa kwa bodi ya HELB, hazina ya UF na Asasi ya Kuteua Wanafunzi wanaojiunga na Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kadri (KUCCPS) ili kuundwe asasi moja ya kutoa ufadhili kwa masomo ya juu.