Pambo

Vijana wa kiume watekwa na mashugamami

March 17th, 2024 3 min read

NA BENSON MATHEKA

IMEFICHUKA kwamba vijana wa kiume hujisalimisha kwa wawindaji wa mahaba kutokana na tamaa, umaskini na hali ngumu wanazopitia wakiwa vyuoni.

Haya yamesemwa na mtaalamu wa maswala ya kijamii, Jenifer Nzioka, aliyeeleza ni vigumu kwa vijana wa vyuo vikuu na taasisi za kozi za kiufundi kuepuka kunaswa na wanawake wenye pesa.

“Licha ya ukweli kwamba vijana wa kiume hupitia katika hali ngumu mno wakiwa chuoni, ni wazi kuwa wengi huwa na tamaa ya kutaka kuishi maisha ya starehe, hali inayochangia kukithiri kwa tabia hii,” asema Bi Nzioka.

Anasema vijana wa siku hizi hukimbilia maisha ya anasa.

“Wanatamani kuendesha magari ya kisasa na kuvalia mavazi ya pesa nyingi. Hivyo basi ni rahisi kutumbukia katika mitego kama hii,” asema.

Wanaokubali kutumiwa katika ukahaba, wao wenyewe wakiwa wakware wa kutoa huduma za mapenzi kwa mashugamami, baadaye hujuta kwa kupoteza muda ambao wangetumia kutengeneza maisha yao.

Taifa Jumapili ilichukua wiki nzima kufuatilia mienendo ya vijana wa vyuo wawapo mjini.

Kilichojitokeza ni kwamba aina mpya ya ukahaba imeibuka jijini Nairobi inayotishia maisha ya vijana hasa mabarobaro wa vyuo vikuu na taasisi mbalimbali.

Katika hali ya kusikitisha, mabarobaro wamenaswa katika lindi la ukahaba unaoendeshwa makusudi na wanawake matajiri wanaowateka kwa kuwapatia pesa kisha kuwatumia kutimiza haja zao za kimwili.

Cha ajabu ni kwamba kinyume na hapo awali ambapo ni wanaume mabwanyenye almaarufu ‘masponsa’ ndio waliokuwa wakiwasaka wasichana kushiriki ukahaba nao, mabarobaro wanalengwa na akina mama matajiri.

Baadhi ya vijana wanakubali kuwekwa unyumba na wanawake hao na kutelekeza shughuli za masomo.

Ili kuwanasa vijana, wanawake wenye ushawishi wa kifedha wamekuwa wakitembelea maeneo ya burudani wanakovinjari wanafunzi kwa njia kujistarehesha.

“Hii ni tabia iliyoenea sana hapa. Vijana wamepotelea katika anasa baada ya kumwagiwa pesa na mashuga mami,” asema mhudumu mmoja wa kilabu maarufu jijini Nairobi.

Kulingana na mhudumu huyo aliyeomba tusichapishe jina lake, wanawake matajiri wamekuwa wakifika kujiburudisha huku wakiwa na lengo la kuwapata vijana wa vyuo vikuu.

“Wanachagua hapa kwa sababu vijana wa vyuo vikuu huja kustarehe nyakati za jioni na mwishoni mwa wiki. Yanayoendelea hapa ni kinyume kabisa na maadili ya mila za kiafrika,” mhudumu huyo aliambia Taifa Jumapili.

Anasema kwa miaka mitatu ambayo amefanya kazi katika kilabu hicho ameshuhudia wanawake wenye mali wakiwanasa vijana na kushiriki nao mapenzi.

“Wanafika hapa wakiendesha magari ya kifahari. Wakijinyakulia windo lao wanaondoka,” asema mlinzi mmoja anayehudumu katika kilabu hicho.

Mlinzi huyo aliyejitambulisha kwa jina moja tu, Omondi, asema kuwa wanawake wanaovinjari hapo huwa ni nadhifu na wa kuheshimika.

“Baadhi yao ni wafanya biashara maarufu jijini,” asema Omondi.

Uchunguzi wa Taifa Jumapili uliochukua siku saba katika maeneo tofauti jijini, umebainisha kuwa hata wanawake walio katika ndoa, wanajihusisha katika tabia hii.

“Nilijishindia mama mmoja tajiri aliyeniambia kuwa aliamua kutafuta mtu wa kumridhisha baada ya mumewe kuanza kuwaburudisha wanawake wengine,” afichua mwanafunzi mmoja wa chuo kimojawapo jijini Nairobi.

Mwanafunzi huyo anakiri kuwa mwanamke huyo humpatia pesa za matumizi na kumnunulia mavazi ya kisasa.

“Changu ni kuwa karibu shugamami anaponihitaji,” asema.

Na hana wasiwasi wowote kuhusu maisha yake ya baadaye.

“Nina mpenzi wangu ninayekusudia kumuoa nikimaliza chuo. Kwa wakati huu ni burudani tu,” asema na kuongeza kuwa mchumba wake hana habari kuhusu uhusiano wake na mwanamke huyo aliye mama ya watoto watatu.

Katika siku yetu ya pili ya uchunguzi, tulimpata mwanamke mmoja akivinjari katika kilabu kimoja kinachotembelewa na vijana wanafunzi jijini.

Alijaribu kumrai barobaro mmoja karibu na meza tuliyoketi.

Kwanza alimuagizia kinywaji kabla ya kuanza kumsimulia yaliyokuwa moyoni mwake.

“Hakuna utakachokosa kwangu. Ninachohitaji ni mtu wa kuwa karibu nami,” akamwambia.

Aliahidi kumtimizia mahitaji yote.

“Na kama utanihakikishia kuwa mwaminifu nitakuonyesha mambo makubwa yakukufaidi maishani,” akamwambia.

Tabia hii imeshamiri katikati mwa jiji baada ya vyuo vikuu  mbalimbali  kufungua vitivo jijini na idadi ya wanafunzi kuongezeka jijini.

Katika siku yetu ya tano tulivinjari katika mtaa wa Buruburu tulipompata kijana mmoja aliyetumiwa kisha akatemwa na mwanamke mmoja.

“Nakubali nilitumiwa kisha nikatemwa” akasema kijana aliyejitambulisha kwa jina Omar.

Huku akiwa mwenye majuto, alitusimulia jinsi alivyokutana na mwanamke mmoja aliyemshawishi kwa kumuahidi mambo makuu.

“Baada ya kuniharibia masomo yangu sasa amenitelekeza na kuchukua kijana mwingine wa chuo chetu,” akasema Omar mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo kimoja jijini.

Asema alikutana na mwanamke huyo anayemiliki biashara kadha jijini kwenye kilabu kimoja na baada ya kujuana kwa siku kadha akahamia kuishi kwake.

“Siku moja alinidhulumu na kunitupa nje,” asema.

Wataalamu wa maswala ya jamii wanasema wanawake hawa huwalenga vijana wa vyuo vikuu kwa sababu ni barobaro na wanaweza kuangukia mtegoni kwa haraka.

“Baadhi yao walikuwa wanafunzi na wanaelewa tabia zao,” asema Bi Nzioka.

Awali, vijana waliokuwa wakishiriki tabia hii waliiweka kuwa siri lakini kwa wakati huu, wanaifanya kwa uwazi, jambo ambalo limewafanya wenzao kuiga tabia zao.

“Sasa imekuwa ni kama mashindano. Vijana wengi wanafunzi wanaotembelea hapa hujaribu kujishindia shuga mami,” asema mhudumu wa kilabu kimoja magharibi wa jiji.

Na mlinzi mmoja katika kilabu kingine alikiri kuwa amekuwa wakala wa wanafunzi wavulana na wanawake matajiri.

“Nimekuwa nikiwaunganisha kwa malipo,” asema.

Mlinzi huyo asema alianza kazi hiyo baada ya kumfumania mwanamke mmoja maarufu akipapasana na kijana mwanafunzi katika gari lake katika eneo la kuegesha magari.

“Niliwashtua.Walinichotea na nikaanza kazi ambayo nimekuwa nikiifanya kwa miaka miwili sasa,” asema.