Makala

Wa Muchomba aongoza kupinga ujenzi wa nyumba za bei nafuu eneo ‘takatifu’  

March 18th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

BARAZA la Wazee wa Agikuyu pamoja na mbunge wa Githunguri, Bi Gathoni wa Muchomba wameungana kukataa Rais WilliamRuto kuzindua mradi wa nyumba za bei nafuu katika eneobunge la mwanasiasa huyo wa chama cha UDA.

Kwa pamoja, wameteta kwamba mradi huo unanuiwa kutekelezwa katika mahala patakatifu ambapo panafaa kutengewa makavazi ya kukumbuka vita dhidi ya mbeberu.

“Nilipounga mkono manifesto ya Rais Ruto ya kujenga nyumba za bei nafuu, sikujumuisha uungaji mkono unyakuzi wa mashamba na vita dhidi ya maeneo yetu ya kijamii ambayo ni takatifu.

“Sasa wanataka kunyakua shamba la kitamaduni katika eneo la Githunguri ili wajenge nyumba,” Wa Muchomba akaambia Taifa Dijitali.

Mwenyekiti wa baraza la Agikuyu Bw Wachira Kiago aliteta kwamba “kumezuka masuala mengi yanayotudhihirishia wazi kwamba serikali hii iko katika mkondo wa vita na masuala yetu ya kitamaduni”.

Alisema ujenzi wa nyumba katika uwanja huo ulioko katika makao makuu ya Kaunti Ndogo ya Githunguri, hautaendelezwa kwa vyovyote vile ikiwa serikali itasisitiza kutekeleza mradi wa nyumba za bei nafuu katika kipande hicho cha ardhi.

“Hili ni eneo takatifu kimila na kitamaduni. Ni uwanja ulio na historia kuu kuhusu jamii ya Agikuyu. Kina baba na babu zetu waliapa kwamba ikiwa wangeibuka na ushindi kutoka vita vya ukombozi, wangejenga pahali patakatifu pa kumshukuru Mungu wao wa Kirinyaga katika uwanja huo,” akasema Bw Kiago.

Bw Joseph Kaguthi ambaye amehudumu katika serikali zote ijapokuwa ya sasa ya Rais Ruto kama afisa mkuu wa kiutawala alisema kwamba “hata mimi ninapinga kwa dhati eneo hilo la Githunguri kuhujumiwa kupitia ujenzi wa majengo yanayokinzana na imani yetu ya kimila”.

Alisema anaelewa kwamba eneo hilo la Githunguri linabeba historia muhimu kuhusu vita vya ukombozi “na aliyekuwa nabii mkuu wa jamii yetu Bw Mugo wa Kibiru alikuwa ametabiri kwamba eneo hilo lilikuwa sawa na kasri ya Mungu wa kijamii”.

Mzee Mburu wa Gitau alisema kwamba kujenga nyumba za kuuza katika shamba hilo ni sawa na kudunisha jamii zote za Mlima Kenya na pia historia ya taifa hili, hali ambayo anasema, inaweza ikatumbukiza jamii nzima katika hatari ya laana ya waliokwenda kuzimu.

“Mimi ninajua kwamba eneo hilo lilitumika hata kuangamiza wapiganaji wetu wa Maumau. Wale ambao nina uhakika kwamba walinyongwa katika kipande hicho cha ardhi ni 58. Shamba hilo ni la kujenga mnara wetu wa ukumbusho, tuweke makavazi na pia pawe mahali pa ibada katika harakati zetu za kitamaduni,” akasema.

Bi Wamuchomba aliapa kutetea kipande hicho cha ardhi hadi mwisho akisema kwamba “ikiwa serikali hii ni ya kuskiza haki na kuheshimu mila za jamii hii, basi itafakari upya msimamo wake kuhusu kujenga nyumba za bei nafuu hapa Githunguri”.

Bw Kaguthi anamtaka Waziri wa Ardhi, Bi Alice Wahome kudhihirishia taifa kwamba anaelewa umuhimu wa utamaduni wa kijamii na aingile kati kuhusu suala la Githunguri.

“Bi Wahome aelewe kwamba tunamuona kama dada wa kijamii, ambaye anaelewa kuhusu mila na desturi. Tunatazamia kwamba atakuwa daraja letu na serikali ili kuifanya ielewe kwamba shamba hilo la Githunguri sio la kuchezewa mzaha,” akasema.