Habari Mseto

Wakazi wa South B wataka nyumba za bei nafuu kukamilishwa upesi

Na KEVIN CHERUIYOT September 3rd, 2024 1 min read

SERIKALI ya Rais William Ruto imehimizwa kukamilisha mradi wa nyumba za bei nafuu kwa muda mfupi iwezekanavyo, ili kutoa nafasi kwa Wakenya kusaidika nazo.

Hili ndilo ombi la wakazi wa Marigoini, Nairobi South wanaohoji kwamba wako tayari kuhama mtaa huo wa mabadand kuruhusu utekelezaji wa mradi wa nyumba za bei nafuu.

Kwenye Jumatatu, Septemba 2, 2024 kwenye kikao na mwakilishi wadi wao (MCA), Waithera Chege, walieleza kufurahishwa kwao na mpango wa nyumba za bei nafuu wakisema utasaidia kuboresha maisha yao.

Serikali ya Kenya Kwanza imeipa mbele mradi huo ikiwa na lengo la kupunguza idadi ya mitaa ya mabanda nchini.

Aidha, wenyeji wa Marigoini wamedokeza kwamba mradi huo utawafaa na kuwapa fursa ya kutoka katika makazi duni ambayo huadhiriwa mara kwa mara na mikasa ya moto.

Isitoshe, wakati wa mvua kubwa au mafuriko, nyumba na mali zao husombwa na kasi ya maji.

Wametoa wito kwa serikali kuhakikisha kwamba nyumba hizo ziwe za bei nafuu ili ziwafae.

“Msituwekee kodi ya juu sana ili tuweze kuingia kwa nyumba hizo. Tunataka kazi ifanyike kwa haraka ili kufikia Desemba 2024, tuwe tumezitwaa tuishi kama Wakenya wengine,” akasema mmoja wa wenyeji.

Pia, wameelezea furaha yao kwa serikali ya Rais Ruto kwa kuwakumbuka katika mradi huo.

“Na muendelee kutuangalia na kutushikilia hata wakati huu ambapo watu wamebomolewa makazi yao.”

MCA wao Bi Waithera amekuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha kwamba mradi huo unatimizwa ili kuwapa wenyeji fursa ya kupata nyumba za kisasa.

“Mambo ya ujenzi wa nyumba imepewa kipaumbele na serikali ya Kenya Kwanza na tutahakikisha mradi huu umekamilika kwa haraka.”

Bi Waithera alisema kwamba mradi huo utahakikisha kwamba wakazi wanapata maji, vyoo, mabafu, na hawatalazimika tena kulipia vyoo mtaani jinsi hali ilivyo kwa sasa.

Kulingana na Afisa kutoka Wizara ya Ardhi na Ujenzi wa Nyumba, Bi Mary Wanjiku, serikali inatarajiwa kujenga nyumba 1, 000, 000, kufikia mwishoni mwa Mwaka wa Fedha 2027/2028.