Habari za Kitaifa

Wako wapi? Mawaziri waliofutwa kazi waingia vichakani

Na DAVID MWERE July 18th, 2024 2 min read

WENGI wa mawaziri ambao walitimuliwa na Rais William Ruto wiki jana sasa wameingia mitini, baadhi yao wakikwepa umma kabisa wakilenga kuanza maisha yao upya.

Hadi wiki jana walipofutwa, mawaziri hao walikuwa wakifurahia mamlaka na manufaa yanayoandamana na kushikilia afisi hizo.

Haikuwa rahisi kwao kutangamana na umma na walipofanya hivyo, walinzi wao walikuwa chonjo.

Walipokuwa mamlakani, mawaziri hao walikuwa wakionekana sana mitandaoni wakivumisha miradi ya serikali.

Wengi wao hasa walikuwa wakiwaeleza Wakenya hatua ambazo wamepiga na jinsi utawala wa Rais Ruto ulivyokuwa ukiendeleza nchi.

Hata hivyo, wengi wao sasa hawaonekani sana, hata kwenye mtandao wa X ambao walikuwa wakitumia sana kuwasiliana.

Mitandao ya mawaziri hao sasa imekaa bila chochote baadhi yao wakiamua kurejelea maisha yao kama raia.

Wengi wa mawaziri hao walikataa mahojiano na Taifa Leo wakisema wanastahili kuachwa kuendelea na maisha yao kibinafsi.

Wengine walihofia kuwa wanaweza kujikwaa ulimi ilhali bado wana matumaini ya kujumuishwa kwenye orodha mpya ya baraza la mawaziri.

Hata hivyo, duru zinaarifu kuwa huenda hakuna hata waziri mmoja ambaye alihudumu atakayeunga baraza jipya kwani imeamuliwa wafutwe kabisa kwa kuzingatia matukio ya kisiasa yanayoendelea nchini.

Aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria jana alisema kuwa amejizuia kufanya mahojiano na vyombo vya habari huku akimakinikia kuendelea na maisha yake nje ya siasa.

Waziri wa zamani wa Ulinzi Aden Duale naye alisema alikuwa na shughuli nje ya Nairobi japo akasema yuko tayari kwa mahojiano baadaye.

Baada ya kufutwa, mawaziri wote mbali na Bw Duale walichapisha habari za shukrani kwa Rais Ruto.

Walimshukuru kiongozi wa nchi kwa kuwapa nafasi ya kufanya kazi katika wizara hizo.

Mbali na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki, wengine wote walibadilisha habari katika mtandao wa X zilizoonyesha kuwa walikuwa mawaziri.

Bw Duale anaonekana bado anatumia sana mtandao wake wa X na mnamo Jumatatu aliweka video iliyoonyesha Rais Ruto akikemea wakfu wa Ford aliodai unafadhili maandamano nchini.

Pia alijichapisha maoni yake kwenye mtandao wa X ambao ulionyesha kuwa anaunga mkono kauli ya Rais Ruto.

“Uhuru wa nchi yetu ni kitu cha thamani sana kwetu. Hatutaruhusu ghasia ambazo zimedhaminiwa kuvuruga nchi yetu. Wale ambao wanalenga kusambaratisha nchi hii tunawajua na tunafahamu mipango yenu,” akaandika Bw Duale.

Mawaziri Kipchumba Murkomen, Susan Nakhumicha na Mithika Linturi ambao wamekuwa wakikashifiwa sana na Gen-Z kutokana na jinsi walivyosimamia wizara zao, walichapisha maandishi katika mtandao wao wa X wakati ambapo walifutwa kazi.