Habari za Kitaifa

Wakulima wa kahawa waandamana Nyeri kulalamikia bei duni

Na STEPHEN MUNYIRI August 23rd, 2024 1 min read

USAFIRI katika barabara kuu yenye shughuli nyingi ya Karatina-Nairobi ulilemazwa kwa saa kadhaa Alhamisi wakati wakulima wa kahawa walipoifunga wakilalamikia malipo duni kwa mazao yao.

Wakulima hao walio memba wa Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Kahawa cha Baricho, Kaunti ya Mathira, Nyeri, walifurika barabarani mwendo wa saa tano asubuhi wakilalamikia makato “ambayo hayakufafanuliwa” kwenye malipo ya mazao yao msimu uliopita.

Waandamanaji hao waliobeba matawi ya mikahawa waliwasha mioto kwenye barabara kuu na kuwazuia waendeshaji magari wanaotumia waliolazimika kutumia njia mbadala.

Walimzuia Kamanda wa Polisi Kaunti ya Nyeri, Benjamin Rotich, aliyekuwa akisafiri kuelekea Nairobi akitumia gari lake rasmi na kumlazimisha awahutubie.

Aliwaambia kwamba kufunga barabara sio njia bora ya kueleza malalamishi yao lakini ushauri wake ukaambulia patupu na kumlazimu kuwaita polisi wa kuzima ghasia kutoka kituo cha polisi cha Karatina.

Maafisa wa polisi waliojihami kwa mavazi ya kuzima ghasia wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Mathira Mashariki, Samson Leweri, waliwarushia vitoa machozi waandamanaji na kuwalazimu kufungua barabara.

Mkulima akikagua zao la kahawa alilowasilisha katika kiwanda Nyeri, mnamo Juni 2024. PICHA | JOSEPH

Wakulima waliozungumza na vyombo vya habari walisema wanahisi kuhadaiwa na serikali iliyoahidi wakati wa kampeni kwamba wangehakikishiwa bei ya chini zaidi ya Sh80 kwa kila kilogramu ya kahawa.

Baadhi walisema walipokea kiasi cha hadi Sh60 kwa kila kilo kabla ya kupunguzwa zaidi na “makato ambayo hayakufafanuliwa.”

“Tunahisi serikali hii ilitulaghai kwa sababu hatukuwa tunatarajia hili. Baadhi yetu tulikuwa tumkopa kwingineko tukitumai tutapata hela za kutosha kulipa, sasa tumekwama,” alisema Patrick Kariuki.

Maandamano hayo ambayo yamekuwa jambo la kawaida eneo hilo yanaashiria changamoto linalotokota katika sekta ya kahawa.

Katika Chama cha Ushirika wa Wakulima Ndaroini, kilicho karibu, hali ilikuwa sawia huku wakulima wakilalamika kuwa walipokea Sh62 ilihali walikuwa wanatarajia zaidi ya Sh100 kwa kila kilo.