Habari za Kitaifa

Walimu wataka donge nono kusimamia KCSE

Na DAVID MUCHUNGUH September 17th, 2024 2 min read

WALIMU wa Shule za Upili sasa wanataka wapewe nyongeza ya marupurupu ya kusimamia Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) ulioratibiwa kuanza Oktoba 22, 2024.

Kupitia chama cha kutetea masilahi yao (Kuppet) walimu hao wanataka marupurupu hayo yaongezwe kwa kati ya asilimia 750 na asilimia 900.

Kupitia barua kwa Waziri wa Elimu Julius Ogamba, Katibu Mkuu wa chama hicho Akello Misori anapendekeza viwango vipya vya malipo vya Sh3,000 kwa siku kwa kila msaidizi wakati wa mtihani huo kutoka malipo ya zamani ya Sh400 kwa siku.

Kuppet inataka wasimamizi wa wasaidizi hao nao walipwe Sh3,500 kutoka Sh450 wanazolipwa wakati huu na Sh4,500 zilipwe walimu wakuu kila siku kwa huduma wanazotoa kama mameneja wa vituo vya mitihani.

Wakati huu walimu wakuu wanalipwa marupurupu ya Sh500 kila siku katika kipindi chote cha mtihani wa KCSE.

“Wanachama wetu wameapa kukataa viwango vya sasa vya malipo ya marupurupu ya usimamizi wa mtihani wa kidato cha nne (KCSE). Kama Waziri anayesimamia Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchini (Knec), tunakuomba uhakikishe kuwa baraza hilo linawalipa walimu kulingana na sera inayotumika katika utumishi wa umma,” anasema Bw Misori katika barua hiyo.

“Viwango vya chini vya malipo ya usimamizi wa mitihani unashuhudiwa katika ngazi zote kuanzia usaidizi, usimamizi hadi usahihishaji. Viwango hivyo vya malipo haviridhishi na havijaafiki viwango hitajika na hivyo vinawavunja moyo walimu. Aidha, malipo hayo yanaweza kuathiri uhalali wa mitihani ya kitaifa,” akaongeza.

Matakwa hayo ya nyongeza ya marupurupu kwa walimu wanaohudumu nyakati za mitihani ya kitaifa ni miongoni mwa yale yaliyochangia Kuppet kuitisha mgomo.

Mgomo huo ulioanza Agosti 26, 2024, ulidumu kwa wiki moja kabla viongozi wa chama hicho kukubaliana na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) na kuusitisha mnamo Septemba 2.

“Walimu ndio wafanyakazi pekee wa umma ambao hawana sera kuhusu malipo ya marupurupu wanapohudumu nje ya vituo vyao rasmi vya kazi. Malipo hayo ni duni kiasi cha kuwageuza walimu hao kuwa watumwa,” akaeleza Bw Misori.

Katika siku za hivi karibuni, KNEC imezongwa na changamoto za kifedha kiasi kwamba huchelewesha malipo ya walimu wanaohudumu kama wasimamizi wa mitihani ya kitaifa na wakati wa usahihishaji wa mitihani hiyo.

Hii ni baada ya serikali kusitisha mtindo wa zamani wa utozaji ada ya mitihani ya kitaifa.