Habari za Kitaifa

Washirika wa Gachagua wahojiwa kuhusu maandamano, njama ya kumtimua ikisukwa


WASAIDIZI watatu wa karibu wa Naibu Rais Rigathi Gachagua Jumanne walihojiwa na polisi kuhusiana na maandamano ya hivi majuzi yaliyoongozwa na vijana huku kukiwa na mazungumzo ya kupanga njama ya kumuondoa ofisini.

Watu hao waliandikisha taarifa kwa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) katika Kituo cha Polisi cha Karen kuhusu madai ya kuingilia na kufadhili maandamano yaliyomlazimu Rais William Ruto kuondoa Mswada wa Fedha wa 2024 na kuvunja Baraza lake la Mawaziri.

Orodha ya waliohojiwa awali ilikuwa na wafanyakazi watano lakini ilipunguzwa hadi watatu na wapelelezi baada ya kuwaondolea wawili lawama.

Mmoja wa wale waliotakaswa alikuwa amesafiri hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika kilele cha maandamano na maafisa walitaka kujua maelezo zaidi kuhusu ziara hiyo. Inasemekana alitoa maelezo ya kuridhisha.

Afisa mwingine aliombwa kueleza shughuli ‘zinazotiliwa shaka’ alizofanya wakati wa kilele cha maandamano hayo.

Afisa mkuu wa DCI, ambaye ni miongoni mwa waliochukua taarifa hizo, aliambia Taifa Leo kwamba gavana wa zamani na mbunge maarufu wa Nairobi pia wamehojiwa kuhusiana na hilo.

Walihojiwa siku ambayo washirika wa Bw Gachagua walidai kuwa tayari kuna mipango ya baadhi ya washirika wa Rais Ruto kumuondoa Naibu Rais mamlakani.

Rais Ruto aliwahi kudai kuwa maandamano ‘halali’ ya Gen Z dhidi ya mapendekezo ya ushuru yalitekwa nyara na ‘wahalifu waliopangwa’.

Siku ambayo Rais aliondoa Mswada wa Fedha wa 2024, naibu wake ambaye alihutubia taifa kutoka Mombasa dakika chache baada ya hotuba ya kiongozi wa nchi alidai kulikuwa na majaribio ya kumhusisha na maandamano. Alimshutumu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ujasusi (NIS) Noordin Haji kwa kujaribu kumhusisha pamoja na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.

“Noordin Haji alikuwa anajaribu kutoa propaganda na kuhusisha viongozi na machafuko hayo akiwemo mimi na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta. Ni wazi kabisa na Rais amekiri kuwa maandamano hayo yalisababishwa na hasira za Wakenya kuhusu Mswada wa Fedha,” Bw Gachagua alisema.

Mbunge wa Embakasi Kaskazini Bw James Gakuya Jumanne aliambia Kameme FM kwamba ‘kuna mwanasiasa kutoka Kaunti ya Kiambu ambaye amekuwa akikusanya saini ili kuanzisha mchakato wa kumuondoa Bw Gachagua ofisini’.

Alisema washirika wa Bw Gachagua wanasubiri kuona jinsi mpango huo utakavyokuwa, akisema eneo la Mlima Kenya lazima lisalie macho kwani hilo litakuwa janga la kisiasa iwapo litatimia.

Alisikitikia kile alichodai kuwa tabia ya Mlima Kenya ya kupiga vita viongozi wa kutoka eneo hilo akisema kuna ‘viongozi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakipiga Bw Gachagua ili kuwafurahisha wafadhili wao ambao wana nia mbaya kwa watu wetu’.

Kulingana na Mbunge Maalum Sabina Chege, mpango huo anaoutaja kama ‘bahati mbaya’ unapendekezwa na iwapo utatimia, utaonyesha jinsi “siasa za ulaghai” zinatekelezwa.

“Hata kuta zina masikio, mazungumzo hayo yamekuwa yakiendelea. Rais Ruto anapaswa kuwa mwangalifu sana kuhusu ushauri kutoka kwa marafiki na washauri wake. Natumai hajasahau mashaka yake ya 2018-2022 ya kufanya kazi kama Naibu Rais na mkubwa wake ambaye alikuwa akimhujumu.”

“Rais Ruto anapaswa kukumbuka kuwa hata wakati tofauti zake na Rais Kenyatta zilipofikia kilele, hakuna aliyewasilisha hoja ya kumfukuza kutoka kwa wadhifa wake wa pili wa uongozi,” alisema Bi Chege.

Bi Chege alisema, “ikiwa hoja itawasilishwa na kufikia umma, basi anayepaswa kuisimamisha mara moja ni rais mwenyewe.”

Bi Chege alisema kwamba udhaifu mkubwa ambao huenda ukamsababishia Bw Gachagua kuangamia ni kwamba “sisi jamii ya Agikuyu hatupendani tofauti na jamii zingine”.

Majina kadhaa yameorodheshwa kama yanayoweza kuchukua nafasi ya Bw Gachagua. Miongoni mwao ni pamoja na waziri mteule Alice Wahome, mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, waziri wa usalama mteule Kithure Kindiki, gavana wa Kirinyaga Bi Anne Waiguru na mwenzake wa Embu Cecil Mbarire.