Habari za Kitaifa

Wasomi wakosoa hatua ya Kiswahili kufanywa somo la hiari

Na TITUS OMINDE July 15th, 2024 2 min read

WATAALAMU wa lugha ya Kiswahili na Chama cha Walimu wa Kiswahili nchini Kenya wamekosoa sera ya serikali inayolenga kuifanya lugha hiyo kuwa somo la hiari katika mtihani wa Kitaifa.

Wanasema hatua hiyo inalenga kushusha hadhi ya Kiswahili nchini.

Sera hiyo ikitekelezwa, watahiniwa wa Gredi ya Nane ambao ni waanzilishi wa Mtaala wa Umilisi (CBC) watafanya chaguo kati ya Kiswahili na Lugha Ishara.

Wakizungumza mjini Eldoret wakati wa warsha ya Kiswahili, wadau hao walitaja hatua hiyo kuwa pigo kwa kwa ufanisi wa lugha hii inayozungumzwa Afrika Mashariki na inayokuchukua nafasi kubwa katika ushirikiano wa kikanda.

“Ni ajabu kusikia kuwa Kiswahili halitakuwa tena somo la lazima katika mitihani ya kitaifa ya Gredi ya Nane, kulingana na sera mpya ya serikali. Huu kwangu naomba niuchukulie kuwa uvumi tu,” alisema Gabriel Mbeka, mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Kiswahili cha Sekondari (CHAWAKIAMA).

Mbeka anayefunza Kiswahili katika shule ya Matunda SA, Kaunti Ndogo ya Likuyani alitaka wasomi wa Kiswahili kupinga pendekezo hilo kwa kila hali.

Bw Mbeka aliitaka serikali kuimarisha Kiswahili shuleni badala ya kufanya somo hilo kuwa la hiari.

Aidha, aliiomba Wizara ya Elimu kubatilisha uamuzi huo na kuhusisha wasomi wa Kiswahili katika ushirikishwaji wa umma ili kupata maoni sahihi kuhusu jinsi ya kukuza Kiswahili kama lugha.

“Kenya inapaswa kufanya Kiswahili kuwa somo la lazima kutoka shule za msingi hadi ngazi za juu badala ya kulifanya kuwa la hiari,” alisema Bw Mbeka.

Aliwataka wabunge kupitisha mswada unaonuiwa kuanzisha Baraza la Kiswahili la Kenya.

Maoni hayo pia yaliradidiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kenya (CIPK) North Rift, Sheikh Abubakar Bini.

“Tunaomba wabunge wetu wapitishe mswada wa Kiswahili unaolenga kubuniwa kwa Baraza la Kiswahili nchini ili kuweka mikakati ya kulinda Kiswahili kama urithi wetu,” alisema Sheikh Bini.

Sheikh Bini alisema Kiswahili lazima kipewe kipaumbele katika ngazi zote za serikali kama njia ya kukuza utamaduni wetu badala ya kukuza lugha za kigeni.

Mkufunzi wa Kiswahili chuo Kikuu cha Moi, Dkt Allan Opijah, aliongeza uzito kwenye hoja hiyo akisema kwamba wakati umewadia Baraza la Kiswahili kubuniwa.

“Wakati umefika wa kubuniwa kwa Baraza la Kiswahili ili kulinda Kiswahili, kuanzia shule za msingi hadi vyuoni,” alisisitiza Dkt Opijah.