Habari

Zaidi ya nusu ya mapato ya nchi yalitumiwa kulipa madeni – Takwimu

May 21st, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

SERIKALI ilitumia zaidi ya Sh600 bilioni kulipa madeni katika muda wa miezi 10 kufikia Aprili 2019.

Kwa muda huo, serikali ilitumia Sh635.35 bilioni kulipa madeni, kuonyesha athari za mikopo mikubwa iliyochukuliwa nchini.

Takwimu za hivi punde kutoka Hazina ya Fedha zinaonyesha pesa zilizotumiwa kulipa deni la umma ni mara tatu ya kiwango kilichotumiwa katika miradi ya maendeleo katika muda huo.

Hii ni asilimia 64.06 zaidi ikilinganishwa na muda huo mwaka mmoja uliopita kutokana na kupevuka kwa mikopo ya muda mfupi iliyochukuliwa miaka kadhaa iliyopita.

Malipo kwa wakopeshaji kutoka humu nchini na nje ya nchi yalikuwa ya pili kwa matumizi ya fedha za umma, baada ya mishahara, marupurupu na gharama ya usimamizi serikalini ambapo serikali ilitumia Sh739.15 bilioni.

Gharama ya matumizi ya fedha za umma kati ya Julai 2018 na Aprili 2019 ilizidi kwa Sh22.57 bilioni, juu zaidi ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka wa kifedha uliotangulia kulingana na data hiyo.

Pesa zilizolipwa wakopeshaji zilikuwa ni Sh132.72 bilioni au asilimia 26.41 zaidi ya pesa zote zilizotolewa kwa kaunti zote 47 (Sh234.29 bilioni) ambapo miradi ya maendeleo ilitengewa Sh215.68 bilioni na pensheni Sh52.65 bilioni.

Asilimia 54.74 za mapato yote (Sh1.16 trilioni) zilitumiwa kulipa madeni katika muda huo, ambazo zi asilimia 9.83 zaidi ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.