Habari

'Hasla' akunja mkia

September 24th, 2020 2 min read

LEONARD ONYANGO na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto, Jumatano alilazimika kukunja mkia na kukubali uamuzi wa Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju kuwa chama hicho hakitawasilisha mwaniaji wa ubunge katika uchaguzi mdogo wa Msambweni.

Hii ni baada ya chama cha Jubilee kupuuza shinikizo zake kuwa na mgombeaji Msambweni, na badala yake kupitia Katibu Mkuu kikatangaza kitaunga mkono mwaniaji wa ODM.

Hapo Jumatano Dkt Ruto alielekea katika makao makuu ya Jubilee mtaani Pangani, Nairobi, muda mfupi baada ya Bw Tuju kutoa tangazo lake, hii ikiwa ni ziara yake kwa siku ya pili mfululizo akifuatilia suala hilo.

Baada ya mkutano wa takribani masaa mawili na maafisa wa Jubilee akiwemo Bw Tuju, Naibu Rais alisema kuwa amekubaliana na uamuzi huo.

“Mimi nilikuwa na mawazo tofauti kuhusu uchaguzi mdogo wa Msambweni. Nilitaka tuwasilishe mwaniaji wa Jubilee. Lakini kwa kuwa uamuzi umeshafanywa na tangazo kutolewa kwa Wakenya, nimekubaliana nao,” akasema Dkt Ruto ambaye ni Naibu Kiongozi wa Jubilee.

Alikuwa akiunga mkono Bi Mariam Sharlete aliyehama ODM majuzi.

“Namhurumia sana Bi Sharlete na namhimiza pamoja na wengine waliotaka kuwania ubunge wa Msambweni kupitia Jubilee kutumia vyama tofauti au kuwa wagombeaji wa kujitegemea,” akasema Naibu wa Rais.

Dkt Ruto alimtaka mwaniaji wa ubunge anayetaka amsaidie kufanya kampeni katika eneobunge la Msambweni ajitokeze: “Mwaniaji yeyote anayetaka mimi nimsaidie kufanya kampeni azungumze name vizuri tuchape kazi,” akasema.

Uamuzi wa Jubilee kutokuwa na mgombeaji Msambweni kumezima azma ya Naibu Rais William Ruto ya kutumia uchaguzi huo kupimana nguvu na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Lakini ushauri wake kwa Bi Sharlete kuwa awanie kwa chama kinginge ama ajitegemee unaashiria kuwa huenda akaongoza kampeni za mpinzani wa ODM jinsi alivyofanya katika uchaguzi mdogo wa Kibra mwaka jana.

Katika Kibra, chama cha Jubilee kiligawanyika baada ya Bw Tuju kutangaza Jubilee hakingekuwa na mgombeaji.

Lakini Bw Tuju alisalimu amri kufuatia shinikizo kutoka kwa Dkt Ruto ambaye alimuunga mkono MacDonald Mariga dhidi ya Imran Okoth wa ODM, ambaye alishinda.

Uchaguzi huo ulibadilika kuwa ushindani kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto, hali ambayo inatarajiwa kujirudia Msambweni.

Awali, Bodi ya Uchaguzi ya Jubilee ilikuwa imealika wanachama wanaotaka kugombea kiti hicho na vingine vitano vya udiwani kuchukua fomu za uteuzi kabla ya leo.

Kiti cha Msambweni kilibaki wazi kufuatia kifo cha Suleiman Dori wa ODM mnamo Machi mwaka huu.

“Kufuatia mashauriano ndani ya chama, imeamuliwa kwamba Jubilee hakitakuwa na mgombeaji kwenye uchaguzi mdogo wa Msambweni,” Bw Tuju alisema.

Dakika chache baada ya kutoa taarifa hiyo, Dkt Ruto aliwasili katika makao makuu ya Jubilee kukutana na Bw Tuju na maafisa wengine wa chama, hatua ambayo ilionyesha hakuridhishwa na uamuzi huo.

Mnamo Jumanne, Dkt Ruto alifika katika makao hayo kushinikiza chama hicho kuteua mgombeaji Mswambweni.

Bw Tuju alieleza kuwa uamuzi wa chama tawala kutosimamisha mgombeaji ulifikiwa ili kupatia chama cha ODM nafasi ya kukihifadhi kiti hicho katika moyo wa handisheki, ambayo Dkt Ruto amekuwa akipinga.

“Ushirikiano wa hivi majuzi kati ya ODM na Jubilee katika bunge na ikizingatiwa kwamba kiti cha Mswambweni kilikuwa kiti cha ODM, uamuzi umefikiwa kuwa Jubilee hakitasimamisha mgombeaji kwa manufaa ya ushirikiano huu,” Bw Tuju alisema. Alisema kwamba nchi hii inakabiliwa na changamoto kadhaa za kikatiba ukiwemo ushauri wa Jaji Mkuu David Maraga kwa rais avunje bunge kwa kushindwa kupitisha sheria ya kutekeleza usawa wa jinsia.

Bw Tuju alisema Jubilee kitasimamisha wagombeaji katika chaguzi ndogo za udiwani za wadi za Kahawa Wendani iliyo Kaunti ya Kiambu, Lakeview (Nakuru), Kisumu Kaskazini, Wudanyi/Mbale (Taita Taveta) na Dabbaso (Kilifi).

Dkt Ruto amekuwa akivamia Pwani ambayo ni ngome ya ODM na angetumia uchaguzi mdogo wa Msambweni kuthibitisha ubabe wake dhidi ya Bw Odinga.