• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Makahaba wapiga kambi Murang’a kumumunya mabilioni ya majani chai

Makahaba wapiga kambi Murang’a kumumunya mabilioni ya majani chai

Na KNA

WAKAZI katika Kaunti ya Murang’a wameeleza hofu yao kuhusu ongezeko la makahaba eneo hilo wanaopanga kunyemelea wakulima ambao wanatarajiwa kulipwa bonasi ya majani chai.

Baadhi ya wafanyabiashara wanasema kuwa vyumba vya kulala na lojing’i mjini Murang’a vimejaa huku makahaba kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kama vile Mombasa, Bomet, Nairobi na Eldoret wakilenga kuwapora wakulima wa chai baada ya kulipwa.

Diwani wa wadi ya Kangari, Bw Charles Kahoro amewaonya wakulima wa eneo hilo dhidi ya kuanguka kwenye mtego wa makahaba hao wanaojifanya kuwa madaktari au wahubiri wanapokodisha vyumba.

Bw Kahoro alidai kuwa wasichana hao awali waliripotiwa kuwapora wakulima wa chai na kuwaacha bila chochote cha kugharamia mahitaji ya familia zao.

Alisema makahaba hulenga wakulima wanaume ambapo huwawekea dawa za kuwalemaza ndani ya vileo vyao kabla ya kuwaibia.

Baadhi ya miji ambako makahaba hao wameripotiwa kuonekana kwa wingi ni Kangari, Kahuro, Kigumo na Kangema ambako wakulima wanatarajia kulipwa bonasi mwezi huu.

Katika soko la Kangari viwanda vinne vya majani chai vya Nduti, Makomboki, Ikumbi na Gacharage vinatarajia malipo ya mabilioni ya fedha.

Alisema kuwa wakulima wa majani chai wanafaa kukumbuka kuwa wamefanya kazi ngumu kwa muda wa mwaka mmoja, hivyo pesa watakazopata wanafaa kuzitumia kuimarisha hali ya maisha ya familia zao.

Mwakilishi huyo aliomba maafisa wa polisi kuwa makini kwa lengo la kutambulisha makahaba ambao kazi yao ni kupora wakulima na kuvunja familia zao.

Afisa Mkuu Msimamizi wa Kilimo katika Kaunti ya Murang’a, Bw Peter Njangi aliwashauri wakulima kutumia pesa zao kwa njia inayofaa.

“Baadhi ya wanaume huacha familia zao na kurudi pesa zinapoisha. Hilo ni jambo la kuhuzunisha sana,” alisema Bw Njangi.

Hali sawa na hiyo inatarajiwa katika kaunti zingine kunakokuzwa majani chai kwa wingi kama vile Nyeri, Kirinyaga, Meru, Kericho, Kisii, Nandi na Bomet.

You can share this post!

Raia wa Mali na Mkenya ndani kwa kunaswa na Sh1 bilioni feki

Raila na Ruto waonywa dhidi ya kuibua uhasama

adminleo