Habari

Mawakili kugoma kulalamikia mazoea ya serikali kukaidi maagizo ya mahakama

February 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili nchini (LSK) Bw Isaac Okero. Picha/ Maktaba

Na KENNEDY KIMANTHI

Kwa muhtasari

  • LSK chasema mgomo huo utafanyika kote nchini na kudumu kwa siku tano
  • Maaandamano ya amani katika miji mbalimbali nchini 
  • Jaji Mkuu ameikejeleli serikali kwa kupuuza maagizo ya mahakama

SHUGHULI za mahakama Jumatatu zitakwama kote nchini, mawakili watakapoanza mgomo kupinga hatua ya serikali kudharau maagizo ya mahakama na kukiuka haki za waliozuiliwa kwenye korokoro za polisi.

Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) Jumamosi kilisema mgomo huo utafanyika kote nchini na kudumu kwa siku tano, hadi Ijumaa wiki hii.
Naye kiongozi wa NASA, Bw Raila Odinga ameikashifu serikali kwa kukiuka Katiba na haki za raia kwa kudharau mahakama.

“Utawala wa Jubilee umegeuka kuwa dhalimu kwa kukaidi mahakama huku ikitumia polisi kuwahangaisha wananchi bila sababu,” akasema alipohudhuria mazishi ya babake mkurugenzi wa mawasiliano wa ODM Philip Etale, Bw Justus Etale.

LSK ilisema serikali ambayo inastahili kuonyesha mfano mzuri kwa umma kwa kutii maagizo ya mahakama, imefeli kutekeleza wajibu huo.

“Wanachama wetu wote watasusia mahakama kwa siku tano kuanzia Jumatatu kupinga tabia ya serikali, na maafisa wake wakuu, kutoheshimu amri za mahakama,” akasema mwenyekiti wa chama hicho, wakili Isaac Okero kwe

nye taarifa kwa vyombo vya habari.

“Ni wajibu wa kila mtu kuheshimu sheria. Ikiwa serikali inadharau sheria haifai kutarajia wananchi kuheshimu sheria hizo. Na nchi ambayo haiheshimu katiba na sheria hutumbukia katika machafuko,” akaeleza.

 

Maandamano

Wanachama wa LSK pia watafanya maandamano ya amani katika miji mbalimbali nchini. Watavalia mavazi yao rasmi ya kazi na kufunga ukanda wa manjano kuashiria kuwa wanagoma.

“Utawala wa kisheria nchini umekuwa ukikabiliwa na changamoto kuu katika siku chache zilizopita, baada ya maafisa wa serikali kuamua kuvunja haki za wananchi na kudharau maagizo ya mahakama,” akaeleza Bw Okero.

Hata hivyo, mahakama zinazoshughulikia kesi za uchaguzi hazitaathiriwa kutokana na kile ambacho LSK inasema ni makataa yaliyowekewa kesi hizo.
Msimamo huo wa LSK unajiri siku chache baada ya Jaji Mku David Maraga kuikashifu serikali kwa kupuuza mahakama, akisema maagizo yake yanafaa kuheshimiwa na wote.

Jaji Maraga alisema kuwa mwenendo wa kupuuzilia mbali maagizo ya mahakama unakwenda kinyume na Katiba na utawala wa sheria.
Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, serikali na maafisa wake wakuu wamekuwa wakipuuza maagizo yanayotolewa na serikali kuhusu masuala yenye umuhimu wa kitaifa.

Kwanza, serikali ilipuuza agizo lililotolewa na mahakama kuu kuitaka Mamlaka ya Mawasiliano (CA) kufungua mitambo ya matangazo ya runinga nne zilizozimwa mnamo Januari 30.

 

Runinga kuzimwa

Mitambo ya kupeperusha matangazo ya vituo vyo NTV, Citizen, KTN na Inooro TV ilizimwa kwa kupeperusha moja kwa moja matukio katika halfa ya kuapishwa kwa kingozi wa NASA Raila Odinga katika bustani ya Uhuru Park, Nairobi.

LSK ilisema itawasilisha kesi mahakamani kutaka kuadhibiwa kwa maafisa waliohusika moja kwa moja katika hatua hiyo ya kudharua mahakama.
Polisi, wakiongozwa na Inspekta Jenerali (IG) Joseph Boinnet, walipuuzilia mbali agizo la mahakama la kutaka wakili Miguna Miguna aachiliwe huru baada ya kupewa dhamana ya Sh50,000.

Isitoshe, IG alipuuza amri ya kumtaka kufika mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Luka Kimaru, kuelezea ni kwa nini alikataa kumwachilia Dkt Miguna.
Hii si mara ya kwanza kwa maafisa wakuu serikalini kudharau maagizo ya mahakama.

Itakumbubwa kuwa Makatibu wa Wizara wakiwemo Karanja Kibicho, Saitoti Torome, na Monica Juma (sasa waziri mteule) wamewahi kudharau amri za mahakama nyakati tofauti.