Landilodi kula hu kwa kumezea mke wa polo
Na LEAH MAKENA
Kwa Muhtasari:
- Landilodi alikuwa akizuru plotini kukusanya kodi lakini ikabainika alikuwa akimnyemelea mke wa mpangaji
- Siku ya kisanga, polo alimuachia mkewe amkabili landilodi
- Iliwalazimu wawili hao kufungua mlango baada ya wakazi kutisha kuuvunja na kuwavamia
SANSIRO, LIKONI
JOMBI wa hapa, alikataa kulipa kodi ya nyumba baada ya kumpata landilodi akirushana roho na mke wake.
Inasemekana kuwa landilodi alikuwa akizuru plotini mara mbili kwa mwezi akidai alitaka kukusanya kodi lakini ikabainika alikuwa akimnyemelea mke wa mpangaji.
Penyenye zasema kuwa landilodi alikuwa na tabia ya kufika polo akiwa kazini na hata kupikiwa na mkewe.
Duru zilidai kuwa jamaa aliponong’onezewa tabia ya landilodi, aliamua kufanya uchunguzi na haikuchukua muda mrefu kabla ya kubaini ukweli wa mambo.
Siku ya kisanga, polo alimuachia mkewe amkabili landilodi.
Kulingana na mdokezi, bibi alitumia sehemu ya hela hizo kununua nusu kilo ya nyama pamoja na mapochopocho mengine kisha akamuita landilodi kwa chakula cha mchana.
Punde tu baada ya kumaliza mlo, wawili hao walianza starehe zao ambazo zilikatizwa na jamaa aliyebisha mlango kwa fujo. Kijasho chembamba kilianza kuwatoka wasijue wafanye nini.
Habari zasema kuwa wawili hao walipokawia kufungua mlango, jombi alipiga kamsa kuwavutia majirani na wapita njia.
Iliwalazimu wawili hao kufungua mlango baada ya wakazi kutisha kuuvunja na kuwavamia. “Samahani, sema utakacho na nitakupa tumalize hili suala bila ya kunisababishia aibu zaidi,” aliomba landilodi huku akitetemeka mwili mzima.
Kulingana na mdokezi, polo alichagua kutolipa kodi tena na baada ya mwenye nyumba kutia sahihi mkataba huo, alimwachilia huru.
Mke wa polo alilazimika kutoroka akihofia kuadhibiwa na polo pamoja na aibu aliyokuwa amepata.
Haikujulikana iwapo landilodi alifika tena hapo kukusanya kodi ila mpangaji aliapa kusalia hapo hadi kaburini.