PICHA: Nderemo nje ya mahakama baada ya Obado kuachiliwa
NA RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA Kuu Jumatano imemwachilia huru Gavana wa Migori Okoth Obado kwa dhamana ya Sh5 milioni pesa taslimu.
Punde tu baada ya kupewa dhamana, wafuasi wake walijitokeza kucheza na kuimba nyimbo za furaha nje ya mahakama ya Milimani, nairobi.
Ulinzi mkali uliwekwa huku maafisa wa polisi wenye vitoa machozi wakishika doria.
Hata hivyo, washukiwa wengine wawili walioshtakiwa pamoja Michael Oyamo na Caspal Obiero walinyimwa dhamana.
Jaji Jessie Lesiit alisema ushahidi dhidi ya Oyamo na Obiero unawalenga katika mauaji ya Sharon Otieno.
Akimwachilia Bw Obado jaji huyo alisema ushahidi uliowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma dhidi ya Obado haujamlenga moja kwa moja. Jaji Lesiit alimwamuru Obado asisafiri zaidi ya kilomita 20 kutoka nje ya Migori.
Pia alimwamuru Obado asivuruge mashahidi na pia awe akipiga ripoti mara moja kwa mwezi kwa.msajili wa mahakama kuu kitengo cha kushughulikia kesi za uhalifu.
Jaji Lesiit pia alimtahadharisha kwamba akikaidi masharti sita aliyopewa dhamana aliyopewa itaondolewa.
Awali ilibidi maafisa wa polisi wafunge milango na kuwazuia wafuasi hao wa Bw Obado kutoingia mahakamani.
Wanahabari, mawakili na jamaa za washtakiwa walizuiliwa kuingia ndani ya mahakama uamuzi ulipokuwa unasomwa.
Walioruhusiwa kuingia mahakamani ni mawakili waliowawakilisha washtakiwa na watu wachache na wapeperushaji wa habari wa runinga.
Wafuasi hao walipiga kambi nje ya mahakama kusubiri mawakili wamlipie dhamana ya Sh5milioni pesa tasilimu ndipo atoke seli.