Habari Mseto

Khalwale ashtaki ‘Toto’ kwa kudai aliua mfanyakazi

February 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RICHARD MUNGUTI na SAM KIPLAGAT

SENETA wa Kakamega amemshtaki mfanyabiashara mashuhuri wa Kakamega Cleophas Shimanyula almaarufu Toto kwa kudai kwamba mwanasiasa huyo alimuua mfanyakazi wake aliyeuawa na fahali wake.

Katika kesi iliyowasilishwa na mawakili Danstan Omari na Shadrack Wambui, Dkt Khalwale, wake zake watatu na watoto wake 17 wanaomba mahakama imwamuru Bw Shimanyula kuwafidia kitita cha Sh1.3 bilioni.

Dkt Khalwale amekana kwamba alimuua mfanyakazi wake Kizito Amukune Moi mnamo Januari 28, 2024.

Mwanasiasa huyo ameeleza mahakama kuu kwamba Toto amekataa kuomba msamaha na kufuta katika mitandao ya kijamii habari za uwongo alizochapisha akimhusisha na kifo cha Kizito.

Kizito alishambuliwa na kuuawa na fahali wa Khalwale alipokuwa anamlisha zizini.

Mawakili Danstan Omari, Aranga Omaiyo na Shadrack Wambui wamedokeza kwamba ripoti ya upasuaji uliofanywa na madaktari wanne imethibitisha kwamba Kizito aliaga kutokana na majeraha ya kufumwa na fahali huyo kwa pembe zake mnamo Januari 28, 2024.

Kizito alizikwa Feburuari 5, 2024 na fahali huyo aliyesababisha kifo chake akauawa kulingana na mila na desturi za jamii ya Isukha.

Mahakama imeelezwa kwamba Toto alikataa kumuomba msamaha Dkt Khalwale na kumtaka wakutane kortini.

Katika kesi iliyowasilishwa kortini, Bw Omari anaomba mahakama imwamuru Shimanyula akome kabisa kueneza uwongo na kuchapisha habari za kumkejeli yeye na familia yake.

Kwenye kesi hiyo, Dkt Khalwale amesema mshtakiwa ameeneza habari ambazo hawezi kuthibitisha kuhusu.

Katika nakala za kesi alizowasilisha mahakama kuu ya Milimani, Dkt Khalwale amedokeza kwamba yeye pamoja na wake zake watatu na watoto 17 wamesononeshwa na habari hizo za uwongo kuhusu kifo hicho cha Kizito.

“Licha ya kumsihi Toto afute madai hayo ameendelea kuchapisha habari za kupotosha zaidi na kumfedhehesha Khalwale,” Bw Omari ameeleza katika kesi aliyoshtaki mahakamani.

Khalwale ameeleza kwamba habari hizi za uwongo zimemdunisha na kumharibia sifa kama kiongozi wa kaunti ya Kakamega.

Wakati wa uchaguzi mkuu uliopita alichaguliwa kwa zaidi ya kura 249,000.

“Matusi dhidi ya Khalwale ni matusi dhidi ya wakazi wa kaunti yote ya Kakamega,” Bw Omari amesema.