Habari Mseto

Tutasambaratisha masomo Januari 'uhamisho kiholela' usipokomeshwa, walimu waapa

December 20th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

WALIMU wametangaza mgomo mkubwa wa kitaifa kuanzia Januari 2 2019, kwa kile wametaja kutozingatiwa kwa maslahi yao na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC).

Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) Wilson Sossion alisema juhudi zao kuirai tume hiyo kushughulikia matakwa hayo zimegonga mwamba, na hivyo kulazimika kuchukua hatua hiyo.

Miongoni mwa matakwa wanayotaka yashughulikiwe ni kuondolewa kwa haki ya walimu kupandishwa vyeo, walimu kutenganishwa na familia zao kupitia uhamishaji wa kiholela, kuwafanyia walimu tathmini ya utendakazi bila kushirikishwa na kuanzishwa kwa mfumo wa mafunzo ambapo walimu wanalazimika kuyagharamia kupitia mishahara yao.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, Bw Sossion alisema kwamba tume hiyo imekuwa ikipuuzilia mbali kila juhudi za kuishinikiza kutathmini upya mfumo wa kuwahamisha walimu.

Mnamo Jumanne, Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Nancy Macharia, alitangaza kuhamishwa kwa walimu 3,094 wa shule za msingi na upili, jambo ambalo KNUT ilipinga vikali.

“Uhamisho huo haukupitishwa na kamati maalum inayopaswa kuidhinisha uhamisho wa mwalimu kutoka shule moja hadi nyingine. Ni kinaya kwamba walimu hao wamepewa maagizo tu, bila kufahamishwa lolote kuhusu hatua hizo,” akasema Bw Sossion.

Hata hivyo, TSC inashikilia kuwa uhamisho huo ulifanywa baada ya taratibu zote zinazohitajika, kabla ya kuidhinishwa na kamati maalum.

Tume pia iliwapa walimu hao hadi Desemba 28 wawe wamehamia katika shule mpya watakakoanza kuhudumu.

Bi Macharia aliwaagiza Wakurugenzi wa Elimu wa Kaunti (CDE) kuhakikisha kuwa agizo hilo limezingatiwa .

Lakini kulingana na Bw Sossion, ambaye alikuwa ameandamana na maafisa wakuu wapya wa chama hicho, walimu hawawezi kuendelea kuvumilia ukiukwaji wa haki zao hata baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuiagiza tume kutowahamisha tena.

“Inasikitisha kwamba TSC inaenda kinyume na agizo la rais kutowahamisha walimu kwani hilo linawafanya baadhi kutengana na familia zao,” akasema Bw Sossion.

Tayari, walimu wamepinga hatua ya seriiali kuwatoza asilimia 1.5 ya mishahara yao kama ada ya Mpango wa Kitaifa wa Ujenzi kuanzia Januari, wakitishia kuwa huenda wakajumuisha hilo miongoni mwa masuala watakayogomea.

Walimu wanautaja mpango huo ukiukaji wa haki zao, wakidai kwamba hawakushirikishwa katika uidhinishaji wake.

Hii ni licha ya Rais Kenyatta kusisitiza kwamba unawiana na utekelezaji wa Nguzo Nne Kuu za Maendeleo za serikali yake.

Mgomo huo huenda ukawaathiri wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Kwanza, ikizingatiwa kuwa wengi wao washapokea barua kutoka kwa shule za upili watakazojiunga nazo.