Masaibu ya walimu wa JSS ni mwiba wa kujidunga binafsi
NA BENSON MATHEKA
HATUA ya Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) kuwafuta kazi walimu wa Sekondari Msingi (JSS) waliokuwa kwenye mgomo haikunishangaza.
Hii ni kwa sababu walimu hao walikaidi ushauri wa vyama vya kutetea walimu ambavyo vilijitolea kuwasaidia ili TSC iweze kushughulikia matakwa yao ya kuajiriwa kazi za kudumu.
Ninasema kuwasaidia kwa sababu wakiwa walimu wanagenzi, walimu wa sekondari msingi sio wanachama wa vyama vya walimu kwa kuwa hawakuwa wameajiriwa rasmi. Huu ndio ukweli wa mambo.
Licha ya hali yao, vyama hivyo, Muungano wa vyama wa walimu Kenya (KNUT) na Chama cha Walimu wa shule za Sekondari na Taasisi za Elimu ( KUPPET) viliwashauri warudi kazini na kuvipatia muda viweze kuzungumza na TSC kwa niaba yao.
Kuppet, kwa kutaka kulinda maslahi yake, ilitia saini na baadhi ya walimu hao warudi kazini.
Hata hivyo, walimu hao, walipuuza ushauri wa vyama hivyo ambao viliwapa bila malipo na kutii viongozi wa vuguvugu lao ambalo, lilitaka kuzungumza na TSC moja kwa moja. Vuguvugu hilo lilisema mkataba wa kurudi kazini unapaswa kuwa kati ya walimu wa JSS na mwajiri wao TSC.
Kile ambacho hawakufahamu ni kuwa, kama mwajiri, TSC iliishiwa na uvumilivu hata kama ilifuata mchakato unaohitajika wa kuwatimua.
Iliwapa barua za kueleza sababu za kutochukuliwa hatua kwa kususia kazi ambazo, naweza kusema kwamba walichukulia kama mzaha hadi pale walipong’amua kuwa kitumbua chao kingeingia mchanga lakini walikuwa wamechelewa.
Walipotangaza kusitisha mgomo wao na kurudi kazini, TSC ilikuwa tayari imeandika barua za kuwafuta kazi.
Japo hakuna anayeweza kufurahia kuona mtu akiachishwa kazi, na ni haki ya kila mfanyakazi kugoma kulalamikia hatua kandamizi kutoka kwa mwajiri wake, masaibu ya walimu hao yanaweza kutajwa kuwa mwiba wa kujidunga.
Walikosa kutambua kuwa kazi yao ilikuwa ya kibarua na kwamba hawakuwa na mtetezi kama walimu ambao wameajiriwa kazi ya kudumu wanaotetewa na vyama vyao ambavyo vinatambuliwa kisheria.
Ni kweli TSC haikutimiza ahadi ya kuwaajiri kazi ya kudumu ilivyowaahidi baada ya kuhudumu kwa mwaka mmoja, lakini pia ni kweli tume hiyo haikukanusha ahadi hiyo.
Ilichofanya ni kuwaambia kuwa wangeajiriwa baada ya kuhudumu kwa mwaka mmoja zaidi, jambo ambalo hawakukubaliana nalo.
Japo ni haki yao kutokubaliana na uamuzi huo, ukweli ni kwamba ni vigumu kushindana na mwajiri wako hasa ukiwa umeajiriwa kama kibarua.