Kimataifa

Mmoja afariki wakati wa kampeni za Rais Kagame

Na MASHIRIKA June 24th, 2024 2 min read

Kigali, Rwanda

MTU mmoja amefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati rabsha zilipotokea katika mkutano wa kampeni za Rais Paul Kagame.

Rais Kagame anawania kuhifadhi kiti chake kwa muhula wa nne, kwenye uchaguzi utakaofanyika Julai 15, 2024.

Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la Rwanda, hali hiyo ilitokea kabla ya upigaji kura unaotarajiwa kurefushwa kwa miaka 24 ya utawala wa Rais Kagame haujafanyika.

Bw Kagame amekuwa Rais wa Rwanda tangu mwisho wa mauaji ya halaiki yaliyofanyika 1994 na ambapo watu 800,000, wengi wao wakiwa Watutsi walifariki.

Baadhi ya Wahutu pia walifariki.

Aidha, alichaguliwa mara ya kwanza mwaka 2000.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 66, atatoana kijasho na wapinzani sawa na aliopambana nao 2017.

Miongoni mwa wanaowania urais ni pamoja na

kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Green Party, Frank Habineza, na aliyekuwa mwanahabari, Philippe Mpayimana, ambaye anagombea mwaniaji wa kujitegemea.

Kampeni zilianza Jumamosi, Juni 22, 2024 huku Kagame akihutubia mikutano kadhaa ya umma katika eneo la Musanze na Rubavu, Kaskazini mwa.

“Mtu mmoja alifariki na wengine 37 kujeruhiwa katika mkanyagano uliotokea wakati wa kampeni za RPF-Inkotanyi mjini Rubavu siku ya Jumapili,” Shirika la Utangazaji la serikali la Rwanda liliripoti, likitumia jina rasmi la chama cha Kagame.

“Wizara ya Serikali za Mitaa iliwataka wanaoshiriki katika kampeni hiyo kufuata maelekezo na kanuni zinazolenga kuhakikisha kuna ulinzi na usalama wakati na baada ya wa kampeni,” liliongeza shirika hilo.

Mahakama za Rwanda zilikataa rufaa kutoka kwa viongozi mashuhuri wa upinzani Bernard Ntaganda na Victoire Ingabire kuondoa hukumu za awali ambazo ziliwazuia kugombea.

Tume ya uchaguzi pia ilimzuia mkosoaji wa Kagame, Diane Rwigara, ikisema ameshindwa kutoa taarifa ya rekodi ya uhalifu inavyotakiwa, na hajaafikia kizingiti cha kupata sahihi 600 kutoka kwa raia.

Aliyechaguliwa na bunge mwaka wa 2000 baada ya kujiuzulu kwa Rais wa zamani Pasteur Bizimungu, Kagame ameshinda chaguzi tatu kwa zaidi ya asilimia 90 ya kura mwaka 2003, 2010 na 2017, huku akizoa karibu asilimia 99 ya kura katika kura za hivi karibuni.

Amesifiwa kwa kuimarika kwa uchumi wa Rwanda baada ya mauaji ya halaiki lakini anakabiliwa na ukosoaji kuhusu ukiukwaji wa haki na ukandamizaji wa kisiasa.

Taarifa hii imekusanywa na SAMMY KIMATU