Habari za Kitaifa

Waandamanaji walivyozuiwa kuvamia Ikulu ndogo za Mombasa, Nakuru wakilenga pia makazi ya wabunge

Na WAANDISHI WETU June 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WATU kadha wakiwemo maafisa wa polisi walijeruhiwa Mombasa wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024/2025.

Vurugu zilizuka wakati waandamanaji walipokuwa wakijaribu kuelekea katika Ikulu ya Mombasa, kupitia bustani ya Mama Ngina.

Maandamano yalipoanza mwendo wa saa tatu asubuhi na kuvutia maelfu ya watu jijini, yalikuwa ya amani na polisi hawakuingilia.

Hata hivyo, mambo yalienda mrama pale waandamanaji wapoonyesha nia ya kutaka kuenda Ikuluni.

Polisi walianza kwa kuwachapa kwa marungu, hali iliyosababisha waandamanaji kutawanyika. Hata hivyo, walikusanyika tena baadaye ndipo wachache kati yao wakaanza kuzozana na polisi.

Mjini Nakuru mwendo wa saa kumi jioni, polisi walipambana kiume kuzuia waandamanaji waliokuwa wanataka kuingia katika Ikulu ndogo.

Raia waliwarushia polisi mawe huku polisi wakijibu kwa kufyatua vitoa machozi, na milio ya risasi pia ilisikika hewani wakati wa rabsha hizo.

Waandishi wetu walihesabu polisi wasiopungua watano wakisaidiwa na wenzao baada ya kupata majeraha, huku raia kadha pia wakisaidiwa na wahudumu kutoka Shirika la Kenya Red Cross kuenda kupokea matibabu.

Katika Kaunti ya Kilifi, maandamano yalishuhudiwa mjini Kilifi na Malindi ambapo mamia ya wakazi walijitokeza.

Mjini Malindi, polisi walilazimika kufyatua vitoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji walioanza fujo.

“Kulikuwa na vijana wachache waliokuwa wakisumbua watu lakini tulifanikiwa kutuliza hali,” akasema mmoja wao aliyejitambulisha kama Peter Pogba.

Waandamanaji Taita Taveta walitatiza usafiri katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi kwa muda wakitaka pingamizi zao dhidi ya Mswada wa Fedha lisikike.

Maandamano zaidi yalishuhudiwa Kaunti za Lamu, Tana River na Kwale ambapo wito ulikuwa uo huo mmoja wa kupinga Mswada wa Fedha.

Katika Kaunti ya Kwale, walioandamana walijaribu kuvamia afisi ya Mbunge wa Msambweni, Bw Feisal Bader, lakini wakazuiwa na polisi.

Ripoti za Jurgen Nambeka, Brian Ocharo, Nehemiah Okwembah, Maureen Ongala, Kalume Kazungu, Lucy Mkanyika, Siago Cece na Stephen Oduor