Wacha jeshi lisaidie polisi kupambana na waandamanaji, mahakama yaamua
MAHAKAMA Kuu leo Alhamisi imehalalisha uamuzi Maafisa wa Kijeshi (KDF) kusaidia Kikosi Polisi kudumisha amani kufuatia maandamano ya kupinga mswada wa Fedha 2024/2025 yaliyopelekea zaidi ya watu 50 kufariki na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali.
Jaji Lawrence Mugambi alikataa kuamuru maafisa wa KDF warudi katika kambi zao na kuwataka wazingatie sheria wanaposaidia polisi kudumisha amani chini ya uongozi wa Inspekta Jenerali Japhet Koome.
Jaji Mugambi alisema uamuzi wa Waziri wa Usalama Aden Duale kupeleka maafisa wa KDF kusaidia polisi kudumisha amani ulifaa.
Wakati wa maandamano hayo ya siku tatu, maduka yaliporwa na biashara kusambaratishwa.
Watu zaidi ya 300 walijeruhiwa wakati wa makabiliano ya waandamanaji na polisi katika kaunti 35 ambapo maandamano hayo yalishamiri.
Jaji Mugambi alisema uamuzi huu ulisababishwa na hatua ya waandamanaji kuwashinda nguvu polisi na kuvamia Bunge la Kitaifa na Afisi ya Jaji Mkuu na kusababisha uharibifu mkubwa.
Hata hivyo, alimwamuru Bw Duale achapishe katika Gazeti rasmi la Serikali upeo, muda na maeneo ambayo wanajeshi hawa watasaidia maafisa wa polisi.
Jaji Mugambi alisema ijapokuwa Bw Duale alichukua hatua mwafaka, ilimpasa kwanza awasilishe suala hilo katika Bunge kupata idhini.
Jaji huyo alikubaliana na tetezi za chama cha wanasheria nchini LSK kwamba kuweko kwa maafisa wa KDF wakidumisha amani “kunaweza kueleweka kwamba Kenya ni Nchi inayotawaliwa na Jeshi.”
Jaji Mugambi alisema lazima Serikali ifuate sheria kila mara.
“Hii mahakama imejipata katika njia panda katika kuhakikisha kwamba haki imetendeka. Kwa upande mmoja lazima ihakikishe haki za wananchi za kuandamana zimedumishwa na upande mwingine lazima ihakikishe nayo sheria imefuatwa na kila mmoja,”alisema Jaji Mugambi.
Mahakama ilisema ni jukumu la serikali kulinda maisha ya wananchi pamoja na mali zao.
Pia ilisema lazima nao wananchi wajue wakitekeleza haki zao lazima wadumishe sheria na wasiharibu mali katika jina la kufurahia haki zao.
“Ijapokuwa hii mahakama imeipa serikali fursa ya kutumia maafisa wa KDF kusaidia polisi, iko huru wakati wowote kuharamisha uamuzi wa Bw Duale na kuamuru maafisa wa KDF warudi katika kambi zao,” Jaji Mugambi alisema.
LSK iliwasilisha kesi ikiomba mahakama kuu ifutilie mbali uamuzi wa Bw Duale kuamuru majeshi yasaidie polisi kupambana na waandamanaji wanaopinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024/2025.
LSK ilieleza mahakama ni ukiukaji wa sheria kuamuru maafisa wa kijeshi (KDF) kuungana na polisi kudhibiti hali ya usalama.
Katika mawasilisho yake rais wa LSK Faith Odhiambo alisema hatua ya Bw Duale inakinzana na sheria.
Bi Odhiambo alisema maafisa wa KDF wanaweza tu kuagizwa wadhibiti hali iwapo kuna hatari kwa usalama nchini ama kutokana na uvamizi kutoka nje au wakati wananchi wamekaidi sheria na kutisha hali ya usalama.
Pia Bi Odhiambo alisema Bw Duale alichapisha katika Gazeti rasmi la Serikali uamuzi huo kabla ya kupata idhini ya Bunge.
Ili kujifahamisha na utaratibu wa kuruhusu KDF kuingilia masuala ya usalama wa ndani, Jaji Mugambi alimtaka wakili wa Serikali Emmanuel Mbita amfafanulie kwa kina suala hilo.
Jaji Mugambi alimtaka Bw Mbita aeleze sababu za Bw Duale kuagiza maafisa wa KDF wasaidie polisi kudhibiti usalama
Bw Duale aliamuru KDF iingilie baada ya waandamanaji kuvamia bunge Jumanne wiki hii na kutisha kuvamia Ikulu ya Nairobi kufanya mashauri na Rais William Ruto.
Jaji Mugambi alifahamishwa na LSK kwamba Kifungu cha Katiba nambari 241 kimetoa sababu za KDF kuingilia masuala ya usalama
“KDF inaweza kuuliza kusaidia ikiwa kuna dharura, mkasa wa kitaifa ama utovu wa usalama,” Bi Odhiambo alimweleza Jaji Mugambi.
Alisema Duale alitumia kifungu cha Katiba nambari 241(b) ambacho kinaruhusu KDF kusaidia kisha aripoti kwa Bunge la Kitaifa.
Kuhusu kifungu nambari 241(c) cha Katiba, KDF inapasa kuingilia kurejesha hali ya usalama baada ya kuruhusiwa na Bunge.