Viongozi wa kidini waomba vijana msamaha kwa kukosa kuwapa mwongozo
VIONGOZI wa kidini kutoka Uasin Gishu, wameomba msamaha Vijana wa Kenya kufuatia matukio ya hivi majuzi ya ukatili na mauaji wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa ushuru wa mwaka wa 2024.
Chini ya mwavuli wa Eldoret Gospel Ministers Association, wahubiri hao walijuta kuwa ilichukua muda mrefu kwa viongozi kusikiliza masuala halali ya vijana kuhusu mswada huo hadi kufikia kiwango cha maafa na uharibifu ulioshuhudiwa nchini.
Walisema maandamano hayo yamewafundisha viongozi wa dini na serikali kutopuuza kilio cha vijana.
“Kwa niaba ya wachungaji na viongozi wengine wa dini nchini na hata serikali ya Kenya Kwanza kwa jumla, tunawaomba radhi vijana wetu kwa kushindwa kuwapa mwongozo sahihi na kusikiliza masuala yao kwa wakati. Ni kweli kwamba kanisa na serikali kwa njia moja au nyingine zimefeli vijana wetu,” akasema Askofu Wilson Kurui, mlezi wa Jumuiya ya Wahudumu wa Injili ya Eldoret.
Askofu Kurui alikariri haja ya wachungaji na viongozi wengine wa kiroho kutowapa wanasiasa majukwaa ya kuwahutubia waumini makanisani na akawaonya dhidi ya kushawishiwa na fedha za wanasiasa.
“Kama makanisa lazima tuwachukulie wanasiasa kama washiriki wengine wowote wa makanisa yetu. Ni lazima tuache utamaduni huu wa kuwapa wanasiasa madhabahu yetu kueleza ajenda zao za kisiasa. Sio Kibiblia kutangaza matoleo yanayotolewa na wanasiasa hadharani,” akasema Askofu Kurui.
Alisema ujumbe wa vijana wakati wa maandamano umesikika kwa nchi nzima na ni wakati wa kuweka mazingira mazuri kwa vijana kushiriki katika masuala ya utawala na uongozi pamoja na kufanya maamuzi muhimu katika nyanja zote.
“Ujumbe kutoka kwa vijana wetu umetufikia, rais William Ruto na viongozi wengine wote wamesikia, kuanzia sasa lazima tuwasikilize vijana wetu kuanzia nyumbani. Ni lazima tuwape vijana fursa ya kutoa maoni yao katika masuala yote yanayohusu jamii,” akasema Askofu Kurui.
Aliitaka serikali kuweka mikakati ya kupunguza umaskini nchini ili kuwawezesha vijana kiuchumi.
Maoni sawa na hayo yalitolewa na askofu David Ndiema ambaye aliwataka vijana kufika makanisani kesho ili kupewa ushauri nasaha kutokana na madhara ya maandamano.