Simanzi yatanda Idara ya Mahakama wakiomboleza ‘mchapakazi’ Jaji Majanja
WINGU la simanzi lilitanda katika idara ya mahakama kufuatia kifo cha ghafla cha Jaji David Majanja Julai 10, 2024 katika hospitali moja Nairobi.
Majaji wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome, mawakili na watu wa tabaka mbali mbali waliambia Taifa Leo kwamba “kifo cha Jaji Majanja ni pigo kuu kwa idara ya mahakama.”
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Jaji Koome alisema “Jaji Majanja alikuwa mtumishi wa umma aliyejitolea mhanga.”
Jaji mkuu huyo alisema Jaji Majanja alienzi utekelezaji wa haki na udumishaji sheria.
“Idara ya mahakama itashirikiana na familia ya Jaji Majanja katika mipango ya mazishi,” alisema Jaji Koome.
Pia, alisema idara ya mahakama itatangaza siku ya kumuomboleza Jaji Majanja.
“JSC itatangaza siku ya kufunga mahakama kuwezesha wahudumu wote wa mahakama kuhudhuria maombi ya Jaji Majanja,” Jaji Koome alidokeza katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Jaji Majanja aliyekuwa mkwasi na mwenye tajriba ya juu katika masuala ya sheria alienziwa na majaji wenzake na mawakili kuwa mwadilifu katika utendakazi wake.
Jaji Majanja aliyekuwa Kamishna katika tume ya kuajiri watumishi idara ya mahakama (JSC) aliyeteuliwa Jaji Mahakama Kuu 2011 alihudumu katika Mahakama Kuu za Nairobi, Homa Bay, Migori, Kisumu na Kisii.
Alihudumia Mahakama kwa miaka 13 ambayo majaji na mawakili walimenzi na kumtunuku sifa kedekede.
Watumishi katika Idara ya -Civil Division High Court- alikohudumu Jaji Majanja iliongozwa kumuomboleza Jaji Majanja na kinara wake- Jaji Christine Meoli alisema idara yote ya mahakama imepigwa na butwaa kuu kufuatia kifo cha jaji huyo aliyekuwa kiungo muhimu.
“Nachukua fursa hii kuwaeleza kwamba mmoja wa majaji katika idara hii ya Civil Division-Jaji David Majanja, ameaga,” Jaji Meoli aliwaeleza majaji, makarani na wanahabari waliohudhuria hafla hiyo ya dharura.
Jaji Meoli aliyeandamana na Jaji Joe Omido na Jaji Julius Nang’ea walituma risala za rambi rambi kwa familia ya marehemu, majaji wenzake, marafiki, na idara yote ya mahakama.
Jaji Meoli alitia sahihi kitabu cha risala za rambi rambi katika ukumbi wa Mahakama Kuu, Milimani Nairobi.
Pia, alisema mahakama kuu zote nchini zitaweka mipango ya kumuenzi na kumuomboleza Jaji Majanja ambaye sifa za msimamo wake wa kutoa maamuzi ya haki zimeenea kote.
Katika sekta ya uanasheria wakili mkongwe mwenye tajriba ya juu katika masuala ya sheria Dkt John Khaminwa, Danstan Omari, Shadrack Wambui, Pauline Kiteng’e, Aldelaide Kwamboka na Suyianka Lempaa walimtunuku sifa tele Jaji Majanja wakisema “alikuwa shupavu na mkakamavu katika utenda kazi yake.”
Jaji Majanja alitoa maamuzi yaliyotikiza misingi ya sheria kama ule wa kufutilia mbali Sheria ya Ushuru wa Nyumba (housing levy) Novemba 2023).
Katika uamuzi huo Jaji Majanja, Jaji Meoli na Jaji Lawrence Mugambi walisema sheria hii ya kodi ya nyumba inakizana na Katiba.
Majaji hao waliipiga kalamu sheria hiyo ya Kodi ya Nyumba na kuiharamisha kabisa.
Majaji hao waliikosoa na kusema mamlaka ya ushuru nchini (KRA) haipasi kupokea pesa kutoka kwa Wakenya kwa vile hakuna bodi iliyoteuliwa kushughulikia suala la ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
Mawakili wakiongozwa na Dkt John Khaminwa, Danstan Omari, Shadrack Wambui, Pauline Kiteng’e na Aldelaide Kwamboka walimtunuku sifa tele Jaji Majanja wakisema “alidumisha haki na sheria katika maamuzi yake.”
Dkt Khaminwa alimhenzi Jaji Majanja akisema “maamuzi yake yalizingatia Katiba na aliinukuu katika maamuzi yake yote.”
“Nchi hii inahitaji majaji kama Jaji Majanja ambaye alikuwa shupavu na mkakamavu katika utenda kazi wake,” Dkt Khaminwa alisema Alhamisi katika Mahakama kuu ya Milimani alipohutubia wanahabari.