Pigo tena kwenye Idara ya Mahakama Jaji Ogembo akiaga dunia
IDARA ya Mahakama ipata pigo tena baada ya kumpoteza jaji wa pili ndani ya wiki mbili.
Marehemu Jaji Daniel Ogembo, alipatikana Jumatano, Julai 17, 2024 akiwa ameaga dunia katika makazi yake rasmi mjini Siaya.
Alitarajiwa kuongoza kikao asubuhi katika majengo ya Mahakama Kuu ya Siaya lakini akakosa kujitokeza hali iliyoibua shaka.
Jaji Ogembo amehudumu kwa miaka miwili katika Mahakama Kuu ya Siaya alipokuwa jaji mkazi.
Kamanda wa Polisi, Kaunti ya Siaya, Cleti Kimaiyo, alithibitisha kifo chake na kusema polisi na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.
“Tutawafahamisha kuhusu matokeo, bado tunachunguza kiini cha kifo chake,” alisema mkuu wa polisi kaunti hiyo.
Kulingana na afisa mmoja wa mahakama aliyechelea kutajwa kwa sababu ya uzito wa suala hilo, Jaji Ogembo alipatikana akiwa mfu asubuhi baada ya kukosa kujibu dereva wake alipokwenda kumchukua nyumbani kwake.
“Dereva alimpeleka nyumbani Jumanne jioni lakini aliporejea asubuhi, jaji hakujibu hali iliyofanya dereva kuripoti kwa maafisa katika korti ya Siaya,” alisema afisa huyo wa ngazi ya juu.
Kifo cha Jaji Ogembo kililemaza vikao vya korti huku wafanyakazi wakikumbwa na mshtuko kufuatia habari hizo.
Kifo cha Jaji Ogembo kimetokea hata kabla ya wiki kuisha baada ya Jaji David Majanja kufariki dunia.
Mwezi uliopita, Hakimu Mkuu wa Korti ya Makadara, Monicah Kivuti, aliuawa kwa kupigwa risasi na afisa mkuu wa polisi kutoka kituo cha Londiani.