Tumeachia ODM watengeneze uchumi, na wasithubutu kuongeza ushuru – Moses Kuria
ALIYEKUWA Waziri wa Utumishi wa Umma, Moses Kuria amedai kuwa Rais William Ruto aliwateua washirika wa kinara wa Azimio Raila Odinga kusimamia wizara zinazokabiliwa na changamoto.
Akizungumza hadharani kwa mara ya kwanza tangu Rais Ruto abadilishe baraza la mawaziri kufuatia wiki kadhaa za maandamano ya vijana, Bw Kuria alikejeli mabadiliko hayo akisema washirika wa Bw Odinga walioteuliwa katika baraza la mawaziri watakabiliwa na kibarua kigumu watakapoidhinishwa.
Alizungumza katika eneo la Kalimbini kaunti ya Makueni wakati wa mazishi ya Naleous Mwende ambaye alikuwa mke wa mfanyabiashara James Mbaluka.
Ingawa ni miongoni mwa mawaziri 11 waliofutwa, Bw Kuria alijitambua kama kiongozi wa serikali ya Kenya Kwanza.
“Kama Serikali, tulifanikisha mengi lakini pia tulishindwa katika baadhi ya maeneo. Katika Kaunti ya Makueni, kwa mfano, gavana amekuwa akiniomba nihakikishe kuwa kaunti inapata sehemu ya mapato ya shaba na madini mengine yanayochimbwa hapa lakini sikuwa na jibu. Gavana, mtafute (waziri mteule wa madini Hassan) Joho ili kupata jibu,” Bw Kuria alisema.
“Takriban Wakenya milioni 12 wamekopa kutoka Hazina ya Hasla lakini wakakataa kulipa. Tulijaribu kuwasaka lakini hatukuweza. Tulimtafuta Wycliffe Oparanya na kumwambia kwamba anaonekana kuwa na uwezo wa kutusaidia kurejesha pesa hizo. Katika eneo la Mlima Kenya, tumekuwa tukikabiliwa na changamoto na wakulima wa kahawa kwa sababu vyama vya ushirika vimekataa kuwalipa wakulima. Kama utawala wa Kenya Kwanza tulijaribu kutatua tatizo hilo bila mafanikio. Tulimtafuta Bw Oparanya aje atusaidie kushughulikia masaibu ya wakulima wa kahawa. Mlipiga kelele kuhusu gharama ya juu ya mafuta. Tuliposhindwa kushughulikia tatizo hilo tulienda Ugunja kumchukua Opiyo Wandayi. Tulimwambia atupe fomula ya kupunguza gharama ya mafuta,” aliongeza.
“Jambo lenye changamoto kubwa ambalo serikali ilikabiliana nalo lilikuwa la ushuru. Kwa kukabiliwa na madeni, tulijaribu kuongeza ushuru kujenga nyumba, kutoa huduma za afya na mipango ya elimu. Ilikuwa ni changamoto kubwa. Tulikwenda Suba na kumchukua John Mbadi. Tulimwambia aje atupe fomula ya kuendesha programu za serikali ili ushuru ukiongezeka tumuulize” Bw Kuria alisema.
Bw Kilonzo Jnr na Bw Maanzo waliushambulia serikali ya Kenya Kwanza wakiishutumu kwa utawala mbaya. Alikosoa mawaziri wateule wa Rais Ruto huku akilaani vikali ukatili wa polisi dhidi ya waandamanaji.
“Kwa jinsi ninavyokaribisha amani na serikali kuu ya mseto, nimebaki na maswali. Je! watoto wadogo walilazimika kufa ili wazee waingie serikalini? Je, watu walilazimika kuzamishwa majini ili watu wawe serikalini? Sielewi. Tunaweza kuwanyamazisha vijana kwa bunduki, lakini hawatasahau kamwe. Ni lazima tuiambie serikali hii; Mumewaangusha vijana wa nchi hii. Watu mliowachagua kujiunga na serikali ni wazee. Wengine ni wazee sana. Inasikitisha,” alisema.