Habari za Kitaifa

Oparanya: Tulioteuliwa mawaziri bado tutasalia waaminifu kwa ODM

Na BRIAN OCHARO July 29th, 2024 2 min read

WAZIRI mteule wa Vyama vya Ushirika na Biashara ndogo ndogo Wycliffe Oparanya amesema kuwa viongozi wakuu wa upinzani walioteuliwa kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza hawajagura vyama vyao.

Bw Oparanya, ambaye pia ni Naibu kiongozi wa Chama cha ODM, alifafanua kuwa wanachama wa chama hicho watakaojiunga na serikali ya Rais William Ruto baada ya kuidhinishwa na bunge la taifa, watahudumu kwa nyadhifa zao binafsi huku wangali wakionyesha uaminifu wao kwa chama.

“Haimanishi kuwa tumekiacha chama chetu cha ODM, sisi bado ni wanachama wa chungwa lakini tunatumikia serikali katika nyadhifa zetu. Lakini sijapigwa msasa kwa hivyo nisingependa kuzungumzia hilo,” akasema Bw Oparanya.

Gavana huyo wa zamani wa Kakamega, hata hivyo, alitetea uamuzi wa upinzani kuhudumu katika serikali ya Kenya Kwanza, akisema walifanya hivyo kuitikia wito wa Rais Ruto wa kuunda serikali ya muungano.

Alisisitiza kuwa kila Mkenya, wakiwemo wale wa mrengo wa upinzani, wana haki ya kikatiba ya kutumikia nchi katika wadhifa wowote, mradi tu wana sifa zinazohitajika.

“Sisi ni Wakenya, na hii ni nchi yetu; kila mtu aliye na elimu na ujuzi anastahili kuhudumu katika serikali yoyote. Mnakumbuka Rais alitamka wazi kuwa anaunda serikali ya muungano, kwa hiyo serikali hiyo itawashirikisha viongozi wa upinzani,” akasema.

Bw Oparanya alikuwa akizungumza mjini Mombasa mnamo Jumamosi wakati wa mkutano na jamii ya Waluhya wanaoishi Mombasa  chini ya kikundi cha Wereca Real Focus.

Wereca Real Focus ni kikundi kilichoundwa katika Kaunti ya Mombasa kwa lengo la kuwaunganisha Waluhya wanaoishi Mombasa ili kusaidiana, kubadilishana mawazo ya kiuchumi, na kutiana moyo kuhusu uwekezaji na vyama ya wanawake.

Huku akiahidi kuwa atasaidia kundi hilo, Bw Oparanya alishukuru kwamba jamii hiyo imetambua umuhimu wa kujiimarisha ili kubuni ajira, na kukabiliana na umaskini.

“Ili kikundi kiweze kustawi na kuinua jumuiya yetu, lazima wajitose katika biashara; ajira pekee haiwezi kutosha. Hata kama umeajiriwa, ni muhimu kuwa na biashara ya kando ambao inaweza kukusaidia na wengine katika jamii,” alisema.

Bw Oparanya, ambaye alisisitiza kwamba bado yuko katika ODM. Aliahidi kuwa chama hicho hakitasita kutoa wito wa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka maafisa wa polisi walioua na kuwajeruhi waandamanaji, pamoja na kupigania fidia kwa familia za waathiriwa.

“Mimi bado ni naibu kiongozi wa chama cha ODM, na ni kweli kwamba huu ndio msimamo wetu. Tumekuwa na maandamano na watu wetu wengi wameuawa na kulemazwa. Ni muhimu kwamba wale ambao wamepoteza maisha yao walipwe fidia ikiwa tunataka kupata amani,” alisema.

Kundi hilo la Wereca Real Focus, kupitia kwa Meneja wa eneo la Pwani Jonathan Wepukhulu, lilikaribisha uteuzi wa Bw Oparanya kuhudumu katika serikali ya Rais Ruto, likisema kuwa anafaa kwa kazi hiyo.

“Tunafurahi kama Wereca kwa sababu uteuzi wake unastahili. Amehudumu kama gavana na kufanya kazi nzuri. Ujuzi na uzoefu wake katika utawala utasaidia kuipeleka nchi hii mbele. Tunamtakia kila la heri anapoungana na wenzake kuleta mageuzi katika nchi hii,” akasema Bw Wepukhulu.