Hayo maandamano yenu ya Agosti 8 hatutaki kuyasikia, Supkem yaambia Gen Z
BARAZA Kuu La Dini ya Kislamu (SUPKEM) limetoa wito kwa vijana wasitishe maandamano ambayo wanapanga kufanya Alhamisi, Agosti 8 wiki hii na badala yake waipe serikali jumuishi nafasi ya kutimiza ahadi iliyotoa kwa raia.
Vijana wa kizazi cha Gen Z wanapanga kuandaa kile wanachosema kitakuwa ni maandamano makubwa nchini maarufu kama ‘Nane Nane’ wakilenga kusukuma utawala wa sasa uondoke mamlakani ni pia uwajibikie matakwa yao.
Mitandaoni, wito huo tayari unaendelea kushika kasi huku vijana kutoka kaunti mbalimbali wakitarajiwa Nairobi kwa shughuli hiyo wanayodai ni ya kupigania haki.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Supkem Hassan Ole Naado amesema kuwa vijana hao wanastahili kusitisha maandamano yao na watoe nafasi kwa baraza jipya la mawaziri lifanye kazi.
“Nimekuwa nikifuatalia jinsi mchakato wa kupigwa msasa kwa mawaziri unavyoendelea na nimeshawishika kuwa maswali yanayoulizwa yanahusu yale ambayo Wakenya wamekuwa wakiyapigania,” akasema Sheikh Ole Naado.
“Nawaomba vijana wazime maandamano yao na watoe nafasi kwa baraza la mawaziri lifanya kazi yake. Maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika yameishia mauti na uharibifu wa mali na ni wakati ambapo hilo linastahili kukoma,” akaongeza Sheikh Ole Naado.
Aliongeza kuwa kama Supkem wameamua kuunga mkono utawala wa sasa ambao unajumuisha wandani wa Rais William Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga.
Ingawa hivyo, kama Supkem watakuwa wakifuatilia kile ambacho kila waziri ameahidi na kuhakikisha kuwa wanatimiza walichosema wakati wa mahojiano.
“Hatusemi tu kuwa tunawaunga mkono bali pia tutakuwa tukifuatilia kuhakikisha wanatimiza ahadi walizotoa kwa raia. Wale wazembe ambao watalewa mamlaka na kusawahau Wakenya, tutawafichua,” akasema Bw Ole Naado akionyesha imani kuwa mawaziri wote wataidhinishwa.
Wiki jana, Supkem ilijiondoa katika kesi ya kuwatimua mamlakani Rais William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua. Kesi hiyo iliwasilishwa na mwanaharakati Cyprian Nyamwamu, Khelef Khalifa, Janet Muthoni, Paul Rukaria, Fred Ogolla na wengine sita.
Kwenye kesi hiyo wahusika waliwataka Rais Ruto na Bw Gachagua wajiondoe mamlakani kwa kushindwa kutimiza wajibu wao wa uongozi bora kwa Wakenya tangu wachaguliwe mnamo 2022.
Walisema kuwa uongozi wa nchi nao pia umekiuka katiba huku wakitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) iamrishwe na mahakama kuandaa kura ya maamuzi.
Kura hiyo inastahili kuandaliwa kuamua iwapo rais na naibu wake wanaweza kuondolewa mamlakani kwa msingi wa kukiuka katiba, kutumia mamlaka yao vibaya na kupoteza imani ya umma.