Habari za Kitaifa

Kenyatta kukohoa, atarajiwa kuitisha mkutano wa vinara wa Azimio


RAIS Mstaafu, Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuitisha mkutano na vyama tanzu vya Muungano wa Azimio la Umoja – One Kenya, kufuatia hali ya wasiwasi inayoendelea katika muungano huo wa upinzani, kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema.

Akiwa mwenyekiti wa muungano huo, Bw Kenyatta anatarajiwa kuita vinara wenza kutoa mwelekeo na kudhibiti hali ya wasiwasi katika muungano huo kufuatia kubuniwa kwa Serikali Jumuishi.

“Tunatarajia Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ambaye ni mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio la Umoja aitishe mkutano ili tuweze kujadili kwa uwazi masuala yanayotikisa muungano,” Bw Musyoka alisema.

Muungano huo umeonekana kuporomoka baada ya chama ODM cha Bw Raila Odinga kuamua kushirikiana na Rais William Ruto na baadhi ya viongozi wa chama chake kuwa mawaziri.

Mkutano huo unatarajiwa kujiri huku vinara wenza wakionekana kutofurahishwa na hatua ya Bw Odinga ya kuunga mkono serikali ya Kenya Kwanza.

Kwa hivyo, mkutano na Bw Uhuru unapaniwa kuokoa Azimio au kilichosalia kuhusu muungano huo.

Tayari, kiongozi wa Chama cha Narc-Kenya Martha Karua ametoa notisi ya kujiondoa Azimio.

Hatua hiyo ilijiri huku mvutano ukiongezeka kati ya baadhi ya viongozi wa Azimio baada ya Rais Ruto kuteua viongozi wa chama cha ODM kuwa mawaziri.

Kiongozi wa Chama cha Wiper alisema kuwa misukosuko ni ya “kawaida” katika muungano wowote wa vyama vya kisiasa na kwamba Azimio la Umoja bado ni imara.

“Si rahisi kamwe kusimamia miungano. Azimio la Umoja haiwezi kuepuka hali kama hiyo. Lakini inapotokea, inatupatia fursa ya kujadiliana zaidi,” akasema Bw Musyoka, na kueleza kuwa ni katika hali kama hiyo ambapo wahusika huelewana vyema.

Hata hivyo, alisema, “Chochote kinawezekana. Na kuanzia sasa na kwenda mbele, hatupuuzi uwezekano wowote. Tuko tayari pia kwa changamoto yoyote,” kauli ambayo inaonekana kuashiria uwezekano wa Azimio la Umoja kuvunjika iwapo hakutakuwa na muafaka.

Bw Kalonzo alikuwa akizungumza Alhamisi, Agosti 15, 2024 wakati wa Kongamano la Vijana la Oslo Centre Africa ambapo alizungumza kuhusu maandamano ya kupinga serikali yaliyoongozwa na vijana, Gen Z, akisema yalifanikiwa na kuhimiza vijana wajumuishwe katika mazungumzo ya kitaifa.

Pia, alitoa wito wa haki kwa wahasiriwa wa maandamano wakati wa mkutano ulioleta pamoja watetezi wa vijana, viongozi wa serikali, wataalamu kutoka bara zima kushughulikia maswala yanayowakabili vijana Afrika, kubadilishana maarifa na kutafuta suluhu za kiubunifu kwa maendeleo endelevu.