Habari za Kitaifa

Tayarisheni watoto wafike shuleni mapema, serikali yaomba wazazi

Na CHARLES WASONGA August 25th, 2024 2 min read

DAKIKA chache baada ya Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kufutilia mbali mgomo wa walimu Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba amewataka wazazi, na walezi, kuhakikisha kuwa watoto wao wanaripoti shuleni bila kuchelewa.

Bw Migos alikuwa mwepesi kusifu hatua hiyo ya Knut kuondolea mbali mgomo huo ambao ungevuruga shughuli za masomo shuleni akitaja kitendo hicho kama cha kizalendo.

“Tunatoa shukrani kubwa kwa walimu wetu na viongozi wao kwa kuweka kando ubinafsi na kukumbatia uzalendo na kuyapa kipaumbele masilahi ya wanafunzi wetu,” waziri akasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Waziri Migos aliwahakikishia walimu wanachama wa Knut kwamba serikali imejitolea kutimiza matakwa yao yote licha ya kukumbwa na changamoto ya uhaba wa fedha.

“Kwa mfano kufuatia mazungumzo kati ya Tume ya Huduma za Walimu (TSC) na Knut, serikali imeahidi kutelekeza awamu ya pili ya Mkataba wa makubaliano ya pamoja (CBA) ya 2021-2025 kuanzia Julai 1, 2024,” akaeleza.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Upili (KESSHA) Willy Kuria amewahakikishia wazazi kwamba usalama na masilahi ya wanafunzi watakaoripoti shule yatalindwa wakiwa katika taasisi hizo.

“Kwa hivyo, wazazi na walezi wanashauriwa kuwaandaa wanafunzi kwa ufunguzi wa shule kwa muhula wa tatu kuanzia Jumatatu Agosti 26, 2024,” akaeleza Bw Kuria ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Murang’a.

Mwenyekiti huyo ametoa hakikisho hilo baada ya Chama cha Kutetea Masilahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (KUPPET) kutangaza kuwa mgomo wa wanachama wao utaanza Jumatatu Agosti 26, 2024.

.“Wanachama wa Baraza la Kitaifa la Uongozi (NGC) katika mkutano wa leo (Jumapili) wamesema hatua hiyo ya TSC haitoshi. Hii ndio maana wamepiga kura ya kutoa nafasi mgomo kuanza Jumatatu Agosti 26, 2024,” akasema Katibu Mkuu Akelo Misori.

Idadi kubwa ya walimu wa shule za upili ni wanachama wa Kuppet.

Hii ina maana kuwa shughuli za masomo katika taasisi hizo zitavurugika walimu hao wakitii agizo la chama hicho na kususia kazi.

Wiki jana, Tume ya Huduma za Walimu (TSC) ilitangaza kuwa imetoa Sh13.3 bilioni za kufadhili utekelezaji wa awamu ya pili ya CBA ya wanachama wa Kuppet.

Lakini viongozi wa chama hicho walitaka hatua hiyo kama ambayo haitoshi.