Makala

Tuongee kiume: Kaka, unaweza kuagizwa kutunza mtoto wa kimada wako

Na BENSON MATHEKA September 25th, 2024 2 min read

WAZAZI wanapotengana au kukosana huwa wanakimbia kortini kuomba agizo waume au wake zao walazimishwe kutunza watoto.

Baadhi huwa hawafahamu kuwa mahakama inaweza kukataa kutoa agizo wanaloomba wakikosa kuthibitisha kuwa wanaoshtaki hawawajibikii jukumu lao la ulezi.

Kulingana na sheria ya watoto ya Kenya, ni jukumu la pamoja la wazazi wote wawili kumtunza mtoto ima wawe wameoana au la.

Hivyo basi,  mtu hawezi kuhepa jukumu la kutunza mtoto anayezaa nje ya ndoa.

Pia,  ni jukumu la pamoja la wazazi wote wawili kulea mtoto wawe wanaishi pamoja au la. Hii inamaanisha kuwa mtu hawezi kuepuka jukumu la ulezi kwa kutengana na mume au mkewe.

Hata kesi ikiendelea kortini wazazi wakitengana, mtu anaweza kuagizwa kukimu mahitaji ya mtoto.

Mahitaji haya yanajumuisha malazi, elimu, matibabu, chakula, mavazi, na mengine yoyote yanayotokea kuhusu mtoto.

Agizo la kukimu huwa linaelekeza mtu kuwa akitoa kiasi fulani cha pesa kwa kipindi fulani  kufadhili mahitaji ya kimsingi ya mtoto kwa masharti ambayo mahakama inaweza kuamua yanafaa.

Agizo hili linaweza kutolewa hata kesi ya talaka inapoendelea mahakama ikiaminishwa kuwa mmoja wa wazazi ametelekeza jukumu lake la ulezi.

Mahakama inaweza kutoa agizo kwa mtu kutunza mtoto wa kambo ambaye alichukua kuwa wake kwa msingi wa kuoa mama yake.

Agizo la kukimu mahitaji ya mtoto huwa linatolewa baada ya mahakama kuthibitishiwa kuwa anayetakiwa kufanya hivyo ana uwezo.

Mahakama inazingatia hali kadhaa ikiwa ni pamoja na  uwezo wa mapato, mali na rasilimali nyingine za kifedha za wazazi husika, mahitaji ya kifedha, wajibu, au majukumu ambayo kila mhusika anayo au anaweza kuwa nayo katika siku za usoni, ulemavu wowote wa kimwili au kiakili, ugonjwa au hali ya kiakili ya mtoto na jinsi mtoto anavyoelimishwa.

 Mahakama inaweza kubadilisha makubaliano ya wazazi kuhusu jinsi ya kukidhi mahitaji kwa manufaa ya mtoto husika.

Inachofanya mahakama ni kuangalia maslahi ya mtoto na kuhakikisha kuwa yanachukua kipaumbele katika kesi ya talaka au mvutano ukizuka mmoja wa wazazi akilalamika mwenzake ametelekeza jukumu la uzazi.

Kama nilivyotangulia kusema ulezi ni jukumu la pamoja na wazazi na iwapo mzazi anayelalamika ana uwezo wa kimapato kuliko anayeshtakiwa, ombi lake la kutaka alipwe pesa za kumtunza mtoto linaweza kukataliwa.