SHAMBULIO: Mitandao ya kijamii ilivyotumika kupasha ulimwengu habari
Na PETER MBURU
INTANETI Jumanne ilitumiwa pakubwa kufahamishana kuhusu uvamizi katika hoteli ya Dusit huku baadhi ya waliokuwa kwenye eneo hilo la Riverside, Nairobi, wakiitumia kuomba usaidizi.
Watu waliokuwa katika eneo hilo pamoja na wengine walitumia mitandao mbalimbali ya kijamii hasa Twitter, WhatsApp na Facebook kueleza matukio yaliyokuwa yakiendelea, wengine wakieleza namna walivyokuwa wamejificha ndani ya majengo wakihofia maisha yao.
Bwana mmoja kwa jina Ron Ng’eno alisambaza jumbe kadhaa akieleza namna alivyokuwa amejificha chooni, na kueleza namna alivyohofia maisha yake.
“Niko eneo la 14 Riverside Drive na nimejificha ndani ya bafu na tumevamiwa,” Bw Ng’eno akatuma ujumbe mwendo was saa tisa na dakika 40 alasiri. “Nikifariki, nampenda Mungu na ninaamini nitaenda mbinguni, tafadhali ambieni familia yangu nawapenda, nakupenda Caleb, Mark na Carol,” akasema dakika nne baadaye.
“Tafadhalini fahamisheni ubalozi wa US humu nchini na idara ya polisi. Niko Riverside drive karibu na dusitd2. Kumetokea mlipuko mkubwa kisha milio ya risasi, sasa nimejificha chooni,” akasema dakika 16 baadaye.
Habari zilisema baadaye kuwa Bw Ng’eno aliokolewa.
Mtumizi mwingine wa twitter kwa jina Kebaya@armchairtycoon alisema: “Nimeponea shambulio la kigaidi eneo la Riverside. Miili imetapakaa kila mahali. Mabomu kila mahali.”
Geoffrey Njenga naye alichapisha: “14 Riverside imevamiwa. Tafadhali tusaidieni tunajificha. Tumevamiwa na magaidi.”