Habari za Kitaifa

Sababu ya viongozi wa Azimio kuzuiwa kuhubiri siasa kanisani Mlolongo

Na STANLEY NGOTHO September 30th, 2024 2 min read

VIONGOZI kadhaa wa upinzani Jumapili walizuiwa na polisi kuhudhuria ibada ya Kanisa mjini Mlolongo ambapo walilenga kuungana na mwanaharakati na ndugu wawili ambao walitekwa na kuachiliwa hivi majuzi.

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa DAP Kenya Eugene Wamalwa, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni na mwanasiasa Jimmy Wanjigi walizuiwa kuingia katika Kanisa la AIC Kasina, Mlolongo.

Wanasiasa hao walikuwa waungane na mwanaharakati Bob Njagi ambaye alitekwa nyara na kuachiliwa hivi majuzi. Bw Njagi aliachiliwa pamoja na nduguze Jamil na Aslam Longton baada ya kutowekamnamo Agosti 19 Mlolongo na Kitengela mtawalia.

Waliachiliwa Septemba 20 maeneo tofauti Kaunti ya Kiambu na juhudi za kushinikizwa kuachiliwa kwao zilishuhudia mahakama ikimhukumu aliyekuwa kaimu Inspekta Jenerali Gabriel Masengeli lakini hukumu hiyo ikafutwa baadaye.

Bw Musyoka na viongozi walioandamana naye walikuwa wenye nia ya kuandaa maombi na watatu hao na pia kushinikiza kunyakwa kwa polisi ambao wanashukiwa waliwateka nyara.

Hata hivyo, uongozi wa AIC Mlolongo na Kitengela ulifuta ziara zao kutokana na maagizo ya polisi na wakaachwa wakiwa wamekwama katika hoteli moja Kitengela kwa saa kadhaa.

Baadaye waliamua kuhudhuria ibada katika Kanisa la Kitengela Glorious huku polisi waliokuwa wamevalia kiraia wakijaa mjini Kitengela.

“Tulikuwa tuhudhurie ibada ya Kanisa AIC lakini tumekuja kufahamu kuwa vyombo vya usalama vya serikali vilitishia uongozi wa kanisa na ziara yetu ikafutwa,” akasema Bw Musyoka.

Kutokana na hilo, waliamua kutohutubia mikutano waliyokuwa wameipanga, Bw Musyoka akisema waliafikia hilo kuwazuia wakazi kupigwa au kunyanyaswa na polisi.

“Kuna maafisa wa polisi kila mahali kana kwamba sisi ni mahabusu wanaosakwa. Hatutanyamazishwa kwa kuikosoa serikali ya Rais William Ruto,” akasema makamu huyo wa rais wa zamani.

Bw Musyoka alishangaa kwa nini serikali ilikuwa ikiwanyima viongozi wa upinzani haki yao ya kuabudu na wakati uo huo kuwatumia polisi kuwateka nyara Wakenya ambao hawana hatia.

“Serikali lazima ichukue hatua kutokana na utekaji nyara ambao unaendelea. Gen Z walikomboa nchi hii na utawala wa Rais Ruto hauna mashiko tena kwa Wakenya, wanastahili wakome kuzua mgawanyiko,” akasema.

Bw Wamalwa naye alisema utawala wa sasa umekumbatia udikteta baada ya kukosa imani kutoka kwa Wakenya.

Alisema ni udikteta huo ndio umechangia baadhi ya Wakenya wanaoonekana kama mwiba kwa serikali kutekwa nyara.

“Ni hapa Kitengela ambapo serikali ya Ruto imewadhulumu Wakenya. Tunalaani dhuluma za polisi na tutahakikisha kuwa kesi za ukiukaji wa haki za raia zinawasilishwa katika mahakama ya kimataifa,” akasema.

Bw Kioni naye alisema kile ambacho Kenya Kwanza inajivunia ni kuleta mgawanyiko na kutokomeza utulivu ambao ulikuwa nchini.

“Ili nchi hii ipone kutokana na ukandamizaji wa polisi, Rais na watu wake wanastahili wajiuzulu,” akasema.

Akizungumza Bw Wanjigi alisema Kenya kwa sasa limegeuzwa taifa ambalo polisi wanatumiwa kuwanyanyasa raia huku serikali ikishabikia tu na kuendeleza unyanyasaji.

“Mimi hufuatwa na magari ambayo hayana alama na wamevuruga intaneti na masafa ili nisipige simu nikiwa nyumbani kwangu au hata kutazama runinga. Serikali hii ilipoteza uhalali wake wakati wa maandamano ya Gen Z na uchaguzi mpya unastahili kuandaliwa,” akasema Bw Wanjigi.

Bw Njagi aliwashukuru wageni wake na akazidiwa na hisia huku akiwashukuru Wakenya waliomwombea kwa siku 32 ambazo alitekwa nyara.

Viongozi wengine ambao waliandamana na wanasiasa hao wa upinzani ni Seneta wa Machakos Agnes Kavindu, Naibu Gavana wa Kajiado Martin Moshisho, Mbunge wa Kajiado Mashariki Kakuta Mai Mai, aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na madiwani kadhaa kutoka Kajiado na Machakos.