Habari za Kitaifa

Waititu adai amekamatwa kwa kusema ‘Gachagua akienda, Ruto pia amfuate’

Na SIMON CIURI, STEVE OTIENO September 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Kiambu Ferdinand Waititu Jumatatu alikamatwa kwa tuhuma za kutoa matamshi ya uchochezi.

Bw Waititu aliambia Taifa Leo kuwa polisi walimvamia akiwa eneo la Northern Bypass Kiambu kisha kumsafirisha hadi makao makuu ya Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) aandikishe taarifa.

Alisema alikuwa anashuku kukamatwa kwake ni kutokana na matamshi aliyoyatoa kanisani Jumapili ambapo alisema kuwa iwapo Naibu Rais Rigathi Gachagua atang’atuliwa, anastahili kuenda nyumbani na bosi wake Rais William Ruto.

“Jinsi tunavyozungumza nipo kwenye gari la polisi na tunaelekea makao makuu ya DCI. Ishara zote zinaonyesha ni kutokana na matamshi niliyoyatoa jana (Jumapili) Ruiru kuhusiana na kung’atuliwa kwa Naibu Rais.”

Kunyakwa kwake kunatokea siku moja baada ya Bw Waititu pamoja na wanasiasa wengine wa upinzani akiwemo Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kuzuiwa kuingia na kuabudu kwenye kanisa moja kule Kitengela.

Viongozi wengine ambao waliandamana na Bw Musyoka ni Kinara wa DAP K Eugene Wamalwa, Katibu wa Jubilee Jeremiah Kioni  na mwanasiasa Jimi Wanjigi.

Wanasiasa hao pia walilazimika kufuta mikutano ambapo wangehutubia umma Mlolongo na Kitengela. Bw Musyoka alisema walichukua hatua hiyo kuepusha raia na ukatili na kipigo cha polisi.

Kuhusu Bw Waititu, Wiper ilituma taarifa ikisema kuwa alikuwa amenyakwa na kutekwa kinyume cha sheria na watu ambao hawajulikani na walikuwa wakituhumiwa kuwa maajenti wa serikali.

Bw Musyoka pamoja na wabunge kadhaa wa Wiper walitarajiwa kufika katika makao makuu ya DCI kupambana ili Bw Waititu aachiliwe.

Pia walisema gavana huyo wa zamani anastahili kuruhusiwa aonwe na familia yake, wakili na daktari.

Wiper ilisema iwapo serikali ina tatizo na matamshi ya Bw Waititu inastahili kuagiza ashtakiwe kortini.