Habari Mseto

Yafichuka moto msitu wa Arabuko Sokoke uliwashwa na wanyakuzi wa ardhi

Na JURGEN NAMBEKA, SAMMY KIMATU October 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MKUTANO ulioandaliwa baada ya moto kuchoma ekari 17 za msitu asili wa Arabuko Sokoke, Kaunti ya Kilifi, umefichua kuwa mioto hiyo huanzishwa makusudi na watu katika jamii kama njia ya kuingilia msitu huo kuweka makao.

Mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi wa eneo hilo, maafisa wa Shirika la Kuhifadhi Misitu nchini (KFS) na wanajamii kujadili moto uliotokea Septemba 27.

Wakiongozwa na msimamizi wa Kaunti Ndogo ya Malindi, Bw Dadu Chome, mkutano huo ulihoji kuwa uchunguzi na maafisa kadhaa wa kulinda misitu, ulibaini kulikuwa na njama ya wakazi kuchoma maeneo kadha ili kutenga nafasi ya kuishi.

Msimamizi wa Msitu wa Arabuko Sokoke, Bw Willima Ochi, alithibitisha kuwa moto huo wa Ijumaa, ulikuwa hatua makusudi ya kujaribu kuingilia msitu huo.

Moto huo ulikuwa hatua ya hivi punde iliyojiongeza katika kesi za kujaribu kuondoa msitu huo ili watu wapate makazi.

Katika taarifa nyingine inayofungamana na mazingira, zaidi ya vijana 900 waliopata kazi ya kukomboa kingo za mto Ngong, Nairobi waliripoti kazini jana huku kukiwa na madai kwamba vijana wengi waliachwa nje wakati wa mchujo wa waliotuma maombi siku ya Jumapili.

Naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Starehe, Bw John Kisang, aliambia wanahabari kuwa serikali ina matumaini kuwa mto wa Ngong utasafishwa ung’are.

Pia aliwaonya wanaotumia mto huo kama eneo la kutupa takataka kuwa watakamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uchafuzi wa mazingira.

“Vijana ambao wamepata kazi hiyo watasimamiwa na Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS). Watafanya kazi kwa zamu mbili. Serikali inalenga kubuni nafasi za kazi na pia kudhibiti viwango vya uhalifu kupitia mpango huo,” Bw Kisang alisema akiwa Mukuru-Hazina, South B.

Jana, vijana waliokuwa wamesajiliwa baada ya kutuma maombi ya kazi kwa njia ya kielektoniki walikusanyika katika ofisi tatu katika tarafa ya South B.

Kwa mujibu wa Bw Kisang, vijana waliosajiliwa katika wadi ya Land Mawe walikusanyika katika ofisi ya chifu ya Landi Mawe na katika ofisi ya chifu ya Mukuru-Kayaba.

Vilevile, wengine wanaoishi katika wadi ya Nairobi Kusini walikusanyika katika uga wa chifu wa Mukuru-Mariguini na wenzao katika uwanja wa chifu ulioko Mukuru-Hazina.

Hayo yakijiri, baadhi ya Vijana walidai majina yao yaliondolewa kutoka kwa sajili ya waliotuma maombi ya kazi hiyo.