Makala

Mlipuko wa magonjwa watikisa Kakamega ulaji mizoga ukizidi

Na SHABAN MAKOKHA, BENSON MATHEKA October 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAAFISA wa afya Kaunti ya Kakamega wamezindua kampeni ya mashirika mbalimbali ya kukomesha ulaji wa mizoga ya wanyama waliokufa baada ya ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa kimeta kutikisa kaunti ndogo za Ikolomani na Shinyalu.

Ulaji wa nyama kutoka kwa wanyama waliokufa unazidi kuongezeka katika kaunti ndogo hizo mbili ndogo kwani huuzwa kwa bei nafuu au kutolewa kwa kubadilishana nafaka ikilinganishwa na nyama iliyokaguliwa kutoka kwa bucha ambayo inauzwa kwa Sh500 kwa kilo.

Uelewa mdogo wa mbinu za kisasa za utunzaji wa afya katika jamii za Kaunti ya Kakamega hapo awali ulitatiza ufuatiliaji wa magonjwa na hatua za mapema kuyakabili.

Mbinu mpya ya maafisa kutoka Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya inayoitwa mpango wa Afya Moja, inaleta pamoja mitindo ya kitamaduni, ushirikishaji wa jamii, na elimu ili kupunguza mambo yanayochangia milipuko ya magonjwa na kukuza afya ya umma kwa ujumla.

Katika muda wa miaka minne iliyopita, Kakamega imeshuhudia mfululizo wa milipuko ya magonjwa na matukio ya afya ya umma, na kuathiri pakubwa wakazi na sekta ya afya ya wanyama.

Mlipuko wa ugonjwa wa Kimeta katika eneo la Musol, Ikolomani ulisababisha vifo vya watu wanne na zaidi ya wanyama 27 kati ya Aprili na Julai 2023.

Mlipuko wa ugonjwa wa Kimeta eneo la Shinyalu mnamo Aprili 2023 uliathiri zaidi ya mifugo 30, na mlipuko wa kichaa cha mbwa Butere mnamo Oktoba 2023 ulisababisha zaidi ya watu 15 kuumwa na zaidi ya wanyama 40 kuathiriwa.

Huko Ikolomani na Shinyalu, inaaminika kuwa hakuna mzoga unaoweza kutupwa na hakuna mnyama anayepaswa kuzikwa.

Wenyeji hata hufukua nyama hiyo ili kugawana wao wenyewe kuila iwapo mnyama anayeshukiwa kufa kutokana na ugonjwa unaozua utata anazikwa.

Tabia ya kitamaduni Kaunti ya Kakamega inachangia pakubwa katika uwezekano wa kuzuka kwa magonjwa.

Kiutamaduni, inaaminika kuwa mzoga lazima ufunguliwe na kuchunwa ngozi ili mkulima aendelee kufuga wanyama. Iwapo mnyama atazikwa bila kufunguliwa itapelekea mfugaji kutowahi kufuga wanyama wengine.

Hii imeleta upinzani dhidi ya mbinu bora za utupaji wanyama waliokufa kutokana na kimeta na magonjwa mengine.