SHAMBULIO: Gaidi alikuwa katika WhatsApp ya ‘Nyumba Kumi’ Ruaka
Na STELLA CHERONO
MAJIRANI wa mmoja wa wagaidi walioaminika kuhusika katika shambulizi la DusitD2 walimtaja kama jamaa aliyekuwa anakaa pweke na ambaye alikuwa tayari amewekwa katika kikundi cha ‘Nyumba Kumi’ katika mtandao wa WhatsApp wa majirani.
Gaidi huyo aliweka bidhaa zake za nyumbani kwenye mitandao akitangaza kuziuza na kudai kuwa anahama Nairobi wiki hii.
Jamaa huyo ambaye nambari yake ya simu imesajiliwa kwa jina Ali Salim Gichunge pamoja na mkewe Violet Kemunto Omwoyo walitangaza kuuza bidhaa 17 kwa bei nafuu.
Gaidi huyo anayesemekana kutoka Kiambu alijisajili kuwa mkaazi wa eneo hilo kwa jina Idriss na alikuwa majirani walikuwa wanamuita Farouk.
Majirani wanasema alikuwa anapenda kucheza muziki wa juu katika gari lake hata wakati alikuwa anawasili nyumbani usiku wa manane.
Saa chache baada ya kutokea kwa shambulizi hilo eneo la 14 Riverside Drive, maafisa wa kupambana na ugaidi (ATPU), walivamia nyumba ya gaidi huyo, nyumba nambari 9 mtaani Guango na kuwakamata wanawake wamili.
“Maafisa waliokuwa wamejihami walikuja hapa na magari zaidi ya kumi na kufululiza hadi kwa nyumba hiyo mwendo was aa tano usiku. Hatukujua walichopata huko ndani lakini wakitoka walienda kasi huku magari yakiwasha vingora,”alisema jirani mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Jirani huyo alimtaja mshukiwa huyo kama mwanamume wa umri wa makamu aliyekuwa ‘amejenga mwili’
“Alikuwa anaishi na mwanamke wa umri wa makamu lakini hakuna anatengana na watu wengine isipokuwa muuzi nyama nje ya lango la mtaa. Amefuga paka na nashuku ndio alikuwa anawanunulia nyama.”
Majirani walimtambua mshukiwa huyo baada ya gari alilokuwa akitumia lenye usajili KCN 340E kupatika miongoni mwa magari yaliyotumiwa na magaidi kuingia katika lango la hoteli ya Dusit D2.
Majirani walisema gaidi huyo alihamia mtaani humo kati ya Oktoba na Novemba na akawekwa katika kikundi cha Nyumba Kumi mnamo Novemba 10.
“Hakuwa anasema chochote katika kundi letu la na hata Whatsapp yake haikuwa na picha,”alisema jirani mmoja.
Gari hilo lililotumika imesajiliwa chini ya kampuni ya Cynkim Investment na maafisa wa polisi walisema kuwa umiliki wa gari hilo bado haukuwa umehashwa kwa mshukiwa huyo.
Walioshuhudia dakika za mwanzo za shambulizi hilo walisema walinzi walijaribu kusimamisha magaidi hao bila kufaulu.
Gari hilo lilifululiza hadi kwenye lango kuu la hoteli hiyo na magaidi hao wakawalazimisha walinzi kufungua lango hilo kwa kuwatishia kuwapiga risasi.
Magaidi wengine walikuwa wakitumia gari lingine ambalo walilipua baada ya kuliegesha kati kati mwa magari mengine mawili yaliyoteketea papo hapo.
Maafisa wa ujasusi sasa wanaendelea kudukua mawasiliano yote ya mshukiwa huyo ili kusaidia katika uchunguzi.
Tukienda mitamboni, maafisa wa ujasusi bado walikuwa wamekita kambi katika nyumba hiyo yake ya vyumba vitatu.