Tambua kwa nini majaji sita watavuna Sh126 milioni sababu ya ‘ujeuri’ wa Uhuru
MAJAJI sita wamefidiwa jumla ya Sh126 milioni kwa haki zao kukiukwa na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta aliyekataa kuwateua kama ilivyopendekeza Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) mwaka wa 2019.
Jaji wa Mahakama Kuu Chacha Mwita Jumanne alisema Rais William Ruto hakuwa na chaguo ila kuwateua majaji hao jinsi ilivyopendekezwa na JSC, na kwamba hatua ya kuwalazimisha kusubiri kwa miaka mitatu iliharibu sifa na utu wao.
JSC ilikuwa imependekeza kuteuliwa kwa Majaji Aggrey Muchelule, Weldon Korir, Prof Joel Ngugi na George Odunga katika Mahakama ya Rufaa na Majaji Judy Omange, na Evans Makori katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi.
Majaji hao sita hatimaye waliapishwa na Rais Ruto, punde tu baada ya kuingia mamlakani mnamo 2022.
Jaji Mwita aliongeza kuwa hatua ya Rais Mstaafu kutilia shaka uadilifu wa majaji hao, hasa kutoka kwa mtu anayeshikilia wadhifa wa juu zaidi nchini, iliweka sifa za majaji hao hatarini.
“Katika hali hiyo, ninashikilia kuwa kukataa au kutochukua hatua kwa Rais Mstaafu hakukuwa na msingi wa sheria yoyote na hivyo alikiuka haki na uhuru wao wa kimsingi,” alisema jaji.
Aliwapa majaji hao Sh16 milioni kila mmoja kama fidia ya jumla na Sh5 milioni kila mmoja kwa athari walizopata kutokana na matumizi mabaya ya mamlaka ya kiongozi wa serikali.
Jaji huyo alisema ni wazi kuwa Rais Kenyatta alionyesha ubaguzi mbele ya sheri, alipochagua majaji 34 kama ilivyopendekezwa na JSC na kuwaacha sita. Alisema Rais Mstaafu hakutoa maelezo ya maandishi kueleza kwa nini alikataa uteuzi huo.
Jaji Mwita aliongeza kuwa baada ya kupendekezwa na JSC, rais hakuwa na mamlaka ya kuchagua baadhi na kuwaacha wengine.
Majaji hao waliteta katika kesi yao kwamba licha ya kuhudumu kama maafisa wa ngazi za juu mahakamani, walivumilia kudhalilishwa hadharani baada ya Rais Kenyatta kukataa uteuzi wao.