Jamvi La Siasa

Nimeponea majaribio mawili ya serikali kunitilia sumu, Gachagua asema

Na CECIL ODONGO October 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NAIBU Rais aliyetimuliwa afisini Rigathi Gachagua Jumapili alizidisha uhasama kati yake na Rais William Ruto akidai kuwa kulikuwa na majaribio mawili ya kumuua kabla ya mpango wa kumng’oa mamlakani kukumbatiwa.

Bw Gachagua alisema kuwa kulikuwa na jaribio la kumuua mnamo Agosti 30 wakati ambapo chakula chake karibu kitiliwe sumu jijini Kisumu akiwa ziarani Nyanza na Rais Ruto.

Pia alisema watu ambao alidai walikuwa ni maafisa wa Shirika la Ujasusi Nchini (NIS) walitia sumu chakula ambacho alikuwa ale na Baraza la Wazee wa Agikuyu mnamo Septemba 3.

“Nataka kuwaambia Wakenya kuwa sihisi niko salama kutokana na matukio haya mawili,” akasema Bw Gachagua.

Alikuwa akiongea jana baada ya kuondoka Hospitali ya Karen ambako alikuwa amelazwa kwa siku tatu kutokana na maumivu ya kifua. Bw Gachagua alilazwa hospitalini humo mnamo Alhamisi usiku wakati ambapo mchakato wa kumwondoa mamlakani ulikuwa ukiendelea kwenye Bunge la Seneti.

Alifunguka kuwa aliarifu NIS kuhusu matukio hayo mawili na akawaomba maafisa waliokuwa wamewekwa katika afisi yake waondoke. Alifichua kuwa ni baada ya majaribio haya mawili ya kumuua kufeli ndipo hoja ya kumtimua iliwasilishwa bungeni kumkata miguu kisiasa.

Akiwa hospitalini, Bw Gachagua alisema kuwa maafisa wanaomlinda waliondolewa na watu wanaoaminika walikuwa maafisa wa NIS walitumwa kumwangalia hospitalini humo na akahofia usalama wake.

“Nilimpigia mke wangu na watoto wangu waje wakae kwenye chumba changu ili iwapo watu wanaonitibu wangeingiliwa na kushawishiwa wanidhuru basi ningeepuka hilo. Rigathi na familia yake kwa sasa hawapo salama kwa sababu wamejaribu kutuua na sasa wanataka kutuondoa afisini,” akaongeza.

Kufikia jana jioni, serikali wala Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed hakuwa ametoa taarifa kuhusu madai ambayo yalitolewa na Bw Gachagua.

Wakati wa kikao hicho na wanahabari, huzuni iliwateka mkewe Bw Gachagua, Bi Dorcas Rigathi na wanawe wawili,  mmoja wa wavulana wake akionekama kudondokwa na machozi kwa kulemewa na hisia.

Ilikuwa dhahiri kuwa naibu rais alikuwa akianza maisha mapya kwa kuwa baada ya kikao hicho aliondoka na familia yake kama raia wa kawaida bila maafisa wengi wa usalama ambao kawaida  humlinda na kuandamama na msafara wake.

Mnamo Jumamosi, serikali iliondoa wafanyakazi katika makazi ya Naibu Rais na pia nyumbani kwake kule Mathira. Japo Profesa Kithure Kindiki aliteuliwa naibu rais, bado kuna kesi mahakamani ambayo inamzuia kuchukua usukani.

Naibu Rais aliyetimuliwa pia aliamua kumshukia Rais Ruto akisema hakuamini kuwa angemgeuka kisiasa licha ya ukuruba ambao walikuwa nao wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Alihusisha masaibu yake serikalini kutokana na kusema ukweli kuhusu sera mbovu ambazo zimekuwa zikitekelezwa za kuwaumiza raia kiuchumi.

“Mimi ndiye mwanaume pekee kwenye baraza la mawaziri na serikali ambaye angesimama na kumkataza Rais kuwa anafanya jambo baya. Hili suala la Adani si zuri, kuna ufisadi mwingi, haya makazi ya gharama nafuu unawalazimishia Wakenya,

“Tuko katika hali ambayo tenda ya kutoa vifaa vya kimatibabu ambayo ilikuwa ikitolewa na Wakenya kwa Wizara ya Afya sasa imepewa raia wa Asia. Nilimwaambia,” akasema.

Kuhusu sherehe za mashujaa zilizofanyika katika Kaunti ya Kwale, Bw Gachagua alifichua kuwa usimamizi wa uwanja wa ndege wa Wilson uliamrishwa asikubali atumie uwanja huo hadi mahali ambapo sherehe za kitaifa zilikuwa zikiendelea.

Pia alisema wamiliki wa ndege za helikopta walionywa dhidi ya kumruhusu azitumie kufika katika sherehe. Alishangaa kwa nini adhulumiwe hivyo, wakati ambapo naye alikuwa anapambana kuwa hai ilhali alimsaidia sana Rais kupata kura za Mlima Kenya kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

“Hakuna mtu ambaye aliamini rais tulipokuwa tukiunda UDA. Kila mtu akiwemo Moses Wetangúla (Ford Kenya), Musalia Mudavadi (ANC), Amos Kingi (PAA) walisisitiza tuandikiane mkataba. Ni mimi pekee yangu sikufanya hivyo kwa sababu nilimwaamini,” akasema.

Katika kile kilichoonyesha anaumia kwenye nafsi yake, Bw Gachagua alimtaka Rais amwaache pamoja na familia yake na kuwa hana kinyongo na mtu yeyote.

“Fanya kile ambacho unataka lakini niwache niwe hai. Niache niwaangalie watoto wangu na unaweza kufanya chochote kile unachotaka na nchi. Nilikuwa pamoja nawe wakati ulihitaji mtu na ulikuwa mashakani,

“Umetulipa kwa maovu na sisi ni watu wa kawaida na familia ndogo. Fanya kile unachotaka lakini usituue kwa kuwa umenitesa sana kwa muda wa mwaka moja,

“Mungu atanilinda na kwa kuwa umenipokonya walinda usalama, niruhusu niwe na amani lakini kumbuka nilikusaidia wakati ulihitaji mtu wa kusimama nawe,” akasema.

Gachagua alisema ana matumaini katika idara ya mahakama kuwa haki itatendeka akisema aliondolewa afisini kinyume cha sheria na bado yupo tayari kujitetea mbele ya Bunge la Seneti.