Baridi yawasumbua wanasiasa waliotemwa, wajuta kuunga Ruto 2022
RAIS William Ruto sasa anaonekana kutengana na baadhi ya wanasiasa wakuu ambao walimuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 baada ya kuanza ushirikiano na Kinara wa Upinzani Raila Odinga.
Wanasiasa waliotemwa ni wale wa UDA ambao walikuwa mstari wa mbele kumfanyia Rais kampeni katika uchaguzi huo ambao Bw Odinga alikuwa mshindani wake mkuu.
Kando na Naibu Rais aliyetimuliwa Rigathi Gachagua, wanasiasa wengine ambao sasa wametalikiwa na Rais Ruto ni aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi, aliyekuwa Katibu wa UDA Cleophas Malala na mbunge wa zamani wa Bahati Kimani Ngunjiri.
Waliokuwa mawaziri Aisha Jumwa, Ababu Namwamba na Zack Njeru pia sasa hawaonani uso kwa macho na rais. Masenata John Methu (Nyandarua), Joe Nyutu (Murang’a), James Murango (Kirinyaga), Karungo Thangwa (Kiambu) na Gavana Kahiga Mutahi (Nyeri) pia wamehama mrengo wa Rais Ruto
Bw Linturi amejutia kufanya kazi na Rais Ruto bila kuwa na mkataba wowote wa kisiasa.
“Kuelekea uchaguzi wa 2022 tulijituma sana kuhakikisha Rais Ruto anashinda. Hata hivyo, najutia sana kukosa kutia saini mkataba ili kuzingatia maslahi yangu,
“Wakati wengine walikuwa wakitumia vyama vyao kutia saini mikataba, Gachagua na mimi tulimwaamini Rais Ruto. Sasa hatuna kazi,” akasema Bw Linturi.
Bw Ngunjiri ambaye alikuwa kati ya watu walioongoza kampeni za Rais Ruto Kusini mwa Bonde la Ufa naye sasa yuko kwenye kijibaridi kisiasa.
Hata hivyo, amemlaumu Bw Odinga kwa kuingia serikalini na kumvuruga Rais Ruto akisema ndiyo sababu Bw Gachagua ametupwa nje ya serikalini.
“Rais wetu alikuwa mtu mzuri lakini kuingia kwa Raila na wandani wake serikalini kumesababisha mgawanyiko ndani ya Kenya Kwanza. Namwomba Mungu amsaidie Rais Ruto aone nuru tena,” akasema Bw Ngunjiri.
Magharibi mwa Kenya, Bw Malala amemtoroka Rais baada ya kutimuliwa kama Katibu Mkuu wa UDA. Seneta huyo wa zamani wa Kakamega amemshutumu Rais vikali kwa kuwasaliti watu ambao walimuunga mkono mnamo 2022.
“Rais Ruto umekuwa na roho mbaya kiasi hiki? Naibu wako ni mgonjwa na bado unampiga vita. Rais tulikusaidia na kukupigania wala hatukujua utakuwa mtu ambaye hajali marafiki zake lakini tumeachia Mungu,” akasema Bw Malala.
Kwa mujibu wa Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa Steve Kabita, Rais Ruto huenda aliona baadhi ya wandani wake walikuwa wamepanga kumkata miguu kisiasa ndiposa akapata mwokozi kwa waliokuwa wapinzani wake mnamo 2022.
“Rais anajiandaa kwa 2027 na baadhi ya watu ambao wanadai ni marafiki zake ndio pengine amegundua wanapanga kummaliza kisiasa. Ruto, Musalia Mudavadi na Raila wamewahi kufanya kazi pamoja na sasa wanaunda muungano dhabiti wa mnamo 2027,” akasema Bw Kabita.
Mchanganuzi mwengine Jesse Karanja naye anasema kuwa Bw Gachagua huenda alichongewa na ushindani kati ya dhidi ya Rais huku akionekana kama aliyekuwa na ndoto ya kuwa Rais.