Jamvi La Siasa

Wakenya wapewa mapumziko leo Ijumaa kutoa nafasi ya Kindiki kuapishwa

Na CHARLES WASONGA November 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MKUU wa Mawaziri Musalia Mudavadi ametangaza Ijumaa, Novemba 1, 2024 kuwa siku ya mapumziko kutoa nafasi kwa Wakenya kufuatilia kuapishwa kwa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais.

Mudavadi ametoa tangazo hilo Alhamisi Oktoba 31, 2024 kupitia toleo maalum la gazeti rasmi la serikali dakika chache baada ya Rais William Ruto kumteua kuwa Kaimu Waziri wa Usalama wa Ndani.

“Umma unajulishwa kwamba Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa kwa mujibu wa mamlaka ya sehemu ya 3 ya Sheria ya Sikukuu za Kitaifa na sehemu ya 3 (b) na 12 (3) ya Sheria kuhusu Rais Kuingia Afisini, ametangaza Ijumaa Novemba 1, 2024 kuwa siku ya mapumziko, kwani ni siku ya kuapishwa na Naibu Rais Mteule,” Bw Mudavadi akasema.

Profesa Kindiki amekuwa akihudumu kama Waziri wa Usalama hadi Oktoba 18, 2024 Bunge la Kitaifa lilipoidhinisha uteuzi wake kuwa Naibu Rais.

Hii baada ya Seneti kupitisha hoja ya kumtimua afisini aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Haya yanajiri baada ya Katibu wa Baraza la Mawaziri Mercy Wanjau, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya kuandaa hafla ya kumwapisha Profesa Kindiki kutangaza kuwa shughuli hiyo itafanyika saa nne asubuhi katika uwanjwa wa KICC, Nairobi.

Majina ya wanachama 21 wa kamati hiyo yalichapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali dakika chache baada ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu kuondoa agizo la Jaji Richard Mwongo (wa Kerugoya) lililositisha kwa muda kuapishwa kwa Profesa Kindiki.

Katika uamuzi waliotoa katika Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi, Alhamisi, Majaji Eric Ogola, Antony Mrima na Freda Mugambi alisema walizingatia haja ya afisi hiyo kuwa na mshikilizi ili “kuzuia kutokea kwa mgogoro wa kikatiba”.

“Mahakama hii inazingatia kuwa afisi ya Naibu Rais haiwezi kusalia wazi na hiyo itazingatia hitaji la Katiba kuwa sharti kuwe na mshikilizi wake nyakati zote,” majaji hao wakasema.

Walisema kesi hiyo inavutia masilahi ya umma na hivyo wamejitolea “kuhakikisha kuwa inaamuliwa haraka.”

Waliratibu Novemba 7, 2024 kuwa siku ambayo kesi iliyowasilishwa mbele yao na Bw Gachagua kupinga kutimuliwa kwake itasikizwa.

Kuondolewa kwa agizo la kusitishwa kuapishwa kwa Profesa Kindiki ni pigo kwa Bw Gachagua ambaye amekuwa akitegemea mahakama kumnusuru.

Awali, Mahakama ya Rufaa ilidinda kuzuia Mahakama Kuu kutoa uamuzi kuhusu agizo la kuzimwa kwa hafla ya kumwapisha Naibu Rais mpya.